(Mfululizo wa majibu ya mwanachuoni mkubwa Ata' bin Khalil Abu al-Rashtah, Ameer wa Hizb ut-Tahrir, kwa maswali ya wafuasi wa ukurasa wake wa Facebook "Fiqhi")
Jawabu la Swali Al-Illah ash-Shar'iyyah Kwa Eyad Dana
Swali:
Assalamu Alaikum wa Rahmatullahi wa Barakatuh. Tafadhali Sheikh, tusaidie kwa kujibu swali hili linalohusu al-illah ash-shar’iyyah; ni wapi inapojumuishwa katika hotuba ya Mpaji Sheria (khitab ash-shari’) inayofungamana na vitendo vya waja? Je, inaingia chini ya hotuba ya al-iqtida (takwa), al-wadh’ (hali), au at-takhyir (kuhitari)? Na kuna tofauti gani kati ya al-illah na as-sabab?
Jawabu:
Wa Alaikum Salam wa Rahmatullahi wa Barakatuh,
Hukm Shar’i inafasiriwa kama hotuba ya Mpaji Sheria inayofungamana na vitendo vya waja kwa njia ya al-iqtida, at-takhyir, au al-wadh’... Al-Iqtida ni takwa, nayo inajumuisha takwa la kufanya na takwa la kuacha. Inajumuisha takwa la lazima na takwa lisilo la lazima. Takwa la kufanya lililo la lazima ni al-fardh (faradhi), na takwa la kufanya lisilo la lazima ni al-mandub (sunna). Takwa la kuacha lililo la lazima ni al-haram (haramu), na takwa la kuacha lisilo la lazima ni al-makruh (makruhu). Hizi ni hukmu nne, na ya tano ni at-takhyir ambayo ni al-ibahah (mubah/halali). Hukmu hizi tano ndizo hukmu za utekelezaji (ahkam at-taklif)... Mkabili wake ni hukmu za hali (ahkam al-wadh’) nazo ni tano: as-sabab (sababu), ash-shart (sharti), al-mani’ (kizuizi), ar-rukhsah na al-’azimah (ruhusa na azimio), na as-sihhah, al-butlan na al-fasad (usihi, ubatili na uharibifu).
Kama unavyoona, al-illah haimo chini ya ufafanuzi wa hukm shar’i, si chini ya hukm shar’i at-taklifi wala chini ya hukm al-wadh’... kwani al-illah ni kama ushahidi (dalil) wa hukm shar’i. Kwa upande wa mpangilio, inakuja kabla ya hukm shar’i na hukmu hujengwa juu yake, yaani ni dalili na si hukmu tanzu... Hivyo basi, al-illah ni kichocheo au msukumo (al-ba'ith) wa hukmu. Ama as-sabab, yenyewe ni ishara na kitambulisho cha kuwepo kwa hukmu tu, si kingine. Kinachowajibisha hukmu ni dalili iliyokuja katika amri ya lazima, ama dalili ya sababu ndiyo ile inayobeba alama ya kutambua kuwepo kwa hukmu.
Kwa ufafanuzi zaidi tunasema: Al-Illah ni jambo linalochochea hukmu, yaani kichocheo cha utungaji sheria kwani hukmu imetungwa kwa ajili yake. Al-Illah ni dalili ya hukmu, alama yake, na kitambulisho chake, lakini pamoja na hayo, yenyewe ndiyo jambo linalosukuma kuwepo kwa hukmu, kwani ndiyo jambo ambalo hukmu imetungwa kwa ajili yake, na ndiyo maana inaitwa ma’qul an-nass (mantiki ya maandiko). Ikiwa andiko halina illah, basi litakuwa na mantuq (tamko la wazi) na mafhum (dhana iliyofahamika), lakini halitakuwa na ma’qul, hivyo jambo jingine haliwezi kuunganishwa nalo kabisa. Lakini ikiwa lina illah, kwa hukmu kuambatanishwa na sifa inayoeleweka, basi litakuwa na mantuq, mafhum, na ma’qul, hivyo jambo jingine linaweza kuunganishwa nalo. Kuwepo kwa illah kunafanya andiko lijumuishe aina nyingine na matukio mengine ya matukio si kupitia tamko lake wala dhana yake, bali kupitia njia ya muambatano (al-ilhaq) kutokana na ushirikiano wao katika illah iliyoelezwa. Al-Illah inaweza kuja ndani ya dalili ya hukmu, hivyo hukmu ikawa imeonyeshwa na hotuba na pia ikaonyeshwa na illah iliyomo ndani ya hotuba hiyo, kama kauli yake Mwenyezi Mungu (swt):
مَّا أَفَاءَ اللَّهُ عَلَىٰ رَسُولِهِ مِنْ أَهْلِ الْقُرَىٰ فَلِلَّهِ وَلِلرَّسُولِ وَلِذِي الْقُرْبَىٰ وَالْيَتَامَىٰ وَالْمَسَاكِينِ وَابْنِ السَّبِيلِ كَيْ لَا يَكُونَ دُولَةً بَيْنَ الْأَغْنِيَاءِ مِنكُمْ
"Mali aliyo mpa Mwenyezi Mungu Mtume wake kutoka kwa watu wa vijiji hivi, basi ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, na kwa ajili ya Mtume, na jamaa zake, na mayatima, na maskini, na msafiri, ili yasiwe yakizunguka baina ya matajiri tu miongoni mwenu." (Surah Al-Hashr [59]: 7)
Kisha akasema:
لِلْفُقَرَاءِ الْمُهَاجِرِينَ...
