Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

Jibu la Swali: Hadithi Ambazo Udhaifu Wake Unatofautiwa na Wataalamu wa Hadithi

November 06, 2016
5530

(Mfululizo wa majibu ya mwanazuoni mtukufu Ata Bin Khalil Abu al-Rashtah, Amir wa Hizb ut-Tahrir, kwa maswali ya wageni kwenye ukurasa wake wa Facebook "Fiqhi")

Jibu la Swali

Hadithi Ambazo Udhaifu Wake Unatofautiwa na Wataalamu wa Hadithi

Kwa Mahmoud Ahmed

Swali:

Assalamu Alaikum, mimi ni Mmisri na ni mara yangu ya kwanza kuingia kwenye tovuti yenu. Kuna baadhi ya mambo yananitatiza kutokana na taarifa nilizokuwa nazo awali, na nilipoingia kwenye majibu yenu kwa maswali ya watu, kumejitokeza utata fulani, hivyo naomba uvumilivu wenu katika hili na shukrani...

"Wala hakuna hadithi yoyote kati ya hizo mbili isiyokuwa na kasoro (maqal), na ndiyo maana baadhi ya wataalamu wa hadithi wameidhoofisha, lakini sisi tunaichukulia hadithi hiyo kuwa ni Hasan kwa sababu imetajwa katika vitabu vya mafuqaha na wameitumia katika kutoa hukumu (istinbat)". Sentensi hii ilitajwa katika jibu la Sheikh Abu al-Rashtah kuhusu hadithi ya 'Maswahaba wangu ni kama nyota', lakini ninachojua ni kwamba wataalamu wa hadithi ndio wanaohukumu hadithi, au inawezekana hadithi ikawa ni Swahih kwa Faqihi na ikawa ni Maudhu' (ya kutungwa) kwa mtaalamu wa hadithi kwa mfano... hili ndilo tatizo langu.

Jibu:

Wa Alaikum Salaam Wa Rahmatullahi Wa Barakatuh,

Inaonekana kuna mkanganyiko umekupata kuhusiana na jibu letu kuhusu hadithi ya "Maswahaba wangu ni kama nyota", ukadhani kuwa wataalamu wa hadithi wanaidhoofisha hadithi kisha mafuqaha wanaifanya kuwa ni Hasan, na jambo sivyo lilivyo. Ikiwa wataalamu wa hadithi wamekubaliana (ijmai) juu ya udhaifu wa hadithi, basi mafuqaha hawaifanyi kuwa ni Hasan.

Suala hili ndugu yangu, linahusu hadithi dhaifu ambayo watu wa hadithi wanatofautiana kuihusu; kuna miongoni mwao wanaoiona kuwa ni dhaifu na haitolewi ushahidi kwayo, na kuna miongoni mwao wanaoiona kuwa inafaa kutoa ushahidi kwayo. Hiyo ni kwa sababu kuna wapokezi ambao wanachukuliwa kuwa ni waaminifu (thiqah) kwa baadhi ya wataalamu wa hadithi, na wanachukuliwa kuwa si waaminifu kwa wengine, au wanachukuliwa kuwa hawajulikani (majhul) kwa baadhi ya wataalamu wa hadithi, na wanajulikana kwa wengine. Pia kuna hadithi ambazo hazikuwa sahihi kupitia njia moja lakini zikawa sahihi kupitia njia nyingine... Hivyo yule anayemuona mpokezi kuwa hajulikani katika silsila (sanad) ya hadithi anaichukulia kuwa ni dhaifu na haitolewi ushahidi kwayo, na yule anayemtambua huyo aliyekuwa hajulikani na akamuona kuwa ni mwaminifu, anaichukulia hadithi hiyo kuwa ni Hasan na kuitolea ushahidi... Na anayeona kuwa mmoja wa wapokezi katika silsila hakusikia kutoka kwa wale aliowapokea basi anaichukulia hadithi kuwa ni dhaifu kwa sababu kuna mkatiko (inqitaa), na yule anayethibitishiwa kuwa usikivu ulifanyika kulingana na kanuni basi hadithi kwake inakuwa ni Hasan na anaolea ushahidi...

