Mfululizo wa Majibu ya Mwanachuoni Mtukufu Ata bin Khalil Abu al-Rashtah, Ameer wa Hizb ut-Tahrir, kwa Maswali ya Wageni kwenye Ukurasa wake wa Facebook "Fiqhi"
Jibu la Swali
Tofauti Kati ya Upokezi wa Usomaji wa Aya za Qur’an Kwetu na Upokezi wa Maandishi ya Aya za Allah Kwetu
Kwa: Bakr Al-Shami
Swali:
Assalamu Alaikum wa Rahmatullahi wa Barakatuh.
Tafadhali nieleze hadithi hii kwani imenitatiza, na niliporejea kauli za wanachuoni, tatizo bado halijaondoka:
قَالَ ابْنُ شِهَابٍ: وَأَخْبَرَنِي خَارِجَةُ بْنُ زَيْدِ بْنِ ثَابِتٍ، سَمِعَ زَيْدَ بْنَ ثَابِتٍ قَالَ: فَقَدْتُ آيَةً مِنْ الْأَحْزَابِ حِينَ نَسَخْنَا الْمُصْحَفَ، قَدْ كُنْتُ أَسْمَعُ رَسُولَ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم يَقْرَأُ بِهَا، فَالْتَمَسْنَاهَا فَوَجَدْنَاهَا مَعَ خُزَيْمَةَ بْنِ ثَابِتٍ الْأَنْصَارِيِّ: ﴿مِنْ الْمُؤْمِنِينَ رِجَالٌ صَدَقُوا مَا عَاهَدُوا اللَّهَ عَلَيْهِ﴾.
Bado sijaelewa ni vipi Masahaba waliikubali kutoka kwake wakati yeye ni mmoja tu na haikufikia kiwango cha tawatur, na hata tukikubali kwamba ushahidi wake ni sawa na ushahidi wa watu wawili, jambo bado ni lile lile kwani haikufikia kiwango cha tawatur?!!
Barakallahu fikum Sheikh wetu.
Jibu:
Wa Alaikum Salam wa Rahmatullahi wa Barakatuh,
Inaonekana jambo limekutatiza kati ya upokezi wa usomaji (tilawa) wa aya za Qur'an kwetu kutoka kwa Mtume wa Allah (saw) na upokezi wa maandishi (rasm) ya aya za Allah kama zilivyoandikwa mbele ya Mtume (saw). Ama upokezi wa usomaji wa aya, huo ni kwa upokezi wa mutawatir kutoka kwa makundi ya Masahaba (ra) kutoka kwa Mtume wa Allah (saw), hadi ulipotufikia kwa njia ya mutawatir na ukiwa umehifadhiwa hadi Siku ya Kiyama kwa hifadhi ya Allah na taufiki Yake, Aliyesema:
إِنَّا نَحْنُ نَزَّلْنَا الذِّكْرَ وَإِنَّا لَهُ لَحَافِظُونَ
"Hakika Sisi ndio tulioteremsha Ukumbusho huu (Qur’ani), na hakika Sisi ndio tutakaoulinda." (QS. Al-Hijr [15]: 9)
Ama upokezi wa maandishi ya aya, Masahaba hawakukubali kuandika aya kutoka kwenye hifadhi ya vifua vyao tu, bali walitaka kukusanya maandishi yale yale yaliyoandikwa mbele ya Mtume wa Allah (saw). Ilitosha kwao kukusanya karatasi/ngozi (suhuf) zilizoandikwa zilizokuwa kwa Masahaba, lakini wao (ra) walijilazimisha kuwa na mashahidi wawili kwa kila karatasi kwamba iliandikwa mbele ya Mtume (saw) ili kuongeza umakini. Na hii ni taufiki kutoka kwa Allah (swt) kwa ajili ya kuhifadhi Kitabu Chake kitukufu ambacho hakifikiwi na upotofu:
لَا يَأْتِيهِ الْبَاطِلُ مِنْ بَيْنِ يَدَيْهِ وَلَا مِنْ خَلْفِهِ تَنْزِيلٌ مِنْ حَكِيمٍ حَمِيدٍ
"Hautaufikia upotofu mbele yake wala nyuma yake; umeteremshwa na Mwenye hikima, Msifiwa." (QS. Fussilat [41]: 42)
Hili ndilo suala lenyewe, na huu hapa ndio ufafanuzi:
Kwanza: Maudhui ya kukusanywa kwa Qur'an:
