(Mfululizo wa Majibu ya Mwanachuoni Mtukufu Ata bin Khalil Abu al-Rashtah, Amir wa Hizb ut-Tahrir, kwa Maswali ya Wageni wa Ukurasa wake wa Facebook "Fiqhi")
Majibu ya Maswali: Maswali Kuhusu Usul al-Fiqh Kwa Muhammad Ayyad
Maswali:
Assalamu Alaikum Warahmatullahi Wabarakatuh
Sheikh wetu mtukufu, Mwenyezi Mungu akusaidie na ajalie heri kupitia mikono yako.
Mada: Maswali Kuhusu Usul al-Fiqh
Mwanzoni, natumai sitakuwa nimekuletea uzito kwa maswali haya, hasa tukiwa tunajua ukubwa wa mizigo unayobeba na majukumu uliyojitwika kuyatekeleza. Mwenyezi Mungu akusaidie, aongoze hatua zako, na afurahishe macho yetu na yako kwa kuona utekelezaji wa sheria ya Mwenyezi Mungu katika Daulah ya Khilafah ya pili.
Kuhusu maswali, ni kama ifuatavyo:
Nimesoma katika tafiti mbalimbali kuwa kuna njia zaidi ya moja kwa wana-usul (al-usuliyyun), kama vile njia ya al-mutakallimin, njia ya al-fuqaha, al-istiqra al-kulli, na takhrij al-furu’ ‘ala al-usul... Je, ukweli wa njia hizi ni upi? Na je, sisi tuko karibu na njia ipi miongoni mwa hizo, au tuna rangi yetu maalumu katika usul wetu?
Imeelezwa katika kitabu cha Ash-Shakhsiyyah al-Islamiyyah Juzuu ya Tatu, ukurasa wa 11: "Ama Fiqhi, kilugha ni ufahamu, na miongoni mwa hayo ni kauli Yake Mwenyezi Mungu: ﴿مَا نَفْقَهُ كَثِيرًا مِمَّا تَقُولُ﴾. Na katika istilahi ya wanasharia, ni elimu ya hukumu za kisheria za vitendo zilizovuliwa (stimbati) kutoka kwenye dalili za kina. Na makusudio ya elimu ya hukumu, kwa upande wa mwanachuoni, si maarifa tu, bali ni kupatikana kwa malakah (ustadi uliokita) wa hukumu za kisheria, yaani maarifa haya na kuzama ndani yake kufikie kiwango cha kumpatika mwanachuoni huyo malakah ya hukumu hizo. Na kupatikana kwa malakah pekee kunatosha kwa aliyeyapata kuchukuliwa kuwa ni mwanachuoni (faqihi), si lazima kuzijua zote kikamilifu. Isipokuwa ni lazima kuwa na elimu ya jumla ya hukumu za kisheria za matawi kwa njia ya mtazamo na kutoa dalili." Je, istilahi ya malakah ina asili ya kilugha au kisheria, au ni istilahi waliyokubaliana wana-usul? Na je, ni ya kimaumbile anayozaliwa nayo mwanadamu au ni ya kuchuma, au ina misingi ya kimaumbile lakini hupatikana kwa kuzama na mazoezi ya muda mrefu?
Imeelezwa katika kitabu hicho hicho ukurasa wa 42 kanuni ya "Lile ambalo wajibu hautimii ila kwalo, basi nalo ni wajibu" kama ukamilisho wa mada ya al-wajib. Kisha imeelezwa katika kitabu hicho hicho ukurasa wa 444 mada ya Kanuni za Kijumla (al-Qawa'id al-Kulliyyah) na kwamba hazizingatiwi kuwa ni dalili, bali ni hukumu za kisheria zilizovuliwa kutoka kwenye dalili za kina. Hapo nimepata mushkil: je, kanuni hii na kanuni ya "Njia ya kuelekea kwenye haramu ni haramu" ni miongoni mwa Usul au miongoni mwa Fiqhi?
Barakallahu fikum na Mwenyezi Mungu akulipe kheri kwa ajili yetu na kwa niaba ya Waislamu.
