Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

Jawabu la Swali: Hukumu Zinazohusiana na Khalifah na Amir wa Muda

August 16, 2020
4365

Mfululizo wa Majibu ya Mwanachuoni Mheshimiwa Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah, Amir wa Hizb ut-Tahrir, kwa Maswali ya Wageni kwenye Ukurasa wake wa Facebook "Fikhi"

Jawabu la Swali

Hukumu Zinazohusiana na Khalifah na Amir wa Muda

Kwa: Sohail Dar

Swali:

Assalam Alaikum Wa Rahmatullahi Wa Barakatuh ndugu zangu watukufu, naweka maswali kwa Amir wetu na nataraji yafikishwe kwake Insha’Allah. Zingatieni kuwa lugha ya Kiarabu si lugha yangu ya asili, na ninaomba radhi sana ikiwa nitakosea katika jambo lolote...

Assalam Alaikum Wa Rahmatullahi Wa Barakatuh ndugu yetu mpendwa na Amir wetu mtukufu, namuomba Mwenyezi Mungu akujalie kheri.

Jambo la kwanza ni kukuomba radhi kwa lugha yangu ya Kiarabu kwa sababu ni dhaifu, pamoja na hayo najaribu kuuliza maswali yanayohusiana na mada ya Khilafah:

Kwanza: Imeelezwa katika kitabu cha Nidham al-Hukm fi al-Islam (Mfumo wa Utawala katika Uislamu) kwamba lakabu zinazojuzu ni Khalifah, Imamu, na Amir wa Waumini (Amir al-Mu'minin) na zinazofanana nazo kimaana kama Sultani wa Waumini, lakini katika kitabu cha Ajihizat Dawlat al-Khilafah (Vifaa vya Dola ya Khilafah), maandishi yanaishia kwenye kutaja lakabu ya Amir wa Waumini na hayataji nyinginezo. Je, maoni yaliyopitishwa (at-tabanni) katika lakabu za Khalifah yamebadilika na kuwa tuishie kwenye hizo tatu pekee? Na ikiwa maoni yamebadilika, ni nini dalili ya mabadiliko hayo?

Pili: Kuhusu yaliyokuja katika kitabu cha Al-Ajihizat (Vifaa vya Dola) kuhusiana na yaliyopelekea Umar (ra) kupewa lakabu ya Amir wa Waumini, je, ni sahihi kusema kwamba ndani yake kuna kizuizi cha kutumia lakabu ya Amir wa Waumini pekee, au inaruhusiwa kutumia lakabu nyingine kama Sultani wa Waumini?

Tatu: Nilielewa kuwa mojawapo ya masharti ya kuwepo kwa Ijmaa ya Maswahaba ni kuwepo kwa mgongano na jambo linalojulikana, kama vile kucheleweshwa kwa mazishi ya Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ na wajibu wa kumzika maiti mara moja. Sasa, ni wapi penye mgongano katika kumpa Umar (ra) lakabu ya Amir wa Waumini mpaka iwe ni Ijmaa ya Maswahaba?

Nne: Ulijibu swali huko nyuma kuwa neno Khalifah ni neno la kisheria la kifikihi (shar’iy fiqhiy). Je, inaweza kusemwa hivyo hivyo kwa neno Imamu kuwa ni neno la kisheria la kifikihi kwa kuwa limekuja katika dalili za kisheria, au tuseme kuwa neno Imamu ni neno la kiistilahi (istilahi)? Na kuhusiana na jambo hili, yamekuja hadithi nyingi zikitaja neno Imamu na likiashiria yule anayewaongoza watu katika swala, je, kuna tofauti ya maana kwa yule anayeashiriwa? Yaani, je, maana katika hadithi hizi inarejea kwa Khalifah na wale anaowatawaza miongoni mwa Magavana (Wali) na Maamir... nk pekee, au inajumuisha pia wale wanaowaongoza Waislamu katika swala kama tunavyowaona siku hizi misikitini mwetu?

Tano: "Amir wa Muda" (Al-Amir al-Mu’aqqat), kwa nini Msaidizi wa Utendaji (Mu’awin Tanfidh) hatawazwi katika kusimamia uwekaji wa Khalifah? Aidha, ni nini msingi wa kuchaguliwa kwa Msaidizi mkubwa zaidi kiumri (akbar al-mu’awinin sinnan) ili kusimamia uwekaji wa Khalifah? Na kwa nini asiwe msaidizi mwenye uzoefu zaidi katika nafasi yake ya usaidizi, au aliye mbora wao kwa uadilifu, au mbora wao kwa elimu ya Qur’ani... nk?

