Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

JIBU LA SWALI: HALALI IKO WAZI NA HARAMU IKO WAZI

March 20, 2024
2217

Mfululizo wa Majibu ya Mwanachuoni Mtukufu Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah, Amir wa Hizb ut-Tahrir, kwa Maswali ya Wafuasi wa Ukurasa Wake wa Facebook "Fiqhi"

Jibu la Swali

HALALI IKO WAZI NA HARAMU IKO WAZI

Kwa Hussein Khamayseh

Swali:

Assalamu Alaikum wa Rahmatullahi wa Barakatuh.

Amir wetu na mpendwa wetu, Allah awe radhi nawe na akulinde kwa kile Alichokilinda kacho Kitabu Chake na mawalii Wake.

Imetajwa katika kijitabu cha Izaalat al-Atribah ‘an al-Juzoor ukurasa wa 58, aya ya kwanza, Hadithi: "Halali iko wazi na haramu iko wazi... na yeyote anayetumbukia katika mambo ya shaka ni kama mchungaji..." Inaonekana yameanguka (yamesahaulika) maneno "ametumbukia katika haramu". Naomba uhakiki na ufanye ihsani ya kunijibu, Allah akulinde na akuchunge ewe mpendwa... kwa upendo na heshima tele.

Jibu:

Waalaykum Salaam wa Rahmatullahi wa Barakatuh.

Barakallahu fika kwa dua yako nzuri, ukweli wa maneno yako, na uzuri wa mazungumzo yako. Allah akulinde na kila baya na akuepushe na kila shari.

Kuhusiana na Hadithi tukufu (Halali iko wazi na haramu iko wazi...), kile tulichokitaja katika kijitabu hicho ni Hadithi ya Al-Bukhari, na ni kwa tamko lililopokelewa:

الْحَلاَلُ بَيِّنٌ وَالْحَرَامُ بَيِّنٌ، وَبَيْنَهُمَا مُشَبَّهَاتٌ لاَ يَعْلَمُهَا كَثِيرٌ مِنْ النَّاسِ، فَمَنْ اتَّقَى الْمُشَبَّهَاتِ اسْتَبْرَأَ لِدِينِهِ وَعِرْضِهِ، وَمَنْ وَقَعَ فِي الشُّبُهَاتِ كَرَاعٍ يَرْعَى حَوْلَ الْحِمَى يُوشِكُ أَنْ يُوَاقِعَهُ، أَلاَ وَإِنَّ لِكُلِّ مَلِكٍ حِمىً، أَلاَ إِنَّ حِمَى اللَّهِ فِي أَرْضِهِ مَحَارِمُهُ أَلاَ وَإِنَّ فِي الْجَسَدِ مُضْغَةً إِذَا صَلَحَتْ صَلَحَ الْجَسَدُ كُلُّهُ وَإِذَا فَسَدَتْ فَسَدَ الْجَسَدُ كُلُّهُ أَلاَ وَهِيَ الْقَلْبُ

"Halali iko wazi na haramu iko wazi, na kati ya viwili hivyo kuna mambo yenye kutatanisha (shaka) ambayo watu wengi hawayajui. Basi yeyote anayejiepusha na mambo hayo yenye kutatanisha, anakuwa ameitakasa dini yake na heshima yake. Na yeyote anayetumbukia katika mambo hayo yenye kutatanisha ni kama mchungaji anayechunga kando ya mpaka (wa ardhi iliyohifadhiwa), anaokaribia kuingia ndani yake. Jueni kuwa kila mfalme ana mpaka wake, na hakika mpaka wa Mwenyezi Mungu katika ardhi yake ni mambo Aliyoyaharamisha. Jueni kuwa katika mwili kuna pande la nyama, likitengenea, basi mwili mzima hutengenea, na likiharibika, basi mwili mzima huharibika; nalo ni moyo." (Imepokelewa na Al-Bukhari)

Ama maoni yako kuhusu kuanguka kwa maneno (ametumbukia katika haramu), hayo hayapo katika upokezi wa Al-Bukhari, bali yametajwa katika upokezi wa Muslim kama hivi:

(Swahiyh Muslim (8/290)

2996 - Hadithi ya Muhammad bin Abdullah bin Numayr al-Hamdani, Hadithi ya baba yangu, Hadithi ya Zakaria, kutoka kwa ash-Sha’bi, kutoka kwa al-Nu'man bin Bashir amesema: Nilimsikia akisema: Nilimsikia Mtume wa Allah ﷺ akisema, na Nu'man akaashiria kwa vidole vyake viwili kwenye masikio yake:

إِنَّ الْحَلَالَ بَيِّنٌ وَإِنَّ الْحَرَامُ بَيِّنٌ وَبَيْنَهُمَا مُشْتَبِهَاتٌ لَا يَعْلَمُهُنَّ كَثِيرٌ مِنْ النَّاسِ فَمَنْ اتَّقَى الشُّبُهَاتِ اسْتَبْرَأَ لِدِينِهِ وَعِرْضِهِ وَمَنْ وَقَعَ فِي الشُّبُهَاتِ وَقَعَ فِي الْحَرَامِ كَالرَّاعِي يَرْعَى حَوْلَ الْحِمَى يُوشِكُ أَنْ يَرْتَعَ فِيهِ أَلَا وَإِنَّ لِكُلِّ مَلِكٍ حِمًى أَلَا وَإِنَّ حِمَى اللَّهِ مَحَارِمُهُ أَلَا وَإِنَّ فِي الْجَسَدِ مُضْغَةً إِذَا صَلَحَتْ صَلَحَ الْجَسَدُ كُلُّهُ وَإِذَا فَسَدَتْ فَسَدَ الْجَسَدُ كُلُّهُ أَلَا وَهِيَ الْقَلْبُ