Tumefafanua maudhui ya kukusanya Qur'an Tukufu katika kitabu cha Ash-Shakhsiyyah al-Islamiyyah (Shakhsiyyah ya Kiislamu) Juzuu ya Kwanza, mlango wa "Kukusanywa kwa Qur'an", na kadhalika tulifanya hivyo katika kitabu cha Taysir al-Wusul ila al-Usul chini ya kichwa cha habari "Kuteremka kwa Qur'an na Kuandikwa Kwake" na "Kukusanywa kwa Qur'an". Muulizaji anaweza kurejea kwenye vitabu viwili vilivyoashiriwa ili kufahamu kwa kina suala hili na ushahidi wake wa kina... Nitakunukulu baadhi ya yaliyomo katika vitabu vyetu ili yakusaidie kufahamu suala hili inavyotakiwa kwa idhini ya Allah:
- Nakunukulu kutoka kwenye kitabu changu "Taysir al-Wusul ila al-Usul", mlango wa kukusanya Qur'an:
(... Kwa sababu ya vita vya waasi (murtaddin), Abu Bakr (ra) alichelea kwamba idadi kubwa ya hifadhi wa Qur'an Tukufu (ambao walikuwa wamehifadhi aya zake zikiwa zimepangwa katika sura zake) wangeuawa, akaamuru kukusanywa kwa aya zilizoandikwa za kila sura katika sehemu moja zikiwa zimepangwa kama alivyozithibitisha Mtume (saw). Hivyo, vipande vilivyoandikwa aya za kila sura vilikusanywa vikiwa vimepangwa mfululizo baada ya kuhakikisha kuwa maandishi haya yaliandikwa mbele ya Mtume (saw). Walikuwa wakiomba ushahidi wa Masahaba wawili kwa kila kipande (ruq’ah) kilichoandikwa wakishuhudia kwamba kiliandikwa mbele ya Mtume (saw), na hawakutosheka tu na kwamba maandishi hayo yanaendana na kile kilichohifadhiwa vifuani, pamoja na kufahamu kuwa kila aya ilikuwa imehifadhiwa na kundi la mutawatir la Masahaba. Kwa sababu hiyo, walipokuta mwisho wa Surah At-Tawbah "imeandikwa kwa Khuzaima pekee" na hakushuhudia maandishi yake mbele ya Mtume (saw) isipokuwa Khuzaima (ra), walisita kuikusanya hadi ilipopatikana ushahidi kwao kwamba Mtume (saw) alikuwa amekubali ushahidi wa Khuzaima kuwa ni sawa na Waislamu wawili waadilifu. Wakati huo walikusanya kile kipande kilichoandikwa ambacho Khuzaima alishuhudia, huku wakijua kuwa walikuwa wamehifadhi aya hiyo kwa namna ya kukata (qati’). Jambo hilo lilikuwa ni kuongeza uhakiki tu kutoka kwao (ra), kwa sababu walitaka kukusanya karatasi zilizoandikwa mbele ya Mtume (saw) na si kuziandika kutoka kwenye hifadhi zao.
Kwa hiyo, ukusanyaji wa Abu Bakr al-Siddiq ulikuwa ni ukusanyaji wa vipande (riqa’) vilivyoandikwa aya na kuzipanga katika sura zake kama alivyozithibitisha Mtume (saw), yaani kuweka vipande vilivyoandikwa aya za kila sura kimoja baada ya kingine katika sehemu moja kwa sura zote za Qur’an.) Mwisho.
- Na nakunukulu kutoka Ash-Shakhsiyyah Juzuu ya Kwanza baada ya Abu Bakr kukusanya vipande vilivyoandikwa aya katika sura zake kama zilivyoandikwa mbele ya Mtume (saw):
(...Na juu ya hivyo, amri ya Abu Bakr katika kukusanya Qur'an haikuwa amri ya kuiandika katika Mus-haf mmoja, bali ilikuwa ni amri ya kukusanya karatasi zilizoandikwa mbele ya Mtume (saw) pamoja katika sehemu moja na kuhakikisha kuwa ni zile zile kwa kuungwa mkono na ushahidi wa mashahidi wawili... Karatasi hizi zilibaki zimehifadhiwa kwa Abu Bakr katika maisha yake, kisha kwa Umar katika maisha yake, kisha kwa Hafsah bint Umar, Mama wa Waumini, kulingana na wasia wa Umar...
