Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

Jibu la Swali: Mkutano wa Trump na Putin huko Alaska

August 24, 2025
2509

Jibu la Swali

Mkutano wa Trump na Putin huko Alaska

Swali: Marais Trump wa Marekani na Putin wa Urusi walifanya mkutano huko Alaska mnamo tarehe 16/08/2025, je, kulikuwa na makubaliano kati yao kuhusu masuala ya msingi? Na nini athari ya mkutano huu katika uhusiano kati ya nchi hizo mbili? Na juu ya Ukraine? Na athari yake kimataifa kwa Ulaya na China?

Jibu: Ili kuweka wazi jibu la maswali hapo juu, tunapitia mambo yafuatayo:

  1. Uhusiano kati ya Marekani na Urusi umebadilika katika miongo mitatu iliyopita kutoka uhusiano kati ya madola makuu mawili yaliyodhibiti hatima ya dunia kabla ya kusambaratika kwa Umoja wa Kisovieti mwaka 1991, hadi Urusi kujiondoa kwenye ulingo wa kimataifa na kujifungia ndani huku Marekani ikitazama kina cha kuporomoka kwa Urusi na kujaribu kuchukua maeneo yake ya ushawishi wa Kisovieti. Kisha kukafuata majaribio ya Rais wa Urusi Putin kuirejesha Urusi kama dola kuu yenye hadhi ya kimataifa, jambo ambalo Marekani ililikataa. Kama kiashiria cha kina cha mgongano kati ya malengo ya nchi hizi mbili, vita vilizuka nchini Ukraine mwaka 2022, ambapo kupitia vita hivyo Urusi ilitaka kuinua hadhi yake ya kimataifa kwa nguvu, na Marekani kupitia uungaji mkono wake kwa Ukraine ilitaka kuiondoa Urusi kwenye orodha ya madola makuu. Hali hii iliendelea hadi mwisho wa utawala wa Biden. Wakati Trump alipokuja tena kama rais wa Marekani, alianza kuielekeza upya dira ya Marekani dhidi ya China, na akatangaza kuwa anataka kupunguza mvutano na Urusi. Alikuwa akisema kuwa ana uwezo wa kumaliza vita vya Ukraine ndani ya saa 24, na kwamba vita hivi si vyake, bali ni vita vya Biden. Kwa hivyo, Marekani chini ya utawala wa Trump ilianza kubadili mwelekeo katika uhusiano wake na Urusi. Mabadiliko haya yalionekana wazi kupitia dharau za mara kwa mara alizozielekeza Rais Trump kwa Rais wa Ukraine Zelensky, akosoaji mkubwa wa msaada wa kijeshi wa Marekani kwa Ukraine, na kuitaka nchi za Ulaya kubeba majukumu yao ya kifedha na kijeshi nchini Ukraine.

  2. Vita vya Ukraine vilifanikiwa kudhoofisha hadhi ya kimataifa ya Urusi. Jeshi lake lilionekana kushindwa kufikia malengo ya haraka na ya thamani ya juu nchini Ukraine, takriban nusu ya meli zake za kivita katika Bahari Nyeusi ziliharibiwa, na kambi zake za kimkakati ndani kabisa ya Urusi zilipigwa. Pia ilipoteza vipengele muhimu katika vikosi vyake vya nchi kavu, vikiwemo vifaa na majenerali. Hata hivyo, haikushindwa kabisa na ilibaki na uwezo wa kupiga hatua ndani ya Ukraine, hata kama hatua hizo zilielezewa kuwa kama mwendo wa mchwa. Lakini Urusi, ambayo ilijikuta ikikabiliana na uwezo wa kijeshi wa NATO, kana kwamba iko vitani na nchi za NATO, ilionyesha kutoridhika, na mara kwa mara kauli na maandalizi ya nyuklia yalijitokeza. Hali hii ni hatari sana na Marekani haitaki ifike huko. Hii ina maana kwamba vita vya Ukraine vilionyesha hatari ya kuelekea kwenye vita vya nyuklia. Vita nchini Ukraine vilimfanya Rais wa Urusi Putin kuimarisha ushirikiano wake wa kimkakati na China. Mwelekeo huu, ingawa ulitarajiwa na Marekani, na licha ya China kutomlaki Putin kwa bashasha ile ile ili isipoteze uhusiano wake mkuu wa kibiashara na Marekani na Ulaya, bado mgawanyiko wa dunia katika kambi mbili ndilo jambo la mwisho ambalo Marekani inalitaka. Marekani haitaki kabisa nguvu ya kiuchumi ya China iungane na nguvu ya kijeshi ya Urusi katika kambi moja.

