Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

Jawabu la Swali: Diyah Katika Kuua Bila Kukusudia na Kuua kwa Kukusudia

May 13, 2016
15282

(Silsila ya majibu ya mwanachuoni mtukufu Ata bin Khalil Abu al-Rashtah, Amir wa Hizb ut-Tahrir, kwa maswali ya watembeleaji wa ukurasa wake wa Facebook "Faqihi")

Jawabu la Swali

Diyah Katika Kuua Bila Kukusudia na Kuua kwa Kukusudia

Kwa Abu Ahmed Abd

Swali:

As-Salaamu Alaykum wa Rahmatullahi wa Barakatuh,

Diyah kwa ajili ya kuua bila kukusudia ni wajibu na hulipwa kwa familia ya aliyeuawa, na yale yaliyopokelewa kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ ni kwamba ni ngamia mia moja kwa watu wa vijijini (badia) au dinari elfu moja za dhahabu, au dirhamu elfu kumi na mbili za fedha. Amr bin Hazm ametaja katika kitabu chake kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ aliwaandikia watu wa Yemen:

وَإِنَّ فِي النَّفْسِ الْمُؤْمِنَةِ مِائَةٌ مِنَ الْإِبِلِ، وَعَلَى أَهْلِ الْوَرِقِ أَلْفُ دِينَارٍ

"Na hakika katika nafsi ya muumini (aliyeuawa) kuna ngamia mia moja, na kwa wenye dhahabu ni dinari elfu moja." (Imepokewa na an-Nisai).

Na Ibn Abbas amepokea: Kwamba mtu mmoja katika ukoo wa Bani Adi aliuawa,

فَجَعَلَ النَّبِيُّ ﷺ دِيَتَهُ اثْنَيْ عَشَرَ أَلْفًا

"Basi Mtume ﷺ akaifanya fidia yake iwe (dirhamu) elfu kumi na mbili." (Imepokewa na Abu Dawood na Ibn Majah).

Na Al-Sha’bi amepokea kwamba Umar aliwawekea watu wa dhahabu dinari elfu moja. Na kutoka kwa Amr bin Shu’aib, kutoka kwa baba yake, kutoka kwa babu yake: Kwamba Umar alisimama kutoa khutba akasema: "Fahamuni kwamba ngamia wamepanda bei, basi akawakadiria watu wa dhahabu dinari elfu moja, na watu wa fedha (al-wariq) dirhamu elfu kumi na mbili, na watu wa ng'ombe ng'ombe mia mbili, na watu wa mbuzi mbuzi elfu mbili, na watu wa nguo (al-hulal) nguo mia mbili." (Imepokewa na Abu Dawood).

Sheikh wetu, Mwenyezi Mungu akakuheshimu kwa kuiongoza Umma katika Dola ya Khilafah ya Waongofu hivi karibuni InshaAllah. Tunaona hapa tofauti katika ulipaji wa diyah wakati wa zama za Umar bin al-Khattab na kile alichoamuru. Je, hii inachukuliwa kuwa ni ijma’ as-sahabah (ijitahadi ya pamoja ya maswahaba) hivyo ni lazima kufuata alichoamuru Umar bin al-Khattab? Na je, inajuzu leo kulipa diyah kwa fedha (al-wariq) pamoja na tofauti kubwa iliyopo kati ya bei ya dhahabu na fedha, ambayo leo inakadiriwa kufikia takriban asilimia tisini? Yaani, diyah ya dhahabu ni kubwa mara kumi zaidi kuliko diyah ya fedha, na hapa inaonekana tofauti na pengo kubwa kati ya fidia hizo mbili. Je, ni ipi kati ya hizo mbili ambayo kadhi anapaswa kuhukumu kwayo leo?

Mwenyezi Mungu akulipe kheri.

Jawabu:

Wa Alaykumus Salaam wa Rahmatullahi wa Barakatuh,

Diyah inakuwa kwa mifugo na inakuwa kwa pesa (naqd). Ama diyah ya mifugo bila ya nyongeza ya uzito (taghlidh), ni ngamia mia moja, na huchukuliwa katika kuua bila kukusudia (qatl al-khata’), na katika yale yanayochukuliwa kama ni makosa. Na dalili ya hayo ni kile alichopokea an-Nisai kutoka kwa Amr bin Shu’aib, kutoka kwa baba yake, kutoka kwa babu yake, kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ amesema:

مَنْ قُتِلَ خَطَأً فَدِيَتُهُ مِائَةٌ مِنَ الْإِبِلِ...

"Mwenye kuua bila kukusudia, basi fidia yake ni ngamia mia moja..."

