Home About Articles Ask the Sheikh
null

Jibu la Swali: Kusoma Al-Fatiha katika Swala ya Jamaa na Mchanganyiko (Ikhtilat) katika Ziara za Familia

April 17, 2022
4111
Silsila ya Majibu ya Mwanachuoni Mkubwa Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah, Amir wa Hizb ut-Tahrir, kwa maswali ya wafuasi wa ukurasa wake wa Facebook "Fikhi"

Kwa: Al-Maqdisi

Swali:

Assalamu Alaikum Warahmatullahi Wabarakatuh, Mwenyezi Mungu awasaidie.

Nina maswali mawili; la kwanza kuhusu mada ya swala na la pili kuhusu mada ya ziara za kifamilia.

Swali la kwanza: Ni nini hukumu ya ma’mum (anayeswali nyuma ya imamu) kusoma Al-Fatiha katika swala? Na je, kuwahi kumdiriki imamu akiwa katika rukuu au karibu na kurukuu kiasi kwamba ma’mum hawezi kusoma Al-Fatiha yote, je, hiyo inahesabika kuwa ni rakaa?

Swali la pili: Katika ziara za kifamilia au kuunganisha undugu (silat al-rahim) wakati wa sikukuu na nyakati nyingine, mume wa dada hukutana na mke wa kaka, au mtoto wa kiume wa ami na mtoto wa kike wa ami, au mke wa kaka na kaka na kadhalika, kukiwa na mahram ndani ya nyumba na katika kikao kimoja wakati wa chakula au bila chakula, katika nyumba ya familia au kwingineko. Ni nini hukumu ya kisheria kuhusu jambo hilo?

Tufafanulieni na Mwenyezi Mungu awabariki.

Jibu:

Wa Alaikum Salaam Warahmatullahi Wabarakatuh.

1- Kuhusu kumdiriki imamu bila kuweza kusoma Al-Fatiha, yaani "swala ya masbuq", tumelifafanua hili katika kitabu cha "Ahkam al-Salat" ukurasa wa 67, ambapo tulisema yafuatayo:

"Ikiwa ma’mum atadiriki kusimama (qiyam) pamoja na imamu na akachelea kukosa kisomo, ataacha dua ya ufunguzi (istiftah) na kuanza kusoma (Al-Fatiha), kwa sababu hiyo ni faradhi hivyo asijishughulishe na jambo la sunna badala yake. Ikiwa atasoma sehemu ya Al-Fatiha kisha imamu akarukuu, naye atarukuu na kuacha kisomo, kwa sababu kumfuata imamu ni wajibu zaidi. Na ikiwa atamdiriki akiwa katika rukuu, atapiga takbira ya hihramu (takbirat al-ihram) akiwa amesimama, kisha atapiga takbira ya rukuu na kurukuu. Lakini akipiga takbira moja akikusudia hihramu na rukuu pamoja, haitoshelezi faradhi yake kwa sababu ameshirikisha nia kati ya faradhi na sunna, na hivyo swala yake haitofungika. Na akidiriki rukuu inayokubalika pamoja na imamu, basi ameadiriki rakaa hiyo, na asipoidiriki rukuu hiyo basi hajaidiriki rakaa. Na pindi anapoadiriki rakaa moja pamoja na imamu, basi ameadiriki swala ya jamaa, kutokana na yale yaliyopokelewa kutoka kwa Abu Hurairah (ra) akisema: Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ amesema:

إِذَا جِئْتُمْ إِلَى الصَّلَاةِ وَنَحْنُ سُجُودٌ فَاسْجُدُوا وَلَا تَعُدُّوهَا شَيْئاً وَمَنْ أَدْرَكَ الرَّكْعَةَ فَقَدْ أَدْرَكَ الصَّلَاةَ

“Mkijia swala na tuko katika sijida, basi sujuduni na msihesabu kitu (hiyo si rakaa), na yule atakayewahi rakaa (ruku'u), basi amewahi swala.”