Nitakutajia baadhi ya mifano ya tofauti za watu wa hadithi kulingana na nilivyobainisha hapo juu:

  • Kwa mfano: Abu Dawood, Ahmad, an-Nasa'i, Ibn Majah na at-Tirmidhi wamepokea kutoka kwa Abu Hurairah (ra) amesema:

سأل رجل رسول الله صلى الله عليه وسلم فقال يا رسول الله. إنا نركب البحر ونحمل معنا القليل من الماء فإن توضأنا به عطشنا أفنتوضأ بماء البحر؟ فقال: هو الطهور ماؤه الحل ميتته

"Mtu mmoja alimuuliza Mtume wa Allah (saw) akisema: 'Ewe Mtume wa Allah. Sisi tunasafiri baharini na tunabeba maji kidogo, ikiwa tutatawadha kwayo tutapata kiu, je, tuitawadhe kwa maji ya bahari?' Akasema: 'Maji yake ni safi na yenye kusafisha (twahuru), na nyama yake (ya mnyama aliyekufa humo) ni halali.'"

Hadithi hii, at-Tirmidhi amehadithia kutoka kwa al-Bukhari kuwa ni sahihi, na Ibn Abd al-Barr amehukumu kuwa ni sahihi kwa sababu ya wanazuoni kuipokea kwa kuikubali, na Ibn al-Mundhir ameifanya kuwa sahihi. Ibn al-Athir amesema katika sharh ya al-Musnad: "Hii ni hadithi sahihi mashuhuri iliyotolewa na maimamu katika vitabu vyao, na wameitumia kama hoja, na wapokezi wake ni waaminifu (thiqah)." Wakati ambapo ash-Shafi'i amesema katika isnad ya hadithi hii kuna mtu ambaye simfahamu. Na Ibn Daqiq al-Eid amezitaja sababu za kasoro (ilaal) ambazo hadithi hii inapewa, ikiwemo kutojulikana kwa Said bin Salama na al-Mughira bin Abi Burdah waliotajwa katika isnad yake. Wakati ambapo wapokezi hawa wawili, baadhi ya wataalamu wa hadithi wamesema kuwa wanajulikana. Abu Dawood amesema: "Al-Mughira anajulikana na an-Nasa'i amempa uaminifu (wathaaqah)." Al-Hafiz akasema: "Kutokana na hili imejulikana makosa ya yule aliyedai kuwa yeye ni majhul (hajulikani). Kuhusu Said bin Salama, amefuatwa (taaba’a) na Safwan bin Salim katika upokezi wake kutoka kwa al-Julah bin Kathir..."

  • Na mfano mwingine: Ahmad amepokea kutoka kwa Sa'd bin Abi Waqqas amesema:

سمعت النبي صلى الله عليه وسلم يسأل عن اشتراء التمر بالرطب فقال لمن حوله أينقص الرطب إذا يبس؟ قالوا نعم، فنهى عن ذلك

"Nilimsikia Mtume (saw) akiulizwa kuhusu kununua tende kavu kwa tende mbichi, akawauliza walio karibu naye: 'Je, tende mbichi hupungua uzito zikikauka?' Wakasema: 'Ndiyo', basi akakataza jambo hilo."

Hadithi hii imepewa usahihi na at-Tirmidhi, lakini kundi la wanazuoni limeipa kasoro, akiwemo at-Tahawi, at-Tabari, Ibn Hazm na Abdul Haq, kwa kuwa katika isnad yake kuna Zaid Abu Ayyash naye ni majhul. Imetajwa katika al-Talkhis na jibu ni kwamba al-Daraqutni amesema yeye ni thiqah thabat (yaani Zaid Abu Ayyash), na al-Mundhiri amesema: "Wamepokea kutoka kwake watu wawili waaminifu na Malik amemtegemea pamoja na ukali wake wa kukosoa..."