  3. Hofu ya Urusi dhidi ya kushindwa kimkakati kulikokuwa kumepangwa na Marekani katika uwanja wa Ukraine ilikuwa msukumo kwa Urusi kuongeza silaha za makombora na nyuklia. Makubaliano ya nyuklia na Marekani yako katika kiwango cha chini kabisa baada ya Marekani kujiondoa mwaka 2019 kwenye mkataba wa makombora ya masafa ya kati. Aidha, mbali na Urusi kuingiza mfumo wa makombora ya hypersonic katika vita vyake nchini Ukraine, pia iliingiza mwaka 2024 kombora la "Oreshnik" lenye uharibifu mkubwa sana. Mwishowe, kabla tu ya mkutano wa Putin na Trump, Urusi ilitangaza majaribio ya makombora ya nyuklia yenye injini za nyuklia pia, ambayo Marekani ilikuwa inajua maandalizi yake. Makombora haya yana masafa na kasi isiyo na kikomo. Hali hii mbali na hatari yake kwa Marekani na kwamba inabatilisha ngao yake ya makombora ambayo ilijigamba nayo na kutumia mabilioni ya dola, inathibitisha kwa Marekani kuwa Urusi inaendelea na mashindano mapya ya kijeshi ya kimkakati bila kujali gharama ya kiuchumi. Hili linaitaka Marekani kufikia makubaliano na Urusi ili kusitisha maendeleo yake na kuepuka mashindano ya kijeshi yanayofanana na kipindi cha Vita Baridi.

  4. Urusi ilikuwa inakabiliwa na uwezekano wa kushindwa kijeshi nchini Ukraine, kwani taswira ya jeshi lake kama jeshi la dola kuu ilivunjika na likashindwa kulishinda jeshi la Ukraine. Vita hivyo vilikuwa ni kama kuvutana, yaani Urusi ilipoteza faida ya nguvu ya maamuzi, na hii ilidhuru hadhi yake ya kimataifa. Mbali na udhaifu wake wa kijeshi ulioonekana Ukraine, iliwekewa msururu mzito wa vikwazo vya Magharibi vilivyoifikisha karibu na hatua ya kutolewa kwenye uchumi wa dunia, na iliwekewa kutengwa kukubwa kimataifa. Rais wa Urusi hakuweza hata kuwa na uhuru wa kusafiri nje ya nchi kutokana na hati ya kukamatwa iliyotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC). Kwa hivyo, Urusi ilitumia nishati yake yote ya kiuchumi na kijeshi ili kuondoa tishio la kushindwa kimkakati katika vita vya Ukraine, na uchumi wake ukawa uchumi wa vita. Ilikuwa ikiona kuwa hadhi yake ya kimataifa itaamuliwa na vita vya Ukraine, lakini tishio la kushindwa halikuondoka, na hofu yake kubwa ilikuwa mambo kuelekea kwenye uingiliaji kati wa NATO na kulazimisha makabiliano ya moja kwa moja, jambo ambalo haina uwezo nalo isipokuwa kutumia zana zake za nyuklia, lakini kutumia zana hizo ni hatari sana. Wakati Rais wa Marekani Trump alipokuja na kuanza kuipoza Urusi na kumsifia Rais wake, Urusi ilipata nafuu, kwani hilo liliwakilisha mabadiliko ya Marekani kutoka kwenye mipango ya kuishinda Urusi kimkakati. Labda Urusi ilifikiria kukubali matoleo ya Trump kama yalivyo ili kupunguza kudhoofika kwake, lakini inatazama mlango ambao Trump aliufungua kwa ajili ya kurejea kwake kwenye uwanja wa kimataifa na iko katika hali ya wasiwasi isije mlango huo ukafungwa, hivyo inataka kuingia.

