Mfululizo wa majibu ya mwanachuoni mtukufu Ata bin Khalil Abu al-Rashtah, Amir wa Hizb ut-Tahrir, kwa maswali ya wafuasi wake kwenye ukurasa wake wa Facebook wa "Fikihi".
Kwa: Yeni Camii
Swali:
Assalamu Alaikum Warahmatullahi Wabarakatuh.
Namuomba Allah Aliyetaalika na Muweza kufikisha ujumbe wangu huu kwenu mkiwa katika sitara, afya njema na radhi kutoka kwa Allah, pamoja na taufiki na usahihi katika kauli na matendo.
Wakati nikifanya maandalizi katika kitabu cha Ash-Shakhsiyyah al-Islamiyyah Juzuu ya 1, nimepata utata katika kuelewa baadhi ya mambo kuhusu mada ya Ijtihadi. Ninaomba mnitafadhali kwa kunipa jibu, nanyi mtapata ujira mkubwa na shukrani nyingi:
Kwanza: Katika kitabu cha Ash-Shakhsiyyah al-Islamiyyah Juzuu ya 1, ukurasa wa 203, kulikuja maneno yafuatayo kuhusu mada ya Ijtihadi (kwa sababu Ijtihadi ni kutoa hukumu kutoka kwenye andiko, iwe ni kutoa hukumu ya jumla kutoka kwenye dalili ya jumla, kama vile kutoa hukumu kwamba mnyang’anyi anastahili adhabu kutokana na Shari'a kuweka kukata mkono kuwa ni adhabu ya haddi kwa mwizi, au iwe ni kutoa hukumu ya sehemu kutoka kwenye dalili ya sehemu kama vile kutoa hukumu ya uajiri kutokana na kitendo cha Mtume ﷺ kumkodisha mwajiriwa...)
Na kulikuja katika kitabu cha Ash-Shakhsiyyah Juzuu ya 3, ukurasa wa 445 mada ya Kanuni za Jumla: (Basi kanuni za jumla, na ufafanuzi wa kisheria, ni hukumu za jumla, ama hukumu ya kisheria ni hukumu ya sehemu). Na swali ni:
1- Nini maana ya dalili ya jumla na dalili ya sehemu? Kwa nini dalili ya kukatwa mkono mwizi ikaitwa dalili ya jumla na dalili ya kuruhusiwa uajiri ikaitwa dalili ya sehemu? (Je, hukumu ya kisheria inaweza kuwa hukumu ya jumla na hukumu ya sehemu kama ilivyoelezwa katika mada ya Ijtihadi, au ni hukumu ya sehemu pekee na haiitwi ya jumla isipokuwa katika ufafanuzi wa kisheria na kanuni za jumla kama inavyoeleweka katika Ash-Shakhsiyyah Juzuu ya 3?)
Pili: Katika mada ya masharti ya Ijtihadi ukurasa wa 213: (Malaka inamaanisha nguvu katika ufahamu na uunganishaji wa mambo, na hii inaweza kupatikana kutokana na akili ya ziada pamoja na kujua kiasi fulani cha maarifa ya kisheria na ya kilugha, na haihitaji upeo mpana wa maarifa yote ya kisheria na kilugha).
Na ikaja katika jibu la swali la tarehe 08/08/2017: (Na hakukusudiwi na malaka katika fikihi kipaji cha asili na utayari wa kimaumbile ambao unatafautiana kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine, bali inakusudiwa malaka inayopatikana kwa kujifunza, kusoma, kuzama ndani na kufanya mazoezi... Na ingawa utayari wa kiasili unaweza kuchangia katika kuzaliwa kwa malaka ya kifikihi na kuendelea kwake kwa haraka, lakini utayari huu wa kiasili sio malaka inayokusudiwa).
2- Swali ni je, yale yaliyokuja katika jibu yanakipinga kile kilichokuja katika kitabu kwa upande wa uhusiano wa utayari wa kiasili na ujenzi wa malaka? Kitabu kimeifanya misingi ya malaka kuwa ni nguvu ya ufahamu na uunganishaji mambo, ama jibu limeifanya misingi kuwa ni maarifa yaliyopatikana (kwa masomo)?
Mbarikiwe na Allah awalipe kila la kheri.