Ama mauaji ya nusu-kukusudia (shibh al-amd), an-Nisai amepokea kutoka kwa Abdullah bin Amr, kutoka kwa Mtume ﷺ amesema:

قَتِيلُ الْخَطَإِ شِبْهِ الْعَمْدِ بِالسَّوْطِ أَوِ الْعَصَا، مِائَةٌ مِنَ الْإِبِلِ أَرْبَعُونَ مِنْهَا فِي بُطُونِهَا أَوْلَادُهَا

"Aliyeuawa kwa kukosea nusu-kukusudia kwa mjeledi au fimbo, ni ngamia mia moja, arobaini kati yao wakiwa na mimba matumboni mwao."

Vilevile, hiyo ndiyo diyah ya mauaji ya kukusudia ikiwa walii (wasimamizi) wa aliyeuawa wataridhia kupokea diyah badala ya kisasi (qisas).

Ama diyah ya pesa, kwa watu wa dhahabu ni dinari elfu moja, na kwa watu wa fedha ni dirhamu elfu kumi na mbili. An-Nisai amepokea kutoka kwa Abu Bakr bin Muhammad bin Amr bin Hazm, kutoka kwa baba yake, kutoka kwa babu yake: "Kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ aliwaandikia watu wa Yemen barua ambayo ndani yake kulikuwa na faradhi, sunna, na fidia (diyat)..." na ndani yake mlikuja:

...وَعَلَى أَهْلِ الذَّهَبِ أَلْفُ دِينَارٍ

"...na kwa wenye dhahabu ni dinari elfu moja."

Na Abu Dawood amepokea katika Sunan yake kutoka kwa Ikrima, kutoka kwa Ibn Abbas, kwamba mtu mmoja katika ukoo wa Bani Adi aliuawa,

فَجَعَلَ النَّبِيُّ ﷺ دِيَتَهُ اثْنَيْ عَشَرَ أَلْفًا

"Basi Mtume ﷺ akaifanya fidia yake iwe (dirhamu) elfu kumi na mbili."

Dinari ya kisharia ni sawa na uzito wa gramu [4.25] za dhahabu, nao ndio uzito wa mithqal ya kisharia. Na dirhamu ya kisharia ni sawa na uzito wa gramu [2.975] za fedha. Kulingana na hilo, diyah ya aliyeuawa kwa dhahabu ni sawa na uzito wa gramu [4250] za dhahabu. Na kwa fedha ni sawa na uzito wa gramu [35700] za fedha.

Nazo hulipwa kwa fedha za karatasi kwa kiasi cha thamani ya gramu [4250] za dhahabu kwa upande wa dinari elfu moja, na kiasi cha thamani ya gramu [35700] za fedha kwa upande wa dirhamu elfu kumi na mbili.

Lakini fedha za karatasi za sasa hazina dhamana ya dhahabu wala fedha, hivyo haziangukii chini ya watu wa dhahabu wala chini ya watu wa fedha.

Zenyewe zimehesabiwa kuwa ni pesa kwa njia ya qiyas (ulinganisho) kutokana na kuwepo kwa sababu (‘illah) iliyotolewa katika andiko ambayo ni (naqdiyah) "kuwa ni pesa", kama ilivyofafanuliwa katika mlango wake katika kitabu cha Al-Amwal na vitabu vyetu vingine.

Ukadiriaji wa diyah kwa dhahabu kulingana na pesa za karatasi za sasa ni mkubwa zaidi kithamani kuliko ukadiriaji wa diyah kwa fedha kulingana na pesa za karatasi za sasa. Kuzingatia karatasi hizi katika fidia kunategemea ijtihadi katika suala hili. Na kile ninachoona mimi ni kwamba hakuna neno kuikadiria kwa fedha katika fidia ya kuua bila kukusudia, kwa sababu yule ambaye mauaji ya bila kukusudia yamehusishwa naye hakufanya dhambi, kwani fidia hapa si kwa sababu amefanya haramu, bali fidia hapa ni kwa hekima anayoijua Mwenyezi Mungu. Hivyo, kiwango kidogo zaidi kati ya viwango viwili katika kulipa fidia ya makosa kinaendana na kutofanya haramu kwa muuaji huyo. Ama katika fidia ya kuua kwa kukusudia, naona ikadiriwe kwa dhahabu, kwa sababu muuaji wa kukusudia amefanya haramu, hivyo haimstahiki kufanyiwa wepesi, bali kiwango kikubwa zaidi kati ya viwango viwili ndicho kinachomstahiki.

Namuomba Mwenyezi Mungu (swt) aniwafikishe katika usahihi wa jambo hilo.

Ndugu yenu, Ata bin Khalil Abu al-Rashtah

05 Shaban 1437 H Sawa na 12/05/2016 M

Kiungo cha jawabu kutoka kwa ukurasa wa Facebook wa Amir: facebook

Kiungo cha jawabu kutoka kwa ukurasa wa Google Plus wa Amir: Googleplus

Kiungo cha jawabu kutoka kwa ukurasa wa Twitter wa Amir: Twitter

Kiungo cha jawabu kutoka kwa tovuti ya Amir

Share Article

Share this article with your network