Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

Jibu la Swali: Hukumu ya Kisheria kuhusu: Upandikizaji wa Viungo, Upasuaji wa Maiti (Anatomia), na Kuchanganyika (Ikhtilat)

December 30, 2018
11822

Mfululizo wa Majibu ya Mwanachuoni Mtukufu Ata bin Khalil Abu al-Rashtah, Amir wa Hizb ut-Tahrir

Kwenye Maswali ya Wafuasi wa Ukurasa Wake wa Facebook "Fiqhi"

Jibu la Swali

Hukumu ya Kisheria kuhusu: Upandikizaji wa Viungo, Upasuaji wa Maiti, na Kuchanganyika

Kwa Lotfi Fékih

Swali:

Maswali kwa Amir wa Hizb ut-Tahrir, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh,

S1: Katika kijitabu (Hukumu ya Sheria kuhusu Uumbaji wa Nakala (Cloning) – Upandikizaji wa Viungo...) cha Sheikh Abdul Qadeem Zallum (rehema za Allah ziwe juu yake), Hizb ut-Tahrir inaharamisha upandikizaji wa viungo kutoka kwa maiti kwenda kwa aliye hai, bila kujali viungo hivyo ni vipi, iwe ni kuokoa mwanadamu kutoka kwenye kifo cha uhakika kama vile kupandikiza moyo, au kutibu ugonjwa miongoni mwa magonjwa kama vile kupandikiza kioo cha jicho (cornea). Inaeleweka pia kutoka kwenye kijitabu hiki na kwenye mafaili ya kifikihi (Dossier) kuwa upasuaji wa maiti (anatomia) ni haramu.

Uislamu unahimiza matibabu hata kwa kitu kilichoharamishwa kulingana na ujuzi wangu, kwa mfano kileo (alcohol) kilichopo katika baadhi ya dawa.

S2: Hakika uharamu wa upasuaji wa maiti unawanyima wanafunzi wa vitivo vya udaktari fursa ya kujifunza na kuujua mwili wa mwanadamu. Je, wataanzaje kazi zao na kufanya upasuaji, kwa mfano, hali ya kuwa hawajui mwili wa mwanadamu?? Pia, uharamu wa upasuaji unamnyima daktari wa kisheria (Forensic Doctor) uwezo wa kujua mazingira ya uhalifu, bila kujali uhalifu huo ni wa namna gani. Hivyo, hawezi kutoa taarifa zinazoweza kuisaidia polisi kuelewa mazingira ya uhalifu na kurahisisha utatuzi wake.

Ninataka kupata hukumu zote za kisheria zinazohusiana na kuchanganyika (ikhtilat). Asante sana.

Lotfi Fékih, Mfamasia nchini Tunisia Pharmacien Lotfi Fékih Tunisia, 11/11/2018M

Jibu:

Wa Alaykum Assalam Warahmatullahi Wabarakatuh,

Kabla ya kujibu maswali yako, hasa swali la kwanza na la pili, ningependa kuashiria kuwa hukumu za kisheria huchukuliwa kutoka kwenye dalili zake. Kazi ya mujtahid wakati wa kutoa hukumu (istinbat) ni kuzifanya nusuusi (maandiko) za kisheria zizungumze ili kujua hukumu ya kisheria, na si kutoa hukumu anayoiona mujtahid inamfaa au anayoona kuna haja nayo. Makusudio ya ijtihadi ni kufanya juhudi ya juu kabisa ili kujua hukumu ya Sheria na si hukumu ya akili. Haifai wakati wa kutoa hukumu za kisheria kuzingatia haja na kutafuta hukumu inayoendana na mahitaji ya watu au matamanio yao, kwani hiyo itakuwa ni hukumu ya mtoaji (mustanbit) na hukumu ya akili, si hukumu ya Sheria... Pamoja na kwamba utafiti unaotakiwa wakati wa ijtihadi ni kutafuta hukumu ya Sheria. Ikiwa dalili za kisheria zinaonyesha hukumu fulani katika kadhia fulani, basi hukumu hiyo ndiyo inayotegemewa, na mahitaji ya watu yanarekebishwa kulingana na hukumu hiyo ya kisheria na si kinyume chake. Yaani haijuzu kurekebisha hukumu ya kisheria ili ikubaliane na haja ya watu au kile wanachofikiria kuwa ni haja, bali ni lazima mahitaji ya watu yarekebishwe ili yaendane na hukumu ya kisheria kwa sababu hukumu ya Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) ndiyo haki inayopaswa kufuatwa...