Na nina swali lingine nalo ni... Ikiwa Khalifah atakiuka mojawapo ya masharti ya kufungwa kwa mkataba (shurut al-in’iqad) baada ya kupewa bai’ah, je, bai’ah yake inabatilika? Yaani, ikiwa atakuwa si mwadilifu kwa mfano, au akawa kama wale aliowataja Mtume ﷺ miongoni mwa maimamu ambao Waislamu wanawachukia.

Mwenyezi Mungu awalipe kila la kheri. Nakushukuru sana kwa majibu yako na namuomba Mwenyezi Mungu akujalie wewe na familia yako pamoja na ndugu kheri na afya, na Ramadhan Mubarak.

Ndugu yako, Dkt. Sohail Abu Mus’ab

Jibu:

Wa Alaikum Salaam Wa Rahmatullahi Wa Barakatuh,

Nimefurahi kwamba umeniandikia kwa lugha ya Qur’ani Tukufu, Lugha ya Kiarabu, ingawa unapata ugumu wa kuandika kwayo... Kwa ujumla, ulichouliza kiko wazi isipokuwa baadhi ya sehemu zinazohitaji ufafanuzi zaidi, na huu hapa ni ufafanuzi:

1- Lakabu inayopewa yule anayepigiwa bai’ah kwa Khilafah ni lakabu ya Khalifah, au Imamu, au Amir wa Waumini kama ilivyokuja katika Hadithi tukufu za Mtume na katika Ijmaa ya Maswahaba... Ama yaliyotajwa katika kitabu cha Nidham al-Hukm (Mfumo wa Utawala) baada ya kutaja hizi tatu: [Na si lazima kujifunga na lakabu hizi tatu pekee, bali inajuzu kutoa lakabu nyinginezo kwa yule anayeshika mambo ya Waislamu, miongoni mwa zinazofahamisha maudhui yake, kama vile Mtawala wa Waumini (Hakim al-Mu’minin), au Rais wa Waislamu, au Sultani wa Waislamu, au nyinginezo ambazo hazipingani na maudhui yake. Ama lakabu ambazo zina maana maalum inayopingana na hukumu za Uislamu zinazohusiana na utawala, kama vile Mfalme, Rais wa Jamhuri, (na Kaisari/Emperor), basi haijuzu kuitwa nazo yule anayeshika mambo ya Waislamu, kutokana na kupingana kwa kile zinachofahamisha na hukumu za Uislamu.] Mwisho wa nukuu. Kadhalika yaliyokuja katika kitabu cha Ash-Shakhshiyyah Juzuu ya Pili katika mlango wa Khilafah mwishoni mwa aya: [Na si lazima kujifunga na neno hili, yaani Imamu au Khalifah, bali hujifunga na kile linachomaanisha.] Mwisho wa nukuu.

Maeneo haya mawili yamesahihishwa, na nyongeza zilizotajwa hapo juu katika vitabu vya Nidham al-Hukm na Ash-Shakhshiyyah Juzuu ya Pili zimefutwa, na lakabu zimebaki kuwa ni tatu tu kama ilivyo katika kitabu cha Al-Ajihizat (Khalifah, Imamu, Amir wa Waumini), na lakabu hizi tatu ndizo zitakazotumika katika dola wakati Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Ta’ala atakapotunusuru.

2- Sharti katika Ijmaa ya Kunyamaza (Al-Ijma’ as-Sukuti) kuhusu hukumu ya kisheria ili ihesabike kuwa ni Ijmaa inayokubalika ni "kuwa hiyo hukumu ya kisheria iwe ni miongoni mwa mambo ambayo kwa kawaida hukemewa na Maswahaba hawawezi kuyanyamazia; na hiyo ni kutokana na muhali kwa Maswahaba kukubaliana kunyamazia jambo la haramu (munkar). Ikiwa ni miongoni mwa mambo ambayo hayakemewi kwa kawaida, basi kunyamaza kwa Maswahaba hakuhesabiki kuwa ni Ijmaa"... Imekuja katika kitabu cha Ash-Shakhshiyyah Juzuu ya Tatu: (Ijmaa ya Kunyamaza ni pale mmoja wa Maswahaba anapoelekea kwenye hukumu fulani na Maswahaba wakaifahamu na kusiwe na yeyote aliyemkemea, basi kunyamaza kwao kunakuwa ni Ijmaa, na huitwa Ijmaa ya Kunyamaza mkabala wa Ijmaa ya Kauli... Na imewekewa masharti katika Ijmaa ya Kunyamaza:

Mosi: Hukumu hiyo ya kisheria iwe ni miongoni mwa mambo ambayo kwa kawaida hukemewa na Maswahaba hawawezi kuyanyamazia...

