Ndugu mtukufu, Assalamu Alaikum Warahmatullahi Wabarakatuh
Hili hapa ni jawabu la swali kuhusu manukato (kolonia... n.k.):
Hakika Mtume (saw) anasema:
كُلُّ مُسْكِرٍ خَمْرٌ وَكُلُّ خَمْرٍ حَرَامٌ
"Kila kileo ni khamr na kila khamr ni haramu." (Imepokelewa na Muslim).
Na anasema Rehema na Amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake:
مَا أَسْكَرَ كَثِيرُهُ فَقَلِيلُهُ حَرَامٌ
"Kile ambacho wingi wake unalewesha, basi kidogo chake ni haramu." (Imepokelewa na Ibn Majah na ad-Daraqutni na kusahihishwa na Ibn Hajar).
Amebainisha Rehema na Amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake ni kioevu gani kinachoitwa khamr, kwani kila kileo, kiwe kidogo au kingi, ni khamr. Hapa ndipo unakuja wajibu wa kuhakiki uhalisia (tahqiq al-manat) ili kujua ikiwa manukato haya au kolonia na mfano wake yanalewesha yakinywewa, kidogo au mengi. Ikiwa yanalewesha, basi hayo ni khamr na yanatumiwa hukumu za khamr kwa kuharamishwa katika aina kumi kulingana na hadith:
لُعِنَتِ الْخَمْرُ عَلَى عَشَرَةِ أَوْجُهٍ: بَعِيْتِهَا وَعَاصِرِهَا وَمُعْتَصِرِهَا وَبَائِعِهَا وَمُبْتَاعِهَا وَحَامِلِهَا وَالْمَحْمُولَةِ إِلَيْهِ وَآكِلِ ثَمَنِهَا وَشارِبِهَا وَسَاقِيِهَا
"Khamr imelaaniwa kwa namna kumi: (katika kuiuza), mkamuaji wake, anayekamuliwa kwa ajili yake, muuzaji wake, mnunuzi wake, mbebaji wake, anayebebewa, anayekula thamani yake (pesa), mnywaji wake, na mnyweshaji wake." (Imepokelewa na Ibn Majah).
Na tumeelewa kuwa manukato kama kolonia na mfano wake hunywewa katika baadhi ya maeneo, hususan kanda ya Ghuba, na kwamba yanalewesha kutokana na kuwepo kwa kiasi fulani cha kilevi (alcohol) ndani yake.
Kwa hivyo, ikiwa kioevu hicho, kiwe ni manukato au si manukato, wingi wake unalewesha, basi kidogo chake ni haramu, na hicho ni khamr na kinatumiwa hukumu za khamr kwa kuharamishwa katika vipengele vyake kumi.
Ama kuhusu kuwa kilevi (alcohol) kiko aina mbili, ethili (ethanol) na methili (methanol), hili ni sahihi. Na tumefahamu kutoka kwa wataalamu yafuatayo:
(Kuna aina mbili za kilevi: mosi ni (ethili), ambayo ndiyo dutu inayofanya kazi katika khamr za aina zote kulingana na viwango tofauti vya ukolezi. Pili ni (methili), ambayo ni kilevi kinachotolewa kutoka kwenye mbao au nyuzi. Hizi ni dutu mbili zinazofanana kwa namna zinavyoathiri mwili na hasa mfumo wa neva, lakini zinatofautiana kabisa katika uchambuzi wa kikemia na uoksidishaji mwilini, na hili ndilo linalosababisha matokeo tofauti. Kuhusu athari, kila moja husababisha kushuka kwa utendaji wa vituo vyote muhimu katika ubongo. Isipokuwa kwamba kilevi cha ethili kinalewesha lakini hakiui, na kunywa kiasi kikubwa sana husababisha kupoteza fahamu kisha usingizi mzito sana, kisha mnywaji huzinduka baada ya hapo. Ama kilevi cha methili, chenyewe kinalewesha, lakini husababisha athari ya sumu yenye madhara inayoweza kufikia: kuharibu seli za macho (retina) na kuua neva ya kuona, jambo ambalo hupelekea upofu au kuua seli za vituo muhimu kwenye ubongo na kuziharibu, na hili hupelekea kifo, kulingana na viwango vilivyotumika. Khamr zote zina kilevi cha ethili na zina kiasi kidogo sana cha kilevi cha methili, ama kolonia, sehemu yake kubwa ni kilevi cha methili).