Aina hizi za hadithi ambazo udhaifu wake unajadiliwa ndizo ambazo hurejewa kutokana na matumizi ya mujtahidina kwazo au kuwepo kwa njia nyingine zinazoiunga mkono (mutaba'aat) na ushahidi mwingine (shawahid) kwa ajili ya kuiimarisha, hivyo inakuwa inafaa kwa ajili ya kutoa ushahidi. Pamoja na kujua kwamba si kila hadithi dhaifu hutafutiwa ushahidi na njia nyingine za kuiimarisha, au kutafutiwa matumizi ya mujtahidina, kwani kuna udhaifu ambao haushindi kwa chochote. Hii ni kwa sababu hadithi dhaifu imegawanyika katika sehemu mbili:

  • Sehemu ambayo haifanyiwi kazi, na haiimarishwi na ushahidi wowote wala njia nyingine.
  • Sehemu ambayo inaimarika kwa ushahidi na njia nyingine, na ikiwa imefanyiwa kazi na mujtahidina na mafuqaha wanaoaminika.

Imekuja katika kitabu chetu Ash-Shakhsiyyah al-Islamiyyah Juzuu ya Kwanza:

"...Ni makosa kusema kuwa hadithi dhaifu ikija kwa njia nyingi dhaifu inapanda kufikia daraja la Hasan au Swahih. Kwani ikiwa udhaifu wa hadithi ni kwa sababu ya ufuska wa mpokezi wake au kutuhumiwa kwake kwa uongo kikweli, kisha ikaja kwa njia nyingine za aina hii, basi udhaifu wake huongezeka juu ya udhaifu mwengine...".

Pia imekuja humo:

(Al-Hasan: Ni ile ambayo chanzo chake kimejulikana na watu wake wamekuwa mashuhuri na ndiyo tegemeo la hadithi nyingi, na ndiyo inayokubaliwa na wanazuoni wengi na kutumiwa na mafuqaha wote. Yaani isiwe katika isnad yake mtu anayetuhumiwa kwa uongo, wala isiwe hadithi shadh (isiyo ya kawaida). Nayo ni aina mbili: Moja: Hadithi ambayo wapokezi wake hawaishiwi na mtu ambaye hali yake haijulikani wazi (mastur) ambaye sifa zake hazijahakikishwa, isipokuwa yeye si mghafilika mwenye makosa mengi, wala hatuhumiwi kwa uongo. Na matini ya hadithi hiyo iwe imepokewa mfano wake kutoka upande mwingine, hivyo inatoka katika kuwa shadh au munkar...) Mwisho.

Aina hii asili yake ni dhaifu lakini kwa sababu ina ushahidi na ufuasi basi ilihesabiwa kuwa ni Hasan. Na kwa namna hii ndivyo wasemavyo watu wa hadithi. Imetajwa katika kitabu al-Muqaddimah cha Ibn al-Salah naye ni miongoni mwa wanazuoni mashuhuri katika elimu ya hadithi:

"- Si kila udhaifu katika hadithi huondoka kwa kuja kwake kupitia njia nyingi, bali hilo linatofautiana: ...Na miongoni mwa hayo ni udhaifu ambao hauondoki kwa namna hiyo, kwa sababu ya ukubwa wa udhaifu na kushindwa kwa hiki kiunganishi katika kurekebisha na kukabiliana nao. Na hilo ni kama udhaifu unaotokana na kuwa mpokezi anatuhumiwa kwa uongo, au kuwa hadithi ni shadh... Na miongoni mwake ni udhaifu ambao huondolewa na hilo kwa kuwa udhaifu wake unatokana na udhaifu wa hifadhi ya mpokezi wake, pamoja na yeye kuwa ni mtu wa ukweli na dini. Hivyo tunapoona alichopokea kimekuja kupitia njia nyingine, tunajua kuwa ni miongoni mwa alivyohifadhi, na hifadhi yake haikuvurugika katika hilo...

