Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

Jibu la Swali: Kulazimishwa kwa Hatari (Al-Ikrah al-Mulji’) na Uharamu wa Kutoa Moyo kama Msaada

December 26, 2020
3859

Mfululizo wa majibu ya mwanachuoni mtukufu Ata bin Khalil Abu al-Rashtah, Amir wa Hizb ut-Tahrir, kwa maswali ya wafuasi wa ukurasa wake wa Facebook "Fiqhi"

Jibu la Swali

Kwa: Saleem Eshaq

Swali:

Assalamu Alaikum Sheikh wetu na rehema za Allah na baraka zake ziwe juu yako,

Miongoni mwa makusudio ya Sharia (Maqasid al-Shari’ah) ni kulinda nafsi, na makusudio hayamaanishi sababu ya hukumu (‘illah) kwa ujumla wala sababu ya hukumu moja moja. Na katika Sharia kuna kanuni isemayo "Dharura huhalalisha vilivyoharamishwa", na ukweli ni kwamba dharura hiyo inahusu mahususi suala la kula na kunywa ili kubaki hai wakati wa njaa kali inayoangamiza.

Na kulazimishwa kwa hatari (al-Ikrah al-mulji’) huhalalisha kutamka neno la ukafiri ikiwa sehemu ya mali itachukuliwa, au nafsi, au kukatwa sehemu ya mwili, au kutishiwa kwa kulawitiwa au kuzini na maharamu.

Swali langu kwa kuzingatia ufahamu huu: Je, inajuzu kwa mtu ambaye madaktari wamemwambia kuwa anahitaji kupandikizwa moyo, na la sivyo, kwa dhana yenye nguvu (ghalabat al-zhann) atakufa, huku ikijulikana kuwa kutoa moyo msaada baada ya kifo ni haramu, na vivyo hivyo kuchukua kiungo kilichotolewa msaada (si kutoa)?

Nifahamishe, Allah akujaze heri.

Jibu:

Wa Alaikum Salaam Wa Rahmatullahi Wa Barakatuh,

Ni wazi kutokana na swali lako kuwa una uelewa kuhusu mada ya makusudio (maqasid), dharura, kulazimishwa kwa hatari (al-ikrah al-mulji’), na uharamu wa kutoa moyo msaada baada ya kifo... Pamoja na hayo, unauliza kuhusu hukumu ya kupandikiza moyo kwa mtu ambaye madaktari wana dhana yenye nguvu kuwa atakufa ikiwa hatapandikizwa moyo, na unaashiria tofauti kati ya kutoa kiungo na kuchukua kiungo kilichotolewa msaada...

Kwanza: Kabla ya kujibu swali lako, ninakuthibitishia baadhi ya yaliyokuja katika jibu la swali tulilotoa mnamo tarehe 23 Rabi’ al-Akhar 1440 H sawia na 30/12/2018 M kuhusu mada ya kuhamisha viungo:

[...Kuhusu swali lako la kuhamisha viungo, ni wazi kuwa umesoma dalili zinazofahamisha uharamu wa kuhamisha viungo kutoka kwa mtu aliyekufa ambaye damu yake imekingwa (ma’sum al-dam) kwenda kwa aliye hai, kama ilivyobainishwa katika kijitabu cha al-Istinsakh (Uundaji wa Viumbe Maabara). Katika kijitabu hicho, kumetolewa dalili za mambo mawili kuhusu uharamu wa kuhamisha viungo kutoka kwa maiti kwenda kwa aliye hai, nayo ni:

  1. Hakuna anayemiliki mwili wa maiti baada ya kifo chake; maiti mwenyewe hana mamlaka juu ya mwili wake baada ya kufa, na warithi pia hawana mamlaka juu ya mwili wa maiti baada ya kifo chake, kama zinavyofahamisha dalili za kisheria... Kwa hiyo, maiti wala warithi hawamiliki haki ya kutoa kiungo cha mwili wa maiti kwa sababu hakiko katika milki yao wala hawana mamlaka nacho...

