Mfululizo wa majibu ya mwanachuoni mtukufu Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah, Amir wa Hizb ut-Tahrir, kwa maswali ya wafuasi wa ukurasa wake wa Facebook "Fiqhi"
Jibu la Swali
Kujiunga na Muungano wa Kitaaluma (Syndicate) ili kuweza kufanya kazi
Kwa Abdullah M Alheeh
Swali:
Assalamu Alaikum wa Rahmatullahi wa Barakatuh... Amani iwe juu yenu ndugu zetu na rehema za Allah na baraka zake... Amani iwe juu yako Amir wetu na rehema kutoka kwa Allah na taufiki kutoka kwake kwako na kwa walio pamoja nawe... Baada ya hayo:
Nina swali, ikiwa mtafanya ihsani kunijibu kwa haraka kutokana na ulazima wake.
Mimi ni mtaalamu wa vipimo vya kitabibu (medical lab analysis) na ili kupata idhini ya kufanya kazi, ninalazimika kufuata baadhi ya mambo na sheria; baadhi yake yanakubalika na mengine yanataliwa, huku ndani yangu kukiwa kumejengeka ushawishi wa uharamu wa kushiriki katika mambo hayo (nikimaanisha baadhi ya sheria na mambo ambayo ni lazima niyafanye ili niwe mwanachama katika muungano wa kitaaluma wa maabara za tiba "Palestine"). Swali langu ni kuhusu mfumo wa dhamana ya kijamii (social solidarity) uliopo katika miungano hiyo. Kwani muungano wangu kila anapofariki mwanachama, hukusanya kiasi cha angalau dinari kumi ili kulipwa familia ya mwanachama huyo aliyefariki. Ambapo muungano huwalazimisha watu walioshindwa kulipa kwa kuwataka walipe kiasi hicho, vinginevyo uanachama wao hautahuishwa, ambao huhuishwa kila mwaka. Ikumbukwe kuwa wamewaambia wanachama kwamba wamepata fatwa kuhusiana na jambo hili inayohalalisha mchakato huu na kwamba hakuna uharamu ndani yake. Tafadhali nijibu kwa haraka na jibu liambatane na dalili. Shukrani.
Jibu:
Wa Alaikum Salam wa Rahmatullahi wa Barakatuh,
Hizb ilishatoa jibu la swali mwanzoni mwa miaka ya sabini kuhusu kutofaa kujiunga na miungano ya kitaaluma (syndicates).
Hata hivyo, ikiwa sheria za nchi haziruhusu wenye taaluma kufanya kazi katika fani zao isipokuwa kwa kujiunga na miungano yao ya kitaaluma, basi kujiunga na muungano katika hali hii ni sawa na kuchukua leseni ya kazi, kama vile mfanyabiashara anavyochukua leseni ya kufungua duka lake... n.k. Na kuchukua leseni inajuzu ikiwa sheria za nchi zinalazimisha hivyo.
Kwa hiyo, inajuzu kujiunga na muungano katika hali hii, yaani kwa ajili ya kuruhusiwa kufanya kazi katika taaluma yake, kwa sharti kwamba kujiunga kwake kuishie tu katika kupata karatasi ya usajili na uanachama, bila kushiriki katika mikutano yake au uchaguzi wake...
Pamoja na hayo, mwingiliano (tafau'l) katika mazingira ya muungano kupitia mawasiliano hai na yenye athari, na kujenga uhusiano wenye tija na mabaraza yake pamoja na wanachama wake hata kama mwanachama wa Hizb (shabab) si mwanachama wa miungano hiyo... yote hayo yanaingia katika mlango wa mawasiliano ya kawaida, bali ni muhimu, ambayo ni lazima kwa shabab kuyafanya kwa juhudi na bidii.
Na kwa kutegemea yaliyotangulia... na kwa kuwa kutoa kiasi hiki kwa hiyari ni mubah (inaruhusiwa) kiasili, na tatizo liko tu katika ulazima kwa mujibu wa sheria ya muungano...
Ikiwa kuendelea kwako katika kazi yako kunategemea kujiunga na muungano na hili linapelekea kulipa kiasi hicho cha dhamana (takaful), na usipofanya hivyo uanachama wako hautahuishwa na hivyo huwezi kufanya kazi katika taaluma yako...
Ikiwa hali ni hiyo, basi inajuzu kwako kukilipa kwa sababu ni miongoni mwa mahitaji ya leseni ya kazi.
Ndugu yenu, Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah
24 Jamada al-Ula 1438 H Sawia na 21/02/2017 M
Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir kwenye Facebook
Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir kwenye Google Plus
Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir kwenye Twitter
Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir Web