Hii ni kuhusiana na ukusanyaji wa Abu Bakr. Ama kuhusiana na ukusanyaji wa Uthman, ilikuwa katika mwaka wa tatu au wa pili wa ukhalifa wa Uthman, yaani mwaka wa ishirini na tano Hijria, Hudhayfah bin al-Yaman alimjia Uthman mjini Madina akiwa anatokea vitani dhidi ya watu wa Sham katika ufunguzi wa Armenia na Azerbaijan pamoja na watu wa Iraq. Hudhayfah alishtushwa na tofauti zao katika usomaji wa Qur'an... akasafiri hadi kwa Uthman. Ibn Shihab amesimulia kuwa Anas bin Malik alimhadithia: "Kwamba Hudhayfah bin al-Yaman alimjia Uthman wakati alipokuwa akipigana na watu wa Sham katika ufunguzi wa Armenia na Azerbaijan pamoja na watu wa Iraq, Hudhayfah alishtushwa na tofauti zao katika usomaji, Hudhayfah akamwambia Uthman: Ewe Amir wa Waumini, iokoe umma huu kabla hawajafitina katika Kitabu kama walivyofitina Mayahudi na Manasara. Uthman akatuma ujumbe kwa Hafsah kwamba: Tuletee zile karatasi tuzinakili katika Misahafu kisha tukurudishie. Hafsah akazituma kwa Uthman, naye akamuamuru Zaid bin Thabit, Abdullah bin al-Zubayr, Said bin al-Aas, na Abdurrahman bin al-Harith bin Hisham, wakazinakili katika Misahafu... hadi walipomaliza kunakili karatasi hizo katika Misahafu, Uthman alizirudisha karatasi hizo kwa Hafsah, na akatuma kila upande Mus-haf mmoja miongoni mwa ile waliyonakili, na akaamuru Qur'an nyingine yoyote iliyo katika karatasi au Mus-haf ichomwe." Idadi ya nakala zilizolanakiliwa ilikuwa nakala saba; Misahafu saba iliandikwa kwenda Makka, Sham, Yemen, Bahrain, Basra, Kufa, na mmoja uliwekwa Madina.
Na kwa msingi huu, kazi ya Uthman haikuwa kukusanya Qur'an bali ilikuwa ni kunakili na kuhamisha kile kile kilichopokelewa kutoka kwa Mtume (saw) kama kilivyo. Kwani hakufanya chochote isipokuwa kunakili nakala saba kutoka kwenye nakala iliyohifadhiwa kwa Hafsah, Mama wa Waumini, na akawakusanya watu kwenye maandishi haya pekee na kuzuia maandishi au imla nyingine yoyote. Jambo likatulia juu ya nakala hii katika maandishi na imla, nayo ni maandishi na imla ile ile ambayo karatasi ziliandikwa mbele ya Mtume (saw) wakati wahyi uliposhuka, na ndiyo nakala ile ile aliyoikusanya Abu Bakr. Kisha Waislamu wakaanza kunakili kutoka kwenye nakala hizi na si vinginevyo, na haukubaki isipokuwa Mus-haf wa Uthman kwa maandishi yake (rasm). Na zilipopatikana mashine za chapa, Mus-haf ukaanza kuchapishwa kutoka kwenye nakala hii kwa maandishi na imla hiyo hiyo...)
- Na kama unavyoona, suala halikuwa upokezi wa usomaji wa Qur'an, kwani huu ulipokelewa na makundi ya Masahaba kutoka kwa Mtume (saw) kwa upokezi wa mutawatir wenye uhakika, bali ni upokezi wa maandishi yaliyoandikwa mbele ya Mtume (saw)... Kwa ajili hiyo, maandishi haya (rasm) yaliyomo kwenye Mus-haf ni maandishi ya tawqifi (yaliyowekwa na Sharia) ambayo ni lazima kufungamana nayo pekee, na ni haramu kuandika Mus-haf kwa maandishi tofauti na haya. Haifai kabisa kuyaacha... Pamoja na hayo, kufungamana na rasm ya Uthmani kwa Qur'an ni maalum kwa uandishi wa Mus-haf mzima. Ama kuandika Qur'an kama ushahidi (kunukuu), au kuiandika ubaoni kwa ajili ya kufundishia au mengineyo yanayoandikwa nje ya Misahafu, inajuzu kuandikwa kwa njia nyingine ya imla, kama vile kuandika:
الرِّبَوا
iliyomo kwenye Mus-haf, unaweza kuiandika kwa ajili ya kufundishia ubaoni kama (الربا), kwa sababu idhini kutoka kwa Mtume na ijmaa kutoka kwa Masahaba ilitokea kwenye Mus-haf pekee na si kwingineko, na haifanyiwi qiyas (ulinganisho) kwa sababu ni jambo la tawqifi lisilo na illah (sababu ya kisheria), hivyo qiyas haingii ndani yake.