  • ...Ikanibainikia na kuwa wazi kwangu kuwa hadithi ya Hasan ni sehemu mbili: Moja: Hadithi ambayo wapokezi wa isnad yake hawaishiwi na mtu aliyesitiriwa (mastur) ambaye sifa zake hazijahakikishwa, isipokuwa yeye si mghafilika mwenye makosa mengi katika anayoyapokea, wala hatuhumiwi kwa uongo katika hadithi, yaani haikudhihirika kutoka kwake kukusudia uongo katika hadithi wala sababu nyingine ya ufuska. Na matini ya hadithi pamoja na hayo iwe imejulikana kwa kupokewa mfano wake au namna yake kutoka upande mwingine au zaidi hadi ikaimarika kwa kufuata (mutaba'ah) kwa yule aliyemfuata mpokezi wake kwa mfano wake, au kwa kile ilicho nacho cha ushahidi (shahid), nako ni kuwepo kwa hadithi nyingine kwa namna yake, hivyo inatoka kwa hilo kuwa shadh na munkar...)" Mwisho.

Nawe unaona kuwa hadithi hii ambayo katika asili yake ni dhaifu inahesabiwa kuwa ni Hasan ikiwa imepokewa namna yake kutoka upande mwingine au ikaimarishwa na mutaba'ah au ina shahid ...nk.

Kwa mujibu wa hayo, ikiwa inasemwa kuhusu hadithi kuwa ni dhaifu kwa baadhi ya wataalamu wa hadithi, basi hili halitoshi kuitupa pembeni na kutoitolea ushahidi, bali huchunguzwa sababu ya udhaifu wake; na je mujtahidina na mafuqaha wanaoaminika wameitumia? Na je ina ushahidi na njia nyingine zinazoimarisha au la? Na je watu wote wa hadithi wameidhoofisha? Au wametofautiana katika sababu ya udhaifu wake... Na kwa kusoma yote hayo, huamuliwa kuitolea ushahidi hadithi hiyo au kutokuitolea ushahidi, na kadhalika... Na kwa msingi huu, tuliichukua hadithi:

أَصْحَابِي كَالنُّجُومِ بِأَيِّهِمُ اقْتَدَيْتُمُ اهْتَدَيْتُمْ

"Maswahaba zangu ni kama nyota, yeyote miongoni mwao mtakayemfuata, mtaongoka."

Ambapo imebainika yafuatayo:

1- Hadithi hii imepokewa kwa zaidi ya isnad moja na katika kila moja kuna maoni (maqal), na yenye nguvu zaidi ni upokezi wa Jabir (ra) nayo ni:

Ametoa Abu Umar Yusuf al-Namari al-Qurtubi (aliyefariki: 463 H), katika kitabu chake Jami' Bayan al-Ilm wa Fadhlihi... amesema:

Ametuhadithia Ahmad bin Umar amesema: ametuhadithia Abdu bin Ahmad, ametuhadithia Ali bin Umar, ametuhadithia al-Qadhi Ahmad bin Kamil, ametuhadithia Abdullah bin Rauh, ametuhadithia Sallam bin Sulaym, ametuhadithia al-Harith bin Ghusain, kutoka kwa al-A'mash, kutoka kwa Abi Sufyan, kutoka kwa Jabir amesema: Mtume wa Allah (saw) amesema:

أَصْحَابِي كَالنُّجُومِ بِأَيِّهِمُ اقْتَدَيْتُمُ اهْتَدَيْتُمْ

"Maswahaba zangu ni kama nyota, yeyote miongoni mwao mtakayemfuata, mtaongoka."

Abu Umar akasema: "Isnad hii haisimami kama hoja; kwa sababu al-Harith bin Ghusain hajulikani (majhul)"...