Na sasa tunakuja kwenye majibu ya maswali yako matatu:

Kwanza: Kuhusu swali lako la upandikizaji wa viungo, ni wazi kuwa umepitia dalili zinazoonyesha uharamu wa kupandikiza viungo kutoka kwa mtu aliyekufa ambaye damu yake imehifadhiwa (ma’sum ad-dam) kwenda kwa aliye hai, kama ilivyoelezwa katika kijitabu cha Cloning. Kijitabu hicho kimetumia mambo mawili kama dalili ya uharamu wa kupandikiza viungo kutoka kwa maiti kwenda kwa aliye hai, nayo ni:

1- Hakuna anayemiliki mwili wa maiti baada ya kifo chake. Maiti mwenyewe hana mamlaka juu ya mwili wake baada ya kufa, wala warithi wake hawana mamlaka juu ya mwili wa maiti baada ya kufa kwake, kama zilivyoonyesha dalili za kisheria... Hivyo, maiti wala warithi hawawezi kutoa kiungo chochote cha mwili wa maiti kwa sababu hakipo katika milki yao wala hawana mamlaka nacho...

2- Haijuzu kumfanyia uadui maiti na kumuudhi, na pia haijuzu kumkata-kata viungo (muthlah)... kama ifuatavyo:

a- Kuhusu uharamu wa uadui na kuudhi, zimepokewa hadithi "zinazoonyesha wazi kwamba maiti ana utakatifu kama wa aliye hai, kama zinavyoonyesha kuwa kufanya uadui dhidi ya utakatifu wa maiti na kumuudhi ni sawa na uadui dhidi ya utakatifu wa aliye hai na kumuudhi. Kama ambavyo haijuzu kumfanyia uadui aliye hai kwa kupasua tumbo lake, au kukata shingo yake, au kung’oa jicho lake, au kuvunja mfupa wake, vivyo hivyo haijuzu kumfanyia uadui maiti kwa kupasua tumbo lake, au kukata shingo yake, au kung’oa jicho lake, au kuvunja mfupa wake. Na kama ilivyo haramu kumuudhi aliye hai kwa kumtukana, au kumpiga, au kumjeruhi, vivyo hivyo ni haramu kumuudhi maiti kwa kumtukana, au kumpiga, au kumjeruhi...", miongoni mwa hadithi hizi ni:

كَسْرُ عَظْمِ الْمَيِّتِ كَكَسْرِهِ حَيّاً

"Kuvunja mfupa wa maiti ni sawa na kuuvunja akiwa hai." (Imepokelewa na Ahmad, Abu Daud, na Ibn Hibban kutokana na Aisha, Mama wa Waumini)

لَا تُؤْذِ صَاحِبَ الْقَبْرِ

"Usimuudhi mwenye kaburi." (Imepokelewa na Ahmad kupitia Amr bin Hazm al-Ansari)

لَأَنْ يَجْلِسَ أَحَدُكُمْ عَلَى جَمْرَةٍ مُتَحَرِّقَةٍ خَيْرٌ لَهُ مِنْ أَنْ يَجْلِسَ عَلَى قَبْرٍ

"Lau mmoja wenu angekalia kaa la moto linalochoma ingekuwa bora kwake kuliko kukalia kaburi." (Imepokelewa na Muslim na Ahmad kupitia Abu Hurairah)

b- Kuhusu kumkata-kata maiti viungo (muthlah), hakika "kung’oa jicho la maiti, au kupasua tumbo lake ili kuchukua moyo wake au figo yake au ini lake au mapafu yake, ili kupandikizwa kwa mtu mwingine anayeyahitaji, kunahesabiwa kuwa ni muthlah (ukataji viungo) kwa maiti, na Uislamu umekataza muthlah":