Pili: Maudhui ya hadithi unayoulizia ambayo imetolewa na Bukhari kama ifuatavyo:
(4604- Musa ametuhadithia, Ibrahim ametuhadithia, Ibn Shihab ametuhadithia kwamba Anas bin Malik alimhadithia kuwa Hudhayfah bin al-Yaman alimjia Uthman wakati alipokuwa akipigana na watu wa Sham katika ufunguzi wa Armenia na Azerbaijan pamoja na watu wa Iraq, Hudhayfah alishtushwa na tofauti zao katika usomaji, Hudhayfah akamwambia Uthman: Ewe Amir wa Waumini, iokoe umma huu kabla hawajafitina katika Kitabu kama walivyofitina Mayahudi na Manasara. Uthman akatuma ujumbe kwa Hafsah kwamba: Tuletee zile karatasi tuzinakili katika Misahafu kisha tukurudishie. Hafsah akazituma kwa Uthman, naye akamuamuru Zaid bin Thabit, Abdullah bin al-Zubayr, Said bin al-Aas, na Abdurrahman bin al-Harith bin Hisham, wakazinakili katika Misahafu. Uthman akawaambia wale watu watatu wa Kikureishi: Mkitofautiana ninyi na Zaid bin Thabit katika kitu chochote cha Qur'an, basi kiandikeni kwa lugha ya Kikureishi, kwani ilishuka kwa lugha yao. Wakafanya hivyo hadi walipomaliza kunakili karatasi hizo katika Misahafu, Uthman akazirudisha karatasi hizo kwa Hafsah, na akatuma kila upande Mus-haf mmoja miongoni mwa ile waliyonakili, na akaamuru Qur'an nyingine yoyote iliyo katika karatasi au Mus-haf ichomwe.
Ibn Shihab amesema: Na Kharijah bin Zaid bin Thabit aliniambia, alimsikia Zaid bin Thabit akisema: Nilikosa aya moja ya Al-Ahzab tulipokuwa tunanakili Mus-haf, nilikuwa nikimsikia Mtume wa Allah (saw) akisoma kwayo, tukaichunguza na tukaipata kwa Khuzaima bin Thabit al-Ansari:
مِنْ الْمُؤْمِنِينَ رِجَالٌ صَدَقُوا مَا عَاهَدُوا اللَّهَ عَلَيْهِ
"Miongoni mwa Waumini wapo watu waliotimiza waliyoahidiana na Mwenyezi Mungu." (QS. Al-Ahzab [33]: 23)
tukaipachika katika sura yake ndani ya Mus-haf.)
Ni wazi kutokana na hadithi kwamba inazungumzia tukio la kunakili Misahafu katika zama za Uthman (ra) ambapo alimkabidhi Zaid bin Thabit pamoja na wenzake watatu kazi ya kunakili Misahafu kutoka kwenye vipande vilivyokusanywa zama za Abu Bakr ambavyo vilikuwa nyumbani kwa Hafsah (ra). Yaani hadithi inahusu kunakili kutoka kwenye maandishi yaliyoandikwa mbele ya Mtume (saw) na si kuhusu upokezi wa usomaji, bali ni kunakili kile kilichokuwa kimeandikwa katika vipande vilivyoandikwa mbele ya Mtume (saw) ili Qur'an iandikwe katika Misahafu kwa maandishi yale yale yaliyoandikwa mbele ya Mtume (saw). Na jambo hili halihitaji lazima tawatur, bali habari sahihi inatosha, lakini wao (ra) walijilazimisha mashahidi wawili juu ya uandishi kwa ajili ya kuongeza umakini na umuhimu... Ama usomaji wa aya za Qur'an ulikuwa ukipokelewa kama tulivyosema kutoka kwa makundi ya Masahaba kutoka kwa Mtume wa Allah (saw).