  2. Haijuzu kumfanyia uadui maiti na kumuudhi, na pia haijuzu kumkata-kata viungo (muthlah)... Na hiyo ni kama ifuatavyo:

a- Kuhusu uharamu wa kufanya uadui na kuudhi, zimekuja hadithi "zinazofahamisha wazi kuwa maiti ana heshima sawa na ya aliye hai, kama inavyofahamisha kuwa kufanya uadui dhidi ya heshima ya maiti na kumuudhi ni kama kufanya uadui dhidi ya heshima ya aliye hai na kumuudhi. Hivyo, kama isivyojuzu kumfanyia uadui aliye hai kwa kumpasua tumbo, au kumkata shingo, au kumng'oa jicho, au kuvunja mfupa wake, vivyo hivyo haijuzu kumfanyia uadui maiti kwa kumpasua tumbo, au kumkata shingo, au kumng'oa jicho, au kuvunja mfupa wake. Na kama ilivyo haramu kumuudhi aliye hai kwa kumtukana, au kumpiga, au kumjeruhi, vivyo hivyo ni haramu kumuudhi maiti kwa kumtukana, au kumpiga, au kumjeruhi...", na miongoni mwa hadithi hizo ni:

  • Kutoka kwa Aisha Mama wa Waumini (ra) kwamba Mtume wa Allah ﷺ amesema:

كَسْرُ عَظْمِ الْمَيِّتِ كَكَسْرِهِ حَيّاً

"Kuvunja mfupa wa maiti ni sawa na kuuvunja akiwa hai." (Imepokewa na Ahmad, Abu Dawood na Ibn Hibban)

  • Amepokea Ahmad kupitia Amr bin Hazm al-Ansari amesema: Mtume wa Allah ﷺ aliniona nikiwa nimeegemea kaburi akasema:

لَا تُؤْذِ صَاحِبَ الْقَبْرِ

"Usimuudhi mwenye kaburi."

  • Amepokea Muslim na Ahmad kupitia Abu Hurairah amesema: Mtume wa Allah ﷺ amesema:

لَأَنْ يَجْلِسَ أَحَدُكُمْ عَلَى جَمْرَةٍ مُتَحَرِّقَةٍ خَيْرٌ لَهُ مِنْ أَنْ يَجْلِسَ عَلَى قَبْرٍ

"Mmoja wenu kuketi juu ya kaa la moto linalomteketeza ni bora kwake kuliko kuketi juu ya kaburi."

b- Kuhusu kuukata-kata mwili wa maiti (al-muthlah), basi "kung'oa jicho la maiti, au kupasua tumbo lake ili kuchukua moyo wake au figo yake au ini lake au mapafu yake, ili kumpelekea mtu mwingine anayevihitaji, huhesabiwa kuwa ni muthlah (kumkata-kata maiti), na Uislamu umekataza al-muthlah":

  • Amepokea Bukhari kutoka kwa Abdullah bin Zaid al-Ansari amesema:

نَهَى رَسُولُ اللهِ ﷺ عَنِ النُّهْبَى وَالْمُثْلَة

"Mtume wa Allah ﷺ amekataza uporaji na kukata-kata viungo (muthlah)."

  • Amepokea Ahmad, Ibn Majah na an-Nasa'i kutoka kwa Safwan bin Assal amesema: Mtume wa Allah ﷺ alitutuma katika kikosi akasema:

سِيرُوا بِاسْمِ اللهِ، وَفِي سَبِيلِ اللهِ، قَاتِلُوا مَنْ كَفَرَ بِاللهِ، وَلَا تُمَثِّلُوا وَلَا تَغْدُرُوا وَلَا تَقْتُلُوا وَلِيداً

"Nendeni kwa jina la Allah, na katika njia ya Allah, piganeni na waliomkufuru Allah, wala msikate-kate viungo (msifanye muthlah), wala msifanye khiyana, wala msiue watoto."

Kulingana na dalili zilizotajwa hapo juu, inadhihirika wazi kabisa kuwa kuhamisha kiungo kutoka kwa mtu aliyekufa ambaye damu yake imekingwa (ma’sum al-dam) kwenda kwa aliye hai ni haramu kisheria...] Mwisho wa nukuu kutoka kwa jibu la swali lililopita.