نَهَى رَسُولُ اللهِ ﷺ عَنِ النُّهْبَى وَالْمُثْلَة

"Mtume wa Allah ﷺ amekataza uporaji na kukata-kata viungo (muthlah)." (Imepokelewa na Bukhari kupitia Abdullah bin Zaid al-Ansari)

سِيرُوا بِاسْمِ اللهِ، وَفِي سَبِيلِ اللهِ، قَاتِلُوا مَنْ كَفَرَ بِاللهِ، وَلَا تَمْثِلُوا وَلَا تَغْدُرُوا وَلَا تَقْتُلُوا وَلِيداً

"Nendeni kwa jina la Allah, na katika njia ya Allah, piganeni na waliomkufuru Allah, na msikate-kate viungo (msifanye muthlah), wala msifanye khiana, wala msiue mtoto mchanga." (Imepokelewa na Ahmad, Ibn Majah, na an-Nasa'i kupitia Safwan bin Assal)

Kulingana na dalili zilizotajwa hapo juu, inaonekana wazi kabisa kwamba kupandikiza kiungo kutoka kwa mtu aliyekufa ambaye damu yake imehifadhiwa kwenda kwa aliye hai ni haramu kisheria... Wala isisemwe kuwa Sheria imeruhusu kutibiwa kwa kitu haramu kama vile kutibiwa kwa kileo kilichopo kwenye dawa, hivyo basi inaruhusiwa kupandikiza kiungo kutoka kwa maiti kwenda kwa aliye hai hata kama upandikizaji huo ni haramu. Haisemwi hivyo kwa sababu matibabu yaliyothibitishwa na Sheria ni kutibiwa kwa haramu na najisi bila ya kufanya uadui au kuwadhuru wengine. Ibn Majah amepokea kupitia Tariq bin Suwaid al-Hadhrami akisema:

قُلْتُ يَا رَسُولُ اللَّهِ إِنَّ بِأَرْضِنَا أَعْنَابًا نَعْتَصِرُهَا فَنَشْرَبُ مِنْهَا قَالَ لَا فَرَاجَعْتُهُ قُلْتُ إِنَّا نَسْتَشْفِي بِهِ لِلْمَرِيضِ قَالَ إِنَّ ذَلِكَ لَيْسَ بِشِفَاءٍ وَلَكِنَّهُ دَاءٌ

"Nilisema Ewe Mtume wa Allah, hakika katika ardhi yetu kuna zabibu tunazozikamua na kunywa (divai) kutokana nazo, akasema hapana. Nikamrejea tena nikasema: Sisi tunazitumia kama tiba kwa mgonjwa, akasema: Hakika hiyo si tiba bali ni ugonjwa."

Huu ni ukatazaji wa kutumia najisi au haramu "pombe" kama dawa. Lakini Mtume ﷺ aliruhusu kutibiwa kwa najisi "mkojo wa ngamia". Bukhari amepokea kupitia Anas (ra):

أَنَّ نَاسًا مِنْ عُرَيْنَةَ اجْتَوْا الْمَدِينَةَ فَرَخَّصَ لَهُمْ رَسُولُ اللَّهِ ﷺ أَنْ يَأْتُوا إِبِلَ الصَّدَقَةِ فَيَشْرَبُوا مِنْ أَلْبَانِهَا وَأَبْوَالِهَا...

"Kwamba watu kutoka kabila la Uraynah walipatwa na maradhi mjini Madina, hivyo Mtume wa Allah ﷺ akawapa rukhsa ya kwenda kwenye ngamia wa sadaka na kunywa maziwa yao na mikojo yao..."