Hivyo basi, jibu la swali lako limekuwa wazi kwa idhini ya Allah ambaye amekihifadhi Kitabu Chake:
إِنَّا نَحْنُ نَزَّلْنَا الذِّكْرَ وَإِنَّا لَهُ لَحَافِظُونَ
"Hakika Sisi ndio tulioteremsha Ukumbusho huu (Qur’ani), na hakika Sisi ndio tutakaoulinda." (QS. Al-Hijr [15]: 9)
Tatu: Masuala mawili yamebaki yanahitaji ufafanuzi:
La kwanza: Ni aya zipi ambazo hazikupatikana zimeandikwa isipokuwa kwa Khuzaima...
Na la pili: Je, zilikuwa kwa Khuzaima au kwa Abu Khuzaima...
Na kwa ajili ya kujibu hilo tunasema na kwa Allah ndiyo taufiki:
- Kuhusu suala la kwanza linalohusu aya, Bukhari ametoa riwaya mbili chini ya namba 4311, na chini ya namba 4604 kama ifuatavyo:
Ya kwanza: (4311 Abu al-Yaman ametuhadithia, Shuaib ametuambia kutoka kwa al-Zuhri amesema: Ibn al-Sabbaq aliniambia kuwa Zaid bin Thabit al-Ansari (ra) – naye alikuwa miongoni mwa walioandika wahyi – amesema: Abu Bakr alinitumia ujumbe baada ya mauaji ya watu wa Yamamah na alikuwa na Umar. Abu Bakr akasema: Umar amenijia na kusema: Mauaji yamekuwa makali siku ya Yamamah kwa watu, na mimi nachelea kuwa mauaji yatakuwa makali kwa wasomaji wa Qur'an katika sehemu nyinginezo, hivyo sehemu kubwa ya Qur'an itapotea isipokuwa mkiikusanya, na mimi naona muikusanye Qur'an. Abu Bakr amesema: Nikamwambia Umar: Nitafanyaje jambo ambalo Mtume wa Allah (saw) hakulifanya? Umar akasema: Wallahi hili ni kheri. Umar hakuacha kunirejea katika hilo mpaka Allah akafungua kifua changu kwa hilo na nikaona lile aliloona Umar. Zaid bin Thabit amesema – na Umar alikuwa ameketi hapo hazungumzi – Abu Bakr akasema: Hakika wewe ni kijana mwenye akili, hatukutilii shaka, ulikuwa ukiandika wahyi kwa Mtume wa Allah (saw), basi ifuatilie Qur'an na ikusanye. Wallahi, lau angenikalifisha kuhamisha mlima miongoni mwa milima isingekuwa nzito kwangu kuliko alichoniamuru katika kukusanya Qur'an. Nikasema: Mtafanyaje jambo ambalo Mtume (saw) hakulifanya? Abu Bakr akasema: Wallahi hili ni kheri. Sikuaacha kumrejea mpaka Allah akafungua kifua changu kwa lile ambalo Allah alifungua vifua vya Abu Bakr na Umar. Nikasimama na nikaifuatilia Qur'an nikiikusanya kutoka kwenye vipande vya ngozi, mifupa ya mabega, kuta za mitende ya tende, na vifua vya watu, mpaka nikapata kutoka Surah At-Tawbah aya mbili kwa Khuzaima al-Ansari, sikujaipata kwa yeyote mwingine ghairi yake:
لَقَدْ جَاءَكُمْ رَسُولٌ مِنْ أَنْفُسِكُمْ عَزِيزٌ عَلَيْهِ مَا عَنِتُّمْ حَرِيصٌ عَلَيْكُم
"Hakika amekwishafikieni Mtume anayetokana na nyinyi; yanamsikitisha yanayokutaabisha, anakuhangaikieni sana..." (QS. At-Tawbah [9]: 128)
hadi mwisho wake, na karatasi ambazo Qur'an ilikusanywa ndani yake zilikuwa kwa Abu Bakr mpaka Allah alipomfisha, kisha kwa Umar mpaka Allah alipomfisha, kisha kwa Hafsah bint Umar...), na kama ilivyo nukuu ya hadithi, hiyo ilikuwa katika zama za Abu Bakr (ra) na ni wazi ndani yake kuwa kile kipande kilichoandikwa walichokipata kwa Khuzaima ni cha aya mbili za mwisho za Surah At-Tawbah.
