Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

Jibu la Swali: Milki ya Biashara (Al-Asl al-Tijari) na Jinsi ya Kukabiliana Nayo

March 12, 2022
4523

Mfululizo wa Majibu ya Mwanachuoni Mkubwa Ata bin Khalil Abu al-Rashtah, Ameer wa Hizb ut-Tahrir, kwa Maswali ya Wageni wa Ukurasa wake wa Facebook "Fiqhi"

Jibu la Swali

Milki ya Biashara (Al-Asl al-Tijari) na Jinsi ya Kukabiliana Nayo

Kwa: Najmeddine Khcharem

Swali:

Bismillahir Rahmanir Rahim

Sheikh wetu mtukufu, Assalamu Alaikum Warahmatullahi Wabarakatuh,

Ningependa kuuliza kuhusu hukumu ya muamala unaofanyika hapa kwetu Tunisia, ambao umekuwa desturi nchi nzima na pia kisheria.

Ambapo mtu hukodisha duka kwa ajili ya biashara, na baada ya miaka mingi kupita, mwenye duka hawezi kulirudisha duka lake isipokuwa kwa kutoa malipo ya kifedha, na wakati mwingine hukadiriwa kuwa kiasi kikubwa cha pesa. Kadhalika, mpangaji anaweza kutoa kile kinachoitwa hapa kwetu (Al-Asl al-Tijari - Milki ya Biashara) kwa ajili ya kuuzwa kwa mpangaji mwingine, na mwenye duka hawezi kuzuia hilo isipokuwa amlipe yeye fidia ya hiyo milki ya biashara. Ikumbukwe kwamba mpangaji anaweza kupata hasara ikiwa mwenye duka atamtoa.

Barakallahu fika, na Allah aharakishe kusimama kwa Khilafah ya pili ya Rashidah kwa njia ya Utume.

Jibu:

Wa Alaikum Salaam Warahmatullahi Wabarakatuh,

Kwanza: Ili kujibu swali hili, ni lazima kwanza tuweke wazi misingi ifuatayo:

  1. Upangaji (Ijarah) ni mkataba wa manufaa kwa badala (malipo). Kwa upande wa upangaji wa vitu kama nyumba za kuishi na maduka ya biashara na mfano wake, ni mkataba wa manufaa ya kuishi au kutumia duka la biashara... n.k., mkabala na malipo anayotoa mpangaji kwa mwenye nyumba (mkodishaji). Mkataba wa upangaji ukikamilika kulingana na hukumu za Sharia, basi manufaa ya kitu kilichokodishwa yanakuwa milki ya mpangaji kwa muda wa upangaji, na mpangaji ana haki ya kuyatumia kwa mujibu wa Sharia.

  2. Mkataba wa upangaji ni mkataba wa lazima (aqd lazim), yaani hakuna upande mmoja wa mkataba (mkodishaji au mpangaji) unaoweza kuvunja mkataba na kuufuta isipokuwa kwa ridhaa ya upande mwingine. Haifai kwa mkodishaji wala mpangaji kujiamulia peke yake kusitisha mkataba wa upangaji kabla ya muda wake kwisha.

  3. Mkataba wa upangaji ni mkataba wa muda maalumu. Ni lazima kuainisha muda wa upangaji kwa siku, mwezi, mwaka... n.k. Haifai kwa upangaji kuwa wa kiholela bila kuainisha muda maalumu unaojulikana.

  4. Mkataba wa upangaji ukimalizika na usijididishwe kati ya mkodishaji na mpangaji, basi mpangaji ni lazima arudishe kitu alichokodisha kwa mmiliki wake (mkodishaji). Hii ni kwa sababu mkataba wa upangaji hauondoi milki ya kitu kutoka kwa mkodishaji, bali unaondoa tu manufaa ya kitu hicho kutoka kwa mkodishaji na kuifanya iwe ya mpangaji kwa muda wa mkataba. Hivyo, mkataba wa upangaji ukimalizika, ni wajibu kwa mpangaji kurudisha kitu alichokodisha pamoja na manufaa yake kwa mmiliki wake, yaani kwa mkodishaji.