Vivyo hivyo ninakunukulia yaliyokuja katika kijitabu cha al-Istinsakh kuhusu kuhamisha viungo katika hali ya dharura:

[...Hali ya dharura ni hali ambayo Allah amemhalalishia mtu aliyepatwa na dharura ambaye amekosa chakula, na maisha yake yakawa yanatishiwa na kifo, kula katika vyakula ambavyo Allah ameviharamisha kula, kama vile mzoga, damu, nyama ya nguruwe, na vinginevyo. Je, katika hali hii inaruhusiwa kuhamisha kiungo miongoni mwa viungo vya maiti ili kuokoa maisha ya mtu mwingine, ambaye kubaki kwake hai kunategemea kuhamishiwa kiungo hicho?

Ili kujibu hilo, ni lazima kujua hukumu ya dharura ili tufikie kujua hukumu ya kuhamisha viungo kutoka kwa mtu ambaye maisha yake yameisha, kwenda kwa mtu mwingine anayevihitaji.

  • Kuhusu hukumu ya dharura, Allah Subhanahu wa Ta'ala amemhalalishia mwenye dharura ambaye amekosa chakula, na maisha yake yakawa yanatishiwa na kifo, kula anachokipata katika vyakula ambavyo Allah ameviharamisha, ili kuhifadhi maisha yake, kama vile mzoga, damu, nguruwe, na vinginevyo katika kila chakula alichokiharamisha Allah. Allah Ta'ala amesema:

إِنَّمَا حَرَّمَ عَلَيْكُمُ الْمَيْتَةَ وَالدَّمَ وَلَحْمَ الْخِنزِيرِ وَمَا أُهِلَّ بِهِ لِغَيْرِ اللّهِ فَمَنِ اضْطُرَّ غَيْرَ بَاغٍ وَلاَ عَادٍ فَلا إِثْمَ عَلَيْهِ

"Yeye amekuharimishieni mzoga tu, na damu, na nyama ya nguruwe, na kilichochinjiwa asiyekuwa Allah. Lakini aliyefikwa na dharura bila ya kutamani wala kupitisha mpaka, basi yeye hana dhambi." (QS. Al-Baqarah [2]: 173)

Basi mwenye dharura anaruhusiwa kula anachopata katika vyakula hivi vilivyoharamishwa kiasi cha kumfanya apate nguvu na kubaki hai, na asipokula na akafa, atakuwa ni mwenye dhambi, na atakuwa ameiua nafsi yake, na Allah Subhanahu wa Ta'ala anasema:

وَلَا تَقْتُلُوا أَنْفُسَكُمْ

"Wala msijiue." (QS. An-Nisa [4]: 29)

  • Kutokana na yaliyotangulia kuhusu hukumu ya dharura, je, inawezekana kutekeleza hukumu hii kwenye hali ya kuhamisha viungo kutoka kwa mtu ambaye maisha yake yameisha kwenda kwa mtu mwingine anayehitaji ili kuokoa maisha yake kwa njia ya kulinganisha (Qiyas)?

  • Jibu la hilo lina utata, kwani sharti la kutekeleza hukumu ya Qiyas katika suala hili, linahitaji kuwa sababu ('illah) iliyopo katika tawi linalolinganishwa (far') - ambalo ni hali ya kuhamisha viungo - iwe inashirikiana na sababu ya asili inayolinganishiwa (asl) - ambayo ni hali ya dharura kwa aliyekosa chakula - ima katika dhati yake, au katika jinsi yake, kwa sababu Qiyas ni kuhamisha hukumu ya asili kwenda kwenye tawi, kupitia sababu ya asili. Ikiwa sababu ya tawi haishirikiani nayo katika sifa ya ujumla wake, wala katika sifa ya uhususi wake, basi sababu ya asili haipo katika tawi, na kwa hivyo haiwezekani kuhamisha hukumu ya asili kwenda kwenye tawi.

