Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

Jibu la Swali: "An-Nu'man ni Taa ya Umma Wangu" ni Hadithi ya Kutungwa

August 02, 2017
6742

(Mfululizo wa majibu ya mwanachuoni mtukufu Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah, Amir wa Hizb ut-Tahrir, kwa maswali ya wafuasi wa ukurasa wake wa Facebook "Fiqhi")

Jibu la Swali

Kwa: Abdul Vakil Seraji

Swali:

Assalam Alaykum ya Amir, mimi ninatokea Afghanistan, ningependa kukuuliza kuhusu usahihi wa hadithi hii; Mtume ﷺ amesema: "An-Nu'man ni taa ya umma wangu." Je, hadithi hii inahusu fadhila za Abu Hanifa (rahimahullah)?

Jibu:

Wa Alaykum Salaam Wa Rahmatullahi Wa Barakatuh.

Katika karne ya nne na ya tano Hijiria, baada ya mijadala na mashindano ya kimadhahabu kupata umaarufu, wakati mwingine yalivuka mipaka ya kawaida na kusababisha kuibuka kwa mapokezi ya kutungwa (mawdu') yaliyokuwa yakimsifu mujtahid mmoja na kumdhalilisha mwingine miongoni mwa maimamu wa madhehebu. Kwa mfano, baadhi ya wafuasi wa Shafi'i walikuwa wakinyanyua hadhi yake juu ya Abu Hanifa, na baadhi ya wafuasi wa Abu Hanifa walinyanyua hadhi yake juu ya Shafi'i, na kadhalika kwa baadhi ya wafuasi wa madhehebu mengine... Katika mazingira haya, walitokea watu wenye malengo yao binafsi wakasimulia hadithi za kutungwa bila ya kumuogopa Allah (swt) wala Mtume Wake ﷺ, wakidai kuitumikia madhehebu yao, hali ya kuwa kiukweli walikuwa hawaitumikii madhehebu yao bali walikuwa wakiichafua... Na miongoni mwa hadithi hizi za kutungwa ni ile uliyoitaja katika swali lako ("An-Nu'man ni taa ya umma wangu"), na nitakutajia baadhi ya yale yaliyopokelewa kuihusu:

1- Imekuja katika kitabu Tarikh Baghdad cha mwandishi wake Abu Bakr Ahmad bin Ali bin Thabit bin Ahmad bin Mahdi al-Khatib al-Baghdadi (aliyefariki: 463 H):

Hadithi nambari 4545:

أَخْبَرَنِي الْقَاضِي أَبُو الْعَلاءِ مُحَمَّدُ بْنُ عَلِيٍّ الْوَاسِطِيُّ، وَأَبُو عَبْدِ اللَّهِ أَحْمَدُ بْنُ أَحْمَدَ بْنِ عَلِيٍّ الْقَصْرِيُّ، قَالا: أَخْبَرَنَا أَبُو زَيْدٍ الْحُسَيْنُ بْنُ الْحَسَنِ بْنِ عَلِيِّ بْنِ عَامِرٍ الْكِنْدِيُّ، بِالْكُوفَةِ، قَالَ: أَخْبَرَنَا أَبُو عَبْدِ اللَّهِ مُحَمَّدُ بْنُ سَعِيدٍ البُورَقِيُّ الْمَرْوَزِيُّ، قَالَ: حَدَّثَنَا سُلَيْمَانُ بْنُ جَابِرِ بْنِ سُلَيْمَانَ بْنِ يَاسِرِ بْنِ جَابِرٍ، قَالَ: حَدَّثَنَا بِشْرُ بْنُ يَحْيَى، قَالَ: أَخْبَرَنَا الْفَضْلُ بْنُ مُوسَى السِّينَانِيُّ، عَنْ مُحَمَّدِ بْنِ عَمْرٍو، عَنْ أَبِي سَلَمَةَ، عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ، عَنْ رَسُولِ اللَّهِ e، قَالَ: "إِنَّ فِي أُمَّتِي رَجُلا"، وَفِي حَدِيثِ الْقَصْرِيِّ: "يَكُونُ فِي أُمَّتِي رَجُلٌ اسْمُهُ النُّعْمَانُ، وَكُنْيَتُهُ أَبُو حَنِيفَةَ هُوَ سِرَاجُ أُمَّتِي، هُوَ سِرَاجُ أُمَّتِي، هُوَ سِرَاجُ أُمَّتِي"

"Hakika katika umma wangu kuna mtu", na katika hadithi ya Al-Qasri: "Atakuwepo katika umma wangu mtu ambaye jina lake ni An-Nu'man, na jina lake la kunia ni Abu Hanifa, yeye ni taa ya umma wangu, yeye ni taa ya umma wangu, yeye ni taa ya umma wangu." (Tarikh Baghdad [13/335])

Al-Khatib al-Baghdadi anaisherehesha kwa kusema: "Hiyo ni hadithi ya kutungwa (mawdu'), na Al-Buraqi pekee ndiye aliyeipokea." Mwisho.