Ijtawu al-Madina: Yaani hali ya hewa haikuwafaa wakaugua. Mtume ﷺ akawaruhusu watibiwe kwa mikojo ya ngamia ambayo ni najisi. Vivyo hivyo, Mtume ﷺ aliruhusu kutibiwa kwa haramu "kuvaa hariri". At-Tirmidhi na Ahmad wamepokea, na tamshi ni la At-Tirmidhi, kupitia Anas:

أَنَّ عَبْدَ الرَّحْمَنِ بْنَ عَوْفٍ وَالزُّبَيْرَ بْنَ الْعَوَّامِ شَكَيَا الْقَمْلَ إِلَى النَّبِيِّ ﷺ فِي غَزَاةٍ لَهُمَا، فَرَخَّصَ لَهُمَا فِي قُمُصِ الْحَرِيرِ. قَالَ: وَرَأَيْتُهُ عَلَيْهِمَا

"Kwamba Abdurrahman bin Awf na az-Zubair bin al-Awwam walimshtakia Mtume ﷺ kuhusu chawa katika vita vyao, naye akawapa rukhsa ya kuvaa mashati ya hariri. Akasema: Nami niliyaona (mashati hayo) yakiwa juu yao."

Hadithi hizi mbili ni kielelezo (qarinah) kwamba ukatazaji katika hadithi ya Ibn Majah si wa mkato, yaani kutibiwa kwa najisi na haramu ni makruhu.

Dalili hizi zinaonyesha kuwa Sheria imeruhusu kutibiwa kwa najisi na haramu kwa makruhu, lakini kutibiwa kwa najisi "mkojo wa ngamia" na kwa haramu "kuvaa hariri" ni tofauti na kutibiwa kwa haramu ambayo inahusisha uadui dhidi ya wengine. Hii ya mwisho haimo katika ubaguzi wa kutibiwa kwa haramu kwa sababu uhalisia wake ni tofauti... Kwa mfano, je, inajuzu kisheria kumfanyia uadui mtu aliye hai kwa kuchukua figo yake kwa lazima ili kumtibu mgonjwa anayehitaji figo (kama inavyotokea katika kile kinachoitwa nchi za ulimwengu wa tatu kwa kutekwa watoto au watu wazima ili kuondoa baadhi ya viungo vyao na kuvipandikiza kwa wagonjwa katika nchi zinazoitwa ulimwengu wa kwanza)? Jibu ni kwamba bila shaka hii ni haramu na haijuzu kwa sababu kuna uadui dhidi ya wengine... Hivyo haramu inayojuzu kutumiwa kwa tiba haijumuishi haramu yenye uadui dhidi ya wengine kwa sababu dalili za kujuzu kutumia haramu kwa tiba hazitumiki kwake. Kwa sababu hiyo, haijuzu kutibiwa kwa kufanya uadui dhidi ya mwili wa maiti kwa kupandikiza viungo vyake kwa aliye hai, kwa sababu jambo hili ni haramu kutokana na uadui dhidi ya mwili wa maiti na kwa sababu dalili za ubaguzi wa kutibiwa kwa haramu hazitumiki kwake.

Pili: Kuhusu swali lako kuhusu upasuaji wa maiti (anatomia) na kwamba kauli ya uharamu wake inazuia wanafunzi kujifunza na kuujua mwili wa mwanadamu, je, wataanzaje kazi zao?! Na kwamba kauli ya uharamu wake inamnyima daktari wa kisheria uwezo wa kujua mazingira ya uhalifu na hivyo kupoteza taarifa muhimu zinazoisaidia polisi kugundua ukweli...

