Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

Jibu la Swali: Sababu ya Kisheria ya Hukmu (Illatul Hukm)

January 14, 2019
6791

(Mfululizo wa Majibu ya Mwanachuoni Mtukufu Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah, Amir wa Hizb ut-Tahrir, kwa Maswali ya Wageni kwenye Ukurasa wake wa Facebook "Feqhi")

Jibu la Swali

Kwa Abu Nizar Al-Shami

Swali:

Assalamu Alaikum, Baraka za Allah ziwe kwako,

Swali letu Sheikh: Je, inastambatiwa (inachukuliwa) kutoka katika aya isemayo: ﴿ذَلِكَ أَدْنَى أَنْ يُعْرَفْنَ فَلَا يُؤْذَيْنَ﴾ sababu ya hukmu (Illah)?

Jibu:

Wa Alaikum Salaam Wa Rahmatullahi Wa Barakatuh.

Hakika aya hiyo tukufu ni hekima (hikmah) ya kufaradhiwa kwa Jilbab na si sababu ya kisheria (illatul hukm). Huu hapa ni ufafanuzi:

1- Kama tulivyoeleza katika jibu la swali la tarehe 10/07/2018, chanzo cha kuteremka kwa aya hii (asbab al-nuzul) kilikuwa ni kuwatofautisha wanawake waungwana (al-hara-ir) na watumwa wa kike (al-imaa). Watumwa wa kike hawakuwa wamefaradhiwa kuvaa Jilbab, na baadhi ya wanafiki walikuwa wakiwaingilia watumwa hao kwa maneno yasiyofaa, wakijua kuwa adhabu ya kuwasumbua watumwa wa kike ilikuwa ni nyepesi na si kama ile ya wanawake waungwana. Ilikuwa inaposikika kuwa mmoja wao amemfanyia hivyo mwanamke muungwana na kupelekwa mahakamani, alikuwa akisema "Nalidhani ni mtumwa" ili apunguziwe adhabu... Ndipo ikashuka aya tukufu kuwakatia kisingizio hiki, ikafaradhisha kwa waumini wa kike waungwana wajipambanue na watumwa wa kike kwa kuvaa Jilbab na kuliteremsha mpaka chini ya miguu. Hivyo, wale (wanafiki) wasiweze kusema "Tulidhani ni mtumwa" na wasipunguziwe adhabu kwa sababu hawana hoja tena... Ibn Saad ametoa katika Al-Tabaqat kutoka kwa Abi Malik akisema: "Wakeze Nabii (saw) walikuwa wakitoka usiku kwa mahitaji yao, na baadhi ya watu miongoni mwa wanafiki walikuwa wakiwafuatilia na kuwaudhi. Walipoulizwa wanafiki kuhusu hilo walisema: 'Sisi tunawafanyia hivyo watumwa tu'. Hapo ikashuka aya hii":

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ قُلْ لِأَزْوَاجِكَ وَبَنَاتِكَ وَنِسَاءِ الْمُؤْمِنِينَ يُدْنِينَ عَلَيْهِنَّ مِنْ جَلَابِيبِهِنَّ ذَلِكَ أَدْنَى أَنْ يُعْرَفْنَ فَلَا يُؤْذَيْنَ

"Ewe Nabii! Waambie wake zako, na binti zako, na wake za Waumini wajiteremshie nguo zao (jilbab). Hivyo ni karibu zaidi ili watambulikane, wasiudhiwe." (QS. Al-Ahzab [33]: 59)

Kwa hiyo, maana ya aya ni kutambuliwa kwa muungwana kutoka kwa mtumwa, na kuteremsha Jilbab ni kwa ajili ya utambulisho huu ﴿ذَلِكَ أَدْنَى أَنْ يُعْرَفْنَ فَلَا يُؤْذَيْنَ﴾... Yaani si kwa ajili ya kumtambua mwanamke kuwa ni fulani bin fulani. Imekuja katika Tafsiri ya Al-Qurtubi (14/244): (Neno lake Allah: ﴿ذَلِكَ أَدْنَى أَنْ يُعْرَفْنَ فَلَا يُؤْذَيْنَ﴾ yaani wanawake waungwana, ili wasichanganyike na watumwa... hivyo tamaa zikatika kwao. Na maana yake si kumtambua mwanamke mpaka ijulikane ni nani hasa).

