Home About Articles Ask the Sheikh
null

Jibu la Swali: Dua ya Kuangamiza Dola ya Kiyahudi

October 08, 2024
102

Silsila ya Majibu ya Mwanachuoni Mtukufu Ata bin Khalil Abu al-Rashtah, Amir wa Hizb ut-Tahrir, kwa Maswali ya Wageni kwenye Ukurasa wake wa Facebook "Fiqhi"

Kwa Agus Trisa

Swali:

Assalamu alaikum wa rahmatullahi wa barakatuhu. Mwenyezi Mungu akulinde popote ulipo. Nataka kukuuliza kuhusu aya hii tukufu, Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Ta’ala anasema:

وَإِذَا سَأَلَكَ عِبَادِي عَنِّي فَإِنِّي قَرِيبٌ أُجِيبُ دَعْوَةَ الدَّاعِ إِذَا دَعَانِ فَلْيَسْتَجِيبُوا لِي وَلْيُؤْمِنُوا بِي لَعَلَّهُمْ يَرْشُدُونَ

"Na waja wangu watakapokuuliza khabari zangu, basi Mimi nipo karibu. Naitikia maombi ya mwombaji anaponiomba. Basi na waniitikie Mimi, na waniamini Mimi, ili wapate kuongoka." (QS. Al-Baqarah [2]: 186)

Je, ni kweli kwamba Mwenyezi Mungu anajibu maombi yote ya mwanadamu?

Je, kuna dua ambayo Mwenyezi Mungu haijibu?

Baadhi ya watu wanauliza, tumewaombea Israel waangamizwe na Mwenyezi Mungu, lakini kwa nini bado wana nguvu na wanaendelea kushambulia Ghaza?

Asante kwa jibu lako, Mwenyezi Mungu akulipe malipo bora zaidi. Wassalamu alaikum wa rahmatullahi wa barakatuhu.

Tafsiri ya Swali:

Assalamu Alaikum wa Rahmatullahi wa Barakatuhu, Mwenyezi Mungu akulinde popote ulipo.

Nataka kukuuliza kuhusu aya hii tukufu ambapo Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Ta’ala anasema:

وَإِذَا سَأَلَكَ عِبَادِي عَنِّي فَإِنِّي قَرِيبٌ أُجِيبُ دَعْوَةَ الدَّاعِ إِذَا دَعَانِ فَلْيَسْتَجِيبُوا لِي وَلْيُؤْمِنُوا بِي لَعَلَّهُمْ يَرْشُدُونَ

"Na waja wangu watakapokuuliza khabari zangu, basi Mimi nipo karibu. Naitikia maombi ya mwombaji anaponiomba. Basi na waniitikie Mimi, na waniamini Mimi, ili wapate kuongoka." (QS. Al-Baqarah [2]: 186)

Je, ni kweli kwamba Mwenyezi Mungu anajibu kila dua ya mwanadamu?

Je, kuna dua ambayo Mwenyezi Mungu haijibu?

Baadhi ya watu wanauliza kwamba wameomba dua ili Mwenyezi Mungu aangamize dola ya Kiyahudi, lakini kwa nini bado dola hiyo ina nguvu na inaendelea na mashambulizi yake dhidi ya Ghaza?

Nakushukuru kwa jibu lako, na namuomba Mwenyezi Mungu akulipe kheri kwa jibu lako zuri.

Wassalamu Alaikum wa Rahmatullahi wa Barakatuhu.

Jibu:

Walaikum Assalam wa Rahmatullahi wa Barakatuhu.

Kuna mambo ambayo ni lazima yajulikane kuhusu dua:

1- Hakika muumini anapomuomba Mwenyezi Mungu kwa moyo mkweli, dua ambayo haina ndani yake madhambi wala kukata undugu, basi Mwenyezi Mungu Subhanahu huijibu kwa njia moja kati ya tatu, kama ilivyo katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu Subhanahu na Sunnah za Mtume wake ﷺ:

Mwenyezi Mungu Subhanahu anajibu dua ya mwombaji anapomuomba, na anamjibu mwenye shida anapomuomba;

وَقَالَ رَبُّكُمُ ادْعُونِي أَسْتَجِبْ لَكُمْ "Na Mola wenu Mlezi amesema: Niombeni, nitakuitikieni." (QS. Ghafir [40]: 60)