Pili: Kulingana na mambo yaliyotajwa katika kipengele kilichotangulia, jibu la swali lako ni kama ifuatavyo:

  1. Ikiwa muda wa mkataba wa upangaji haujamalizika bado na mpangaji anataka kumkodisha mwingine hicho kitu alichokodisha (ambacho ni duka katika swali hili), anayo haki hiyo bila kuhitaji idhini ya mkodishaji wa asili. Hii ni kwa sababu manufaa ya kitu hicho ni mali ya mpangaji, hivyo anaweza kuitumia mwenyewe au kumkodishia mwingine, iwe kwa kiasi cha kodi alicholipa kwa mkodishaji wa kwanza, au pungufu, au zaidi. Hii ni kwa sababu manufaa ya hicho kitu ni mali ya mpangaji wa kwanza, hivyo ana haki ya kuyatumia kwa njia za kisheria anazoona zinafaa... Imetajwa katika kitabu cha Ash-Shakhsiyyah al-Islamiyyah, Juzuu ya Pili, mlango wa "Kukodisha Vitu" yafuatayo:

"Ikiwa mkataba utahusu manufaa ya vitu kama kukodisha nyumba, wanyama, magari na mfano wake, basi kilichofanyiwa mkataba kinakuwa ni manufaa ya kitu hicho. Itakuwa ni lazima kukadiria kodi ya mfano (ajr al-mithl) kwa kuangalia kitu ambacho manufaa yake yanalingana na manufaa ya kilichokodishwa. Pindi kukodisha kitu kunapokamilika, mpangaji anakuwa na haki ya kupata manufaa ya hicho kitu alichokodisha; akipanga nyumba, ana haki ya kuishi ndani yake, au mnyama au gari, ana haki ya kulipanda. Mpangaji anaruhusiwa kukodisha kitu alichokodisha ikiwa amekikabidhi kwa kiasi kile kile alichokipangia au zaidi au pungufu, kwa sababu kukabidhiwa kitu kilichokodishwa kunachukua nafasi ya kukabidhiwa manufaa yake, kwa ushahidi kwamba inajuzu kukitumia, hivyo inajuzu kukifanyia mkataba. Na kwa sababu ni mkataba unaojuzu kwa rasilimali (bei ile ile), basi unajuzu kwa ziada au upungufu. Isipokuwa tu kwamba ikiwa amekodisha kitu kwa ajili ya manufaa fulani, ana haki ya kupata manufaa ya aina hiyo, au yale yaliyo chini yake katika madhara, na hana haki ya kupata manufaa zaidi ya mfano wa manufaa hayo, kwa sababu haijuzu kwake kuchukua zaidi ya haki yake au kitu ambacho hastahiki. Ikiwa amekodisha mnyama kwa ajili ya kumpanda, haijuzu kwake kumtwisha mzigo kwa sababu mpandaji ni mwepesi kuliko mzigo. Na ikiwa amekodisha gari kwa umbali fulani, haijuzu kwake kuliendesha kwa umbali mrefu zaidi ya ule aliokodisha. Na ikiwa amepanga nyumba kwa ajili ya kuishi, hana haki ya kuifanya ghala ya mbao au chuma au mfano wake, miongoni mwa vitu vyenye madhara zaidi kwa nyumba kuliko kuishi. Hitimisho ni kwamba mkataba ikiwa unahusu kitu chenyewe kwa malipo, basi huo ni uuzaji (bai'), na ikiwa unahusu manufaa ya kitu kwa malipo, basi hiyo ni upangaji (ijarah). Kwa msingi huu, mkataba unaweza kuhusu kitu pekee, kama kuuza mti wenye matunda yaliyoanza kuiva bila kuuza matunda yake. Na unaweza kuhusu kitu pamoja na manufaa yake kama kuuza nyumba. Na unaweza kuhusu matunda pekee kama kuuza matunda yaliyoanza kuiva. Na unaweza kuhusu manufaa yasiyoshikika kama kuishi kwenye nyumba. Ikiwa mkataba unahusu manufaa ambayo hayachukuliwi kama kitu (bidhaa), basi hiyo ni upangaji na si uuzaji. Na kama vile mnunuzi wa kitu anavyomiliki kitu hicho na kukitumia kwa namna zote, vivyo hivyo mpangaji anamiliki manufaa aliyoyapata kwa kupanga, na ana haki ya kuyatumia kwa namna zote. Kama vile mnunuzi wa matunda ya mti yaliyoanza kuiva anavyoweza kuyauza yakiwa mtini, vivyo hivyo mpangaji wa kitu anaweza kukikodisha kwa sababu anamiliki manufaa yake kama vile mnunuzi wa matunda anavyomiliki yale matunda aliyonunua. Hivyo basi, inajuzu kwa mpangaji kukodisha kitu alichokodisha ikiwa amekipokea, kwa sababu kupokea kitu wakati wa kukodisha kunachukua nafasi ya kupokea manufaa, kwa ushahidi kwamba inajuzu kukitumia, hivyo mkataba juu yake unajuzu kama kuuza matunda yaliyo mtini. Pindi upangaji wa kitu unapokamilika na mpangaji akapokea manufaa yake, mpangaji anamiliki matumizi yote ya kisheria katika manufaa ya kitu alichokodisha kwa sababu ni milki yake. Hivyo anaweza kukikodisha kwa kodi anayoiona hata iwe kiasi gani; ikiwa amekikodisha kwa hamsini na akakikodisha kwa mia tano, inajuzu, kwa sababu anamiliki manufaa, hivyo anamiliki kukikodisha kwa kiasi anachoona yeye, si kile alichokikodishia. Kwa msingi huu, kile kinachoitwa al-khulu kwa ajili ya maghala, nyumba na vinginevyo – nacho ni kutoa kiasi fulani cha pesa kama ziada ya kodi iliyokadiriwa ya nyumba au ghala kwa mpangaji wa kwanza kutoka kwa yule anayepanga kwake – inajuzu na haina neno, kwa sababu mpangaji anamkodishia mwingine nyumba au ghala iliyo katika upangaji wake kwa kodi iliyokadiriwa, na kwa kiasi cha ziada anacholipwa. Huku ni kukodisha kitu alichokodisha kwa ziada ya kodi aliyokipangia, na ni jambo linalojuzu, kwa sababu inajuzu kwake kukodisha alichokodisha kwa ziada au pungufu ya alivyokodisha, kwa sababu ni mkataba unaojuzu kwa rasilimali, hivyo unajuzu kwa ziada kama kuuza bidhaa baada ya kuipokea kwa ziada ya bei aliyoinunulia." Mwisho wa nukuu kutoka kitabu cha Ash-Shakhsiyyah al-Islamiyyah.