Na ikiwa atadiriki rakaa ya mwisho pamoja na imamu, hiyo itakuwa ni mwanzo wa swala yake kutokana na yale yaliyopokelewa kutoka kwa Ali (ra) kwamba alisema: “Kile ulichodiriki ndio mwanzo wa swala yako.” Na kwa msingi huu, imamu akitoa salamu, yeye atasimama kukamilisha kile kilichobaki katika swala yake. Ikiwa hilo litatokea katika swala yenye qunuti na akasoma qunuti pamoja na imamu, atairudia qunuti hiyo mwishoni mwa swala yake. Na inampasa ma’mum kumfuata imamu na asimtangulie katika kitendo chochote, kwa yale aliyopokea Abu Hurairah kwamba Mtume ﷺ amesema:

إِنَّمَا جُعِلَ الْإِمَامُ لِيُؤْتَمَّ بِهِ فَلَا تَخْتَلِفُوا عَلَيْهِ، فَإِذَا كَبَّرَ فَكَبِّرُوا، وَإِذَا رَكَعَ فَارْكَعُوا، وَإِذَا قَالَ سَمِعَ اللَّهُ لِمَنْ حَمِدَهُ فَقُولُوا اللَّهُمَّ رَبَّنَا لَكَ الْحَمْدُ، وَإِذَا سَجَدَ فَاسْجُدُوا

“Hakika imamu amewekwa ili afuatwe, basi msimuhalifu; akipiga takbira, pigeni takbira, akirukuu rukuuni, akisema 'Sami'allahu liman hamidah', semeni 'Allahumma Rabbana laka al-hamd', na akisujudu sujuduni.”

Na ikiwa imamu atasahau katika swala yake, ikiwa ni katika kisomo, ma’mum atamkumbusha, kutokana na yale aliyopokea Anas akisema: “Maswahaba wa Mtume ﷺ walikuwa wakikumbushana (kisomo) katika swala.” Na ikiwa ni katika dhikri nyingine isiyo kisomo, ma’mum ataitaja kwa sauti ili asikike, na akisahau katika kitendo, atamtasbihia (kusema SubhanAllah) ili ajue. Na ikiwa ma’mum atanuia kujitenga na imamu na akajikamilishia mwenyewe inaruhusiwa, sawa ikiwa ni kwa udhuru au bila udhuru: “Kwa sababu Muadh alirefusha kisomo, hivyo Mwarabu mmoja wa kijijini alijitenga naye, na jambo hilo likatajwa kwa Mtume ﷺ naye hakumkataza.”

2- Ama kuhusu kuunganisha undugu (silat al-rahim), jambo hili limefafanuliwa katika vitabu vyetu:

1- Kutoka katika kitabu cha Nidhamu ya Kijamii – Kuunganisha Undugu (Silat al-Arham):

(...Dhahiri ya hadithi ni ujumla, hivyo inajumuisha kuunganisha kila mmoja wa jamaa (arham), sawa awe ni jamaa mahram au jamaa asiye mahram miongoni mwa upande wa baba (asaba) au upande wa mama (dhawil arham), kwani wote hao wanaitwa ndugu. Na zimepokewa hadithi kadhaa kuhusu silat al-rahim; Mtume ﷺ amesema:

لَا يَدْخُلُ الْجَنَّةَ قَاطِعُ رَحِمٍ

"Hataingia Peponi mkata dhalu (mwenye kukata undugu)." (Imetolewa na Muslim kupitia Jubayr bin Mut'im).

Na kutoka kwa Anas bin Malik kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ amesema:

مَنْ أَحَبَّ أَنْ يُبْسَطَ لَهُ فِي رِزْقِهِ وَيُنْسَأَ لَهُ فِي أَثَرِهِ فَلْيَصِلْ رَحِمَهُ

"Anayependa akunjuliwe riziki yake na arefushiwe umri wake, basi auunge undugu wake." (Muttafaq Alayh). 'Yuns'a lahu fi atharihi' ina maana ya kucheleweshewa ajal yake (kurefushiwa umri).