Jibu:
Walaikum Salam Warahmatullahi Wabarakatuh,
Unauliza kuhusu mambo kadhaa... hili hapa ndilo jibu lake:
Kwanza: Dalili ya Jumla na Dalili ya Sehemu: Jambo hili limefafanuliwa katika Ash-Shakhsiyyah Juzuu ya 3 – mlango wa Kanuni za Jumla, na pia Ash-Shakhsiyyah Juzuu ya 1, na Al-Kurrasah, unaweza kurejea huko... lakini nitakusogezea jibu kwa ufupi:
Ikiwa inawezekana kutoa kanuni ya kisheria kutoka kwenye dalili (au dalili kadhaa) ambayo chini yake zinaingia hukumu nyingine za kisheria mbali na zile zilizotajwa wazi katika dalili au dalili hizo, na sio kwa njia ya Qiyas (ulinganisho), yaani bila ya kulinganisha hukumu mpya na ile iliyotajwa katika andiko, bali zinaingia kama sehemu (جزئيات) za kanuni hiyo, basi wakati huo kanuni hiyo inakuwa ni ya jumla (kulliyyah) na hukumu inayoingia chini yake inakuwa ya jumla. Mara nyingi kati ya kanuni na hukumu inayoingia chini yake huwa kuna kitu kinachofanana na 'illa' (au katika nafasi ya 'illa') na wakati mwingine huwa ni 'illa' ya kweli... Imekuja katika Ash-Shakhsiyyah Juzuu ya 3 mlango wa Kanuni za Jumla ukurasa wa 455 (Na kutokana na hilo inabainika kuwa kanuni ya jumla inaifanya hukumu kuwa katika nafasi ya 'illa' kwa ajili ya hukumu ya jumla kwa kuwa ni sababu yake, yaani kwa kuwa imetokana nayo au imepangwa juu yake, au inaifanya kuwa 'illa' ya kweli kwa ajili ya hukumu ya jumla, basi hiyo ni hukumu ya jumla inayotumika kwa sehemu zake, kwa hiyo inatumika kwa kila hukumu inayolengwa nayo kama inavyotumika dalili iliyokuja nayo na haifananishwi kwayo kwa Qiyas, bali sehemu zake zinaingia chini yake, yaani zinakuwa ndani ya dhana yake au matamshi yake kabisa kama zinavyoingia chini ya kuelekeza kwa dalili, na kutolea ushahidi kwayo kunakuwa kama kutolea ushahidi kwa dalili. Basi kanuni ya jumla inachukuliwa kama inavyochukuliwa Qiyas... isipokuwa tu kwamba kanuni za jumla sio dalili ya kisheria kama Qiyas, wala sio misingi miongoni mwa misingi ya Shari'a, bali yenyewe ni hukumu ya kisheria iliyotolewa kama hukumu nyingine za kisheria, hivyo haiwi dalili;)
Pili: Ili kufafanua hilo tunataja mifano miwili kutoka Ash-Shakhsiyyah Juzuu ya 3 ukurasa wa 454-455, mmoja ukiwa ni nafasi ya 'illa', na mwingine ni 'illa' yenyewe:
1- (Kwa mfano kauli ya Allah Mtukufu:
وَلَا تَسُبُّوا الَّذِينَ يَدْعُونَ مِنْ دُونِ اللَّهِ فَيَسُبُّوا اللَّهَ عَدْوًا بِغَيْرِ عِلْمٍ
"Wala msiwatukane wale ambao wanawaomba (waabudiwa) kinyume na Allah, wasije wakamtukana Allah kwa uadui bila ya elimu." (QS Al-An'am [6]: 108)
Basi harufi ya ﴿فَيَسُبُّوا﴾ ilifaidisha kuwa kutukana kwenu masanamu yao kunapelekea wao kumtukana Allah, na hili ni haramu, hivyo inapelekea kuwa kutukana kwenu masanamu yao katika hali hii ni haramu, basi ni kana kwamba ilikuwa ni 'illa'. Kukatazwa kutukana wale waliokufuru ni dalili ya hukumu, na imeonyesha, kando na kuonyesha hukumu, jambo lingine lililopangwa juu yake pale aliposema: ﴿فَيَسُبُّوا اللَّهَ﴾ basi ikatolewa kanuni kutoka kwenye aya hii: "Njia inayopelekea kwenye haramu ni haramu"...)