Pili: Kitendo hicho kiwe kimeenea na Maswahaba wanakifahamu...

Tatu: Jambo hilo lisiwe miongoni mwa mambo ambayo Amir wa Waumini amepewa mamlaka ya kuyafanyia uamuzi kwa maoni yake kama vile mali ya Baitul Mal...)

Masharti haya lazima yawepo katika Ijmaa ya Kunyamaza ili itumike kama dalili. Ama kuhusu mada ya Ijmaa ya Maswahaba juu ya kutumia lakabu "Amir wa Waumini", jambo hili si katika mlango wa Ijmaa ya Kunyamaza mpaka liwekewe sharti lililotajwa hapo juu, bali ni katika aina ya Ijmaa ya Kauli (Al-Ijma’ al-Qawli) kwa sababu Maswahaba kwa ujumla wao walitumia lakabu hii katika mazungumzo yao na wakawaita kwayo Makhalifah, hivyo hili lilikuwa katika daraja ya Ijmaa ya Kauli na si Ijmaa ya Kunyamaza, na kwa hivyo hailazimu kuwa hukumu hii iwe ni jambo la kukemewa kwa kawaida ili Ijmaa iwe sahihi na kuzingatiwa.

3- Kuhusiana na swali lako kuhusu neno Imamu:

a- Imamu katika lugha ana maana kadhaa miongoni mwazo ni yule anayefuatwa na kuigwa, imekuja katika Mukhtar as-Sihah: (...na Imamu ni yule anayefuatwa na wingi wake ni Maimamu...) na imekuja katika kitabu cha Al-Ayn: (...na kila anayefuatwa, na akawa mbele katika mambo basi yeye ni imamu...), hivyo imamu kwa maana hii ni kila anayefuatwa na kuigwa kwa ujumla.

b- Na Sheria imetumia neno Imamu kama istilahi ya kifikihi (ukweli wa kisheria - haqiqah shar’iyyah) kwa maana ya kiongozi mkuu wa Waislamu ambapo maandiko ya kisheria yamefahamisha hayo, na miongoni mwa maandiko haya ni:

  • Kutoka kwa Abdullah bin Amr bin al-Aas kwamba alimsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ akisema:

وَمَنْ بَايَعَ إِمَامًا فَأَعْطَاهُ صَفْقَةَ يَدِهِ، وَثَمَرَةَ قَلْبِهِ، فَلْيُطِعْهُ... "Na yeyote atakayempa kiapo (bai’ah) imamu, akampa mkono wake na tunda la moyo wake, basi amtii..." (Imepokewa na Muslim).

  • Kutoka kwa Auf bin Malik, kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ amesema:

خِيَارُ أَئِمَّتِكُمْ الَّذِينَ تُحِبُّونَهُمْ وَيُحِبُّونَكُمْ، وَيُصَلُّونَ عَلَيْكُمْ وَتُصَلُّونَ عَلَيْهِمْ... "Wabora wa maimamu wenu ni wale mnaowapenda nao wanawapenda, na wanawaombea nanyi mnawaombea..." (Imepokewa na Muslim).

  • Alitoa Bukhari kutoka kwa Ibn Shihab... kwamba Salim alimhadithia: Kwamba Abdullah bin Umar anasema: Nilimsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ akisema:

كُلُّكُمْ رَاعٍ، وَكُلُّكُمْ مَسْئُولٌ عَنْ رَعِيَّتِهِ، الإِمَامُ رَاعٍ وَمَسْئُولٌ عَنْ رَعِيَّتِهِ... "Kila mmoja wenu ni mchungaji, na kila mmoja wenu ataulizwa kuhusu kundi lake, Imamu ni mchungaji na ataulizwa kuhusu kundi lake..."