Na kutoka kwa Abu Hurairah, kutoka kwa Mtume ﷺ amesema:

إِنَّ اللَّهَ خَلَقَ الْخَلْقَ حَتَّى إِذَا فَرَغَ مِنْ خَلْقِهِ قَالَتْ الرَّحِمُ هَذَا مَقَامُ الْعَائِذِ بِكَ مِنْ الْقَطِيعَةِ قَالَ نَعَمْ أَمَا تَرْضَيْنَ أَنْ أَصِلَ مَنْ وَصَلَكِ وَأَقْطَعَ مَنْ قَطَعَكِ قَالَتْ بَلَى يَا رَبِّ قَالَ فَهُوَ لَكِ قَالَ رَسُولُ اللَّهِ ﷺ فَاقْرَءُوا إِنْ شِئْتُمْ فَهَلْ عَسَيْتُمْ إِنْ تَوَلَّيْتُمْ أَنْ تُفْسِدُوا فِي الأَرْضِ وَتُقَطِّعُوا أَرْحَامَكُمْ

"Hakika Mwenyezi Mungu aliumba viumbe, hata alipomaliza kuwaumba, undugu (rahim) ulisimama na kusema: Hapa ndipo mahali pa anayejikinga kwako kutokana na kukatwa. (Mwenyezi Mungu) akasema: Ndio, je, huridhii nimuunge anayekuunga na nimukate anayekukata? (Undugu) ukasema: Ndio, Ewe Mola wangu. Akasema: Basi hilo ni lako. Kisha Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ akasema: Someni mkipenda: 'Basi yanatarajiwa kwenu mkifawidhiwa (mkapewa mamlaka), mtafanya uharibifu katika nchi na kuwakata jamaa zenu?'" (Muttafaq Alayh, na tamshi ni la Bukhari).

Na amesema ﷺ:

لَيْسَ الْوَاصِلُ بِالْمُكَافِئِ وَلَكِنَّ الْوَاصِلَ الَّذِي إِذَا قَطَعَتْ رَحِمُهُ وَصَلَهَا

"Mwenye kuunga undugu si yule anayelipiza (anayetenda wema akitendewa), bali muungaji ni yule ambaye undugu wake ukikatwa yeye auunga." (Imetolewa na Bukhari kupitia Abdullah bin Amr).

Na haya yote yanahimiza kuunganisha undugu. Kuunganisha undugu kunaonyesha kiasi cha kile alichoweka Mwenyezi Mungu katika kuunga na kupendana kati ya jamii ya Kiislamu, katika kuunga jamaa wao kwa wao, na kusaidiana kati yao, na kiasi cha uzingativu wa Sharia katika kupanga mkusanyiko wa mwanamke na mwanamume, na kupanga mahusiano yanayotokana na mkusanyiko huo na yale yanayotokana nayo. Hivyo, Sharia ya Kiislamu kupitia hukumu ilizoweka kwa upande wa kijamii katika jamii ndiyo nidhamu bora zaidi ya kijamii kwa mwanadamu...)

2- Kutoka katika kitabu cha Nidhamu ya Kijamii – Maisha ya Faragha (Al-Hayat al-Khassah):