"Kwa ajili ya mafakiri walio hama..." (Surah Al-Hashr [59]: 8)
Aya hii imeonyesha hukmu ambayo ni kutoa mali ya fay-i kwa wahamiaji maskini. Kwa sababu hiyo, Mtume (saw) alitoa mali hiyo ambayo aya ilishuka kwa ajili yake - nayo ni mali ya Banu Nadhir - kwa Wahajiri pekee na hakutoa kwa Answar isipokuwa watu wawili tu waliokuwa na umasikini.
Pia illah iliyokuja katika aya ni kauli yake Mwenyezi Mungu (swt):
كَيْ لَا يَكُونَ دُولَةً بَيْنَ الْأَغْنِيَاءِ مِنْكُمْ
"Ili yasiwe yakizunguka baina ya matajiri tu miongoni mwenu." (Surah Al-Hashr [59]: 7)
Yaani ili mali isibaki mikononi mwa matajiri pekee bali ihamie kwa wengineo. Hivyo, aya imeonyesha hukmu na hiyo ndiyo iliyokuwa msukumo wa kutungwa kwake.
Ama as-sabab yenyewe ni: kila sifa ya dhahiri na thabiti ambayo dalili ya kusikia imeonyesha kuwa ni kitambulisho cha kuwepo kwa hukmu na si kwa ajili ya kutungwa kwa hukmu. Mfano wake: Kauli yake Mwenyezi Mungu (swt):
أَقِمِ الصَّلَاةَ لِدُلُوكِ الشَّمْسِ
"Shika Swala jua linapopinduka." (Surah Al-Isra [17]: 78)
Na kauli ya Mtume (saw):
إِذَا زَالَتِ الشَّمْسُ فَصَلُّوا
"Jua likipinduka, basi swalini." (Imepokelewa na Al-Bayhaqi)
Aya na hadithi hii zinabainisha kuwa kupinduka kwa jua ni alama ya utambulisho wa kuwepo kwa swala. Maana yake ni kwamba wakati huu ukipatikana, swala imepatikana, kwa maana ya kujuzu kuitekeleza ikiwa masharti mengine yametimia... Na hivi ndivyo ilivyo kwa sababu zote, kwa mfano, kauli yake Mwenyezi Mungu (swt):
فَمَنْ شَهِدَ مِنْكُمُ الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ
"Basi atakaye kuwa mjini katika mwezi huu na afunge." (Surah Al-Baqarah [2]: 185)
Na kauli ya Mtume (saw):
صُومُوا لِرُؤْيَتِهِ
"Fungeni kwa kuuona (mwezi)." (Imepokelewa na Al-Bukhari)
Inabainisha kuwa kuchomoza kwa mwezi mwandamo na kuonekana kwake ni alama ya kutambua kuwepo kwa funga katika Ramadhani...
Kutokana na hili, tofauti kati ya al-illah na as-sabab inabainika. Sababu (as-sabab) "ni alama ya kutambua kuwepo kwa hukmu, kama vile kupinduka kwa jua ni alama ya kutambua kuwepo kwa swala". Ama al-illah, yenyewe ni "msukumo wa kutungwa kwa hukmu, hivyo ndiyo sababu ya kutungwa kwake na si sababu ya kuwepo kwake. Yenyewe ni dalili miongoni mwa dalili za hukmu sawa na andiko (an-nass)." Hilo ni kama vile kushughulishwa hadi kuacha swala kulikostanbatishwa kutoka katika kauli yake Mwenyezi Mungu (swt):
إِذَا نُودِيَ لِلصَّلَاةِ مِنْ يَوْمِ الْجُمُعَةِ فَاسْعَوْا إِلَى ذِكْرِ اللَّهِ وَذَرُوا الْبَيْعَ
"Inapoadhiniwa kwa ajili ya Swala siku ya Ijumaa, nendeni upesi kwenye dhikri ya Mwenyezi Mungu na acheni biashara." (Surah Al-Jumu'ah [62]: 9)
Kwani kushughulishwa huko ndiko kulikofanya hukmu itungwe, ambayo ni haramu kufanya biashara wakati wa adhana ya Ijumaa. Kwa hivyo, hiyo ilikuwa ni illah na si sababu, kinyume na kupinduka kwa jua, kwani hiyo si illah kwa sababu swala ya Adhuhuri haikutungwa kwa ajili ya kupinduka kwa jua, bali kupinduka huko ni alama tu kwamba Adhuhuri imewajibika kuwepo.
Ndugu yenu, Ata' bin Khalil Abu al-Rashtah
13 Rajab 1437 H 20/04/2016 M
Kiungo cha jawabu kutoka kwa ukurasa wa Facebook wa Ameer:
![]()
Kiungo cha jawabu kutoka kwa ukurasa wa Google Plus wa Ameer:
![]()
Kiungo cha jawabu kutoka kwa ukurasa wa Twitter wa Ameer:
![]()
Kiungo cha jawabu kutoka tovuti ya Ameer