Katika hadithi hizi imetajwa lakabu ya mtawala anayesimamisha hukumu za kisheria katika Uislamu ambayo ni: Imamu, kama ilivyotajwa lakabu ya Khalifah katika maandiko mengine ya kisheria. Yaani maandiko ya kisheria yalibainisha kuwa neno "Imamu" ni sawa na neno "Khalifah" na kuwa ni istilahi za kifikihi (haqiqah shar’iyyah) ambazo Sheria imezitaja na zinamaanisha uongozi mkuu wa Waislamu, na imeitwa Uimamu Mkuu (Al-Imamah al-Uzma) na mwenye nafasi hiyo ameitwa Imamu Mkuu (Al-Imam al-A’dham)...

c- Kadhalika neno Imamu limetumiwa katika Sheria kwa maana ya imamu wa swala, nayo ni uimamu unaoitwa Uimamu Mdogo (Al-Imamah as-Sughra), na yamekuja katika hilo hadithi miongoni mwazo ni:

  • Amepokea Bukhari katika Sahih yake kutoka kwa Aisha Mama wa Waumini kwamba amesema: Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ aliswali nyumbani kwake akiwa mgonjwa, akaswali ameketi na watu wakaswali nyuma yake wakiwa wamesimama, akawaashiria waketi. Alipomaliza alisema:

إِنَّمَا جُعِلَ الْإِمَامُ لِيُؤْتَمَّ بِهِ فَإِذَا رَكَعَ فَارْكَعُوا وَإِذَا رَفَعَ فَارْكَعُوا وَإِذَا صَلَّى جَالِساً فَصَلُّوا جُلُوساً "Hakika Imamu amewekwa ili afuatwe; anaporukuu basi rukuuni, na anapoinuka basi inukeni, na akiswali ameketi basi swalini mkiwa mmeketi."

  • Amepokea Bukhari katika Sahih yake kutoka kwa Abu Hurairah kwamba Mtume ﷺ amesema:

إِذَا أَمَّنَ الْإِمَامُ فَأَمِّنُوا فَإِنَّهُ مَنْ وَافَقَ تَأْمِينُهُ تَأْمِينَ الْمَلَائِكَةِ غُفِرَ لَهُ مَا تَقَدَّمَ مِنْ ذَنْبِهِ "Imamu anaposema 'Amin', basi itikieni 'Amin', kwani yule ambaye 'Amin' yake itaoana na 'Amin' ya Malaika atasamehewa dhambi zake zilizotangulia."

Hivyo neno "Imamu" lililowekwa kisheria mkabala wa imamu wa swala pia ni istilahi ya kisheria kama zinavyofahamisha hadithi zilizotajwa hapo juu.

d- Hakuna mfungamano wa lazima wa kisheria kati ya neno Imamu kwa maana ya Khalifah na neno Imamu kwa maana ya imamu wa swala. Hadithi ambazo ndani yake kumetajwa Imamu kwa maana ya Khalifah hazihusiani kwa ulazima na mada ya swala, na hadithi ambazo ndani yake kumetajwa Imamu kwa maana ya imamu wa swala hazihusiani kwa ulazima na Khalifah na utawala. Na hilo ni kama hadithi zilizotajwa hapo juu ambapo haifahamiki ndani yake mfungamano kati ya uimamu wa utawala na uimamu wa swala...

e- Maandiko yaliyokuja na neno Imamu yanafahamika kulingana na muktadha wake na kulingana na viashiria (qara’in):

  • Neno Imamu linaweza kutumika katika maandiko ya kisheria kwa maana ya kilugha kama kauli yake Mwenyezi Mungu:

وَالَّذِينَ يَقُولُونَ رَبَّنَا هَبْ لَنَا مِنْ أَزْوَاجِنَا وَذُرِّيَّاتِنَا قُرَّةَ أَعْيُنٍ وَاجْعَلْنَا لِلْمُتَّقِينَ إِمَاماً "Na wale wanaosema: 'Mola wetu, tupe katika wake zetu na dhuriya zetu kiburudisho cha macho, na utujaalie kuwa imamu kwa wachamungu'." (Quran 25:74).

Imekuja katika tafsiri ya Ibn Kathir kuhusu aya hii: (Na kauli yake: "na utujaalie kuwa imamu kwa wachamungu", Ibn Abbas, Al-Hasan, Qatadah, As-Suddi, na Ar-Rabi’ bin Anas wamesema: Viongozi wanaofuatwa katika kheri. Na wengineo wamesema: Waongoaji walioongoka na walinganizi kwenye kheri), na ni wazi kutokana na muktadha kwamba kinachokusudiwa na neno Imamu hapa ni mtu anayefuatwa katika ucha Mungu na si Imamu kwa maana ya mtawala au kwa maana ya imamu wa swala.