  1. Kadhalika, ikiwa mkodishaji anataka kurejesha kitu alichokodisha kabla ya mkataba kwisha, inajuzu kwa mpangaji kuomba fidia (iwad) kwa manufaa ambayo hataweza kuyapata katika muda uliosalia wa mkataba wa upangaji. Anaweza kuomba kiasi sawa na alicholipa kwa ajili ya kodi, au kuongeza au kupunguza, akifanya vile anavyoona inafaa... Ikiwa mkodishaji hatakubali kutoa fidia kwa manufaa yaliyobaki ya muda wa mkataba, basi mpangaji ana haki ya kushikilia hicho kitu na kupata manufaa yake hadi muda wa mkataba utakapoisha, na anaweza kukikodisha kwa mtu mwingine asiyekuwa mkodishaji wa awali.

  2. Ama ikiwa mkataba wa upangaji (wa duka kulingana na swali) umekwisha kwa kuisha muda wake, na mkodishaji anataka kurejesha kitu alichokodisha (duka), basi mpangaji analazimika kisheria kurudisha duka hilo kwa mmiliki wake (mkodishaji) kwa sababu ni milki yake. Haijuzu kwake kukataa kulirudisha au kuweka sharti la kulipwa fidia (kiasi cha pesa) ili kumrudishia mwenye nyumba kitu chake cha asili, kama ilivyobainishwa katika nukuu hapo juu kutoka kitabu cha Ash-Shakhsiyyah al-Islamiyyah, Juzuu ya Pili.