Majibu:
Wa Alaikum Salaam Warahmatullahi Wabarakatuh
Barua yako inajumuisha maswali matatu, na kila swali linajitegemea. Tunayajibu kwa ufupi In Sha Allah:
Jibu la Swali la Kwanza:
Inajulikana kuwa Imam Shafi'i ndiye mwanzilishi wa elimu ya Usul al-Fiqh na yeye ndiye wa kwanza kuifanya kuwa taaluma inayojitegemea katika uandishi. Kisha uandishi uliendelea baada ya hapo... Wana-usul walifuata mitindo mbalimbali katika uandishi wao, miongoni mwayo ni:
1- Kuna wanachuoni waliozingatia katika kuweka maudhui ya Usul na kanuni zake upande wa kifikra wa ki-usul, yaani hawakuangalia matawi ya kifiqhi (al-furu' al-fiqhiyyah) ya madhehebu wanayofuata. Badala yake, walichukua kanuni na vigezo vilivyopewa uzito wa usahihi kwao kulingana na majadiliano ya dalili zinazofahamisha hilo. Kwa hiyo, vitabu vyao vimejaa utoaji dalili na majadiliano kuhusu maudhui ya Usul, lakini vina upungufu wa matawi ya kifiqhi... Mtindo huu wa uandishi unaitwa Tariqah al-Shafi'iyyah au Tariqah al-Mutakallimin (Njia ya Wana-kalam).
Katika njia hii, unakithiri mtindo wa al-fanqalah, yaani: "Ikiwa utasema... tutasema," kwa njia ya wanachuoni wa kalam. Matawi ya kifiqhi ni machache ndani yake, na kiuhalisia iko karibu zaidi na ukweli wa kuweka misingi na kanuni ambazo zinazingatiwa kuwa msingi ili matawi yaje kulingana na misingi hiyo. Hivyo basi, Usul hutawala matawi, na ndio mhimili wa Fiqhi na istimbati. Mtindo huu uliwaweka watu mbali na ushabiki wa tawi la kifiqhi au hukumu ya kimadhehebu.
Miongoni mwa vitabu vilivyoandikwa kwa njia hii ni:
- Ar-Risalah ya Imam Shafi'i kilikuwa kitabu cha kwanza kwa njia hii, kisha vikatokea vitabu vingi kwa mtindo huo, muhimu zaidi ni:
- Al-Burhan, cha Imam al-Haramayn, Abi al-Ma'ali, Abdul Malik bin Abdullah al-Juwayni al-Nisaburi al-Shafi'i (aliefariki mwaka 478 AH).
- Al-Mustasfa, cha al-Ghazali, Abi Hamid Hujjatul Islam, Muhammad bin Muhammad al-Ghazali al-Shafi'i (aliefariki mwaka 505 AH).
- Al-Ihkam fi Usul al-Ahkam, cha al-Amidi, Sayf al-Din Abi al-Hasan, Ali bin Abi Ali Muhammad al-Shafi'i (aliefariki mwaka 631 AH).
2- Njia ya Mafaqihi au Hanafi (Tariqah al-Fuqaha au al-Hanafiyyah): Kuna wanachuoni waliozingatia katika kuweka maudhui ya Usul na kanuni zake yale yanayofahamishwa na matawi ya madhehebu yao wanayofuata. Hawakutafiti kanuni na vigezo kwa utafiti wa kinadharia pekee ili kutoa hukumu baada ya kujadili dalili, bali walifikia kanuni hizo kupitia kusoma matawi ya madhehebu yao. Walifanya kanuni ziwe kulingana na yale yanayosemwa na matawi ya madhehebu na yanayoendana nayo... Mtindo huu wa uandishi unaitwa Tariqah al-Hanafiyyah au Tariqah al-Fuqaha.
Hii ni njia iliyoathiriwa na matawi na inaelekea katika kuyatumikia na kuthibitisha usahihi wa ijtihadi ndani yake. Njia hii inasifika kwa kuchukua kanuni za Usul kutoka kwenye matawi na hukumu zilizowekwa na maimamu wa madhehebu ya Hanafi, wakidhani kwamba maimamu hao walizingatia kanuni hizi wakati wa ijtihadi na istimbati. Sababu ya kuelekea kwenye njia hii ni kwamba wanachuoni wa Hanafi hawakupata vitabu vya Usul vilivyowekwa na maimamu wao kama wanachuoni wa Shafi'i walivyopata katika Ar-Risalah, hivyo walitafuta kanuni za ki-usul katika matawi ya kifiqhi kwa kuzingatia kuwa ni lazima ziwe zimejengeka juu ya msingi sahihi.