  5. Marekani ilipoona kusuasua kwa Urusi na kukataa kwake kusitisha vita, na sauti kupazwa huko Magharibi kuwa Putin anatumia fursa ya mwelekeo wa Trump wa hivi karibuni na hamu yake ya kusitisha vita nchini Ukraine, Rais wa Marekani alitangaza kuipa Urusi muda wa siku 50 ili kusitisha vita nchini Ukraine. Licha ya kutoridhika kwa Urusi na muda huu na kuomba ufafanuzi, iliendelea kusuasua ndani ya muda huo ikitaka kuutumia hadi mwisho. Jambo hilo lilimfanya Rais wa Marekani kutishia kubadili mwelekeo kinyume, yaani kufunga mlango na kurejea kwenye misimamo ya utawala wa Biden. Hivyo alitangaza kufupisha muda huo hadi siku 10 tu. Jambo hili lilifanya Urusi, kupitia Naibu Mshauri wa Usalama wa Taifa na Rais wa zamani Medvedev, kuliona kama hatua ya kuelekea vitani. Medvedev aliikumbusha Marekani kuhusu "mkono wa nyuklia wenye mauti" wa Urusi, na Rais wa Marekani akamjibu kwa kumtaka awe mwangalifu kwani anaingia katika eneo hatari sana. Kwa tishio hili la Marekani la kubadili mwelekeo na kuanza tena kuunga mkono Ukraine na kuweka vikwazo vikali zaidi kwa Urusi vinavyojumuisha kila anayenunua mafuta kutoka kwake, yaani China hasa, ndipo saa ilipogonga huko Moscow kuwa ni lazima kuchukua uamuzi.

  6. Hivyo, Urusi iliona kuwa ni lazima ifanye haraka kutoa makubaliano kwa Marekani, kwani haitaki kurejea kwa kasi ya msaada wa Marekani kwa Ukraine ambayo inaiongezea kudhoofika, na inapoteza fursa aliyoitoa Rais Trump ya kuiondoa kwenye kutengwa kimataifa. Hii ni pamoja na shaka ya Urusi kuhusu China; kwani China ikichagua kati ya kufaidika na mafuta ya bei rahisi ya Urusi na uhusiano wake wa kibiashara na Marekani, bila shaka itachagua uhusiano na Marekani kwa sababu ya faida zake nyingi. Aidha, toleo la amani la Trump linaipa Urusi kile inachotaka, ambacho ni makubaliano na Marekani pekee kama ilivyokuwa mkutano wa Yalta mwaka 1945, na haitaki kushirikisha pande nyingine za Ulaya au Ukraine. Badala yake inataka makubaliano na Marekani kisha yawasilishwe kwa pande nyingine kama jambo lililokamilika. Hivyo Urusi ilichukua hatua ya kuomba mkutano na mjumbe wa Rais Trump (Witkoff) ili kumaliza wazo la muda iliopewa Urusi, na hii bila shaka inaitaka kuachana na baadhi ya madai yake. Katika hatua ya kuidhinisha mkutano wa kilele kati ya maraisi hao wawili na wakati wa maandalizi mafupi, pande zote mbili zilionyesha nia ya kutaka mkutano huu. Kweli Trump alikubali ombi la Urusi la kumtuma mjumbe wake maalum Witkoff kwenda Moscow. Trump alizungumza kuhusu fursa na kubadilishana ardhi na mipaka kati ya Urusi na Ukraine. Urusi nayo ilizungumzia ukweli wa Marekani: (Putin alisema kuwa Moscow inafanya kazi kuweka mazingira ya kuleta amani, na kwamba Marekani inafanya juhudi za dhati za kutatua hali ya Ukraine. Putin alisisitiza umuhimu wa kufikia makubaliano na Washington kuhusu kupunguza silaha za kimkakati za mashambulizi. Al-Jazeera Net, 14/08/2025). Urusi ilikubali mkutano huo ufanyike Alaska, yaani nchini Marekani, ili kumridhisha Trump: (Trump anaona kuwa uamuzi wa Rais wa Urusi Vladimir Putin kusafiri kwenda Alaska kufanya mkutano naye, ni "kitendo chenye heshima kubwa". RT, 12/08/2025).