Ya pili: (4604- Musa ametuhadithia, Ibrahim ametuhadithia, Ibn Shihab ametuhadithia kwamba Anas bin Malik alimhadithia kuwa Hudhayfah bin al-Yaman alimjia Uthman... hadithi ile ile iliyotajwa juu... tukaipata kwa Khuzaima bin Thabit al-Ansari:
مِنْ الْمُؤْمِنِينَ رِجَالٌ صَدَقُوا مَا عَاهَدُوا اللَّهَ عَلَيْهِ
"Miongoni mwa Waumini wapo watu waliotimiza waliyoahidiana na Mwenyezi Mungu." (QS. Al-Ahzab [33]: 23)
tukaipachika katika sura yake ndani ya Mus-haf.) na kama ilivyo nukuu ya hadithi, hiyo ilikuwa katika zama za Uthman (ra) na ni wazi ndani yake kuwa kipande kilichoandikwa walichokipata kwa Khuzaima ni cha aya ya Al-Ahzab.
Na kwa kutazama kwa kina hadithi mbili (4311) na (4604) ambazo Bukhari amezitoa, yaani zina sanadi sahihi, inabainika yafuatayo:
a- Mwanzoni tunafafanua kuwa hadithi hizi mbili hazihusu tawatur wa aya, kwani katika riwaya zote mbili maudhui ni kuhusu uandishi na si kuhusu tawatur wa hifadhi, kwani kila aya ilikuwa imehifadhiwa na kundi la Masahaba kutoka kwa Mtume wa Allah (saw). Isipokuwa Masahaba walitaka kunakili kile kile kilichoandikwa mbele ya Mtume (saw) kwa sababu hawakutaka watu waandike kutoka kwenye hifadhi zao kisha herufi zao zitofautiane, bali walitaka kuandika aya kwa maandishi yale yale yaliyoandikwa mbele ya Mtume wa Allah (saw), kama nyongeza ya umakini na taufiki kutoka kwa Allah Mwenye Nguvu, Mwenye Hikima Aliyesema:
إِنَّا نَحْنُ نَزَّلْنَا الذِّكْرَ وَإِنَّا لَهُ لَحَافِظُونَ
"Hakika Sisi ndio tulioteremsha Ukumbusho huu (Qur’ani), na hakika Sisi ndio tutakaoulinda." (QS. Al-Hijr [15]: 9)
Na kwa ajili hiyo, hukumu ya kisheria ilivuliwa kuwa haijuzu kuchapisha Mus-haf isipokuwa kulingana na Mus-haf wa Uthman (ra).
b- Kwamba kukusanywa kwa vipande vilivyoandikwa kulikuwa katika zama za Abu Bakr kama ilivyokuja katika ushahidi sahihi, na pia kusimamisha mashahidi wawili kwa kila kipande kilichoandikwa ni sahihi kadhalika... Ama katika zama za Uthman (ra), kilichofanyika ni kunakili Misahafu kutoka kwenye vipande vilivyokusanywa zama za Abu Bakr ambavyo wakati wa kunakili vilikuwa kwa Hafsah (ra), hivyo Uthman alivihitaji na kumkalifisha Zaid na wale watatu waliokuwa naye kunakili idadi ya Misahafu kutoka kwenye vipande hivyo...