  • Na neno Imamu linaweza kutumika kwa maana ya Khalifah kama katika hadithi aliyoipokea Muslim kutoka kwa Abu Hurairah kutoka kwa Mtume ﷺ amesema:

إِنَّمَا الْإِمَامُ جُنَّةٌ يُقَاتَلُ مِنْ وَرَائِهِ وَيُتَّقَى بِهِ فَإِنْ أَمَرَ بِتَقْوَى اللَّهِ عَزَّ وَجَلَّ وَعَدَلَ كَانَ لَهُ بِذَلِكَ أَجْرٌ وَإِنْ يَأْمُرْ بِغَيْرِهِ كَان عليه مِنْهُ "Hakika Imamu ni ngao, inapiganwa nyuma yake na kwayo watu hujilinda. Akiamrisha ucha Mungu kwa Mwenyezi Mungu Aliyeshinda na Akatukuka na akafanya uadilifu, basi atapata thawabu kwa hilo, na akiamrisha kinyume chake, basi yatakuwa juu yake."

Ni wazi kutokana na hadithi hii kuwa kinachokusudiwa ni mtawala kwa sababu mtawala ndiye anayepiganwa nyuma yake na ndiye anayefanya uadilifu au kudhulumu, na wala hakukusudiwa ufuataji wa kijumla kama ilivyo katika maana ya kilugha wala uimamu wa swala.

  • Na neno Imamu linaweza kutumika kwa maana ya imamu wa swala kama alivyopokea Muslim katika Sahih yake kutoka kwa Abu Hurairah kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ amesema:

إِذَا قَالَ الْإِمَامُ سَمِعَ اللَّهُ لِمَنْ حَمِدَهُ فَقُولُوا اللَّهُمَّ رَبَّنَا لَكَ الْحَمْدُ فَإِنَّهُ مَنْ وَافَقَ قَوْلُهُ قَوْلَ الْمَلَائِكَةِ غُفِرَ لَهُ مَا تَقَدَّمَ مِنْ ذَنْبِهِ "Imamu anaposema 'Sami’allahu liman hamidah', basi semeni 'Allahumma Rabbana laka al-Hamd', kwani yule ambaye kauli yake itaoana na kauli ya Malaika atasamehewa dhambi zake zilizotangulia."

Na ni wazi kuwa maneno hapa ni kuhusu swala na kuhusu imamu wa swala.

4- Kuhusiana na swali lako kuhusu Amir wa Muda:

Haiko wazi sawasawa nini unakusudia kwa kusema kwako: ("Amir wa Muda" kwa nini hatawazwi msaidizi wa utendaji katika kuteua Khalifah)...

Ama mada ya kuchagua Msaidizi (Mu’awin) mkubwa zaidi kiumri kuwa Amir wa muda, tumebainisha sababu ya hilo katika jawabu la swali la tarehe 02 Sha'ban 1435 AH sawia na 31/05/2014 BK, na ninakunukulia kutoka kwa jawabu letu lililoashiriwa yafuatayo:

[... Ama jambo la pili nalo ni namna ya kumteua Amir wa muda ikiwa Khalifah hakumteua Amir wa muda kabla ya kifo chake, na vipaumbele katika hilo, basi hilo ni jambo la kiutawala, na inajuzu kupitisha (tabanni) kipengele kinachofafanua jambo hili la kiutawala. Na kwa msingi huo ndivyo ilivyotajwa katika Kipengele cha "33": (...basi msaidizi mkubwa zaidi kiumri ndiye anakuwa Amir wa muda isipokuwa akitaka kugombea Khilafah, basi anafuata anayemfuatia kwa umri... na kuendelea. Ikiwa wasaidizi wote wanataka kugombea, basi Waziri wa Utendaji (Wazir at-Tanfidh) mkubwa zaidi kiumri kisha anayemfuatia ikiwa anataka kugombea... na kuendelea. Ikiwa Mawaziri wa Utendaji wote wanataka kugombea Khilafah, Amir wa muda ataishia kwa Waziri wa Utendaji mdogo zaidi kiumri).