Miongoni mwa vitabu vilivyoandikwa kwa njia hii ni:
- Kitabu cha al-Usul, cha Imam al-Karkhi, Abi al-Hasan, Ubaydullah bin al-Husayn (aliefariki mwaka 340 AH).
- Kitabu cha al-Usul cha al-Jassas, Abi Bakr, Ahmad bin Ali al-Razi, maarufu kama al-Jassas (aliefariki mwaka 370 AH).
- Kitabu cha al-Usul, cha al-Sarakhsi, Shams al-A'immah Muhammad bin Ahmad (aliefariki takriban mwaka 490 AH), ambaye ni mwandishi wa al-Mabsut katika Fiqhi.
3- Njia ya Kuchanganya kati ya al-Mutakallimin na al-Fuqaha: Katika karne ya saba Hijiria, ilianza kutokea njia ya tatu inayochanganya kati ya mbinu mbili zilizotangulia: mbinu ya al-mutakallimin na mbinu ya al-fuqaha. Kanuni ya Usul inatajwa na kutolewa dalili, na kufanywa ulinganifu kati ya yale waliyosema al-mutakallimin na yale waliyosema al-fuqaha, pamoja na majadiliano na kutoa uzito (tarjih), kisha yanatajwa baadhi ya matawi yaliyovuliwa kulingana na kanuni hiyo.
Miongoni mwa vitabu maarufu vilivyoandikwa kwa mbinu hii:
- Jam'u al-Jawami' cha Taj al-Din: Abdul Wahhab bin Ali al-Subki (aliefariki mwaka 771 AH).
- Al-Tahrir kilichoandikwa na: Kamal al-Din: Muhammad bin Abdul Wahid, maarufu kama Ibn al-Humam, faqihi wa Hanafi (aliefariki mwaka 861 AH).
4- Mwelekeo wa Takhrij al-Furu' 'ala al-Usul: Pamoja na mienendo iliyotangulia, ulitokea mwelekeo wa nne unaoitwa "Kutoa Matawi kwa Mujibu wa Usul" (Takhrij al-Furu' 'ala al-Usul). Kanuni ya Usul inatajwa pamoja na maoni ya wanachuoni ndani yake, bila kuingia ndani katika dalili za kila madhehebu, kisha yanatolewa matawi ya kifiqhi kulingana nayo, ama juu ya madhehebu fulani, au kwa kulinganisha kati ya madhehebu mawili tofauti - kwa mfano, Hanafi na Shafi'i - au Shafi'i, Maliki, na Hanbali na kadhalika.
Miongoni mwa vitabu vilivyoandikwa katika mwelekeo huu:
- Takhrij al-Furu' 'ala al-Usul cha Imam Shihab al-Din Mahmoud bin Ahmad al-Zanjani (aliefariki mwaka 656 AH). Kinataja kanuni ya Usul, kisha kinaifuatanisha na mifano ya kifiqhi ya madhehebu ya Hanafi na Shafi'i.
- Al-Tamhid fi Takhrij al-Furu' 'ala al-Usul cha Imam Jamal al-Din Abdul Rahim bin al-Hasan al-Qurashi al-Isnawi al-Shafi'i (aliefariki mwaka 772 AH). Kinazingatiwa kuwa ni miongoni mwa vitabu muhimu vilivyoandikwa kwa mbinu hii, ambapo kimejumuisha kanuni za Usul, lakini kimefupisha takhrij kwa upande wa Shafi'i pekee.
5- Mwelekeo wa kujenga kanuni za Usul juu ya Malengo ya Sharia (Maqasid al-Shari'ah) yenye ushahidi wa kisheria: Njia hii ilitumiwa na Imam al-Shatibi: Abu Ishaq Ibrahim bin Musa al-Lakhmi al-Gharnati al-Maliki (aliefariki mwaka 790 AH) katika kitabu chake maarufu kiitwacho al-Muwafaqat. Al-Shatibi alifuata katika kitabu chake hiki njia mpya ambayo haikuwahi kufanywa kabla, ambapo anataja kanuni za Usul chini ya milango maalumu inayojumuisha malengo ya sheria ya Kiislamu na madhumuni yake mbalimbali, yanayohusisha kuhifadhi mambo ya lazima (dharuriyyat), mambo ya mahitaji (hajiyyat), na mambo ya kuboresha (tahsiniyyat).