Ndugu yangu, hakika dalili za kisheria zinashirikiana katika kuharamisha uadui dhidi ya mwili wa maiti kama ilivyoelezwa hapo juu. Na maadamu hali ni hiyo, basi upasuaji wa mwili wa maiti ni haramu kisheria kwa sababu ni uadui dhidi ya maiti bila kujali mazingatio mengine yoyote... Ili jambo hili liwe wazi zaidi, nakuuliza: Je, inafaa kwa kisingizio cha haja ya wanafunzi kujifunza udaktari na kuujua mwili wa mwanadamu, kufanya uadui dhidi ya mwili wa mtu aliye hai na kumfanyia upasuaji kwa lazima bila ya kumuua, kama vile kufungua tumbo lake na kuchunguza viungo vyake vya ndani? Jibu lako litakuwa ni kwamba bila shaka hii haijuzu kwa sababu ni uadui dhidi ya mwili wa huyu mwanadamu aliye hai... Kwa nini basi inakuingia akilini kujuzu kwa jambo hilo kwa mwanadamu aliyekufa hali ya kuwa Mtume ﷺ anasema: «كَسْرُ عَظْمِ الْمَيِّتِ كَكَسْرِهِ حَيّاً» (Kuvunja mfupa wa maiti ni sawa na kuuvunja akiwa hai)? Hakika hukumu ya kisheria ina haki zaidi ya kufuatwa, na haijuzu kuiacha kwa kisingizio chochote...

Ama kuhusu wanafunzi wa udaktari kujifunza na kuujua mwili wa mwanadamu, njia mbalimbali za mubah ni nyingi. Pia, ni juu ya Waislamu kuendeleza mbinu za kisasa zinazowawezesha wanafunzi kuujua mwili wa mwanadamu kwa njia bora zaidi bila ya kuelekea kwenye upasuaji wa maiti, kwa mfano kuendeleza programu za kompyuta zinazowawezesha wanafunzi kushughulika kielektroniki na picha za pande tatu (3D) za viungo vya mwili wa mwanadamu n.k. Au kwa njia yoyote ya kupiga picha kutoka nje ya mwili ili kuona ndani yake au njia nyinginezo za teknolojia ya kisasa... Huku ikijulikana kuwa nimepata habari kutoka kwa baadhi ya wanafunzi wa udaktari kuwa hawajafaidika na chochote cha maana kutokana na somo la upasuaji wa maiti, hasa kwa kuwa miili inayopasuliwa huwa imewekwa kwenye kemikali zinazoathiri asili ya misuli na mishipa ya damu na kuwa tofauti sana na asili ya mwili ulio hai...

Pia, kuhusu kugundua ukweli wa uhalifu, haifai kuelekea kwenye kile alichokiharamisha Allah cha upasuaji wa mwili wa maiti, kama vile ambavyo haijuzu kisheria kuelekea kwenye kumtesa mtuhumiwa ili kugundua ukweli wa uhalifu... Suluhisho ni kutafuta njia na mbinu za mubah za kutafiti na kuweka wazi ukweli, na si kwa kuasi amri ya Sheria na kwa kufanya uadui dhidi ya mwili wa maiti ambaye heshima yake iko katika kumzika...

Tatu: Ama kuhusu swali lako juu ya kuchanganyika (ikhtilat), ni swali ambalo halijabainishwa wazi kwani unaomba "kupata hukumu zote za kisheria zinazohusiana na kuchanganyika"!! Ingekuwa bora zaidi uulize kuhusu jambo maalumu ili tukujibu... Vyovyote iwavyo, nitakuwekea baadhi ya majibu yetu ya awali juu ya mada ya kuchanganyika, huenda yakafunika baadhi ya nyanja unazoulizia, na ikiwa una suala maalumu ambalo halijatajwa katika majibu hapa chini, basi litaje:

  • Jibu la swali mnamo 28/02/2010M ambamo ilikuja:

(Uwepo wa wanaume na wanawake katika maisha ya Kiislamu uliothibitishwa na Mtume ﷺ, na dalili za kisheria zinazopanga miamala ya kisheria kati ya wanaume na wanawake... yote hayo yameelezwa wazi, na yameshatolewa majibu zaidi ya moja katika jambo hili, na tulikuwa tukitumaini kusiwe na utata katika jambo hili.

