Mfululizo wa Majibu ya Mwanachuoni Mtukufu Ata bin Khalil Abu al-Rashtah, Amir wa Hizb ut-Tahrir, kwa Maswali ya Wageni kwenye Ukurasa wake wa Facebook "Fiqhi"
Jibu la Swali
Kwa Jaber Thawabta
Swali:
Assalamu Alaikum wa Rahmatullah,
Swali kuhusu mauzo (al-ba’i):
Tunataka kukodisha ardhi kwa ajili ya kutoa mawe ndani yake kwa mkabala wa kiasi fulani cha pesa, na iwapo mawe hayatakuwa na ubora, tunabadilisha mauzo hayo kuwa kwa mfumo wa asilimia. Je, mauzo haya ni sahihi au ni batili kwa sababu ni mkataba ndani ya mkataba? Tafadhali tujibu kwa haraka.
Jibu:
Wa Alaikum Salaam wa Rahmatullahi wa Barakatuh,
Ewe ndugu yangu, kuingiza mkataba ndani ya mkataba mwingine kwa namna ambayo mmoja unakuwa na sharti la mwenzake hairuhusiwi. Wewe hapa unasema kuwa mkataba wa kwanza ni wa ukodishaji (ijarah) na umewekewa sharti kwamba ikiwa mawe hayatakuwa na ubora, basi mkataba unakuwa wa mauzo kwa asilimia... Na ingawa jambo hili halijawa wazi kabisa katika swali lako kwani hukubainisha nini maana ya neno "asilimia"... lakini maana inayopelekea uzito zaidi ni kwamba unakuwa mkataba mwingine, yaani si ule mkataba wa kwanza wa ukodishaji bali unageuzwa kuwa mkataba mwingine...
Kwa msingi wa uzito huu wa maana, hadith za Mtume ﷺ zinazokataza biashara mbili katika biashara moja na mapatano mawili katika patano moja zinatumika hapa:
- Alitoa At-Tirmidhi katika Sunan yake kutoka kwa Abu Salama, kutoka kwa Abu Hurairah amesema:
نَهَى رَسُولُ اللَّهِ ﷺ عَنْ بَيْعَتَيْنِ فِي بَيْعَةٍ
"Mtume wa Allah ﷺ alikataza biashara mbili katika biashara moja." Abu Isa amesema hadith ya Abu Hurairah ni hadith hasan sahih.
- Alitoa Ahmad katika Musnad yake kutoka kwa Abdurrahman bin Abdullah bin Mas’ud (ra) kutoka kwa baba yake amesema:
نَهَى رَسُولُ اللَّهِ ﷺ عَنْ صَفْقَتَيْنِ فِي صَفْقَةٍ وَاحِدَةٍ
"Mtume wa Allah ﷺ alikataza mapatano mawili katika patano moja."
Imekuja katika kitabu cha Ash-Shakhsiyyah al-Islamiyyah Juzuu ya Pili / Mlango wa Mauzo ya Mkopo yafuatayo:
(...Na matokeo yake ni kwamba, ikiwa mmoja wa wafanyabiashara wawili atamwambia mwenzake: nimekuuzia nyumba yangu kwa elfu moja kwa sharti kwamba uniuzie nyumba yako kwa elfu moja, naye akasema nimekubali; basi huu ni mkataba mmoja wa mauzo uliokusanya mauzo mawili, hivyo haijuzu. Hii ni kwa sababu Mtume ﷺ alikataza biashara mbili katika biashara moja, na mapatano mawili katika patano moja...)
Hivyo basi, mkataba huu si sahihi. Na kama nilivyosema, jibu hili limejengwa juu ya uzito wa maana inayokusudiwa na neno "asilimia" kwamba neno hili linamaanisha mkataba mpya na si mkataba wa ukodishaji, bali ni mkataba wa mauzo ya mawe kwa asilimia. Kwa ibara nyingine, unageuza mkataba wa ukodishaji kwa malipo maalum kuwa mkataba wa mauzo ya mawe yatakayozalishwa kwa asilimia... Ama ikiwa makusudio si hayo, basi rudia kuuliza swali kwa uwazi zaidi, na Allah yu pamoja nawe.
Ndugu yenu, Ata bin Khalil Abu al-Rashtah
26 Rabi’ al-Awwal 1440 H Sawa na 04/12/2018 M
Link ya jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir (Allah amhifadhi) kwenye Facebook
Link ya jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir (Allah amhifadhi) kwenye Google Plus
Link ya jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir (Allah amhifadhi) kwenye Web