"Hakika halali iko wazi na hakika haramu iko wazi, na kati ya viwili hivyo kuna mambo yenye kutatanisha ambayo watu wengi hawayajui. Basi yeyote anayejiepusha na mambo ya shaka, anakuwa ameitakasa dini yake na heshima yake. Na yeyote anayetumbukia katika mambo ya shaka, ametumbukia katika haramu; kama mchungaji anayechunga kando ya mpaka, anaokaribia kulisha ndani yake. Jueni kuwa kila mfalme ana mpaka wake, na hakika mpaka wa Allah ni mambo Aliyoyaharamisha. Jueni kuwa katika mwili kuna pande la nyama, likitengenea, basi mwili mzima hutengenea, na likiharibika, basi mwili mzima huharibika; nalo ni moyo.")

Kama unavyoona, Al-Bukhari hakuyataja (maneno hayo) katika upokezi wake, na mapokezi yote mawili ni sahihi. Imetajwa katika Fath al-Bari kuhusu upokezi wa Al-Bukhari:

[Fath al-Bari cha Ibn Hajar (1/82)

50 - Hadithi ya Abu Nu’aym, Hadithi ya Zakaria, kutoka kwa ‘Amir amesema: Nilimsikia al-Nu'man bin Bashir akisema:

«سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ ﷺ يَقُولُ الْحَلَالُ بَيِّنٌ وَالْحَرَامُ بَيِّنٌ وَبَيْنَهُمَا مُشَبَّهَاتٌ لَا يَعْلَمُهَا كَثِيرٌ مِنْ النَّاسِ فَمَنْ اتَّقَى الْمُشَبَّهَاتِ اسْتَبْرَأَ لِدِينِهِ وَعِرْضِهِ وَمَنْ وَقَعَ فِي الشُّبُهَاتِ كَرَاعٍ يَرْعَى حَوْلَ الْحِمَى يُوشِكُ أَنْ يُوَاقِعَهُ أَلَا وَإِنَّ لِكُلِّ مَلِكٍ حِمًى أَلَا إِنَّ حِمَى اللَّهِ فِي أَرْضِهِ مَحَارِمُهُ أَلَا وَإِنَّ فِي الْجَسَدِ مُضْغَةً إِذَا صَلَحَتْ صَلَحَ الْجَسَدُ كُلُّهُ وَإِذَا فَسَدَتْ فَسَدَ الْجَسَدُ كُلُّهُ أَلَا وَهِيَ الْقَلْبُ» Imetolewa na Al-Bukhari:

Kauli yake: كَرَاعٍ يَرْعَى

Hivi ndivyo ilivyo katika nakala zote za Al-Bukhari, ikiwa imefutwa jawabu ash-sharti ikiwa مَنْ itaonekana kama shartiyyah. Na sehemu hiyo iliyofutwa imethibiti katika upokezi wa ad-Darimi kutoka kwa Abu Nu’aym, mwalimu wa Al-Bukhari, ambapo amesema: "وَمَنْ وَقَعَ فِي الشُّبُهَات وَقَعَ فِي الْحَرَام، كَالرَّاعِي يَرْعَى". Na inawezekana kuelezea مَنْ katika muktadha wa Al-Bukhari kama mawsuulah, na hapo hapataonekana kuwepo kwa kufutwa (maneno), kwani makadirio yatakuwa: na yule aliyetumbukia katika shaka ni mfano wa mchungaji anayechunga. Na ya kwanza ni bora zaidi kwa sababu ya kudhibitiwa kwa maneno hayo yaliyofutwa katika Swahiyh Muslim na kwingineko kupitia njia ya Zakaria ambayo mwandishi ameitoa kwayo. Na kwa msingi huu, kauli yake كَرَاعٍ يَرْعَى ni sentensi mpya iliyokuja kwa ajili ya kupiga mfano ili kutanabahisha kwa kitu kinachoonekana kile kisichoonekana...

Faida:... Ibn ‘Awn amesema mwishoni mwa Hadithi: Sijui kama mfano huo ni katika maneno ya Mtume ﷺ au ni maneno ya ash-Sha’bi... Na huenda hii ndiyo siri ya Al-Bukhari kufuta kauli yake "وَقَعَ فِي الْحَرَام" ili kile kilicho kabla ya mfano kifungamanishwe nao, na hivyo kusalimika na madai ya idraaj (kuingiza maneno ya mpokezi katika matini ya Hadithi). Na miongoni mwa yanayotia nguvu kutokuwepo kwa idraaj ni upokezi wa Ibn Hibban uliopita, na kadhalika kuthibiti kwa mfano huo kama marfuu’ katika upokezi wa Ibn Abbas na Ammar bin Yasir pia...]

Natumai katika hili kuna utoshelevu, na Allah Ndiye Mjuzi zaidi na Mwenye Hekima zaidi.

Ndugu yenu, Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah

09 Ramadhan 1445 Hijri Inayoendana na 19/03/2024 Miladi

Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir (Allah amlinde) kwenye Facebook

Share Article

Share this article with your network