(...Hizi ni hukumu za kulinda maisha ya faragha ndani ya nyumba dhidi ya wanaotaka kuingia, hakuna tofauti katika hilo kati ya mgeni na mahram, jamaa wa karibu au mnasaba wa ndoa. Ama hukumu za maisha haya ya faragha ndani ya nyumba, mwanamke huishi humo pamoja na wanawake wenzake, au na mahram zake, kwa sababu wao ndio ambao inajuzu kwake kuwaonyesha sehemu za mapambo yake katika viungo vyake ambavyo haviwezi kuepukika kuonekana katika maisha ya faragha nyumbani. Na wasio wanawake na mahram zake, haijuzu kuishi nao kwa sababu haijuzu kwake kuwaonyesha sehemu za mapambo yake katika viungo vyake, ambavyo huonekana wakati anapofanya kazi zake za nyumbani mbali na uso na viganja vya mikono. Hivyo maisha ya faragha yamefungika kwa wanawake na mahram pekee, na hakuna tofauti kati ya wanawake Waislamu na wasio Waislamu kwani wote ni wanawake. Hivyo kitendo cha mwanamke kukatazwa kuonyesha viungo vyake anavyojipambia kwa watu baki (ajaneeb), na kutokatazwa kuvionyesha kwa mahram, ni ushahidi wa wazi wa kufungika kwa maisha ya faragha kwa mahram pekee. Mwenyezi Mungu Amesema:

وَقُل لِّلْمُؤْمِنَاتِ يَغْضُضْنَ مِنْ أَبْصَارِهِنَّ وَيَحْفَظْنَ فُرُوجَهُنَّ وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا مَا ظَهَرَ مِنْهَا ۖ وَلْيَضْرِبْنَ بِخُمُرِهِنَّ عَلَىٰ جُيُوبِهِنَّ ۖ وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا لِبُعُولَتِهِنَّ أَوْ آبَائِهِنَّ أَوْ آبَاءِ بُعُولَتِهِنَّ أَوْ أَبْنَائِهِنَّ أَوْ أَبْنَاءِ بُعُولَتِهِنَّ أَوْ إِخْوَانِهِنَّ أَوْ بَنِي إِخْوَانِهِنَّ أَوْ بَنِي أَخَوَاتِهِنَّ أَوْ نِسَائِهِنَّ أَوْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُهُنَّ أَوِ التَّابِعِينَ غَيْرِ أُولِي الْإِرْبَةِ مِنَ الرِّجَالِ أَوِ الطِّفْلِ الَّذِينَ لَمْ يَظْهَرُوا عَلَىٰ عَوْرَاتِ النِّسَاءِ

"Na waambie Waumini wanawake wainamishe macho yao, na wazilinde tupu zao, wala wasionyeshe mapambo yao isipokuwa yanayo dhihirika. Na waangushe shungi zao mpaka vifuani mwao, wala wasionyeshe mapambo yao isipokuwa kwa waume zao, au baba zao, au baba wa waume zao, au watoto wao, au watoto wa waume zao, au kaka zao, au wana wa kaka zao, au wana wa dada zao, au wanawake wenzao, au watumwa walio milikiwa na mikono yao ya kuume, au wafuasi wanaume wasio na hamu ya wanawake (kwa ajili ya uzee au upungufu wa akili), au watoto ambao hawajajua siri za wanawake." (QS. An-Nur: 31)

Na wamejumuishwa kwa mahram watumwa wanaowamiliki, kadhalika wale ambao hawana hamu ya wanawake miongoni mwa wazee waliochoka sana au wajinga, au matowashi, au waliokatwa viungo vyao vya siri, au mfano wa hao miongoni mwa wasio na 'irbah', yaani haja ya wanawake. Hawa inajuzu kwao kuwemo katika maisha ya faragha, na wengineo miongoni mwa wanaume wasio mahram – hata kama ni jamaa wasio mahram – basi haijuzu kwao kuwemo katika maisha ya faragha kabisa, kwa sababu haijuzu kwa mwanamke kuwaonyesha sehemu za mapambo yake katika viungo vyake vinavyodhihirika kwa kawaida akiwa nyumbani kwake.

Hivyo, kukutana kwa wanaume wasio mahram na wanawake katika maisha ya faragha ni haramu kabisa, isipokuwa katika hali ambazo Sharia imevua kama chakula na kuunganisha undugu, kwa sharti kuwa mwanamke awe na mahram yake, na awe amesitiri uchi wake wote.)