  7. Lakini kwa upande mwingine, Marekani ilipoona kusuasua kwa Urusi kwa miezi kadhaa baada ya Trump kuingia Ikulu, haikutaka kabisa mkutano huu uishe bila makubaliano kutoka kwa Urusi. Trump alisema kuwa mkutano huu ni wa "ugunduzi" na kwamba atajua kutoka dakika za kwanza za mkutano kama Putin yuko siriazi kumaliza vita nchini Ukraine au la. Alionya dhidi ya kufeli kwa mkutano huo na akaweka asilimia 25 ya uwezekano wa kufeli, na akaionya Urusi kwa matokeo mabaya: (Rais wa Marekani Donald Trump alimwonya mwenzake wa Urusi Vladimir Putin, Jumatano, kwa "matokeo mabaya" ikiwa atazuia juhudi za kuleta amani nchini Ukraine, akitishia uwezekano wa kuweka vikwazo vya kiuchumi ikiwa mkutano wao uliopangwa kufanyika Ijumaa huko Alaska utashindwa kupata matokeo yanayoonekana. Trump alieleza kuwa mkutano na Putin utakuwa wa "maandalizi" kwa ajili ya mkutano wa pili utakaomjumuisha Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, akionyesha kuwa kufanyika kwake kunategemea matokeo ya mkutano wa Alaska. Arab 48, 14/08/2025). Kisha Rais wa Marekani Donald Trump aliuelezea mkutano wake na Vladimir Putin kuwa ni wa ("hatari kubwa" kabla ya kuelekea Anchorage, Alaska, kufanya mkutano wao wa kwanza katika kipindi cha miaka saba. Trump alielezea nia yake ya kuona usitishaji vita "haraka sana". Independent Arabia, 15/08/2025). Trump alisema kuwa atafanya haraka kurejea Washington kutoka Alaska ikiwa Putin hatakuwa siriazi. (Rais wa Marekani Donald Trump aliwasili katika kambi ya anga ya Elmendorf huko Anchorage, jimbo la Alaska, Ijumaa, na Trump alisema kuwa ikiwa mkutano na Rais wa Urusi Vladimir Putin utaenda vibaya, ataondoka. CNN Arabic, 15/08/2025). Kauli hii ya kuondoka kwenye mkutano ina aina fulani ya dharau kwa Rais Putin ambaye alikuja kukutana na Trump nchini Marekani!

  8. Kauli hizi zote zinabeba shinikizo kwa Urusi kuwa lazima itoe makubaliano. Anaitishia matokeo mabaya, vikwazo, na kuondoka kwenye mkutano. Hii ina maana kwamba mkutano kati yao haukuwa wa usawa kama ilivyokuwa mikutano muhimu kati ya viongozi wa Kisovieti na Marekani hapo awali. Si mkutano wa miamba miwili, na hata haufikii kiwango cha mikutano ya kilele kati ya Marekani na China. Ndani yake kuna kukuza kiburi cha Marekani na kuitaka Urusi isalimu amri, pamoja na kushuka kwa hadhi mpya ya Urusi ambayo ilikubali mazingira haya yote, muda na vitisho vya Marekani. Rais wake alisafiri kwenda Marekani kufanya mkutano na Trump badala ya kuwa katika nchi ya tatu. Pengine hatua iliyo kinyume na itifaki, ambapo Rais wa Urusi Putin alikubali ofa ya Rais wa Marekani ya kupanda naye kwenye gari lake binafsi licha ya kuwepo kwa gari la Putin ambalo huambatana naye katika mikutano yake yote ya kimataifa, ni ushahidi wa unyonge wa Urusi na hitaji lake la uhusiano wa karibu na Trump ili kupunguza hasara zake za kimkakati. Kinachothibitisha hili ni kwamba, licha ya hali ya mgogoro mkubwa wa uhusiano kati ya Marekani na Urusi uliowekwa na utawala wa Biden, Rais wa Urusi alikuwa na shauku ya kumvutia Trump. Yuri Ushakov, msaidizi wa Rais wa Urusi, alisema: (Ushirikiano kati ya Urusi na Marekani una uwezo mkubwa sana ambao bado haujatumiwa. Alionyesha kuwa ujumbe wa Urusi utamjumuisha msaidizi wa rais Yuri Ushakov, Waziri wa Mambo ya Nje Sergey Lavrov, Waziri wa Fedha Anton Siluanov, na mkuu wa mfuko wa uwekezaji wa moja kwa moja wa Urusi Kirill Dmitriev. RT, 14/08/2025). Hii ni ishara ya udhaifu wa Urusi ambayo Marekani lazima iwe imeiona. Labda katika kauli za Rais wa Urusi Putin baada ya mkutano kuna kile kinachoashiria udhaifu huo na kina cha wasiwasi wa Urusi kutokana na kuendelea kwa mvutano wa uhusiano kati ya nchi hizo mbili. Rais wa Urusi alianza hotuba yake katika mkutano na waandishi wa habari kwa kukiri kuzorota kwa uhusiano wa Marekani na Urusi katika miaka ya hivi karibuni. Alisema: ("Inajulikana kuwa hakuna mikutano ya kilele iliyofanyika kati ya Urusi na Marekani kwa miaka minne, ambayo ni kipindi kirefu. Kipindi hiki kilikuwa kigumu sana kwa uhusiano wa nchi hizi mbili. Na tuwe wakweli, umefikia kiwango cha chini kabisa tangu Vita Baridi. Naamini kuwa hili halinufaishi nchi zetu na dunia nzima". Aliongeza: "Mkutano wa ana kwa ana kati ya marais wa nchi hizi mbili umechelewa sana". Putin alisema: "Mazungumzo yalifanyika katika hali ya hewa ya kuheshimiana na yalikuwa mapana na yenye manufaa makubwa". CNN Arabic, 16/08/2025).

