Swali: Je, inajuzu kutumia hoja ya hesabu za kifalaki kwa ajili ya nyakati za kufunga na kufuturu kama inavyotumiwa hoja ya hesabu za kifalaki katika nyakati za swala?
Jibu:
1 - Hakika Allah (swt) ametutaka tumuabudu kama Alivyotaka Yeye, na ikiwa tutamuabudu kinyume na Alivyotaka, tutakuwa tumefanya makosa hata kama tutadhani kuwa tunatenda mema.
2 - Allah (swt) ametutaka tufunge na tufuturu kwa kuuona mwezi mwandamo, na Akajaalia kuuona huko kuwa ndio sababu (sabab) ya kufunga na kufuturu:
صُومُوا لِرُؤْيَتِهِ وَأَفْطِرُوا لِرُؤْيَتِهِ
"Somuni kwa kuuona (mwezi) na fungueni kwa kuuona." (Imepokewa na Al-Bukhari na Muslim)
Tukiiona hilali ya Ramadhani tunafunga, na tukiiona hilali ya Shawwal tunafuturu.
3 - Ikiwa hatujaiona hilali ya Shawwal kwa sababu ya mawingu, kwa mfano, yameufunika, basi tunakamilisha funga hata kama mwezi upo kihalisia, lakini hatukuuona kwa sababu ya kizuizi kilichoufunika. Hii ina maana kwamba hatufungi wala kufuturu kwa kuanza kwa mwezi kihalisia (kijogofia). Hadith iko wazi katika jambo hilo:
فَإِنْ أُغْمِيَ عَلَيْكُمْ فَأَكْمِلُوا عِدَّةَ شَعْبَانَ
"Ikiwa mtafunikiwa (na mawingu), basi kamilisheni idadi ya Shaban (siku thelathini)." (Imepokewa na Al-Bukhari)
4 - Allah (swt) hakutukalifisha tumuabudu kwa namna nyingine tofauti na Alivyotaka. Kwa mfano, ikiwa hesabu zinasema kuwa kesho ni Ramadhani kwa yakini – na sasa hivi hesabu za kifalaki zinaamua hali ya mwezi tangu kuzaliwa kwake mpaka kuwa mwezi mpevu kisha kufifia, zikihesabu kwa sekunde – lakini hatukuiona hilali kwa sababu ya mawingu kwa mfano, basi yule anayefunga anakuwa amepata dhambi akijua kuwa Ramadhani kihalisia imeanza. Anapata dhambi kwa sababu mwezi haukuonekana, na wajibu ni kukamilisha siku 30 za Shaban kisha ndipo afunge. Hivyo, yule aliyefunga kwa kufuata uhalisia wa kuanza kwa Ramadhani katika hali hii anakuwa amefanya dhambi kwa sababu amekhalifu (ameenda kinyume), na yule aliyekamilisha idadi ya Shaban asifunge – licha ya kuwa mwezi ulikuwepo lakini mawingu yaliuziba – huyu anapata malipo (ajra) kwa sababu amefuata Hadith.
5 - Kutokana na hili, inabainika kuwa hatufungi wala kufuturu kwa uhalisia wa mwezi (kijogofia), bali kwa kuuona mwezi mwandamo (ru’yah). Tukiuona tunafunga, na tusipouona hatufungi, hata kama mwezi utakuwa umeanza kihalisia kwa mujibu wa hesabu.
6 - Ikiwa mashahidi watakuja na kutoa ushahidi wa kuuona mwezi, basi kushughulika nao ni kama ushahidi mwingine wowote; ikiwa shahidi ni Muislamu na si fasiq, ushahidi wake unakubaliwa. Na ikiwa itabainika kuwa shahidi si Muislamu au si mwadilifu (yaani ni fasiq), basi ushahidi wake haukubaliwi.