Tatu: Tulishatoa jibu la swali kuhusu sehemu ya kadhia hii mnamo tarehe 20/01/2014, ambapo ilitajwa:

"1- Mpangaji kumkodishia mwingine kitu alichopanga... Inajuzu kwa mpangaji wa nyumba kuikodisha nyumba hiyo kwa mwingine katika muda wa upangaji uliotajwa katika mkataba, kwa kodi zaidi au chini ya kodi aliyopangia duka kwa mmiliki wake. Hii ni kwa sababu upangaji ni mkataba wa manufaa kwa malipo, yaani mpangaji anamiliki matumizi ya manufaa ya hicho kitu, lakini katika kile alichokipangia katika muda wa upangaji uliotajwa kwenye mkataba. Ikiwa amekipanga kwa ajili ya kuishi, basi inajuzu kwake kuishi humo, na inajuzu kumruhusu mwingine kuishi humo kwa matumizi yoyote ya kisheria kama zawadi (hibah) au upangaji... na kwa kodi watakayokubaliana na mpangaji huyo mwingine. Lakini haijuzu kwake kukikodisha kwa manufaa mengine; kwa mfano, haijuzu kukikodisha kama ofisi ya biashara ikiwa amekipanga kwa ajili ya kuishi. Kadhalika, ni lazima iwe hivyo katika muda wa upangaji, hivyo asikikodishe kwa muda unaozidi muda wa upangaji wa asili.

Hukumu hii inasemwa na wengi wa mafaqihi (Hanafi, Maliki, Shafi'i na kauli sahihi zaidi kwa Hanbali), maadamu hicho kitu hakiathiriki kwa kubadilika kwa mtumiaji. Na wameiruhusu mafaqihi wengi wa Salaf, iwe ni kwa kodi ile ile au kwa ziada.

Lakini walitofautiana ikiwa upangaji ni kwa mmiliki, yaani mmiliki amekodisha nyumba yake kwa mpangaji kwa muda wa mwaka mmoja, kisha baada ya miezi mitatu kwa mfano mmiliki akaihitaji nyumba, akataka kuikodisha kutoka kwa mpangaji kwa miezi tisa iliyobaki, na mpangaji atoke humo... Swala hili walitofautiana, na wanazo maoni tofauti ndani yake..." Mwisho wa nukuu.

Nne: Imebaki suala la kile kinachoitwa (Al-Asl al-Tijari - Milki ya Biashara), na jinsi ya kukabiliana nayo:

  1. Milki ya biashara imetafsiriwa na baadhi ya wanaoitumia kuwa: (Mali isiyohamishika ya kimaadili/kidhahania inayojumuisha mali zote zinazohamishika zilizotengwa kwa ajili ya kufanya shughuli ya biashara moja au kadhaa). Na wakasema: (Milki ya biashara ni lazima ijumuishe wateja na sifa ya kibiashara, na pia inajumuisha mali nyingine zote muhimu kwa ajili ya kuendesha hiyo milki kama jina la biashara, nembo, haki ya kupangisha, samani za biashara, bidhaa, vifaa, zana, hataza za uvumbuzi, leseni, alama za viwanda, biashara, huduma, michoro na modeli za viwanda, na kwa ujumla haki zote za milki za kiviwanda, fasihi au sanaa zilizounganishwa na milki hiyo). Kulingana na maelezo haya ya uhalisia wa milki ya biashara, inabainika kuwa inajumuisha aina mbili za mali:

a- Vipengele vya kimaada kama samani, vifaa, zana... n.k., na hizi ni mali zenye thamani halisi. b- Vipengele visivyo vya kimaada kama sifa ya kibiashara, hataza za uvumbuzi, haki za milki za kiviwanda... n.k., na hivi ni vipengele vyenye thamani ya kidhahania.

  1. Kwa kusoma uhalisia wa kile kinachoitwa "Milki ya Biashara" (Al-Asl al-Tijari), inabainika kuwa ni kitu tofauti na manufaa ya kitu kilichokodishwa, ambayo ni manufaa ya jengo linalotumika kama duka la biashara... Kwani manufaa ya jengo ni kutumia jengo hilo kwa shughuli za kibiashara... Na hapo hakiingii kile wanachokiita "Milki ya Biashara." Milki ya biashara kwa matawi yake mawili - vipengele vya kimaada na vipengele vya kidhahania - ni kitu cha ziada juu ya manufaa ya kitu kilichokodishwa, yaani jengo katika hali hii... Milki hii ya biashara hupatikana baadaye kutokana na juhudi za mpangaji anapoweka samani katika duka kwa namna inayofaa biashara husika, na kuweka humo vifaa na zana muhimu, na duka likawa na sifa ya kibiashara, wateja na shughuli za kibiashara... n.k.

