Hakika kazi ya mawimbi ya sumakumeme yanayopita hewani ni kama kazi ya meli zinazopita baharini. Kwani anga, bahari na mfano wake, ambapo asili ya maumbile yake inazuia watu binafsi kuyamiliki, yote haya ni mali ya umma (milkiyyah 'ammah).
Hivyo, inaruhusiwa kwa Dola, makampuni, na watu binafsi kuwa na meli baharini, na inaruhusiwa pia kwao kuwa na mawimbi ya sumakumeme angani kwa kuzingatia mambo matatu:
1 - Matumizi ya mawimbi haya yasihitaji kusimamisha nguzo kwenye mali ya umma (kwa mfano barabarani).
2 - Ikiwa unufaika na mali ya umma utamzuia mwingine asipate manufaa hayo au kumsababishia madhara, basi ni wajibu wa Dola katika hali hii kuipanga kiidara ili kuhakikisha uwezekano wa kila mmoja kunufaika na mali ya umma. Hivyo, Dola hupanga njia za meli mtoni na baharini kama inavyopanga msongamano wa magari barabarani na kadhalika; na hii ni katika mlango wa kusimamia mambo ya umma (ri’ayah al-shu’un).
الإِمَامُ رَاعٍ وَمَسْئُولٌ عَنْ رَعِيَّتِهِ
"Imamu ni msimamizi na anawajibika kwa raia wake." (Imepokewa na Al-Bukhari).
3 - Ikiwa unufaika na mali ya umma katika hali fulani utasababisha madhara kwa mtu binafsi, Dola, au jamii, basi hali hii inazuiwa kwa mujibu wa kanuni ya madhara (kila jambo miongoni mwa mambo mubah ambalo linaingiza madhara, basi jambo hilo huzuiwa na yale mambo mengine ya mubah yanabaki katika uruhusiwa wake).
Kwa hivyo, kuhusiana na umiliki wa mawimbi ya sumakumeme, ikiwa haihitajiki kusimamisha nguzo kwenye mali ya umma, au ikiwa nguzo hizo zinasimamishwa kwenye milki za makampuni haya au watu binafsi, basi:
1 - Inaruhusiwa kuyamiliki kwa idhini ya Dola, ikiwa ni katika mlango wa kupanga unufaika wa mali ya umma ya Dola kwa namna inayomuwezesha kila mmoja kunufaika kwa njia sahihi.
2 - Dola ina haki ya kuzuia matumizi ya mawimbi yoyote ya sumakumeme ambayo inaona yana madhara, ikiwa ni katika mlango wa kuzuia jambo mubah kwa mtu binafsi ikiwa litaleta madhara, kama vile upande fulani kutumia mawimbi haya kwa ajili ya mawasiliano ya kijasusi dhidi ya Waislamu na mfano wa hayo.
Ama ikiwa itahitajika kusimamisha nguzo kwenye mali ya umma, basi haijuzu kwa makampuni au watu binafsi kutumia mawimbi haya, bali Dola pekee ndiyo inayoyatumia.
7 Dhul-Hijjah 1426 H 07/01/2006 M