  • Hapa kuhusiana na hali ya kuhamisha viungo, viungo hivi vinavyohamishwa, ima viwe ni miongoni mwa viungo ambavyo kuokoa maisha kunategemea viungo hivyo kwa dhana yenye nguvu, kama moyo, ini, figo mbili, na mapafu, au viwe ni miongoni mwa viungo ambavyo kuokoa maisha hakutegemei viungo hivyo, kama jicho, figo ya pili kwa mwenye figo moja nzima, mkono, mguu, na mfano wake.

  • Kuhusu viungo ambavyo kuokoa maisha hakutegemei kuhamishwa kwake, na ambavyo kukosekana kwake hakumpelekei mwanadamu kwenye kifo, basi sababu ya asili, ambayo ni kuokoa maisha, haipo ndani yake, na hivyo hukumu ya dharura haitumiki juu yake. Kulingana na hilo, haijuzu kisheria kuhamisha jicho, au figo kwa mwenye figo nyingine nzima, au mkono, au mguu kutoka kwa mtu ambaye maisha yake yameisha kwenda kwa mtu mwingine anayevihitaji.

  • Na kuhusu viungo ambavyo kuokoa maisha ya mwanadamu kunategemea kuhamishwa kwake kwa dhana yenye nguvu, ndani yake kuna nyanja mbili:

Ya kwanza: Kwamba sababu ('illah) iliyopo ndani yake - ambayo ni kuokoa maisha na kuyabakisha - haina uhakika wa kupatikana, kama ilivyo katika hali ya dharura, kwa sababu kula kwa mwenye dharura kile alichokiharamisha Allah katika vyakula hupelekea kwa lazima kuokoa maisha yake, lakini kuhamisha moyo, au ini, au mapafu, au figo, hakunapelekea kwa lazima kuokoa maisha ya yule aliyehamishiwa viungo hivyo; kwani kuokoa kunaweza kutokea, na kunaweza usitokee. Na matukio mengi yaliyotokea kwa wale waliohamishiwa viungo hivi yanathibitisha hilo. Kwa ajili hiyo, sababu hiyo haijakamilika.

Ama nyanja ya pili, inahusiana na sharti jingine miongoni mwa masharti ya tawi katika Qiyas, nalo ni tawi lisiwe na mgongano wenye nguvu unaohitaji kinyume cha kile kinachohitajika na sababu ya Qiyas. Na hapa katika tawi - ambalo ni hali ya kuhamisha viungo - pamekuja andiko lenye nguvu (nass rajih) linalohitaji kinyume cha kile kinachohitajiwa na sababu ya Qiyas, nalo ni kuharamisha kufanya uadui dhidi ya heshima ya maiti au kumuudhi au kumkata-kata viungo (muthlah), na andiko hili lenye nguvu, ni kinyume cha kile kinachohitajiwa na sababu ya kuhamisha viungo ambayo ni kujuzu.

  • Kulingana na nyanja hizi mbili, haijuzu kuhamisha viungo ambavyo kuokoa maisha kunategemea kuhamishwa kwake, kama moyo, ini, figo mbili, na mapafu, kutoka kwa mtu aliyepoteza maisha na huku damu yake imekingwa (ma’sum al-dam), awe ni Muislamu au Dhimmi au mwenye ahadi (Mu’ahid) au mwenye kuomba hifadhi (Musta’min), kwenda kwa mtu mwingine ambaye maisha yake yanategemea kuhamishwa kwa viungo hivi kwake] Mwisho wa nukuu kutoka kijitabu cha al-Istinsakh.