  9. Kwa ufupi, kwa kutazama kwa kina na kutafakari mwenendo wa mkutano kati ya Trump na Putin na kile kilichozungumziwa na vyombo vya habari, inaweza kusemwa kuwa mkutano wao ulijadili mambo yafuatayo:

    a- Ukraine: Hili ndilo suala kuu, ingawa si pekee, lakini ndilo maarufu zaidi na la moto zaidi. Licha ya ugumu wa madai ya usalama ya Urusi yanayowakilishwa na kuiondoa Ukraine mbali na NATO na kutokuwa na jeshi lenye nguvu linalotishia Urusi, makubaliano ya wazi yameainisha misingi mikuu, ambapo upande mmoja ni ahadi ya Urusi ya baadaye ya kutovamia Ukraine: (Putin alisisitiza kuwa anakubaliana na umuhimu wa kuhakikisha usalama wa Ukraine, akisema: "Ninakubaliana na (Rais wa Marekani Donald) Trump juu ya umuhimu wa kuhakikisha usalama wa Ukraine, na sisi bila shaka tuko tayari kufanya kazi kwa hilo". Aliongeza: "Natumai kuwa makubaliano tuliyofikia pamoja yatachangia kufikia lengo hili, na yatafungua njia kuelekea amani nchini Ukraine". CNN Arabic, 16/08/2025). Kinachothibitisha pia kuwepo kwa makubaliano ni kwamba Rais wa Marekani aliupa mkutano wake na Putin alama 10 kati ya 10 (Sky News, 16/08/2025). Marekani inapunguza joto la uwanja wa vita nchini Ukraine kama maandalizi ya kuusitisha, na hii inahitaji ahadi ya Marekani ya kupunguza msaada wa kijeshi wa Marekani na Magharibi kwa jeshi la Ukraine hatua kwa hatua, kisha kutangaza usitishaji vita ambao labda utakuwa kupitia mkutano utakaofuata unaowakutanisha marais hao wawili na Rais wa Ukraine Zelensky ndani ya wiki chache, kisha kuendelea na suluhu nchini Ukraine kwa utulivu, na labda kwa kipindi cha miaka mingi. Yaani Marekani inaahirisha suluhu ya mwisho na inataka kasi katika kusitisha vita, na kwamba suluhu ya mwisho iwe kwa kipindi cha miaka mingi ambapo Marekani itailazimisha Ukraine kuachana na ardhi na mipaka kulingana na makubaliano ya Urusi kwa Marekani katika masuala mengine, kana kwamba inaionjesha Urusi kwa kuitambua mipaka ya udhibiti wa Urusi nchini Ukraine kwa masharti ambayo Urusi lazima iyatimize na kuiridhisha Marekani kwayo.