2- Imekuja katika Al-Musnad al-Mustakhraj 'ala Sahih Muslim cha mwandishi wake Abu Nu'aym Ahmad bin Abdullah bin Ahmad bin Ishaq bin Musa bin Mehran al-Asbahani (aliyefariki: 430 H) chini ya nambari 248:

مَأْمُونُ بْنُ أَحْمَدَ السُّلَمِيُّ مِنْ أَهْلِ هَرَاةَ خَبِيثٌ وَضَّاعٌ يَرْوِي عَنِ الثِّقَاتِ مِثْلَ هِشَامِ بْنِ عَمَّارٍ وَدُحَيْمٍ بِالْمَوْضُوعَاتِ وَفِيمَا حَدَّثَ عَنْ أَحْمَدَ الْجُوبَارِيِّ الْكَذَّابِ عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ مَعْدَانَ الأَزْدِيِّ عَنْ أَنَسٍ مُسْنَدًا "يَكُونُ فِي أُمَّتِي رَجُلٌ يُقَالُ لَهُ مُحَمَّدُ بْنُ إِدْرِيسَ أَضَرَّ عَلَى أُمَّتِي مِنْ إِبْلِيسَ وَيَكُونُ فِي أُمَّتِي رَجُلٌ يُقَالُ لَهُ أَبُو حَنِيفَةَ هُوَ سِرَاجُ أُمَّتِي"

"Ma'mun bin Ahmad al-Sulami kutoka watu wa Herat ni khabithi (muovu) na mzushi wa hadithi, anapokea kutoka kwa watu waaminifu kama Hisham bin Ammar na Duhaym hadithi za kutungwa, na miongoni mwa aliyohadithia kutoka kwa Ahmad al-Juybari mwongo, kutoka kwa Abdullah bin Ma'dan al-Azdi, kutoka kwa Anas amepokea hadithi: 'Atakuwepo katika umma wangu mtu anayeitwa Muhammad bin Idris (ash-Shafi'i) ambaye ni mwenye madhara zaidi kwa umma wangu kuliko Iblis, na atakuwepo katika umma wangu mtu anayeitwa Abu Hanifa naye ni taa ya umma wangu.'" (Al-Musnad al-Mustakhraj)

Kisha akatolea maoni kwa kusema: Msimulizi wa hadithi hii anastahili laana kutoka kwa Allah Ta’ala, kutoka kwa Mtume, na kutoka kwa Waislamu.

3- Na imekuja katika kitabu Al-Ta'yin fi Sharh al-Arba'in cha mwandishi wake Suleiman bin Abdul Qawi bin Abdul Karim al-Tufi al-Sarsari, Abu al-Rabi', Najm al-Din (aliyefariki: 716 H): "Ama hadithi ya 'yeye ni taa ya umma wangu', Ibn al-Jawzi ameiweka katika kitabu cha hadithi za kutungwa (Al-Mawdu'at), na akataja kuwa wakati madhehebu ya Shafi'i yalipoenea, baadhi ya wenye kufuata kishabiki walitaka kuipunguza kasi yake, wakazungumza na Ma'mun bin Ahmad al-Sulami na Ahmad bin Abdullah al-Juybari, na wote wawili walikuwa waongo."

4- Na imekuja katika kitabu Kashf al-Khafa' wa Muzil al-Ilbas cha mwandishi wake Ismail bin Muhammad bin Abdul Hadi al-Jarahi al-Ajluni al-Dimashqi, Abu al-Fida (aliyefariki: 1162 H): "Abu Hanifa ni taa ya umma wangu; Al-Qari amesema katika kitabu chake Al-Mawdu'at al-Kubra: Ni hadithi ya kutungwa kwa makubaliano ya wanachuoni wa hadithi."

Hivyo basi, kauli ya "An-Nu'man ni taa ya umma wangu" ni hadithi ya kutungwa.

Ndugu yenu, Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah

09 Dhul-Qa'dah 1438 H Inayowiana na 01/08/2017 M

Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir kwenye Facebook

Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir kwenye Google Plus

Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir kwenye Twitter

Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir wa Tovuti

Share Article

Share this article with your network