2- (Na kwa mfano Mtume ﷺ anasema:
الْمُسْلِمُونَ شُرَكَاءُ فِي ثـَلاَثٍ: فِي الْكَلإِ وَالْمَاءِ وَالنَّارِ
"Waislamu ni washirika katika vitu vitatu: katika malisho, maji na moto." (Imetolewa na Abu Dawood).
Na imethibiti kutoka kwake ﷺ kuwa aliwakubalia watu wa Taif na watu wa Madina juu ya umiliki wa maji kuwa ni milki ya mtu binafsi, na ikafahamika kutokana na hali ya maji ambayo aliruhusu milki ya mtu binafsi kuwa hayakuwa kwa ajili ya mahitaji ya umma, basi ikawa 'illa' ya kuwa watu ni washirika katika vitu vitatu "ni" kuwa kwake ni miongoni mwa maslahi ya umma (miundombinu ya jamii), basi dalili imeonyesha hukumu, na imeonyesha 'illa', yaani imeonyesha hukumu, na imeonyesha jambo lingine ambalo lilikuwa sababu ya kutungwa kwa hukumu, basi ikatolewa kutoka humo kanuni: "Kila kilicho miongoni mwa maslahi ya jamii ni milki ya umma"...)
Baada ya hapo kitabu kinaongeza:
(Na kutokana na hilo inabainika kuwa kanuni ya jumla inaifanya hukumu kuwa katika nafasi ya 'illa' kwa hukumu ya jumla; kwa kuwa ni sababu yake, yaani kwa kuwa imetokana nayo au imepangwa juu yake, au inaifanya kuwa 'illa' ya kweli kwa ajili ya hukumu ya jumla, basi hiyo ni hukumu ya jumla inayotumika kwa sehemu zake; na kwa sababu hiyo inatumika kwa kila hukumu inayolengwa nayo, kama inavyotumika dalili kwa hukumu iliyokuja nayo, na haifananishwi kwayo kwa Qiyas, bali sehemu zake zinaingia chini yake, yaani zinakuwa ndani ya dhana yake au matamshi yake kabisa kama zinavyoingia chini ya kuelekeza kwa dalili, na kutolea ushahidi kwayo kunakuwa kama kutolea ushahidi kwa dalili. Basi kanuni ya jumla inachukuliwa kama inavyochukuliwa Qiyas, na kila kile kinacholengwa na kanuni huchukua hukumu yake, isipokuwa kama patakuja andiko la kisheria kinyume na ilivyo katika kanuni, basi andiko litafanyiwa kazi, na kanuni itafutwa, kama ilivyo hali katika Qiyas, ikiwa andiko la kisheria litakuja basi andiko huchukuliwa na Qiyas hufutwa. Isipokuwa tu kwamba kanuni za jumla sio dalili ya kisheria kama Qiyas, wala sio misingi miongoni mwa misingi ya Shari'a, bali yenyewe ni hukumu ya kisheria iliyotolewa kama hukumu nyingine za kisheria, hivyo haiwi dalili; na kwa sababu hiyo, kile kinacholengwa kwayo kinachukuliwa kuwa ni tawi lake au katika nafasi ya tawi. Na mfano wa kanuni ya jumla ni ufafanuzi wa jumla, basi kila kinacholengwa kwayo huchukua hukumu yake, isipokuwa kama patakuja andiko la kisheria basi andiko hilo huchukuliwa...)