Na hakuna nafasi hapa, yaani katika zama za Uthman, kwa kupotea kwa kipande kilichoandikwa, bali hili hutokea wakati wa kukusanya vipande jambo lililotokea zama za Abu Bakr, yaani ni kile kipande ambacho kilikuwa kimeandikwa aya mbili za mwisho za At-Tawbah:
لَقَدْ جَاءَكُمْ رَسُولٌ مِنْ أَنْفُسِكُمْ عَزِيزٌ عَلَيْهِ مَا عَنِتُّمْ حَرِيصٌ عَلَيْكُمْ بِالْمُؤْمِنِينَ رَءُوفٌ رَحِيمٌ * فَإِنْ تَوَلَّوْا فَقُلْ حَسْبِيَ اللَّهُ لَا إِلَهَ إِلَّا هُوَ عَلَيْهِ تَوَكَّلْتُ وَهُوَ رَبُّ الْعَرْشِ الْعَظِيمِ
"Hakika amekwishafikieni Mtume anayetokana na nyinyi... mtegemeo wangu ni Allah; hapana mungu ila Yeye; nimemtegemea Yeye, na Yeye ndiye Mola wa Kiti Kikubwa cha Enzi." (QS. At-Tawbah [9]: 128-129)
Na haiwezekani kipande hicho kiwe ni wakati wa kunakili katika zama za Uthman kwa sababu ukusanyaji wa vipande ulikuwa zama za Abu Bakr na si zama za Uthman ambapo kulikuwa na unakili... Kwa hiyo, mwisho wa hadithi ya Bukhari namba 4604 unakataliwa kwa upande wa diraya (uchambuzi wa maana) nao ni (Ibn Shihab amesema: Na Kharijah bin Zaid bin Thabit aliniambia, alimsikia Zaid bin Thabit akisema: Nilikosa aya moja ya Al-Ahzab tulipokuwa tunanakili Mus-haf... tukaipata kwa Khuzaima bin Thabit al-Ansari...).
- Kuhusu suala la pili nalo ni je, Sahaba ambaye Zaid alizipata aya mbili za At-Tawbah zikiwa zimeandikwa kwake na hakuzipata zimeandikwa kwa mwingine, ni Khuzaima au Abu Khuzaima? Jibu la hilo ni kama ifuatavyo:
- Bukhari ametoa riwaya mbili: (4311) na (4603)...
Ama riwaya namba 4311 iliyotajwa hapo juu, imekuja ndani yake: [...Nikasimama na nikaifuatilia Qur'an nikiikusanya kutoka kwenye vipande vya ngozi... mpaka nikapata kutoka Surah At-Tawbah aya mbili kwa Khuzaima al-Ansari, sikujaipata kwa yeyote mwingine ghairi yake...]
- Na katika hadithi namba 4603 na hii ndiyo nukuu yake: [4603 – Musa bin Ismail ametuhadithia kutoka kwa Ibrahim bin Saad, Ibn Shihab ametuhadithia kutoka kwa Ubayd bin al-Sabbaq kwamba Zaid bin Thabit (ra) amesema: Abu Bakr alinitumia ujumbe baada ya mauaji ya watu wa Yamamah... basi nikaifuatilia Qur'an nikiikusanya kutoka kwenye kuta za mitende ya tende, mawe meupe membamba (likhaf), na vifua vya watu, mpaka nikapata mwisho wa Surah At-Tawbah kwa Abu Khuzaima al-Ansari, sikujaipata kwa yeyote mwingine ghairi yake...]
Na ni wazi kutokana na kauli yake: [...mpaka nikapata mwisho wa Surah At-Tawbah kwa Abu Khuzaima al-Ansari, sikujaipata kwa yeyote mwingine ghairi yake ﴿لَقَدْ جَاءَكُمْ رَسُولٌ مِنْ أَنْفُسِكُمْ عَزِيزٌ عَلَيْهِ مَا عَنِتُّمْ﴾ mpaka tamati ya Bara’ah (At-Tawbah).]
Na kwa kutazama na kutafakari kwa kina yaliyokuja katika hadithi hizo mbili, inabainika kuwa Sahaba huyo jina lake ni Khuzaima bin Thabit al-Ansari na si Abu Khuzaima. Ushahidi wa hilo ni kwamba Abu Bakr (ra) alisharti kuwa mashahidi wawili washuhudie juu ya kipande kilichotajwa kwamba kiliandikwa mbele ya Mtume wa Allah (saw), na Zaid alipata mashahidi wawili kwa kila aya iliyoandikwa aliyoitegemea Zaid isipokuwa aya mbili za mwisho wa At-Tawbah. Hakuzipata zimeandikwa katika kipande isipokuwa kwa Khuzaima katika riwaya moja, na kwa Abu Khuzaima katika riwaya nyingine. Na matokeo yalikuwa ni kukitegemea kipande hicho. Hivyo basi, ni lazima yule aliyepatikana na kipande hicho ushahidi wake uwe ni sawa na ushahidi wa watu wawili, vinginevyo kipande hicho kisingetegemewa kama alivyosharti Abu Bakr (ra).