وَإِذَا سَأَلَكَ عِبَادِي عَنِّي فَإِنِّي قَرِيبٌ أُجِيبُ دَعْوَةَ الدَّاعِ إِذَا دَعَانِ "Na waja wangu watakapokuuliza khabari zangu, basi Mimi nipo karibu. Naitikia maombi ya mwombaji anaponiomba." (QS. Al-Baqarah [2]: 186)

أَمَّنْ يُجِيبُ الْمُضْطَرَّ إِذَا دَعَاهُ وَيَكْشِفُ السُّوءَ "Au nani yule anayemuitikia mwenye shida anapomwita, na akaiondoa dhiki?" (QS. An-Naml [27]: 62)

Hata hivyo, ujibu wa dua una uhalisia wa kisheria uliowekwa wazi na Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ:

«مَا مِنْ مُسْلِمٍ يَدْعُو اللهَ عَزَّ وَجَلَّ بِدَعْوَةٍ لَيْسَ فِيهَا إِثْمٌ وَلَا قَطِيعَةُ رَحِمٍ، إِلَّا أَعْطَاهُ اللَّهُ بِهَا إِحْدَى ثَلَاثِ خِصَالٍ: إِمَّا أَنْ يُعَجِّلَ لَهُ دَعْوَتَهُ، وَإِمَّا أَنْ يَدَّخِرَهَا لَهُ فِي الْآخِرَةِ، وَإِمَّا أَنْ يَصْرِفَ عَنْهُ مِنَ السُّوءِ مِثْلَهَا. قَالُوا: إِذًا نُكْثِرُ. قَالَ: اللهُ أَكْثَرُ» "Hakuna Muislamu yeyote anayemuomba Mwenyezi Mungu dua ambayo haina dhambi wala kukata undugu, isipokuwa Mwenyezi Mungu humpa mambo matatu: Ima ampe haraka kile alichoomba, au amuwekee akiba kwa ajili ya Akhera, au amuepushie uovu mfano wa dua hiyo. Wakasema: Basi tutazidisha (kuomba). Akasema: Mwenyezi Mungu ni zaidi." (Imepokelewa na Ahmad 3/18).

Vilevile:

«لَا يَزَالُ يُسْتَجَابُ لِلْعَبْدِ مَا لَمْ يَدْعُ بِإِثْمٍ أَوْ قَطِيعَةُ رَحِمٍ مَا لَمْ يَسْتَعْجِلْ. قِيلَ: يَا رَسُولَ اللهِ، مَا الِاسْتِعْجَالُ؟ قَالَ: يَقُولُ قَدْ دَعَوْتُ وَقَدْ دَعَوْتُ فَلَمْ أَرَ يَسْتَجِيبُ لِي فَيَسْتَحْسِرُ عِنْدَ ذَلِكَ وَيَدَعُ الدُّعَاءَ» "Mja ataendelea kujibiwa dua yake madamu haombi dhambi wala kukata undugu, na madamu hafanyi haraka. Ikasemwa: Ee Mtume wa Mwenyezi Mungu, kufanya haraka ni nini? Akasema: Ni kusema nimeomba na nimeomba lakini sijaona nikijibiwa, kisha anakata tamaa wakati huo na kuacha dua." (Imepokelewa na Muslim 4918).

Hivyo basi, tunamuomba Mwenyezi Mungu Subhanahu na ikiwa sisi ni wakweli, wenye ikhlasi na watiifu, basi tuwe na yakini ya kujibiwa kwa maana aliyoibainisha Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ.

2- Hakika dua pekee siyo njia ya kisheria (tariqah shari’iyyah) ya kufikia lengo katika hali zote. Dua ni mandub (inapendekezwa), lakini siyo njia ya kupata ushindi katika vita au kusimamisha dola n.k. Mtume ﷺ alikuwa akitayarisha jeshi katika vita vya Badr, akipanga askari kila mmoja katika nafasi yake, na kuwaandaa vizuri kwa ajili ya mapigano, kisha Mtume ﷺ akaingia katika banda lake (al-arish) akimuomba Mwenyezi Mungu ushindi na kukithirisha dua mpaka Abu Bakr (ra) akamwambia: "Baadhi ya haya yanakutosha ee Mtume wa Mwenyezi Mungu." (Sirah Ibn Hisham 2/626). Hivyo basi, dua haimaanishi kuacha kuchukua sababu (hatua za kimaada), bali dua huambatana nazo.

Pia, yule anayependa Khilafah isimamishwe upya, basi asitosheke tu na kumuomba Mola wake ili kufanikisha hilo, bali afanye kazi pamoja na wafanyao kazi kuitafuta, na amuombe Mwenyezi Mungu msaada katika hilo na kuharakisha utekelezaji wake, na akithirishe dua kwa ikhlasi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu huku akichukua hatua za kimaada (al-akhdhu bil-asbab).