Tatu: Sasa tunakuja kwenye swali lako la kwanza kuhusu wizi na uajiri:
Allah Mtukufu anasema:
وَالسَّارِقُ وَالسَّارِقَةُ فَاقْطَعُوا أَيْدِيَهُمَا جَزَاءً بِمَا كَسَبَا نَكَالًا مِنَ اللَّهِ وَاللَّهُ عَزِيزٌ حَكِيمٌ
"Na mwizi mwanamume na mwizi mwanamke, ikateni mikono yao; ikiwa ni malipo kwa yale waliyoyachuma, na adhabu ya mfano kutoka kwa Allah. Na Allah ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima." (QS Al-Ma'idah [5]: 38)
Basi dalili hii inaweza kutolewa kanuni ya jumla kwamba (Kushambulia mali za watu ni haramu na kuna adhabu kwayo), na hii ni kwa sababu inawezekana kusemwa kuwa andiko la wizi limebeba kitu kinachofanana na 'illa' au kiko katika nafasi ya 'illa' ambacho ni uunganishaji kati ya kukatwa mkono na wizi... kwani pamefanyika mpangilio wa kukata mkono juu ya wizi kwa harufi ya "fa" ambayo hapa ni kwa ajili ya kutoa sababu (as-sababiyah), na kuna kiunganishi kati ya hukumu ﴿فَاقْطَعُوا أَيْدِيَهُمَا﴾ na kati ya chenye kuwajibisha kukatwa ambacho ni wizi katika kauli Yake ﴿وَالسَّارِقُ وَالسَّارِقَةُ﴾, na kukata mkono ni kwa ajili ya wizi pekee, lakini kuwepo kwa huu uunganishaji kati ya hukumu na sababu yake kunamwezesha mujtahidi kutengeneza hukumu ya jumla inayojumuisha hali zinazoingia chini yake, ikasemwa kushambulia mali za wengine ni haramu na kunawajibisha adhabu... na inaingia chini ya hukumu hii kuwa mnyang’anyi anastahili adhabu ingawa hukumu ya mnyang’anyi haikutajwa katika aya hiyo, na kwa ajili hiyo aya imefaidisha kuwa haddi ya mwizi ni kukatwa na imefaidisha kando ya hilo, kwa kutegemea muundo wake wa kilugha, kwamba mshambuliaji wa mali za wengine anastahili adhabu, kwa ajili hiyo dalili ya kukata mkono mwizi ilikuwa ni dalili ya jumla inayofaidisha hukumu ya jumla...
Ama hukumu ya uajiri iliyochukuliwa kwa mfano kutokana na kwamba yeye ﷺ
اسْتَأْجَرَ رَجُلاً مِنْ بَنِي الدِّئْلِ هَادِياً خِرِّيتاً
"Alimkodisha mtu mmoja kutoka kabila la Bani ad-Dil kama mwongozi mwenye ujuzi," (Imetolewa na Al-Bukhari).
Basi ndani yake hakuna kitu cha kijumla wala mpangilio wa kitu juu ya kitu kingine, bali ni dalili inayofaidisha kuruhusiwa kwa uajiri, hivyo ni dalili ya sehemu inayofaidisha hukumu ya sehemu... na kwa maneno mengine ni kwamba dalili ya uajiri haihusu kitu kingine zaidi ya mwajiriwa, na haiwezekani kuingiza chini yake mikataba mingine, yaani mikataba isiyo ya uajiri, kwa hiyo ni dalili ya sehemu... na hili kwa asili yake ni tofauti na ufafanuzi wa uajiri kwa sababu ufafanuzi unasifiwa kwa ujumla wake hivyo vinaingia chini ya ufafanuzi aina za uajiri, basi ufafanuzi kwa upande huu una sifa ya ujumla, lakini dalili ya uajiri yenyewe haisifiwi kwa ujumla kwa sababu haijumuishi mada isiyo ya uajiri.
Nne: Kuhusu swali lako la pili: (Je, hukumu ya kisheria inakuwa hukumu ya jumla na hukumu ya sehemu kama ilivyoelezwa katika mada ya Ijtihadi, au ni hukumu ya sehemu pekee na haiitwi ya jumla isipokuwa katika ufafanuzi wa kisheria na kanuni za jumla kama inavyoeleweka katika Ash-Shakhsiyyah Juzuu ya 3?)
Ewe ndugu yangu, hakika kanuni za jumla, ufafanuzi wa kisheria na hukumu ya kisheria yenyewe yote ni hukumu za kisheria, isipokuwa tu kwamba hukumu inapohusishwa na tamshi la jumla kwa kuunganishwa na 'illa' au kinachofanana na 'illa' (nafasi ya 'illa') basi inakuwa hukumu ya jumla, basi ukisema (Njia inayopelekea haramu ni haramu) wewe hapa umehusisha uharamu na (Njia inayopelekea haramu) yaani umeiunganisha na tamshi la jumla na kwa ajili hiyo hukumu iliyotolewa ikawa hukumu ya jumla na inaingia chini ya kanuni hii (Hukumu ya kisheria ya jumla) mambo mengine mahususi... kwani inajumuisha kila njia inayopelekea kwenye haramu.
Na ukifafanua hukumu ya kisheria kuwa ni (Hitabu ya Mwenye Shari'a inayofungamana na vitendo vya waja kwa kudai kufanya, kuacha, kuweka au hiyari) basi wewe umeufanya ufafanuzi huo ulenge tamshi la jumla (Hitabu ya Mwenye Shari'a inayofungamana na vitendo vya waja...) basi ufafanuzi unakuwa wa jumla na zinaingia chini yake sehemu nyingine... kwani unajumuisha kila kinachofungamana na vitendo vya waja iwe ni faradhi... au sababu... au mubaha... nk.