Hivyo basi, Imam al-Shatibi alifuata mtindo tofauti katika kitabu chake al-Muwafaqat ambapo alitegemea kwa nguvu al-istiqra al-kulli (ukusanyaji wa dalili zote). Imeelezwa katika utangulizi wa kitabu cha al-Muwafaqat kuhusu kitabu chake: "...sikuacha kufunga mambo yake adimu, na kukusanya mambo yake yaliyotawanyika kwa kina na kwa jumla, na nikatoa ushahidi katika vyanzo vya hukumu na maeneo yake kwa kubainisha wala si kwa ufupisho, nikitegemea ukusanyaji wa kijumla (al-istiqraat al-kulliyyah), bila kuishia kwenye mambo ya mmoja mmoja." Makusudio ya al-istiqra al-kulli hapa ni kufuatilia hukumu za kisheria katika kadhia moja ili kutoa hukumu ya kijumla kutokana na ufuatiliaji huo juu ya kadhia aliyoichunguza...
Huu ni ufafanuzi rahisi na wa mkato kuhusu maana ya istilahi zilizokuja katika swali lako kuhusu njia za uandishi wa vitabu vya Usul al-Fiqh...
- Ama kuhusu kitabu cha Hizb katika Usul al-Fiqh: "Ash-Shakhsiyyah al-Islamiyyah Juzuu ya Tatu," kimezingatia tafiti za ki-usul za kisheria kama ifuatavyo:
a- Kimekuwa na hamu ya kutilia maanani tafiti zinazohusiana na nyanja za kisheria (legislative) mbali na nyanja za kinadharia tupu. Hakikugusia masuala ambayo si ya kimsingi katika tafiti za Usul al-Fiqh na katika kutoa dalili kama vile utafiti wa "Je, kumshukuru Mwenye Neema ni wajibu kwa sheria au kwa akili" na mfano wake... Na ikiwa kimegusia masuala ambayo si sehemu ya Usul kwa upande wa kutoa dalili kama vile utafiti wake wa mada ya "Uzuri na Ubaya" (al-Husn wa al-Qubuh) katika mlango wa "Al-Hakim," kilifanya hivyo kwa sababu ya faida ya kisheria iliyopatikana katika kugusia masuala hayo kwa sababu yanaangazia uhalisia wa vitu na hivyo kurahisisha kuvitolea hukumu. Hiyo ni kwa sababu mada ya hukumu hii ni uzuri na ubaya; na lengo la kutoa hukumu ni kuainisha msimamo wa mwanadamu kuelekea tendo, na kuainisha msimamo wake huu kunategemea mtazamo wake kwa kitu hicho, je, ni kizuri au ni kibaya? Kwa sababu hiyo, kiligusia suala hili...
b- Hakikuzama sana katika utafiti wa kimantiki wa kadhia kilizozigusia na hakikutolea matawi yasiyo na faida, bali kilijikita kwenye utafiti wa kisheria na utoaji dalili wa kisheria wenye nidhamu...
c- Kilitegemea utoaji dalili wa kisheria, kilugha, na kiakili ulio wazi na unaofahamika mbali na mijadala, na kwa mtindo rahisi kufahamika, unaopelekea kuelewa kadhia inayofanyiwa utafiti uelewa wa kisheria uliokamilika...
d- Kilitaja kwa kiasi kinachotosha matawi ya Fiqhi katika kutoa mifano ya kadhia kilizozijadili, na si kama baadhi ya vitabu vingine ambavyo mara chache hutaja matawi ya kifiqhi ndani yake. Hiyo ni kwa ajili ya kufafanua masuala yanayofanyiwa utafiti na kubainisha uhalisia wake wa kisheria... Pamoja na hayo, hakikupanuka katika njia ya kutoa matawi kutokana na usul kama ilivyo katika njia ya mafaqihi, kwa sababu lengo la kwanza la tafiti za Usul ni kuthibitisha kanuni na vigezo vya ki-usul si kutaja matawi ya kifiqhi... Hivyo kitabu cha Usul al-Fiqh cha Hizb kimekuwa katikati (cha uadilifu) katika jambo hili...
Kwa yote yaliyotangulia, kitabu cha Ash-Shakhsiyyah al-Islamiyyah Juzuu ya Tatu kinazingatiwa kuwa ni miongoni mwa vitabu bora kabisa vya Usul al-Fiqh, na yeyote anayefanikiwa katika kukisoma na kukielewa, atakuwa ameingia katika ijtihadi kupitia milango yake mipana zaidi kwa idhini ya Mwenyezi Mungu.
