Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

Jawabu la Swali: Ardhi za Makazi Hazina Kharaj

September 05, 2015
4206

(Sfululizo wa majibu ya mwanachuoni mtukufu Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah, Amir wa Hizb ut-Tahrir, kwa maswali ya wafuasi wa ukurasa wake wa Facebook "Fiqhi")

Kwa Bader Ajrab

Swali:

Sheikh wetu mpendwa, mwanachuoni Ata Al-Khair, Assalamu Alaikum Wa Rahmatullahi Wa Barakatuh...

Imekuja katika kitabu cha An-Nidham al-Iqtisadi (Mfumo wa Kiuchumi) ukurasa wa 129: "Ama kharaj juu ya ardhi, ni kile ambacho dola huchukua kutoka kwa mmiliki wa ardhi kwa kiasi maalumu inachokikadiria na kukibainisha kulingana na uzalishaji wa ardhi unaokadiriwa kwa kawaida, si uzalishaji halisi. Na ardhi hukadiriwa kulingana na uwezo wake ili asidhulumiwe mmiliki wa ardhi wala Bayt al-Mal. Na kharaj huchukuliwa kila mwaka kutoka kwa mmiliki wa ardhi, iwe ardhi imelimwa au haijulimwa, na iwe imetoa mazao au imekuwa kame." Na swali langu ni: Je, kharaj huondoka ikiwa jengo limejengwa juu ya ardhi ya kharaj, au mmiliki wake hulipa kharaj bila kujali kama ardhi ni ya kilimo au la?

Na Mwenyezi Mungu akubariki, aongoze shabaha yako, na ajaalie ushindi upatikane kupitia mikono yako.

Ndugu yako anayekupenda, Bader Al-Ajrab.

Jibu:

Wa Alaikum Salaam Wa Rahmatullahi Wa Barakatuh.

Nitakutajia hapa chini baadhi ya mambo yanayohusiana na suala hili:

1- Hakika ardhi ya kharaj ina maana kwamba mmiliki wake anamiliki manufaa yake (manfa'ah) bila kumiliki asili yake (raqabah) na hulipa kharaj juu yake. Nayo hurithiwa kama ardhi ya ushriya, isipokuwa kinachorithiwa katika ardhi ya kharaj ni manufaa yake ya kudumu pekee, na asili yake hairithiwi kwani ni milki ya Waislamu wote. Ama manufaa yake, Umar bin al-Khattab aliwaachia wamiliki wake milki ya manufaa ya kudumu hadi mwisho wa zama. Na manufaa yanamilikiwa na kurithiwa, na mmiliki wa manufaa ana haki ya kuifanyia kila aina ya tasarrufu (matumizi), kuanzia kuuza, kuweka rehani, kutoa zawadi, wasia na tasarrufu nyinginezo.

2- Hakika kile kinachowajibika juu ya ardhi kinabaki hadi mwisho wa zama, bila kujali aina ya mmiliki wa ardhi na hata kama wamiliki watabadilika. Hii ni kwa sababu sifa yake ya kuwa imefunguliwa kwa nguvu (anwa), inabaki hadi mwisho wa zama na haibadiliki. Na kuhamia kwa milki ya manufaa kutoka kwa kafiri kwenda kwa Mwislamu hakubadilishi sifa hii. Kadhalika, hakubadilishi kharaj iliyowajibishwa juu yake, kwa sababu kharaj imefungamanishwa na ardhi iliyofunguliwa ambayo watu wake waliachiwa kuimiliki, na haijafungamanishwa na mmiliki.

3- Na anayemiliki manufaa ya ardhi ana haki ya kuuza manufaa haya na kuchukua thamani yake, kwani manufaa yanauzwa na yanastahiki thamani yake. Na hakuna yeyote anayemiliki haki ya kuinyakua kutoka kwa mmiliki wake, hata kama ni Khalifa wa Waislamu. Abu Yusuf amesema:

أَيُّمَا أَرْضٍ افْتَتَحَهَا الْإِمَامُ عَنْوَةً وَلَمْ يَرَ قِسْمَتَهَا، وَرَأَى الصَّلَاحَ فِي إِقْرَارِهَا فِي أَيْدِي أَهْلِهَا، كَمَا فَعَلَ عُمَرُ بْنُ الْخَطَّابِ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ فِي السَّوَادِ، فَلَهُ ذَلِكَ، وَهِيَ أَرْضُ خَرَاجٍ، وَلَيْسَ لَهُ أَنْ يَأْخُذَهَا بَعْدَ ذَلِكَ مِنْهُمْ، وَهِيَ مِلْكٌ لَهُمْ يَتَوَارَثُونَهَا، وَيَتَبَايَعُونَهَا وَيَضَعُ عَلَيْهِمْ الْخَرَاجَ

