(Mfululizo wa majibu ya mwanachuoni Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah, Amir wa Hizb ut Tahrir, kwa maswali ya wafuasi wake kwenye ukurasa wake wa Facebook)
Kwa: Hafedh Amdouni
Swali:
Assalamu Alaikum wa Rahmatullahi wa Barakatuh. Mwenyezi Mungu akufanikishe wewe na wabeba neno hili lenye kubaki kwa idhini Yake katika kile Anachokipenda na kukiridhia.
Kuna wanaosema kuwa hoja ya Hizb na baadhi ya mafakihi (wanasheria) kwamba kucheleweshwa kuzikwa kwa Mtume wa uongofu (saw) ni dalili ya uwajibikaji wa Bay’ah si sahihi, bali ilikuwa ni kwa sababu nyingine kama kuwapa Waislamu muda wa kuhudhuria mazishi na kadhalika. Badala yake, wanasema dalili ni kwamba mara tu baada ya kifo chake (saw), walisimama kumsimika Imamu na hii ndiyo dalili ya uwajibikaji wa Bay’ah na si kuchelewa kuzikwa. Kwamba hakuna uhusiano kati ya kuchelewa huko na Bay’ah!! Je, unaweza kutufafanulia hilo kwa kina?
Jibu:
Wa Alaikum Salaam wa Rahmatullahi wa Barakatuh.
Ndugu yangu, kabla ya kukujibu kuhusu kuchelewa kuzikwa... nakutajia baadhi ya mambo ya Usul kuhusu hukumu za kisheria:
Asili katika amri ya kisheria, iwe ni kauli au kitendo, ni kwamba inafahamisha takwa (itishao) na inahitaji qarinah (dalili/kiashiria) inayobainisha aina ya takwa hilo. Ikiwa qarinah hiyo inafahamisha mkazo (jazm), basi takwa hilo ni la mkazo, yaani ni Faradhi. Ikiwa qarinah haifahamishi mkazo lakini inafahamisha kupendelewa kwa kheri ndani yake, basi takwa hilo si la mkazo, yaani ni Mandub (sunnah). Na ikiwa qarinah inafahamisha hiyari, basi takwa hilo ni kwa ajili ya uhalali (Mubah).
Hii inatumika kwa kila andiko la kisheria, iwe ni andiko la "kauli" katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu (swt) au katika Sunnah ya Mtume Wake (saw), au iwe ni kitendo cha Mtume (saw), au kitendo ambacho Maswahaba (ra) waliafikiana nacho (Ijmai), au idhini (Iqrar) kutoka kwa Mtume (saw)...:
1- Kwa mfano: Kauli ya Mwenyezi Mungu (swt):
فَإِذَا قُضِيَتِ الصَّلَاةُ فَانْتَشِرُوا فِي الْأَرْضِ وَابْتَغُوا مِنْ فَضْلِ اللَّهِ وَاذْكُرُوا اللَّهَ كَثِيرًا لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ
"Na itakapokwisha Swala, tawanyikeni katika ardhi na mtafute fadhila za Mwenyezi Mungu, na mkumbukeni Mwenyezi Mungu kwa wingi ili mpate kufanikiwa." (QS. Al-Jumu'ah [62]: 10)
Hapa kuna amri "tawanyikeni", yaani takwa la kutoka msikitini baada ya Swala ya Ijumaa. Tunatafuta qarinah ili tuone ikiwa kutawanyika, yaani kutoka msikitini baada ya kumalizika Swala, ni faradhi, mandub, au mubah... Tunakuta kwamba Waislamu walikuwa baada ya kumalizika Swala ya Ijumaa, wapo miongoni mwao waliokuwa wakitoka mara moja na wapo waliokuwa wakiketi kidogo au sana... Na hilo lilikuwa kwa idhini ya Mtume (saw)... Yaani yule anayetoka au anayeketi ni mamoja, na hii inafahamisha kuwa "tawanyikeni" ni amri inayofahamisha takwa la uhalali (Mubah).
2- Na kwa mfano: Kusimama kwa ajili ya jeneza:
Al-Nasa'i ametoa katika Sunan yake: Alituambia Shu’bah, kutoka kwa Abdullah bin Abi Al-Safar, akasema: Nilimshikia Al-Sha'bi akihadithia kutoka kwa Abu Said, "Kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) walimpitia na jeneza naye akasimama." Na Amr akasema: "Kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) lilimpitia jeneza naye akasimama." Hapa Mtume (saw) alisimama kwa ajili ya jeneza lililompita, na kitendo hiki kinafahamisha takwa la kusimama. Kisha tunatafuta qarinah ili kujua ikiwa takwa hili ni la mkazo (faradhi), au si la mkazo lenye kupendelewa (mandub), au ni la hiyari (mubah). Tunakuta katika Sunan al-Nasa’i kutoka kwa Ayyub, kutoka kwa Muhammad, kwamba jeneza lilimpitia Al-Hasan bin Ali na Ibn Abbas, Al-Hasan akasimama na Ibn Abbas hakusimama, Al-Hasan akasema: "Je, si Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) alisimama kwa ajili ya jeneza la Myahudi?" Ibn Abbas akasema: "Ndiyo, kisha aliketi (saw)." Hii inafahamisha kuwa kuketi na kusimama ni kwa hiyari, yaani ni kwa uhalali (Mubah).