    b- Kurejesha uhusiano wa kawaida kati ya Marekani na Urusi: Mchakato huu, ingawa ulianza tangu mkutano wa Istanbul mnamo Aprili 2025, unatarajiwa kushika kasi, na kuna uwezekano kasi hiyo ikaonekana wazi baada ya mkutano wa pili kati ya nchi hizo mbili ambapo Ukraine inaweza kujiunga nazo kwa lengo la kutangaza usitishaji vita. Kurejesha uhusiano kunachukuliwa kuwa ni hitaji la haraka kwa Marekani ili kufungua mazungumzo katika masuala mengine ya kimkakati.

    c- Mashindano ya silaha na nguvu ya kimkakati: Inaelekea sana, kutokana na mahitaji ya pande zote mbili, kwamba mazungumzo ya silaha na nguvu ya kimkakati ya nyuklia na makombora yatafunguliwa haraka. Na inaelekea kuwa Urusi inakubali leo sharti la awali la Marekani kwamba China ijiunge na mazungumzo haya, ili yawe ya pande tatu. Hii ni kwa sababu makubaliano ya Urusi na Marekani kabla ya hapo yalikuwa mwendelezo wa makubaliano kati ya miamba miwili ya kijeshi tangu miongo kadhaa, na Marekani iliyavunja kwa sababu inataka kuijumuisha miamba ya China ndani yake, hasa kwa kuwa China leo inatekeleza programu za silaha za nyuklia ambazo zitaifanya iwe katika safu ya miamba hiyo hivi karibuni. Programu yake ya nyuklia inaelekea kuifanya iwe na takriban vichwa vya nyuklia elfu moja ifikapo mwaka 2030, yaani imeshazipita kwa miaka mingi nguvu za nyuklia za kati kama Uingereza na Ufaransa. Kwa hivyo, inaelekea kuwa sababu zote za Urusi kusita kuialika China kushiriki katika mazungumzo ya Urusi na Marekani kuhusu silaha za kimkakati zimeondoka. Hii inawakilisha hatua kwa Marekani katika njia yake ya kusambaratisha muungano wa Urusi na China. Kwa yote hayo, inaelekea kuwa tumaini la Marekani la kusambaratisha muungano wa Urusi na China ni kubwa, lakini bila kuingia moja kwa moja ili isiumize hisia za Urusi, bali kwa hatua za kukaribiana na Urusi ili kudhoofisha muungano wa China na Urusi hatua kwa hatua.

  10. Mwishowe, inasikitisha kuona nchi za kikafiri zikidhibiti dunia, marais wake wanakutana, wanajadili na kupanga... wakati Umma wa Kiislamu, ambao ni Umma bora uliotolewa kwa ajili ya watu, hauna athari yoyote katika matukio ya kimataifa, bali hata udhibiti wa kujitegemea wa masuala yake hauko mikononi mwake bali unaendeshwa na mikono ya makafiri wakoloni!!

    Tatizo ni kwamba Umma huu unaokaribia watu bilioni mbili ni mwili usio na kichwa. Khilafah inayouunganisha haipo, na Khalifa anayechunga mambo yake, ambaye watu wanapigana nyuma yake na kujikinga kwake, hayupo! Pamoja na hayo, Khilafah itarejea kwa idhini ya Mwenyezi Mungu kwa ahadi ya Mwenyezi Mungu Mtukufu na bishara ya Mtume Wake ﷺ. Lakini kanuni ya Mwenyezi Mungu inaitaka kwamba malaika hawatashuka kutoka mbinguni kutusimamishia Khilafah wakati Umma umekaa bila kufanya kazi ya kuisimamisha, bali Mwenyezi Mungu hushusha malaika kutusaidia wakati tunafanya kazi. Na Hizbut Tahrir, kiongozi asiyewadanganya watu wake, unauita Umma kufanya kazi pamoja nayo ili kuisimamisha, na wakati huo Uislamu na Waislamu watapata utukufu, na ukafiri na makafiri watadhalilika.

وَيَوْمَئِذٍ يَفْرَحُ الْمُؤْمِنُونَ * بِنَصْرِ اللَّهِ يَنْصُرُ مَنْ يَشَاءُ وَهُوَ الْعَزِيزُ الرَّحِيمُ

"Na siku hiyo waumini watafurahi. Kwa nusura ya Mwenyezi Mungu. Yeye humnusuru amtakaye, Naye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu." (QS Ar-Rum [30]: 4-5)

Mnamo tarehe 25 Safar 1447H 19/08/2025M

Share Article

Share this article with your network