Jibu la Swali la Pili:
Kuhusu nini maana ya neno "malakah" katika kauli yake ndani ya kitabu cha Ash-Shakhsiyyah al-Islamiyyah Juzuu ya Tatu:
"...Ama Fiqhi, kilugha ni ufahamu, na miongoni mwa hayo ni kauli Yake Mwenyezi Mungu:
﴿مَا نَفْقَهُ كَثِيرًا مِمَّا تَقُولُ﴾
"Hatuelewi mengi katika unayoyasema." (QS Hud [11]: 91)
Na katika istilahi ya wanasharia, ni elimu ya hukumu za kisheria za vitendo zilizovuliwa kutoka kwenye dalili za kina. Na makusudio ya elimu ya hukumu, kwa upande wa mwanachuoni, si maarifa tu, bali ni kupatikana kwa malakah ya hukumu za kisheria, yaani maarifa haya na kuzama ndani yake kufikie kiwango cha kumpatika mwanachuoni huyo malakah ya hukumu hizo. Na kupatikana kwa malakah pekee kunatosha kwa aliyeyapata kuchukuliwa kuwa ni mwanachuoni, si lazima kuzijua zote kikamilifu. Isipokuwa ni lazima kuwa na elimu ya jumla ya hukumu za kisheria za matawi kwa njia ya mtazamo na kutoa dalili, kwani elimu ya hukumu moja au mbili haitwi fiqhi. Wala elimu ya kuwa aina za dalili ni hoja haitwi fiqhi.) Mwisho wa nukuu.
Imekuja katika kamusi ya al-Qamus al-Muhit: (malakahu... malakah: Alikimiliki akiwa na uwezo wa kukitumia apendavyo).
Na imekuja katika al-Mu'jam al-Wasit: ("al-Malakah" ni sifa iliyokita katika nafsi au utayari maalumu wa kiakili wa kushughulikia kazi fulani kwa ufundi na ustadi kama vile malakah ya kihesabu na malakah ya kilugha).
Na imetajwa katika kitabu cha al-Ta'rifat: (al-Malakah: Ni sifa iliyokita katika nafsi, na uhakika wake ni kwamba nafsi hupata hali fulani kutokana na kitendo miongoni mwa vitendo, na hali hiyo huitwa: sifa ya kinafsi, na huitwa: 'hali' (halah) maadamu inapotea haraka, na inapotajika na nafsi kuifanya mara kwa mara mpaka sifa hiyo ikakita ndani yake na kuwa nzito kupotea, basi inakuwa ni malakah...).
Kwa hivyo, neno "malakah" lina asili ya kilugha, nalo limechukuliwa kutokana na tamko malaka na linamaanisha "alikimiliki akiwa na uwezo wa kukitumia apendavyo". Pia lina maana ya kiistilahi kama ilivyobainishwa katika ufafanuzi wa neno "malakah" hapo juu... Na istilahi hii si maalumu kwa wana-usul pekee bali ni istilahi inayotumiwa katika sayansi nyingine zote... Na maana hii ya kiistilahi ndiyo inayokusudiwa katika yale yaliyokuja ndani ya kitabu cha Ash-Shakhsiyyah al-Islamiyyah... Na ubainifu wa hilo ni kama ifuatavyo:
Maandishi yaliyokuja katika kitabu cha Ash-Shakhsiyyah al-Islamiyyah yameifasiri Fiqhi kuwa ni "elimu ya hukumu za kisheria za vitendo zilizovuliwa kutoka kwenye dalili za kina," kisha yakabainisha makusudio ya elimu hii kwa mwanachuoni kuwa haitoshi kwa mtu kuwa mwanachuoni wa baadhi ya hukumu za kisheria ili awe faqihi, kwa sababu katika hali hiyo atakuwa ni muqalidi (mfuasi) na si mwanachuoni kwani muqalidi hakosi maarifa ya baadhi ya hukumu za kisheria... Vilevile si lazima awe mwanachuoni wa hukumu zote za kisheria ili ahesabiwe kuwa ni mwanachuoni, kwani jambo hili halimo ndani ya uwezo wa yeyote miongoni mwa wanadamu... Bali anapaswa kuwa na uelewa wa jumla ya hukumu za kisheria, akizijua hizo pamoja na dalili zake na namna ya kutoa dalili, na wakati huo huo anapata uwezo kutokana na kusoma kwake Fiqhi na kuzama ndani yake wa kufikia maarifa ya hukumu ambazo bado hajazijua. Na hii ndiyo "malakah", yaani ni lazima afikie daraja ya elimu inayomfanya awe mmiliki wa Fiqhi, masuala yake na funguo zake, na hilo liwe sifa iliyokita katika nafsi yake...