Vivyo hivyo Bay’ah katika Saqifah, ni kitendo ambacho Maswahaba waliafikiana nacho (Ijmai), hivyo kinafahamisha takwa la kutoa Bay’ah kwa Khalifa ikiwa nafasi ya Khilafah iko wazi. Na ili kuamua ikiwa takwa hili ni faradhi, mandub, au mubah, tunatafuta qarinah. Tunakuta inafahamisha mkazo kwa sababu Maswahaba walitanguliza Bay’ah kabla ya kumzika maiti hali ya kuwa kuzika ni faradhi. Hii inamaanisha kuwa Bay’ah ni faradhi na ni muhimu zaidi kuliko faradhi ya kumzika maiti.
Kwa sababu hiyo, dalili ya kwamba kutoa Bay’ah kwa Khalifa ikiwa nafasi iko wazi ni faradhi, dalili ya hilo ni kucheleweshwa kuzikwa kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) mpaka Bay’ah ilipokamilika. Na kwa kuwa kumzika maiti ni faradhi, basi kile kilichofanywa kuwa kipaumbele zaidi kuliko hicho (mazishi) pia ni faradhi.
Hivyo basi, kuchelewa kuzikwa mpaka Bay’ah ilipokamilika, ndiko kulikobainisha kuwa Bay’ah ya Khalifa ni wajibu na faradhi, na ni faradhi kubwa mno.
Huu ni upande wa kifakihi.
Ama kusema kuwa kuchelewa kuzikwa hakuna uhusiano na Bay’ah, bali ni kuwapa Waislamu muda wa kuhudhuria mazishi, hili ni jambo lililo mbali na ukweli uliotokea. Habari za kifo cha Mtume (saw) zilikuwa ni tukio kubwa lililosikiwa na Waislamu mjini Madina na vitongoji vyake, na Waislamu walimiminika Madina na msikitini lakini walishughulika na Bay’ah ya Abu Bakr kwa ajili ya mkataba (In’iqad) na utiifu (Ta’ah)... Na huu hapa ni mtiririko wa matukio kama yalivyoingia katika vitabu vya historia (Siyar):
Mtume (saw) alifariki mchana wa Jumatatu, na akabaki bila kuzikwa usiku wa Jumanne na mchana wa Jumanne ambapo Abu Bakr (ra) alipewa Bay’ah. Kisha Mtume (saw) akazikwa usiku wa manane, kuamkia Jumatano. Abu Bakr alipewa Bay’ah kabla ya kuzikwa Mtume (saw). Hilo lilikuwa ni Ijmai (mwafaka) wa kujishughulisha na kumsimika Khalifa badala ya kumzika maiti, na hilo haliwezi kuwa isipokuwa ikiwa kumsimika Khalifa ni wajibu zaidi kuliko kumzika maiti.
Kwa hivyo, kuchelewa kuzikwa haikuwa ili Waislamu wakusanyike kwa ajili ya jeneza, kwani walikuwa tayari wamekusanyika na hususan Maswahaba, lakini walijishughulisha na Bay’ah. Walipomaliza (Bay’ah ya) mkataba na utiifu, walishughulika na kumzika Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw). Na ni lini? Ni usiku wa manane baada ya kumaliza Bay’ah. Ikiwa kuchelewa huko kungekuwa kwa ajili ya kukusanyika watu kwa ajili ya jeneza, basi ingekuwa mchana wa Jumatatu, au usiku wa Jumanne, au mchana wa Jumanne... Lakini walisubiri kukamilika kwa Bay’ah ya Abu Bakr kwa ajili ya mkataba na utiifu, na baada ya kumalizika, walifanya haraka mara moja kushughulika na kumzika Mtume (saw) usiku wa Jumatano.
Kwa hiyo, kwa kutafakari na kuzingatia kuchelewa kuzikwa, inabainika kuwa haikuwa kwa sababu nyingine yoyote isipokuwa sababu ya kumaliza Bay’ah ya Abu Bakr kwa ajili ya mkataba na utiifu. Hivyo basi, hilo ni sehemu ya msingi ya uhusiano na Bay’ah.
Ndugu yenu Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah
Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir kwenye Facebook
Kiungo cha jibu kutoka kwenye tovuti ya Amir
Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir kwenye Google Plus