Pamoja na hayo, katika barua hii, nitazidi kufafanua jambo hili zaidi kwa idhini ya Allah, nikitumaini kuondoa utata wowote katika suala hili:

  • Maisha ya umma yanamaanisha uwepo wa wanaume na wanawake katika maeneo ya umma ambayo kuingia kwake hakuhitaji idhini, na haya yana hukumu za kisheria zinazowapanga wanaume na wanawake wakati huo.

Na maisha ya faragha ni katika maeneo ambayo kuingia kwake kunahitaji idhini kama vile nyumba, na haya pia yana hukumu za kisheria zinazowapanga wanaume na wanawake wakati huo.

  • Ama maisha ya faragha "nyumbani", jambo lake liko wazi, na halihitaji ufafanuzi zaidi, kwani maisha ya wanawake humo huwa pamoja na maharimu wao na si pamoja na wanaume ajnabi, isipokuwa ikiwa imekuja nusuusi katika hali maalumu kama vile kuunga udugu (silat ar-rahim), ambapo inajuzu kwa jamaa kumtembelea jamaa yake wa kike hata kama si maharimu wake, kama vile mtoto wa ami kwenda kumsalimia binti wa ami yake wakati wa sikukuu, na bila shaka bila ya kuwa na faragha (khalwa), na bila ya kukashifu aurat, kama vile kwenda na baba yake au ami yake na kuunga udugu wake hata kama si miongoni mwa maharimu.

  • Ama maisha ya umma, ikiwa kuna haja inayokubaliwa na Sheria ya kukutana wanaume na wanawake wakati huo, basi inajuzu mkutano huu katika sura yake ya kisheria, na tunasema katika sura yake ya kisheria kwa sababu kuna hukumu za kisheria zinazopanga mkutano huu kama ifuatavyo:

1- Uwajibikaji wa kutenganisha safu za wanaume na wanawake ikiwa haja inayokubaliwa na Sheria kwa uwepo wa wanaume na wanawake ni kwa ajili ya lengo moja kwa waliokutana, kama vile uwepo wa wanaume na wanawake kwa ajili ya swala, au kuhudhuria darsa ya elimu, au muhadhara wa da’wah, au kazi ya jumla miongoni mwa kazi za da’wah... Katika hali hizi, inajuzu uwepo wa wanaume na wanawake pamoja na kutenganisha safu, na hivi wakati mwingine huitwa maisha ya umma yenye hukumu maalumu, yaani kuna namna maalumu ya uwepo wa wanaume na wanawake.

2- Kutowajibika kutenganisha safu katika maisha ya umma ikiwa haja inayokubaliwa na Sheria kwa uwepo wa wanaume na wanawake ni kwa ajili ya malengo tofauti kwa waliokutana, kama vile uwepo wa wanaume na wanawake sokoni, au barabarani, au katika bustani ya umma, au wakati wa kupanda mabasi ya umma... Na haya ni aina mbili:

a- Malengo tofauti hayatekelezwi humo isipokuwa kwa kuchanganyika, yaani mchanganyiko (khultah), kwa kukaa jirani na kuzungumza, kama vile kuuza na kununua sokoni, na aina hii inajuzu kuchanganyika humo.

b- Malengo tofauti yanatekelezwa humo bila ya kuchanganyika, yaani bila ya mchanganyiko wa kukaa jirani na kuzungumza, kama vile kupanda mabasi ya umma, bustani za umma na kutembea barabarani... Aina hii inajuzu uwepo wa wanaume na wanawake humo bila ya kuchanganyika, yaani bila ya mchanganyiko, kukaa jirani na kuzungumza, bali inawezekana kuwepo jirani, kila mmoja kwa lengo na shabaha yake, bila ya kuzungumza pamoja, kama vile kutembea barabarani, bustani za umma, na kupanda mabasi ya umma...