Wala makusudio ya malakah katika Fiqhi si upande wa kimaumbile na utayari wa kimaumbile unaotofautiana kati ya mtu na mtu, bali makusudio ni malakah ya kuchuma inayopatikana kwa kujifunza, kusoma, kuzama, na mazoezi... Ingawa utayari wa kimaumbile unaweza kuchangia katika kuzalisha malakah ya kifiqhi na kuiendeleza haraka, lakini utayari huo wa kimaumbile siyo malakah inayokusudiwa katika maandishi yaliyotajwa hapo juu...
Jibu la Swali la Tatu:
1- Kanuni ya kisheria ya kijumla (al-Qa'idah al-Shar'iyyah al-Kulliyyah) ni ile ambayo ndani yake hukumu hunasibishwa na jambo la kijumla linalotumika kwenye sehemu ndogo ndogo (juz'iyyat) nyingi. Kwa mfano, hukumu ya wajibu katika kanuni "Lile ambalo wajibu hautimii ila kwalo, basi nalo ni wajibu" inafungamana na jambo la kijumla nalo ni "lile ambalo wajibu hautimii ila kwalo". Na hukumu ya uharamu, kwa mfano, katika kanuni "Njia ya kuelekea kwenye haramu ni haramu" inafungamana na jambo la kijumla nalo ni "njia ya kuelekea kwenye haramu". Na jambo hili la kijumla linatumika kwenye matawi mengi katika milango mbalimbali ya Fiqhi.
2- Kanuni za kijumla ni hukumu za kisheria kwa upande wa kuvuliwa kwake (istimbat). Zinavuliwa kutoka kwenye maandishi ya kisheria (Nass) kama inavyovuliwa hukumu yoyote ya kisheria, iwe ni kutoka kwenye dalili moja au dalili nyingi. Isipokuwa dalili ndani yake inajumuisha maana yenye hadhi ya sababu ('illah). Na hili ndilo linaloifanya itumike kwenye sehemu zake zote. Kwa mfano, kanuni: "Njia ya kuelekea kwenye haramu ni haramu" na kanuni: "Lile ambalo wajibu hautimii ila kwalo, basi nalo ni wajibu," kila moja ni kanuni ya kijumla. Inapotazamwa katika dalili zake, inabainika kuwa hukumu hiyo dalili yake inaifahamisha, na inafahamisha kitu kingine kilichopangwa juu yake au kinachotokana nayo, hivyo inaonekana wakati huo kuwa ina hadhi ya sababu ('illah).
Kwa mfano, kauli Yake Mwenyezi Mungu:
﴿وَلَا تَسُبُّوا الَّذِينَ يَدْعُونَ مِن دُونِ اللَّهِ فَيَسُبُّوا اللَّهَ عَدْوًا بِغَيْرِ عِلْمٍ﴾
"Wala msiwatukane wale wanaowaomba badala ya Mwenyezi Mungu, wasije wakamtukana Mwenyezi Mungu kwa uadui bila ya kujua." (QS al-An'am [6]: 108)
Herufi ف katika ﴿فَيَسُبُّوا﴾ ilifanya maana kuwa kutukana kwenu masanamu yao kunapelekea wao kumtukana Mwenyezi Mungu, na hili ni haramu. Hivyo basi, kutukana kwenu masanamu yao katika hali hii ni haramu, kana kwamba hiyo ilikuwa ni sababu ('illah). Katazo la kutukana wale waliokufuru ndiyo dalili ya hukumu, na imefahamisha - kando na kufahamisha kwake hukumu - kitu kingine kilichopangwa juu yake pale Aliposema: ﴿فَيَسُبُّوا اللَّهَ﴾. Hivyo, kutokana na aya hii imevuliwa kanuni: "Njia ya kuelekea kwenye haramu ni haramu."