Lakini Ibn Hazm alimtambua na akasema yeye ni Abu Wahb al-Thaqafi, na vivyo hivyo al-Bukhari alimtambua akamtaja katika al-Tarikh al-Kabir, na al-Hafiz Ibn Hajar al-Asqalani alimfuatilia katika al-Amali al-Mutlaqah akasema: "Ibn Hibban amemtaja katika al-Thiqat (waaminifu)... hivyo haisemwi kwake kuwa ni majhul..."

Hivyo basi, yule aliyemhesabu al-Harith bin Ghusain kuwa ni majhul kama alivyotaja Ibn Abd al-Barr, basi kwake hadithi ni dhaifu. Na yule anayemjua al-Harith bin Ghusain ni nani na akamuona ni miongoni mwa waaminifu kama alivyotaja Ibn Hibban, basi hadithi kwake inafaa kwa ajili ya kutoa ushahidi...

Na kuna mapingamizi mengine kati ya anayeidhoofisha hadithi na anayeifanya kuwa Hasan, na tunatosheka na tuliyoyataja hapo juu...

Kwa hiyo, hadithi hii haina makubaliano ya watu wa hadithi juu ya udhaifu wake. Ikiwa hadithi hii inapatikana kwa mujtahidina na mafuqaha wanaoaminika, basi inafaa kuitolea ushahidi, kwani haina makubaliano juu ya udhaifu wake kutoka kwa watu wa hadithi, na pia inafanyiwa kazi na mujtahidina na mafuqaha wanaoaminika, na kwa msingi huo inatolewa ushahidi kwa utulivu.

Na nitakutajia baadhi ya mujtahidina na mafuqaha wanaoaminika walioitolea ushahidi hadithi hii:

  • Muhammad bin Ahmad Shams al-Aimmah al-Sarakhsi (aliyefariki: 483 H) aliitolea ushahidi katika kitabu chake al-Mabsut katika mada ya ukadhi... Na aliitolea ushahidi Abu al-Abbas Shihab al-Din mashuhuri kama al-Qarafi (aliyefariki: 684 H) katika kitabu chake al-Dhakhirah wakati wa kutafiti misingi (usul) ya Malik... Na aliitolea ushahidi Abu al-Hasan Ali bin Muhammad mashuhuri kama al-Mawardi (aliyefariki: 450 H) katika kitabu chake al-Hawi al-Kabir wakati wa kutafiti kuhusu Maswahaba... Na aliitolea ushahidi Abu Muhammad Muwaffaq al-Din mashuhuri kama Ibn Qudamah al-Maqdisi (aliyefariki: 620 H) katika kitabu chake al-Mughni katika mlango wa "Sehemu ya Sita: Jazaa ya kile kilichokuwa mnyama katika mawindo mfano wake katika mifugo"...

Na kama unavyoona, hadithi hiyo inatumiwa na mujtahidina na mafuqaha wanaoaminika, kwa hivyo inahesabiwa kuwa ni Hasan.

Hivyo basi, suala hili linahusu hadithi ambayo wataalamu wa hadithi wanatofautiana katika kuidhoofisha na si katika hadithi ambayo wamekubaliana kuidhoofisha. Hiyo haizingatiwi kuwa imetajwa katika vitabu vya mujtahidina na mafuqaha wanaoaminika, hata tukijaalia kwa ajili ya mjadala tu kuwa ipo katika vitabu vyao, basi inabaki kuwa ni dhaifu. Na nasema "tukijaalia kwa ajili ya mjadala" kwa sababu mujtahidina na mafuqaha wanaoaminika hawatumii hadithi dhaifu ambayo imekubaliwa udhaifu wake...

Natumai suala hili limekuwa wazi kabisa kwa ndugu mkarimu.

Ndugu yenu Ata Bin Khalil Abu al-Rashtah

06 Safar 1438 H Muwafaka na 06/11/2016 M

Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir kwenye Facebook

Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir kwenye Google Plus

Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir kwenye Twitter

Kiungo cha jibu kutoka kwenye tovuti ya Amir

Share Article

Share this article with your network