3- Kadhalika tumelifafanua hili katika majibu kadhaa yakiwemo:

Kutoka jibu la swali la tarehe 28/02/2010:

(Hakika kuwepo kwa wanaume na wanawake katika maisha ya Kiislamu ambayo Mtume ﷺ aliyaidhinisha, na ushahidi wa kisheria unaopanga miamala ya kisheria kati ya wanaume na wanawake... yote hayo yamebainishwa kwa uwazi, na yameshatolewa majibu zaidi ya moja katika jambo hili, na tulitegemea kusiwe na utata katika jambo hili.

Pamoja na hayo, katika barua hii, nitazidi kufafanua zaidi kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, nikitumai kuondosha utata wowote katika suala hili:

  • Hakika maisha ya kawaida (al-hayat al-ammah) yanamaanisha kuwepo kwa wanaume na wanawake katika sehemu za umma ambazo kuingia kwake hakuhitaji idhini, na hizi zina hukumu za kisheria zinazowaratibu wanaume na wanawake wakati huo.

Na maisha ya faragha (al-hayat al-khassah) ni katika sehemu ambazo kuingia kwake kunahitaji idhini kama nyumbani, na hizi kadhalika zina hukumu za kisheria zinazowaratibu wanaume na wanawake wakati huo.

  • Ama maisha ya faragha "nyumbani", jambo lake liko wazi na halihitaji ufafanuzi zaidi; kwani kuishi kwa wanawake humo ni pamoja na mahram zao na sio na watu baki, isipokuwa ikiwa imekuja nukuu katika hali fulani kama kuunganisha undugu (silat al-rahim); inajuzu kwa ndugu kumtembelea ndugu yake mwanamke hata kama si mahram, kama vile mtoto wa ami kwenda kumsalimia mtoto wa kike wa ami yake wakati wa sikukuu, na bila shaka pasina faragha (khalwa), na bila kufunua uchi, kama vile kwenda pamoja na baba yake au ami yake na kuunga undugu wake hata kama ni miongoni mwa wasio mahram.

  • Ama maisha ya kawaida, ikiwa kuna haja inayokubaliwa na Sharia kwa mkusanyiko wa wanaume na wanawake, basi inajuzu mkusanyiko huu kwa sura yake ya kisheria, na tunasema kwa sura yake ya kisheria kwa sababu kuna hukumu za kisheria zinazouratibu mkusanyiko huu kama ifuatavyo:

1- Wajibu wa kutenganisha safu za wanaume na wanawake ikiwa haja inayokubaliwa na Sharia kwa ajili ya kuwepo kwa wanaume na wanawake ni kwa lengo moja kwa waliokusanyika, kama kuwepo kwa wanaume na wanawake kwa ajili ya swala, au kuhudhuria darsa la elimu, au mhadhara katika Da'wah, au kazi yoyote ya kawaida ya Da'wah... Katika hali hizi inajuzu kuwepo wanaume na wanawake pamoja na kutenganisha safu, na hizi nyakati nyingine huitwa maisha ya kawaida yenye hukumu maalum, yaani kuna namna maalum ya kuwepo kwa wanaume na wanawake.

2- Kutokuwepo wajibu wa kutenganisha safu katika maisha ya kawaida ikiwa haja inayokubaliwa na Sharia kwa ajili ya kuwepo kwa wanaume na wanawake ni kwa malengo tofauti kwa waliokusanyika, kama kuwepo kwa wanaume na wanawake sokoni, au barabarani, au katika bustani ya umma, au wakati wa kupanda mabasi ya umma... Na hizi ni aina mbili:

a- Malengo tofauti hayatimizwi ndani yake isipokuwa kwa mchanganyiko (ikhtilat), yaani kuchanganyika kwa kukaa jirani na kuzungumza, kama vile kuuza na kununua sokoni, na aina hii inaruhusu mchanganyiko ndani yake.

b- Malengo tofauti yanatimizwa ndani yake bila mchanganyiko, yaani bila kuchanganyika kwa kukaa jirani na kuzungumza, kama vile kupanda mabasi ya umma, bustani za umma na kutembea barabarani... Aina hii inaruhusu kuwepo kwa wanaume na wanawake bila mchanganyiko, yaani bila kuchanganyika kwa kukaa jirani na kuzungumza, bali inawezekana kuwepo jirani kila mmoja kwa lengo lake, bila kuzungumza pamoja, kama kutembea barabarani, bustani za umma, na kupanda mabasi ya umma...