  • Kama unavyoona, hukumu za uwepo wa wanaume na wanawake ziko wazi na zimebainishwa katika maisha ya faragha na maisha ya umma:

Maisha ya faragha "nyumba" ni yale ambayo kuingia kwake kunahitaji idhini, na maisha ya umma ni yale ambayo kuingia kwake hakuhitaji idhini. Na miongoni mwa maisha haya ya umma kuna yale yanayohitaji kutenganisha safu na miongoni mwake kuna yale hayahitaji kutenganisha safu. Vivyo hivyo, miongoni mwa maisha ya umma kuna yale ambayo inajuzu kuchanganyika humo yaani mchanganyiko, kukaa jirani na kuzungumza, na miongoni mwake kuna yale hayajuzu mchanganyiko humo, bali inajuzu tu kukaa jirani bila kuzungumza...) Mwisho.

Natumaini katika hayo kutakuwa na utoshelevu.

  • Jibu la swali mnamo 06/02/2011M ambamo ilikuja:

(... Lakini kuwa na vikosi vya wanawake katika jeshi kwa ajili ya uuguzi wa majeruhi wa vita, jambo hili imekuja kuwa Mtume ﷺ aliruhusu wanawake kuwepo katika uwanja wa vita kwa ajili ya uuguzi na matibabu, hivyo mkutano katika hali ya matibabu unakuwa ni mubah. Na hivyo ndivyo. Bukhari amepokea katika al-Adab al-Mufrad na at-Tarikh al-Saghir kwa isnadi aliyoishahihisha al-Albani kutoka kwa Mahmoud bin Labid amesema:

لَمَّا أُصيبَ أَكْحَلُ سَعْدٍ يَوْمَ الخَنْدَقِ فَثَقُلَ، حَوَّلوهُ عِنْدَ امْرَأَةٍ يُقالُ لَها: رُفَيْدَة، وَكانَتْ تُداوي الجَرْحى، فَكانَ النَّبِيُّ ﷺ إِذا مَرَّ بِهِ يَقولُ: كَيْفَ أَمْسَيْتَ؟ وَإِذا أَصْبَحَ: كَيْفَ أَصْبَحْتَ؟ فَيُخْبِرُهُ

"Alipoumia mshipa wa mkono wa Saad siku ya handaki (Khandaq) na hali ikawa nzito, walimpeleka kwa mwanamke aitwaye Rufaydah, ambaye alikuwa akitibu majeruhi. Mtume ﷺ alikuwa akipita kwake na kusema: Umeshindaje? Na anapopambazuka: Umeamkaje? Naye anamfahamisha." Rufaydah huyu ni mwanamke kutoka kabila la Aslam aliyekuwa akitibu majeruhi.

  • Kuchanganyika (ikhtilat) ni kama nilivyotaja hapo awali, yaani kukutana kwa wanaume na wanawake ajnabi kwa ajili ya jambo lisilo na haja inayokubaliwa na Sheria ambayo haitekelezwi isipokuwa kwa kukutana. Katika hali hii, yaani kwa ajili ya jambo lisilo na haja, haijuzu. Ama ikiwa ni kwa ajili ya haja inayokubaliwa na Sheria ambayo haitekelezwi isipokuwa kwa kukutana, basi inajuzu.

Zimekuja dalili zinazokubali mkutano kwa ajili ya mahitaji yaliyobainishwa na Sheria, iwe ni katika maisha ya faragha au ya umma. Kwa mfano, katika maisha ya faragha ni kuunga udugu (silat ar-rahim), chakula, na kumtembelea mgonjwa... Na katika maisha ya umma ni kutibu majeruhi vitani... na kwenda masokoni, swala misikitini, kuhudhuria majlisi za elimu, na hija... Yote hayo ni kulingana na hukumu za kisheria kwa upande wa kutenganisha safu kama misikitini na mihadhara ya umma, au bila ya kutenganisha kama sokoni na hija...

Na kuunga udugu si kwa ajili ya jamaa maharimu tu, bali ni kwa ajili ya jamaa wasio maharimu pia kama vile binti wa ami... "Angalia silat ar-rahim katika mfumo wa kijamii", basi hili linajuzu kwa jamaa kutembeleana katika sikukuu au katika matukio mbalimbali, na kukaa pamoja, lakini iwe ni kwa ajili ya kuunga udugu, yaani kuulizana afya na hali, na kumtembelea mgonjwa wao, na kukidhi mahitaji na mfano wa hayo. Lakini si kukaa pamoja "wakicheza karata kwa mfano" au watoke pamoja kwa ajili ya matembezi, na kukaa pamoja bustanini wakipiga soga... hili halijuzu.