Na yule ambaye ilithibiti kutoka kwa Mtume wa Allah (saw) kwamba ushahidi wake ni sawa na ushahidi wa watu wawili ni Khuzaima bin Thabit al-Ansari. Na ni kama vile hadithi hiyo ilikuwa kwa ajili ya hali hii, yaani hali ya kukusanya vipande vilivyoandikwa. Basi ametakasika Allah Mwenye Nguvu, Mwenye Hikima, Mhifadhi wa Kitabu Chake kwa upande wa usomaji na maandishi. Na hadithi ya Khuzaima ni kama ifuatavyo:
Ahmad ametoa katika Musnad yake na Abu Daud katika Sunan yake na lafudhi ni ya Ahmad: (Abu al-Yaman ametuhadithia, Shuaib ametuhadithia kutoka kwa al-Zuhri, Umarah bin Khuzaima al-Ansari alinihadithia kwamba ami yake alimhadithia – naye ni miongoni mwa Masahaba wa Mtume (saw) – kwamba Mtume (saw) alinunua farasi kutoka kwa mbedui, kisha Mtume (saw) akamtaka amfuate ili amlipe thamani ya farasi wake. Mtume (saw) akaenda haraka na mbedui akachelewa, watu wakaanza kumzuia yule mbedui na kumfanyia mnada wa yule farasi, hawajui kwamba Mtume (saw) ameshamnunua, mpaka baadhi yao wakamzidi yule mbedui katika mnada kwa thamani kubwa kuliko farasi aliyonunuliwa nayo na Mtume (saw). Mbedui akamwita Mtume (saw) na kusema: Ikiwa unamnunua farasi huyu basi mnunue, vinginevyo nitamuuzia mwingine. Mtume (saw) akasimama aliposikia mwito wa mbedui akasema: Kwani si nimeshamnunua kwako? Mbedui akasema: Hapana, wallahi sikukuuzia. Mtume (saw) akasema: Kwani, nimeshamnunua kwako. Watu wakaanza kumzunguka Mtume (saw) na yule mbedui huku wakibishana, mbedui akaanza kusema: Lete shahidi atakayeshuhudia kwamba nimekuuzia. Muislamu yeyote aliyekuja akamwambia mbedui: Ole wako! Mtume (saw) hawezi kusema isipokuwa ukweli. Mpaka Khuzaima akaja na kusikiliza mabishano ya Mtume (saw) na mabishano ya mbedui, mbedui akaanza kusema: Lete shahidi atakayeshuhudia kwamba nimekuuzia. Khuzaima akasema: Mimi nashuhudia kwamba umemuuzia. Mtume (saw) akamgeukia Khuzaima na kusema: Unashuhudia kwa nini? Akasema: Kwa kukusadikisha wewe, Ewe Mtume wa Allah. Basi Mtume (saw) akafanya ushahidi wa Khuzaima kuwa ni ushahidi wa watu wawili.) Na akaitoa kadhalika al-Hakim katika al-Mustadrak ‘ala al-Sahihayn na akasema: (...Hii hadithi ina sanadi sahihi na watu wake kwa makubaliano ya Masheikh wawili (Bukhari na Muslim) ni waaminifu na hawakuitoa.)
Haya yote yanathibitisha kuwa Sahaba ambaye kilipatikana kwake kile kipande kilichoandikwa aya mbili za At-Tawbah na hakikuonekana kwa mwingine ni Khuzaima na si Abu Khuzaima, kwa sababu aya hiyo ilitegemewa kwa kuzingatia kuwa ushahidi wa mbebaji wake ni sawa na ushahidi wa watu wawili, na hili linaambatana na Khuzaima na haliambatani na Abu Khuzaima... Na inaonekana jina liliwatatiza wasimulizi kati ya Khuzaima na Abu Khuzaima na hili hutokea wakati mwingine... Vyovyote iwavyo, yeye ni Khuzaima bin Thabit al-Ansari kama tulivyobainisha hapo juu.
Hivyo basi, jibu limekamilika kwa swali lako... na jibu kadhalika kwa masuala mawili yaliyo juu... na Allah ni Mjuzi zaidi na Mwenye Hikima zaidi.
Ndugu yenu Ata bin Khalil Abu al-Rashtah
12 Rabi’ al-Awwal 1441 H Sawa na 09/11/2019 M