  2. Katika milki ya biashara, kuna vipengele vya kimaada vinavyoruhusiwa kisheria (mubah) kama samani, zana na vifaa na mfano wake ikiwa viko kulingana na hukumu za Sharia... Na vinaweza kuwemo vitu vilivyoharamishwa kama sanamu... Kadhalika, kuna vipengele visivyo vya kimaada vinavyoruhusiwa kama sifa, nembo ya biashara, alama ya biashara na mfano wake... Na pia kuna vipengele vya kidhahania visivyojuzu katika Uislamu kama baadhi ya haki za kimaadili zinazohusiana na milki ya kifikra kama haki za kunakili (copyright), hataza za uvumbuzi na mfano wake...

  3. Ikiwa "Milki ya Biashara" inayokusudiwa kuuzwa, kuhamishwa au kukodishwa inajumuisha vipengele vya kimaada au vya kidhahania vilivyoharamishwa, basi haijuzu kuifanyia muamala kwa kuchukua malipo badala yake, bali ni lazima kwanza kujiepusha na vipengele vilivyoharamishwa vilivyomo. Ama ikiwa haijumuishi vipengele vya kimaada au vya kidhahania vilivyoharamishwa, yaani ikiwa ni mubah, basi inasihi kuibadilisha kwa kuchukua malipo badala yake kulingana na yatakayobainishwa baadaye.

  4. Ikiwa mkataba wa upangaji haujaisha, inajuzu kwa mpangaji kulikodisha duka la biashara na kubadilishana milki ya biashara kwa malipo kwa mpangaji mwingine, na halazimiki kupata idhini ya mkodishaji wa asili kwa muda uliosalia wa mkataba wa upangaji wa duka hilo... Kadhalika, anayo haki ya kumrudishia jengo (duka) mmiliki wake (mkodishaji) mkabala na fidia ya manufaa na milki ya biashara, yote hayo ikiwa milki hiyo ya biashara iko chini ya mambo yanayoruhusiwa... na iwe ndani ya muda wa upangaji.

  5. Ikiwa mkataba wa upangaji wa jengo (duka) umekwisha, basi kile kinachoitwa milki ya biashara kinaangaliwa upya. Na kile ninachokipendekeza (kukirejelea) ni:

Mpangaji ni lazima alirudishe duka la biashara kwa mmiliki wake wa asili (mkodishaji). Ama kuhusu milki ya biashara, kile kilichokuwa cha kimaada, anayo haki ya kukichukua au kukiuza kwani ni mali yake, kama samani na mfano wake... Ama sifa ya duka na umaarufu wake wa kibiashara, manufaa ya mpangaji kwayo huisha kwa kuisha kwa mkataba wa upangaji. Baada ya hapo, mpangaji huyo hamiliki sifa hiyo ili aiuze au achukue fidia kwayo kama haki yake... Kwani hii milki ya biashara ya kidhahania si manufaa anayomiliki mpangaji baada ya kuisha mkataba wa upangaji hadi iwe halali kweye kuiuza. Bali kwa kuisha kwa mkataba wa upangaji, milki ya mpangaji katika manufaa haya ya kidhahania aliyokuwa akiimiliki wakati wa muda wa upangaji nayo pia huisha.