Hivyo basi, ziara ya jamaa kutembeleana, na kukaa kwao pamoja, wanaume na wanawake, inajuzu maadamu ni kwa ajili ya kuunga udugu, yaani kukaa pamoja kuwe kwa kiasi kinachohusiana na kuunga udugu. Ikiwa kukaa huko kutageuka na kuwa ni kupiga soga katika masuala yasiyohusu kuunga udugu, basi wanawake wakae chumba chao na wanaume chumba chao... Vivyo hivyo, inajuzu kwao wakati wa kula kukaa pamoja, na chakula kinapomalizika wanawake wakae chumba chao na wanaume chumba chao...

فَإِذَا طَعِمْتُمْ فَانْتَشِرُوا وَلا مُسْتَأْنِسِينَ لِحَدِيث

"Na mkishakula, basi tawanyikeni, wala msikae kwa mazungumzo." (QS. Al-Ahzab [33]: 53)

Hivyo kuunga udugu na chakula zimekuja dalili ndani yake.

Na bila shaka wanawake wawe wamesitiri aurat zao, na maharimu wao au waume zao wawepo, kama ilivyo katika mfumo wa kijamii.) Mwisho.

  • Jibu la swali mnamo 06/06/2016M ambamo ilikuja:

(a- Kuchanganyika (ikhtilat), yaani kukutana kwa wanaume na wanawake ajnabi, ni haramu ikiwa ni kwa ajili ya jambo lisilo na haja inayokubaliwa na Sheria... Ama ikiwa ni kwa ajili ya haja inayokubaliwa na Sheria ambayo haitekelezwi isipokuwa kwa kukutana, basi inajuzu.

b- Zimekuja dalili zinazokubali mkutano kwa ajili ya mahitaji yaliyobainishwa na Sheria, iwe ni katika maisha ya faragha au ya umma. Kwa mfano, katika maisha ya faragha pamoja na jamaa, zimekuja dalili za kisheria zinazojuzisha kuunga udugu, chakula, na kumtembelea mgonjwa... Na katika maisha ya umma ni kutibu majeruhi vitani... na kwenda masokoni, swala misikitini, kuhudhuria majlisi za elimu, na hija... Yote hayo ni kulingana na hukumu za kisheria kwa upande wa kutenganisha safu kama misikitini na mihadhara ya umma, au bila ya kutenganisha kama sokoni na hija...

c- Na kuunga udugu si kwa ajili ya jamaa maharimu tu, bali ni kwa ajili ya jamaa wasio maharimu pia kama vile binti wa ami... "Angalia silat ar-rahim katika mfumo wa kijamii", basi hili linajuzu kwa jamaa kutembeleana katika sikukuu au katika matukio mbalimbali, na kukaa pamoja, lakini iwe ni kwa ajili ya kuunga udugu, yaani kuulizana afya na hali, na kumtembelea mgonjwa wao, na kukidhi mahitaji na mfano wa hayo. Lakini si kukaa pamoja "wakicheza karata kwa mfano" au watoke pamoja kwa ajili ya matembezi, na kukaa pamoja bustanini wakipiga soga... hili halijuzu...) Mwisho.

Natumaini katika haya majibu ya maswali yako matatu kuna utoshelevu.

Ndugu yenu, Ata bin Khalil Abu al-Rashtah

23 Rabi’ al-Akhar 1440H Sawiya na 30/12/2018M

Link ya jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir (Allah amhifadhi) kwenye Facebook

Link ya jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir (Allah amhifadhi) kwenye Google Plus

Link ya jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir (Allah amhifadhi) kwenye Web

Share Article

Share this article with your network