Ama ukisema (Mzoga ni haramu) kama ilivyo katika aya tukufu:
حُرِّمَتْ عَلَيْكُمُ الْمَيْتَةُ
"Mmeharimishiwa (kula) nyama ya mnyama aliyekufa (mzoga)." (QS Al-Ma'idah [5]: 3)
Basi andiko hili halitumiki isipokuwa kwa mzoga tu, na haifahamiki kutoka humo kwamba pombe ni haramu, yaani hakuna sehemu nyingine zinazoingia chini yake, kwa ajili hiyo ikasemwa kuhusu andiko hilo kuwa ni la sehemu... na kwa maneno mengine halivuki hukumu iliyotajwa katika andiko, hivyo likasifiwa kwa usehemu (juz'iyyah).
Lakini kanuni ya jumla, ufafanuzi wa kisheria wa jumla, na hukumu za sehemu, zote ni hukumu za kisheria kwa sababu zimetolewa kutoka kwenye dalili za kisheria, na kwa ajili ya mgawanyo wa kifikihi yakaitwa kanuni na ufafanuzi kuwa ni (ya jumla/kulliyyah) na hukumu za kisheria ambazo hazitumiki kwa kisichokuwa kile kilichokuja katika andiko kuwa ni (za sehemu/juz'iyyah) ingawa zote ni hukumu za kisheria. Na muhtasari ni kwamba hukumu ya kisheria ikiwa sio kanuni ya jumla au ufafanuzi wa kisheria basi inakuwa ni hukumu ya sehemu...
Na kwa ajili hiyo hakuna mgongano kati ya yale yaliyotajwa katika Ash-Shakhsiyyah Juzuu ya 1 ukurasa wa 207-208: (kwa sababu Ijtihadi ni kutoa hukumu kutoka kwenye andiko... iwe ni kutoa hukumu ya jumla kutoka kwenye dalili ya jumla, kama vile kutoa hukumu kwamba mnyang’anyi anastahili adhabu kutokana na Shari'a kuweka kukata mkono kuwa ni adhabu ya haddi kwa mwizi, au iwe ni kutoa hukumu ya sehemu kutoka kwenye dalili ya sehemu kama vile kutoa hukumu ya uajiri kutokana na kitendo cha Mtume ﷺ kumkodisha mwajiriwa) na kati ya yale yaliyotajwa katika Ash-Shakhsiyyah Juzuu ya 3 ukurasa wa 451: (Basi kanuni za jumla, na ufafanuzi wa kisheria, ni hukumu za jumla, ama hukumu ya kisheria ni hukumu ya sehemu;)
Tano: Kwa taarifa, hakika ujumla na usehemu ni sifa za neno moja (مفرد) lakini kwa njia ya istiara (majaz) hutumika kwa neno lililounganishwa (مركب) kama ilivyokuja katika kitabu cha Ash-Shakhsiyyah Juzuu ya 3 ukurasa wa 451: [Ili utambue ujumla na usehemu katika hukumu ya kisheria, ni lazima izingatiwe kuwa matumizi haya ni ya istiara na sio ya uhalisia. Kwani ujumla na usehemu ni katika maana za neno moja na si maana za maneno yaliyounganishwa, basi hayana nafasi katika maana ya muundo. Na hukumu ya kisheria ni sentensi iliyounganishwa na si jina moja, iwe ni hukumu, au kanuni, au ufafanuzi, basi kusema kwako: nyama ya mzoga ni haramu ni sentensi iliyounganishwa, na kusema kwako: uajiri ni mkataba juu ya manufaa kwa malipo ni sentensi iliyounganishwa, na kusema kwako: njia ya kuelekea haramu ni haramu ni sentensi iliyounganishwa, basi haziingiliwi na ujumla wala usehemu; kwa sababu hizo ni miongoni mwa maana za jina, yaani maana za neno moja.