Na kwa mfano, kauli Yake Mwenyezi Mungu:
﴿فَاغْسِلُوا وُجُوهَكُمْ وَأَيْدِيَكُمْ إِلَى الْمَرَافِقِ﴾
"basi osheni nyuso zenu na mikono yenu mpaka vifundoni." (QS al-Ma'idah [6]: 6)
Na kauli Yake:
﴿ثُمَّ أَتِمُّوا الصِّيَامَ إِلَى اللَّيْلِ﴾
"kisha timizeni saumu mpaka usiku." (QS al-Baqarah [2]: 187)
Neno إلى katika kauli Yake: ﴿إِلَى الْمَرَافِقِ﴾ na katika kauli Yake: ﴿إِلَى اللَّيْلِ﴾ lilifahamisha kuwa maadamu sehemu ya kifundo haikuoshwa, basi kuoshwa kwa mkono mpaka kifundoni hakujatimia, hivyo ni lazima kufikiwa kwa ukomo huo. Na kwamba maadamu sehemu ya usiku haijaingia, hata kama ni dakika moja, utimilifu wa saumu haufikiwi. Hivyo, kuosha sehemu yoyote ile ya vifundo, na kufunga sehemu yoyote ile ya usiku ikawa ni wajibu kwa kufahamishwa na aya hizi mbili; kwa sababu kile Alichokiwajibisha - nacho ni kuosha mikono na kufunga mchana - hakitimii ila kwa kufanya hivyo. Hivyo basi, ukomo huu ulifanya kile kinachokamilisha uoshaji wa mikono na funga ya mchana - nacho ni wajibu - kuwa ni wajibu pia. Kana kwamba hiyo ilikuwa ni sababu ('illah). Aya imefahamisha hukumu, na imefahamisha kitu kingine kinachoikamilisha pale Aliposema: ﴿إِلَى اللَّيْلِ﴾. Hivyo, kutokana na aya hizi mbili imevuliwa kanuni: "Lile ambalo wajibu hautimii ila kwalo, basi nalo ni wajibu."
3- Kama unavyoona, uvuluaji wa kanuni ya kijumla unaambatana na kile kinachofanana na sababu au kilicho katika hadhi ya sababu, na kwa hiyo ni kana kwamba yenyewe ni dalili. Kwa sababu hiyo, kanuni hizi mbili na mfano wake, kama tulivyotaja hapo awali, ni hukumu za kisheria. Lakini hukumu hizi si hukumu za kina (fadhili), bali ni kanuni zinazotumika kutoa dalili juu ya hukumu za kisheria. Hiyo ni kwa sababu njia ya kuzivua ina kile kinachofanana na sababu au kilicho katika hadhi ya sababu. Kwa hivyo, kutoa dalili kwa kutumia kanuni juu ya hukumu huchukua sura ya kutoa dalili kwa kutumia dalili (source evidence) kutokana na kanuni hiyo kuwa na kile kinachofanana na sababu au kilicho katika hadhi ya sababu. Utoaji dalili huu unatofautiana na kutoa dalili juu ya hukumu kupitia hukumu nyingine ya kisheria; kwani hapo hauchukui sura ya kutoa dalili kwa kutumia dalili bali sura ya utekelezaji, ambapo kinachozingatiwa ni kuendana kwa hukumu na uhalisia...
4- Kutokana na uhalisia huu katika njia ya istimbati (uvuluaji), basi kanuni za kijumla ziko karibu zaidi kuwa miongoni mwa tafiti za elimu ya Usul al-Fiqh kuliko kuwa miongoni mwa tafiti za Fiqhi ya kina. Na kwa sababu hiyo, mazungumzo kuzihusu yamekuja katika masuala ya Usul al-Fiqh na yakatafitiwa katika kitabu cha Ash-Shakhsiyyah al-Islamiyyah Juzuu ya Tatu katika mada maalumu chini ya kichwa cha habari "Kanuni za Kijumla" (al-Qawa'id al-Kulliyyah), kama ambavyo baadhi ya kanuni hizo zimeguswa katika kitabu hicho kwa ufafanuzi na ubainifu...
Ndugu yenu, Ata bin Khalil Abu al-Rashtah
16 Dhul Qa'dah 1438 AH 8/8/2017 AD
Kiungo cha jibu kutoka kwa ukurasa wa Amir kwenye Facebook
Kiungo cha jibu kutoka kwa ukurasa wa Amir kwenye Google Plus
Kiungo cha jibu kutoka kwa ukurasa wa Amir kwenye Twitter
Kiungo cha jibu kutoka kwa Tovuti ya Amir