Hii ina maana kwamba kilevi cha ethili na kiasi kidogo cha methili kinalewesha, na kiasi kikubwa cha methili kinaua. Kwa hivyo kolonia, iwe imetengenezwa kwa ethili au methili kwa kiwango kinachofaa, basi inalewesha (kama ilivyoripotiwa kuhusu visa vya ulevi katika Ghuba kutokana na kolonia). Ikiwa inalewesha na kutia sumu bila kuua, basi ni haramu kwa kuwa ni khamr, na pia ni haramu kwa kuwa ni sumu (hata kama haiui). Ama ikiwa kilevi cha methili kitatumiwa kwa kiwango kinachoua katika kioevu au kolonia, basi kioevu hicho kinakuwa haramu kwa sababu ni sumu kulingana na kanuni ya madhara (Asili katika vitu vyenye madhara ni uharamu).
Hivyo basi, vimelea ambavyo kilevi huingizwa ndani yake, vinahakikiwa uhalisia wake (tahqiq al-manat):
Ikiwa kiwango cha kilevi kilichomo kinaifanya ileweshe, wingi wake au kidogo chake, basi hiyo ni khamr na ni haramu katika vipengele kumi.
Na ikiwa haileweshi lakini inatia sumu, basi ni haramu kwa sababu ni sumu, na katika hali hii inaharamishwa katika kile kilichokuja kwenye nass (andiko), yaani kunywa sumu au kuila, na pia kuiuza au kuizawadia kulingana na hadith:
وَإِنَّ اللهَ إِذَا حَرَّمَ عَلَى قَوْمٍ أَكْلَ شَيْءٍ حَرَّمَ عَلَيْهِمْ ثَمَنَهُ
"Na hakika Mwenyezi Mungu anapoharamisha kwa watu kula kitu, basi anaharamisha kwao thamani yake." (Imepokelewa na Abu Dawood na Ahmad).
قَاتَلَ اللهُ الْيَهُودَ إِنَّ اللهَ لَمَّا حَرَّمَ عَلَيْهِمُ الشُّحُومَ جَمَلُوهَا ثُمَّ بَاعُوهَا وَأَكَلُوا أَثْمَانَهَا
"Mwenyezi Mungu awaangamize Mayahudi! Hakika Mwenyezi Mungu alipowaharamishia mafuta (ya wanyama), waliyeyusha kisha wakayauza na wakala thamani yake." (Imepokelewa na Ahmad). Jamaluha maana yake waliyeyusha. Ama vipengele vingine vilivyobaki katika vile kumi, nass zake zimekuja katika khamr.
Hii ni kuhusu sehemu ya kwanza ya swali: Manukato au Kolonia.
Ama sehemu ya pili: Kwa nini tunapitisha msimamo kisheria (tabanni) katika hili huku tukijua kuwa hatupitishi misimamo katika mambo ya ibada? Jawabu la hili lina sura mbili: Kwanza, khamr si katika ibada. Pili, sisi hapa hatupitishi msimamo (tabanni) katika kuharamishwa khamr, kwani hiyo ni haramu bila shaka yoyote, lakini suala hapa ni kuhakiki uhalisia (tahqiq al-manat) wa kioevu hiki, je kinalewesha au hakileweshi. Na yule anayehakiki uhalisia akakuta kwamba kioevu hicho hakileweshi wingi wake wala kidogo chake, basi wakati huo kioevu hicho hakitakuwa khamr.
Wassalamu Alaikum Warahmatullahi Wabarakatuh.
08/08/2004 M.
Ndugu yenu