7 - Kuthibitisha ufasiki wa shahidi kunafanyika kwa dalili za kisheria na wala si kwa hesabu za kifalaki. Yaani, usitoe hoja dhidi yake kwa kusema kuwa saa chache tu zimepita tangu kuzaliwa kwa mwezi kwa hiyo hauwezi kuonekana... – na inajulikana kuwa kuna khitilafu kati ya wanazuoni wa falaki kuhusu muda wa saa baada ya kuzaliwa mwezi ili uweze kuonekana – hivyo hoja haitolewi dhidi ya shahidi kwa hesabu za kifalaki, bali anaweza kuhojiwa na kuhakikishiwa kuonekana kwake, na anaulizwa uko wapi mwezi, na wengine wanatazama na kadhalika. Kisha ushahidi unakubaliwa kwa kuonekana au unakataliwa kwa msingi huo.
8 - Hakika anayefuatilia nusuusi (maandiko) yaliyokuja kuhusu saumu atayakuta yanatofautiana na nusuusi zilizokuja kuhusu swala. Funga na kufuturu vimeunganishwa na kuuona mwezi (ru’yah):
صُومُوا لِرُؤْيَتِهِ وَأَفْطِرُوا لِرُؤْيَتِهِ
"Somuni kwa kuuona na fungueni kwa kuuona."
فَمَنْ شَهِدَ مِنْكُمُ الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ
"Basi atakayekuwa mjini katika mwezi huu na afunge." (QS. Al-Baqarah [2]: 185)
Hivyo basi, kuonekana (ru’yah) ndiyo hukumu. Lakini nusuusi kuhusu swala zimefungamanishwa na wakati:
أَقِمِ الصَّلَاةَ لِدُلُوكِ الشَّمْسِ
"Simamisha Swala jua linapopinduka." (QS. Al-Isra [17]: 78)
إِذَا زَالَتِ الشَّمْسُ فَصَلُّوا
"Jua linapopinduka (kuelekea magharibi), basi swalini."
Hivyo swala imesimama juu ya wakati, kwa hiyo kwa njia yoyote ile utakayohakikisha wakati, basi unaswali. Ukilitazama jua ili uone wakati wa kupinduka kwake (zawal), au ukitazama kivuli ili uone kivuli cha kila kitu kimekuwa mfano wake au mara mbili yake kama ilivyokuja katika Hadith za nyakati za swala, ukifanya hivyo na ukahakikisha, basi swala ni sahihi. Na usipofanya hivyo bali ukaihesabu kifalaki na ukajua kuwa wakati wa zawal ni saa fulani, ukatama saa yako bila kutoka nje kuona jua au kivuli, swala yako ni sahihi. Yaani, unahakikisha wakati kwa njia yoyote ile. Kwa nini? Kwa sababu Allah (swt) amekutaka uswali kwa kuingia kwa wakati na amekuachia uhakikishe kuingia kwake bila kuainisha namna ya kuhakikisha. Ama kuhusu saumu, Amekutaka ufunge kwa kuuona mwezi (ru’yah), hivyo akakuainishia sababu (sabab), na zaidi ya hapo Akakuambia ikiwa mawingu yataziba uoni usione, basi usifunge hata kama mwezi upo nyuma ya mawingu na ulikuwa na yakini ya kuwepo kwake kwa hesabu za kifalaki.
9 - Hakika Allah (swt) ndiye Muumba wa ulimwengu, na Yeye Ndiye Aliyemfundisha mwanadamu yale aliyokuwa hayajui. Hivyo, elimu ya mwendo wa sayari na mambo yake madogo madogo ni katika fadhila za Allah kwa watu. Lakini Allah (swt) hakututaka tutegemee hesabu kwa ajili ya saumu, bali Alitutaka tuuone mwezi, hivyo tunamuabudu (swt) kama Alivyotaka na hatumuabudu kwa jambo ambalo Hakulitaka.
Hivyo basi, kuuona mwezi pekee ndiyo hukumu katika kufunga na kufuturu na si hesabu za kifalaki. Na kwa msingi huo, tunasema kutofaa (kutojuzu) kwa hesabu za kifalaki katika kufunga na kufuturu, bali ni kuuona mwezi pekee kwa sababu ndivyo vilivyokuja katika nusuusi.
2 Shawwal 1424 H 25/11/2003 M