Na hivyo ndivyo ilivyo katika matendo yote; mtu afanye kazi kwa ikhlasi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na ukweli kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ, na aombe na kukithirisha dua, na Mwenyezi Mungu ni Msikivu na Mwenye kujibu.

3- Tayari tulishajibu swali kama hili tarehe 4 Dhul-Qi'dah 1432 H - 01/10/2011 M, ambapo ilikuja ndani yake:

[.........

  • Ama dua pamoja na kuchukua hatua za kimaada (al-akhdhu bil-asbab), basi ina athari katika matokeo, na hivi ndivyo alivyokuwa Mtume ﷺ, na Masahaba wake (ra). Mtume ﷺ anaandaa jeshi na kuingia katika banda (al-arish) akiomba, na Waislamu huko Qadisiyah wanaandaa zana za kuvuka mto huku Sa’d (ra) akimuelekea Mwenyezi Mungu akiomba... na hivyo ndivyo waumini wa kweli wanavyoandaa zana na kuanza kuomba. Mwenye kutafuta riziki anajitahidi na kutaabika huku akiomba, na mwanafunzi anasoma na kujitahidi huku akimuomba Mwenyezi Mungu Subhanahu apate mafanikio, na jambo hilo linakuwa na athari katika matokeo kwa idhini ya Mwenyezi Mungu.

Ilikuja katika kitabu Mafahim (dhana) ukurasa wa mwisho (uk. 58): (Hata hivyo, lazima ijulikane kwamba ingawa kitendo ambacho njia (tariqah) imekionyesha ni kitendo cha kimaada chenye matokeo yanayohisika, lakini ni lazima kitendo hicho kiongozwe na amri na makatazo ya Mwenyezi Mungu, na kukusudiwa katika kukiendesha huko kwa amri na makatazo ya Mwenyezi Mungu ni radhi za Mwenyezi Mungu. Kadhalika, ni lazima Muislamu atawaliwe na utambuzi wake wa uhusiano wake na Mwenyezi Mungu Ta’ala, hivyo ajikurubishe Kwake kwa swala, dua, kusoma Qur’ani na mfano wake, na lazima Muislamu aamini kwamba ushindi unatoka kwa Mwenyezi Mungu. Na kwa ajili hiyo, ilikuwa ni lazima kuwe na uchamungu uliokita vifuani kwa ajili ya kutekeleza hukumu za Mwenyezi Mungu, na ilikuwa ni lazima kuwe na dua, na ni lazima kumdhukuru Mwenyezi Mungu, na ni lazima kudumu katika uhusiano na Mwenyezi Mungu wakati wa kufanya matendo yote). Ni wazi hapa umuhimu wa kuoanisha dua na kuchukua sababu katika matendo yote ya muumini, na umuhimu huu umeongezeka kwa kurudia neno "ni lazima" ili kuonyesha umuhimu mkubwa wa kuoanisha matendo yote na dua na kudumu katika uhusiano na Mwenyezi Mungu...

  • Hakika matumizi ya dua pamoja na kuchukua sababu ndiyo yale, kama tulivyosema, aliyokuwa nayo Mtume ﷺ na Masahaba wake (ra) na waumini. Na yote mawili yakioanishwa yanakuwa na athari katika matokeo kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, na kuyatumia yote mawili pamoja hakupingani na njia ya Uislamu, bali kinachopingana nayo ni kutosheka na dua pekee bila njia (tariqah) iliyobainishwa na maandiko kwa ajili ya kutekeleza fikra ya Kiislamu...].

Kwa hivyo, yale yaliyokuja katika swali lako kuhusu dua ya kuangamiza dola ya Kiyahudi... hili haitoshi ndani yake dua pekee, bali ni lazima kuoanishwa kwa jeshi la dola linalopigana na Wayahudi pamoja na dua kama alivyokuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ na Masahaba wake (ra), na Mwenyezi Mungu ndiye wa kuombwa msaada.

Ndugu yenu, Ata bin Khalil Abu al-Rashtah

04 Rabi' al-Akhar 1446 H Sawiya na 07/10/2024 M

Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir (Mungu amuhifadhi) kwenye Facebook: https://www.facebook.com/AtaabuAlrashtah.A.HT/posts/122125130186447297

Share Article

Share this article with your network