2- Kuna tofauti kati ya Illah na Hikmah. Illah ni kichocheo cha kutungwa kwa sheria (al-ba’ith ala al-tashree’), na hupatikana kutoka katika andiko (nass) - kama tulivyoeleza huko nyuma. Hata hivyo, kuna maandiko ambayo maana ya kisharia (illiyyah) inaonekana kulingana na zana za kisharia zilizotumika au muundo wa sentensi, lakini viashiria vingine (qarain) - iwe ndani ya andiko lenyewe au nje yake - huzuia maana hiyo ya illah na kutoa maana nyingine ambayo ni lengo la Mwenye Sheria analokusudia kufikia kupitia sheria hiyo, na si kichocheo cha kuisharia. Imezoeleka kitaalamu kuita lengo hili au matokeo yanayobainisha kusudio la Mwenye Sheria kutokana na hukmu kuwa ni "hekima" (hikmah) na si sababu (illah), kwa sababu siyo iliyopelekea kutungwa kwa sheria hiyo.

Illah inaenda sambamba na hukmu; ikiwepo na hukmu ipo, na isipokuwa na hukmu haipo. Ama hekima si hivyo. Kwa mfano:

  • ﴿لِيَشْهَدُوا مَنَافِعَ لَهُمْ

"Ili washuhudie manufaa yao" (QS. Al-Hajj [22]: 28).

  • ﴿وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ

"Nami hakuwaumba majini na watu ila waniabudu Mimi." (QS. Adh-Dhariyat [51]: 56).

  • ﴿إِنَّ الصَّلاَةَ تَنْهَى عَنْ الْفَحْشَاءِ وَالْمُنْكَرِ

"Hakika Sala inazuia mambo machafu na maovu." (QS. Al-Ankabut [29]: 45).

Miundo ya maandiko yaliyotangulia pamoja na viashiria vyake, iwe kutoka andiko lenyewe au kwingineko, inabainisha kutokuwepo kwa sababu (illiyyah) kwa maana ya kichocheo cha sheria. Kwani kama ingekuwa ni illah, basi isingeachana na hukmu. Illah haitengani na hukmu, kwani hukmu inakuwepo na kutoweka nayo kwa sababu imesharishwa kwa ajili yake. Lakini hekima (hikmah) inaweza kupatikana katika baadhi ya hali na isipatikane katika hali nyingine, yaani inaweza kukosekana wakati mwingine:

  • ﴿لِيَشْهَدُوا مَنَافِعَ لَهُمْ﴾... Wapo wengi wanaohiji na hawashuhudii manufaa.

  • ﴿وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ﴾... Wapo viumbe wengi ambao hawamuabudu Allah.

  • ﴿إِنَّ الصَّلاَةَ تَنْهَى عَنْ الْفَحْشَاءِ وَالْمُنْكَرِ﴾... Na kuna wanaoswali lakini hawachi maovu.

Kwa ajili hiyo, mifano kama hii huitwa (hekima/hikmah) na si (sababu/illah) kwa sababu hukmu inaweza kuwepo bila hekima hiyo kupatikana. Na hivyo ndivyo ilivyo kwa kila jambo ambalo ni sahihi kuitwa hekima.

3- Sasa tuitafakari aya tukufu ambayo ni mada ya swali letu:

a- Hukmu ya kisheria inatokana na: ﴿يُدْنِينَ عَلَيْهِنَّ مِنْ جَلَابِيبِهِنَّ﴾, huu ndio ushahidi (dalili).

b- Ni wazi kuwa ﴿ذَلِكَ أَدْنَى أَنْ يُعْرَفْنَ فَلَا يُؤْذَيْنَ﴾ siyo kichocheo cha sheria, yaani si ushahidi wa kufaradhiwa kwa Jilbab, na hivyo si illah. Bali ni matokeo yanayotokana na kuvaa Jilbab, yaani ni lengo la Mwenye Sheria analokusudia.

c- Na matokeo haya yanaweza yasipatikane; mwanamke muungwana anaweza kuvaa Jilbab na kusiwe na watumwa wa kike wa kutofautishwa nao ili asiudhiwe...

d- Kwa hivyo, ﴿ذَلِكَ أَدْنَى﴾ ni hekima katika istilahi ya Usul al-Fiqh na si sababu (illah).

Hiki ndicho ninachoona, na Allah ni Mjuzi zaidi na Mwenye Hekima zaidi.

Ndugu yenu, Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah

07 Jumada Al-Ula 1440 H Sawa na 13/01/2019 M

Link ya jibu kutoka kwenye ukurasa wa Facebook wa Amir (Allah amuhifadhi)

Link ya jibu kutoka kwenye ukurasa wa Google Plus wa Amir (Allah amuhifadhi)

Link ya jibu kutoka kwenye tovuti ya Amir (Allah amuhifadhi)

Share Article

Share this article with your network