"Ardhi yoyote ambayo Imam ameifungua kwa nguvu (anwa) na hakuona haja ya kuigawanya, na akaona heri kuiacha mikononi mwa watu wake, kama alivyofanya Umar bin al-Khattab (ra) katika ardhi ya Sawad, basi anayo haki hiyo, na hiyo ni ardhi ya kharaj, na haruhusiwi kuichukua kutoka kwao baada ya hapo, nayo ni milki yao wanayoitharithi, wanauziana na kununuliana, na anaiwekea kharaj."

Na kwa msingi huo, ikiwa dola inahitaji kuchukua ardhi miongoni mwa ardhi za kharaj kwa ajili ya maslahi ambayo Waislamu hawawezi kuyaacha, basi ni wajibu wake kumlipa mmiliki wa ardhi thamani ya milki yake ya manufaa ya ardhi hiyo iliyochukuliwa, na si thamani ya asili yake (raqabah). Hii ni kwa sababu mmiliki wa ardhi ya kharaj anamiliki manufaa ya ardhi pekee na si asili yake, kwani asili yake inamilikiwa na Waislamu. Hivyo basi, ni lazima imlipe thamani ya kile anachokimiliki, nacho ni manufaa yawe makubwa au madogo. Na isitosheke tu na kulipa thamani ya kile kilichojengwa juu yake kama majengo au miti, kwani kufanya hivyo kunachukuliwa kuwa ni unyakuzi wa haki anayoimiliki. Kwani yeye anamiliki majengo au miti iliyopandwa juu yake, na anamiliki uwezo wa uzalishaji uliomo, na manufaa ya kudumu katika ardhi. Hivyo basi, ni lazima ikadiriwe thamani ya yote hayo, hasa kwa kuzingatia kuwa huenda mmiliki wa ardhi aliinunua kwa makumi ya maelfu, wakati majengo au miti iliyopo haifikii hata thamani ya maelfu kumi. Kwa hivyo, kutosheka na kulipa thamani ya jengo na miti pekee ni dhuluma kwake na ni kupoteza haki yake. Na ikiwa dola haitalipa thamani ya manufaa yote yaliyomo katika ardhi yake, itakuwa ni mnyakuzi, na hiyo ni kama manufaa mengine yoyote yanapouzwa, ni lazima thamani yake ilipwe kikamilifu.

4- Hii ni ikiwa ardhi ya kharaj imetayarishwa kwa ajili ya kilimo. Ama ardhi za makazi katika nchi zilizofunguliwa, hakika hukumu yake ni tofauti na hukumu za ardhi za kilimo. Hakika ardhi za makazi hazina kharaj juu yake, na asili yake pamoja na manufaa yake yanamilikiwa. Na hili ni kwa ijmai ya Maswahaba. Waislamu walipofungua Iraq, walijenga miji ya Kufa na Basra, na wakazigawanya baina yao, na zikawa milki yao; wakimiliki asili yake na manufaa yake katika zama za Umar bin al-Khattab kwa idhini yake. Na wakakaa ndani yake Maswahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw). Kadhalika kule Sham, Misri na nchi nyinginezo zilizofunguliwa; na hawakulipa kharaj kwa chochote katika hizo. Na zilikuwa zikiuzwa na kununuliwa kama milki nyingine yoyote. Vilevile, hakuna zaka juu yake, isipokuwa ikiwa zimefanywa kuwa bidhaa za biashara, kwani hapo hutolewa zaka kama zaka ya bidhaa za biashara.

Muhtasari ni kwamba kharaj hulipwa kwenye ardhi ya kilimo ya kharaj. Ama ardhi ya makazi katika ardhi ya kharaj, hailipwi kharaj juu yake, na umiliki wake unajumuisha manufaa na asili (raqabah), yaani umiliki kamili, na si umiliki wa ardhi ya kharaj pekee.

Wassalamu Alaikum Wa Rahmatullahi Wa Barakatuh

Ndugu yenu, Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah

Link ya jibu kutoka kwa ukurasa wa Amir kwenye Facebook

Link ya jibu kutoka kwa tovuti ya Amir

Link ya jibu kutoka kwa ukurasa wa Amir kwenye Google Plus

Share Article

Share this article with your network