Pili: Ni wazi kutokana na yaliyotajwa katika kipengele cha "Kwanza" kwamba kuhamisha moyo (na mfano wake viungo vingine vyote ambavyo kuokoa maisha kunategemea kuhamishwa kwake, kama ini, figo mbili, na mapafu) kutoka kwa mtu ambaye damu yake imekingwa ni haramu kisheria. Hii ina maana kwamba kutoa msaada kwa moyo wake kwa mtu mwingine haijuzu, na ina maana pia kwamba kuchukua moyo uliotolewa msaada kutoka kwa mtu mwenye damu iliyokingwa haijuzu kwa sababu maana ya uadui uliopaswa kuharamishwa ipo pia wakati wa kuchukua moyo wa mtu mwenye damu iliyokingwa uliotolewa msaada. Hivyo, haramu katika suala la kuhamisha moyo si tu kutoa msaada wa mtu mwenye damu iliyokingwa au walii wake kwa moyo wake, bali kuchukua moyo wa mtu mwenye damu iliyokingwa uliotolewa msaada na kuupandikiza katika mwili wa mtu mwingine pia ni haramu kwa sababu maana ya kufanya uadui dhidi ya mwili wa maiti inapatikana katika hali ya kutoa msaada, yaani katika hali ya kuutoa moyo wa mtu mwenye damu iliyokingwa kutoka kwenye mwili wake, na inapatikana wakati wa kuuweka moyo wa mtu mwenye damu iliyokingwa katika mwili wa mtu mwingine. Wajibu katika hali kama hii, yaani katika hali ya kung'oa kiungo kutoka kwenye mwili wa maiti mwenye damu iliyokingwa, ni kukizika kiungo kilichong'olewa kutoka kwenye mwili wa mtoaji msaada mwenye damu iliyokingwa na si kukitumia kutibu mtu mwingine. Abu Dawood ametoa kupitia njia ya Aisha (ra) kwamba:

أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ ﷺ قَالَ: كَسْرُ عَظْمِ الْمَيِّتِ كَكَسْرِهِ حَيّاً

"Kwamba Mtume wa Allah ﷺ amesema: Kuvunja mfupa wa maiti ni sawa na kuuvunja akiwa hai."

Na imekuja katika Awn al-Ma'bud Sharh Sunan Abi Dawood: As-Suyuti amesema katika kubainisha sababu ya hadithi hii, kutoka kwa Jabir (ra) amesema: Tulitoka pamoja na Mtume wa Allah ﷺ katika jeneza, Mtume ﷺ akaketi ukingoni mwa kaburi na tukaketi pamoja naye, mchimba kaburi akatoa mfupa wa muundi au wa mkono, akaenda kuuvunja, Mtume ﷺ akasema:

لَا تَكْسِرْهَا فَإِنَّ كَسْرَكَ إِيَّاهُ مَيِّتاً كَكَسْرِكَ إِيَّاهُ حَيّاً، وَلَكِنْ دُسَّهُ فِي جَانِبِ الْقَبْرِ

"Usiuvunje, kwani kuuvunja kwako ukiwa maiti ni sawa na kuuvunja kwako ukiwa hai, lakini ufiche (uzike) upande wa kaburi."

Hivyo, Mtume ﷺ aliamrisha kulingana na riwaya hii kurudisha na kuzika mfupa wa maiti, na inafahamika kutokana na hayo kuwa kiungo cha maiti kilichotengana naye ni lazima kizikwe.

Muhtasari ni kwamba haijuzu kuchukua kiungo ambacho maisha yanategemea kiungo hicho kama moyo kutoka kwa aliye hai mwenye damu iliyokingwa, na vivyo hivyo haijuzu kukitoa msaada hata kama ni kwa ajili ya kuokoa mwingine... Na pia haijuzu kuusia kichukuliwe baada ya kifo kwa sababu mtu hamiliki mwili wake baada ya kifo chake, na vivyo hivyo warithi hawamiliki isipokuwa fungu lao la mali, lakini hawamiliki mwili wa marehemu, na hivyo hawawezi kutoa msaada wa sehemu yoyote ya mwili wa marehemu kwa sababu ni uadui dhidi yake na ni haramu.

Natumai ufafanuzi huu utakuwa unatosheleza, na Allah ni Mjuzi zaidi na Mwenye Hekima zaidi.

Ndugu yenu Ata bin Khalil Abu al-Rashtah

11 Jumada al-Ula 1442 H Sawia na 26/12/2020 M

Link ya jibu kutoka ukurasa wa Facebook wa Amir (Allah amhifadhi): Facebook

Link ya jibu kutoka tovuti ya Amir (Allah amhifadhi): Web

Share Article

Share this article with your network