Isipokuwa tu kwamba ilivyokuwa neno la jumla katika jina ni lile ambalo inafaa kwa wengi kushirikiana katika dhana yake, kama vile mnyama, mwanadamu na mwandishi, na ilikuwa ufafanuzi ni miongoni mwa mambo ambayo inafaa kwa wengi kushirikiana humo kwani ufafanuzi wa uajiri unakuwa sahihi kwa uajiri wa mwajiriwa maalum, mwajiriwa mshirika, kukodisha nyumba, kukodisha gari, kukodisha ardhi... nk basi yakaitwa hukumu ya jumla kwa njia ya istiara, na kadhalika kanuni ya jumla.
Na ilivyokuwa neno la sehemu katika jina ni lile ambalo haifai kwa wengi kushirikiana humo, kama vile Zaid likiwa ni jina la mwanamume, na Fatima likiwa ni jina la mwanamke, na kama viwakilishi mfano wa yeye mwanamume na yeye mwanamke, na ilikuwa hukumu ya kisheria ni miongoni mwa yale ambayo haifai kwa wengi kushirikiana humo, kama vile nyama ya mzoga ni haramu, na kunywa pombe ni haramu, na mfano wa hayo, kwani hayawi sahihi isipokuwa kwa mzoga, na isipokuwa kwa pombe, basi yakaitwa hukumu ya sehemu kwa njia ya istiara, basi hiyo kwa upande wa kuonyesha kwake watu fulani au kutokuonyesha kwake husemwa kuwa ni ya jumla na ya sehemu kwa istiara, lakini kwa upande wa uhalisia wake ni hukumu ya kisheria iliyotolewa kutoka kwenye dalili ya kisheria. Hakuna tofauti kati ya kanuni, ufafanuzi, na hukumu.]
Sita: Ama kuhusu swali lako juu ya mada ya Malaka, basi haya hapa yafuatayo:
1- Hakika malaka ambayo mazungumzo yalihusu katika jibu la swali la tarehe 16 Dhul-Qi'dah 1438 H sawia na 08/08/2017 M, sio malaka yoyote tu bali ni malaka maalum ya kifikihi, na inafungamana na ufafanuzi wa mtaalamu wa fikihi (faqih), basi faqih katika istilahi ni yule aliyepata malaka katika fikihi, na kinachokusudiwa na malaka kwa mtaalamu wa fikihi kama tulivyotaja katika jibu la swali: [Na hakukusudiwi na malaka katika fikihi kipaji cha asili na utayari wa kiasili ambao unatafautiana kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine, bali inakusudiwa malaka inayopatikana kwa kujifunza, kusoma, kuzama ndani na kufanya mazoezi... Na ingawa utayari wa kiasili unaweza kuchangia katika kuzaliwa kwa malaka ya kifikihi na kuendelea kwake kwa haraka, lakini utayari huu wa kiasili sio malaka inayokusudiwa kwa faqih...]
Ama malaka kwa upande wa mujtahidi yenyewe ni kama ilivyokuja katika kitabu cha Ash-Shakhsiyyah al-Islamiyyah Juzuu ya 1 ukurasa wa 213:
[... Na kwa sababu malaka inamaanisha nguvu ya ufahamu na uunganishaji mambo, na hii inaweza kupatikana kutokana na akili ya ziada pamoja na kujua kiasi fulani cha maarifa ya kisheria na ya kilugha, na haihitaji upeo mpana wa maarifa yote ya kisheria na kilugha...]
Na muhtasari ni kwamba jambo la msingi kwa mtaalamu wa fikihi (faqih) ni malaka inayopatikana kwa kujifunza, kusoma na kukusanya maarifa ya kisheria... na utayari wa kiasili huchangia katika kutimia kwa hilo kwa haraka...
Na ama jambo la msingi kwa mujtahidi ni nguvu ya ufahamu, uunganishaji mambo, akili ya ziada na uwezo wa kutoa hukumu (istinbat)... pamoja na kujua kiasi fulani cha maarifa ya kisheria na ya kilugha na haihitaji kukusanya maarifa hayo yote...
Kwa hiyo, hakuna mgongano kati ya malaka iliyotajwa katika jibu la swali kwani hiyo ni kwa upande wa faqih... na kati ya malaka iliyotajwa katika kitabu cha Ash-Shakhsiyyah al-Islamiyyah Juzuu ya 1 kwani hiyo ni kwa upande wa mujtahidi.
Natumai kuwa jambo hili sasa limekuwa wazi.
Ndugu yenu, Ata bin Khalil Abu al-Rashtah
25 Jumada al-Akhirah 1444 H Sawia na 18/01/2023 M
Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir (Allah amuhifadhi) kwenye: Facebook