Kwa ufahamu, kumezingatiwa katika utaratibu huu sababu za lazima, kwani wasaidizi (al-mu’awinun) ndio watu wanaojua zaidi utawala na wenye ufahamu zaidi wa mtiririko wa mambo wakati wa zama za Khalifah aliyepita, na wanafuatiwa kwa elimu na uzoefu na Mawaziri wa Utendaji kutokana na ukaribu wao na Khalifah na kazi zake. Hawa ndio watu bora zaidi wa kushika uamir wa muda. Na kwa kuwa wasaidizi wako sawa na hakuna upendeleo kati yao katika usaidizi, na mawaziri kadhalika, umri ulikuwa ndio kigezo kinachofaa kwa ajili ya upendeleo kama ilivyo katika uimamu wa swala; ikiwa waswaliji wako sawa katika masharti ya uimamu, hutangulizwa aliye mkubwa zaidi kiumri. Alitoa Muslim katika Sahih yake kutoka kwa Shu'bah, kutoka kwa Ismail bin Rajaa amesema: Nilimsikia Aus bin Dam’aj akisema: Nilimsikia Abu Mas'oud akisema: Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ alituambia:

يَؤُمُّ الْقَوْمَ أَقْرَؤُهُمْ لِكِتَابِ اللهِ، وَأَقْدَمُهُمْ قِرَاءَةً، فَإِنْ كَانَتْ قِرَاءَتُهُمْ سَوَاءً، فَلْيُطِعْهُمْ أَقْدَمُهُمْ هِجْرَةً، فَإِنْ كَانُوا فِي الْهِجْرَةِ سَوَاءً، فَلْيَؤُمَّهُمْ أَكْبَرُهُمْ سِنّاً، وَلَا تَؤُمَّنَّ الرَّجُلَ فِي أَهْلِهِ، وَلَا فِي سُلْطَانِهِ، وَلَا تَجْلِسْ عَلَى تَكْرِمَتِهِ فِي بَيْتِهِ إِلَّا أَنْ يَأْذَنَ لَكَ، أَوْ بِإِذْنِهِ "Atawaongoza watu (katika swala) yule anayeijua zaidi Kitabu cha Mwenyezi Mungu, na mwenye uzoefu zaidi wa kusoma. Ikiwa katika usomaji wako sawa, basi awaongoze aliyetangulia kuhiji (hijra). Ikiwa katika hijra wako sawa, basi awaongoze aliye mkubwa zaidi kiumri. Na usimuongoze mtu katika familia yake, wala katika mamlaka yake, wala usiketi kwenye heshima yake (kitanda chake au kiti chake) nyumbani kwake isipokuwa akikutolea idhini, au kwa idhini yake."

Hivyo basi, jambo la kiutawala lililopitishwa katika suala hili ni kumtanguliza msaidizi mkubwa zaidi kiumri kisha anayemfuatia, kisha waziri wa utendaji mkubwa zaidi kisha anayemfuatia, na kuendelea.] Mwisho wa nukuu kutoka katika jawabu la swali lililopita.

5- Kuhusiana na swali lako kuhusu kuharibika kwa sharti miongoni mwa masharti ya kufungwa kwa mkataba wa Khilafah baada ya bai’ah ya Khalifah kukamilika, kama vile kuharibika kwa sharti la uadilifu, basi jawabu la jumla kwa hilo ni kwamba kuharibika kwa sharti miongoni mwa masharti ya kufungwa mkataba haimaanishi kwa ulazima kubatilika kwa mkataba wa Khilafah mara moja. Kwa mfano, kuharibika kwa sharti la uadilifu kumemfanya Khalifah astahili kuondolewa lakini haondolewi moja kwa moja, bali lazima kuwe na uamuzi kutoka kwa Mahakama ya Malalamiko (Mahkamat al-Madhalim) katika hilo. Yaani Khilafah yake inabaki kuwa ipo hadi wakati wa uamuzi wa Mahakama ya Malalamiko kuhusu jambo lake... Na tumeeleza kwa kina suala hili katika maeneo zaidi ya mmoja katika vitabu vyetu, na tukalibainisha katika Muqaddimat ad-Dustur (Utangulizi wa Katiba) Juzuu ya Kwanza katika Vipengele vya (40+41) pamoja na ufafanuzi wake, na unaweza kurejea kwenye kitabu cha Al-Muqaddimah ili kufahamu undani wa hilo.

Mwishoni, ninakushukuru kwa dua yako kwetu, na nakuombea kheri, na ninarudia yale niliyoyataja mwanzoni mwa jawabu kuhusu furaha yangu kwa kuniandikia kwa lugha ya Qur’ani, Lugha ya Kiarabu.

Ndugu yenu Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah

26 Dhul-Hijjah 1441 AH Sawia na 16/08/2020 BK

Kiungo cha jawabu kutoka kwenye ukurasa wa Amir (Mwenyezi Mungu amuhifadhi) kwenye: Facebook

Share Article

Share this article with your network