  • Na kama unavyoona, hukumu za kuwepo kwa wanaume na wanawake ziko wazi na zimeainishwa katika maisha ya faragha na maisha ya kawaida:

Maisha ya faragha "nyumbani" ni yale ambayo kuingia kwake kunahitaji idhini, na maisha ya kawaida ni yale ambayo kuingia kwake hakuhitaji idhini. Na miongoni mwa maisha haya ya kawaida kuna yanayohitaji kutenganishwa safu na kuna yasiyohitaji kutenganishwa safu. Kadhalika miongoni mwa maisha ya kawaida kuna yanayojuzu mchanganyiko yaani kuchanganyika kwa kukaa jirani na kuzungumza, na kuna yasiyojuzu kuchanganyika, bali inajuzu tu kukaa jirani bila kuzungumza...) Mwisho.

Natumai katika hili pana kutosheleza.

- Kutoka jibu la swali la tarehe 06/06/2016 ambapo ilikuja ndani yake:

(a- Mchanganyiko (ikhtilat), yaani kukutana kwa wanaume na wanawake wasio mahram, ni haramu ikiwa ni kwa ajili ya jambo ambalo si haja inayokubaliwa na Sharia kwa ajili ya kukutana huko... Ama ikiwa ni kwa haja inayokubaliwa na Sharia kiasi kwamba haitekelezeki isipokuwa kwa kukutana, basi inajuzu.

b- Zimekuja dalili zinazoidhinisha kukutana kwa ajili ya mahitaji yaliyobainishwa na Sharia, sawa iwe katika maisha ya faragha au ya kawaida; kwa mfano katika maisha ya faragha pamoja na jamaa, zimekuja dalili za kisheria zinazohalalisha kuunganisha undugu na chakula, na kumtembelea mgonjwa... Na katika maisha ya kawaida, kutibu waliojeruhiwa vitani... kwenda sokoni, kuswali misikitini, kuhudhuria vikao vya elimu, Hijja... Na yote hayo ni kwa mujibu wa hukumu za kisheria katika suala la kutenganisha safu kama misikitini na mihadhara ya umma, au bila kutenganisha kama sokoni na Hijja...

c- Na kuunganisha undugu si kwa jamaa mahram pekee, bali hata kwa jamaa wasio mahram kama mtoto wa kike wa ami... "Angalia silat al-rahim katika (kitabu cha) Kijamii". Hivyo hili linajuzu kwa jamaa kuungana wakati wa sikukuu au shughuli mbalimbali, na kukaa pamoja, lakini iwe ni kuunganisha undugu, yaani kuulizana hali, kumtembelea mgonjwa wao, kutekeleza mahitaji na mfano wa hayo; lakini si kukaa pamoja "wakicheza kadi (shadda) kwa mfano" au kutoka pamoja kwa ajili ya matembezi, na kukaa pamoja bustanini wakipiga soga... hili halijuzu...) Mwisho.

Natumai katika majibu haya kwa maswali yako pana kutosheleza, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi zaidi na Hakimu zaidi.

Ndugu yenu Ata bin Khalil Abu Al-Rashtah

16 Ramadhan 1443 H Sawa na 17/04/2022 M

Kiungo cha jibu kutoka ukurasa wa Amir (Mungu amuhifadhi) kwenye Facebook

Kiungo cha jibu kutoka tovuti ya Amir (Mungu amuhifadhi) Web

Share Article

Share this article with your network