  1. Ama kuhusu baadhi ya watu wa sasa wanaoona manufaa haya ya kidhahania kuwa ni kama haki ya ushufaa (haqq ash-shuf'ah) au haki ya mgawanyo wa siku kwa mke pamoja na mwenza wake (dhurrah), na kwamba baadhi ya mafaqihi wanaruhusu kuchukua badala ya haki hiyo, basi ulinganishi kati ya haki hizi na haki ya sifa ya kibiashara ni jambo tofauti kabisa na si sahihi kwa sababu zifuatazo:

a- Imetajwa katika Ensaiklopidia ya Fiqhi ya Kuwait (Al-Mawsu'ah al-Fiqhiyyah al-Kuwaitiyyah) kuhusu mada ya manufaa: (d - Haki ya Mutlaki... Ama kuhusu kuchukua malipo kwa ajili ya haki, kanuni kwa baadhi ya mafaqihi wa Hanafi ni kwamba haki ikiwa haina milki, basi haijuzu kuchukua malipo badala yake, kama haki ya ushufaa. Ikiwa atafanya suluhu kwayo kwa mali, haki yake ya ushufaa inabatilika na anairudisha... Ama wasio Hanafi, hawakuashiria kanuni inayoweza kutegemewa katika kujua hilo. Lakini baada ya kufuatilia baadhi ya masuala, inaweza kusemwa kwa ujumla: Kwamba Shafi'i na Hanbali wanaona kuwa haki ambayo haileti mali, au kile ambacho si kitu (ayn) wala manufaa (manfa'ah) kama haki ya ushufaa, na haki ya hiyari ya sharti (khiyar ash-shart), na mke kumtunukia mwenzake siku yake, basi hii haijuzu kuchukua malipo badala yake. Ama kile kinacholeta mali kama haki ya kisasi na kurudisha kitu kwa sababu ya aibu (ar-radd bil-'ayb), basi inajuzu kuchukua malipo kwayo. Na hii ni kwa ujumla, kwani Ibn Taymiyyah aliruhusu kwa mke kuchukua fidia kwa kutoa siku yake kwa mwenzake na kwa haki zake nyingine za mgawanyo. Kama ilivyo katika riwaya kutoka kwa Imam Ahmad kuhusu kujuzu kwa kuchukua malipo kwa haki ya ushufaa kutoka kwa mnunuzi na si kwa mwingine. Na inachukuliwa kutokana na masuala yaliyopokelewa kwa Maliki kwamba wao wanaruhusu kuchukua fidia kwa kila haki iliyothibiti kwa mwanadamu, hivyo inajuzu kwao kuchukua fidia ya ushufaa na ya mke kutoa siku yake kwa mwenzake na mengineyo.)

b- Mafaqihi wanaosema kuchukua fidia kwa haki ya ushufaa au haki ya siku ya mke kwa mwenzake, jambo hili huwa maadamu haki hiyo ipo, na si baada ya kutoweka kwake... Kuhusu haki ya ushufaa, ni pale mmiliki wa ushufaa anapokuwa jirani, lakini akihama kutoka ujirani wake na kwenda mbali, basi amepoteza haki ya ushufaa... Kadhalika kwa mke, anamiliki haki hii akiwa bado ni mke, na si ikiwa ameachwa kwa mfano... Na hapa pia, haki ya mpangaji kunufaika na sifa na umaarufu ni wakati wa upangaji wake. Ikiwa muda wa upangaji umeisha, basi haki yake katika sifa hiyo imekwisha, hivyo haitwi tena kuwa ni haki yake ya kuiuza na kuchukua malipo badala yake, bali ni lazima auondokee ukodishaji baada ya muda wake kwisha, isipokuwa akikubaliana kuongeza muda...

Ama yaliyotajwa katika sheria zilizotungwa na wanadamu kuhusu kuifanya milki hii ya biashara ya kidhahania kuwa ni haki ya mpangaji wakati wa muda wa upangaji na baada yake, akiitumia kwa kuuza na kununua, na hatoki kwenye ukodishaji muda wake unapoisha isipokuwa alipwe thamani ya milki hiyo ya biashara ya kidhahania, basi jambo hili halina thamani wala uzito mbele ya hukumu za Sharia.

Hiki ndicho ninachokipendekeza katika suala hili, na Allah ni Mjuzi zaidi na Mwenye hekima zaidi.

Ndugu yenu, Ata bin Khalil Abu al-Rashtah

08 Sha'ban 1443 H 11/03/2022 M

Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Ameer (Allah amhifadhi) kwenye: Facebook

Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Ameer (Allah amhifadhi) kwenye: Web

Share Article

Share this article with your network