Swali: Imepokewa katika kitabu cha An-Nidham al-Ijtima'i (Mfumo wa Kijamii), uk. 41:
إِذَا زَوَّجَ أَحَدُكُمْ خَادِمَهُ عَبْدَهُ أَوْ أَجِيرَهُ فَلَا يَنْظُرُ إِلَى مَا دُونَ السِّرَّةِ وَفَوْقَ الرُّكْبَةِ فَإِنَّهُ عَوْرَةٌ
"Ikiwa mmoja wenu atamwoza mtumishi wake kwa mtumwa wake au mwajiriwa wake, basi asitazame sehemu iliyo chini ya kitovu na juu ya goti, kwani hiyo ni awra."
Hadithi hii imetajwa katika muktadha wa kutoa dalili ya kuruhusiwa kwa mwanamume kutazama sehemu isiyo awra ya mwanamke, na mwanamke kutazama sehemu isiyo awra ya mwanamume. Sasa, kuna tofauti gani kati ya kutazama sehemu iliyo chini ya kitovu na juu ya goti kwa mtumishi wake kabla ya kumwoza na baada ya kumwoza?
Jibu: Inaonekana kuna mkanganyiko katika kuelewa swali. Maana ya hadithi ni: Ikiwa mmoja wenu atamwoza mtumishi wake, yaani mjakazi wake (amah), kwani neno (khadim) hutumika kwa mwanamume na mwanamke sawia. Mjakazi kabla ya bwana wake kumwoza kwa mtu mwingine, anakuwa ni halali kwake (milk al-yamin) na inajuzu kwa bwana huyo kuona awra yake. Lakini akishaolewa, inakuwa haramu kwa bwana wake (yule aliyemwoza) kutazama awra yake, na inajuzu kwake kutazama sehemu isiyo awra ya mjakazi huyo; yaani sehemu zilizo chini ya goti na juu ya kitovu, maadamu amebakia kuwa ni mjakazi wake na hajamuacha huru. Amemwoza tu kwa mtumwa wake au mwajiriwa wake na amebaki kuwa mjakazi, yaani hajawa muungwana (mwanamke huru), la sivyo ingekuwa haramu kwake kutazama mwili wake wote isipokuwa uso na vitanga vya mikono pekee.
Kwa hivyo, nukuu inasema:
«إذا زوَّج أحدُكم خادَمَه عبدَه أو أجيرَه ...»
Basi أحدُكم ndiye mtendaji (fa'il), خادَمَه ni mtendwa wa kwanza (maf'ul bihi) wa kitendo zawwaja, na عبدَه أو أجيره ni mtendwa wa pili (maf'ul bihi) wa zawwaja, na wala si sifa au ufafanuzi (atf bayan) wa خادَمَه. Hadithi hii ni dalili kwamba uhalali wa bwana kutazama mjakazi wake mzima (kwa sababu ni milk al-yamin), uhalali huu unafutwa kwa kile kinachohesabiwa kuwa ni awra kwa mjakazi huyo baada ya kuolewa kwani anakuwa si halali kwake tena. Hivyo inakuwa haramu kwake kutazama awra yake, yaani sehemu iliyo chini ya kitovu na juu ya goti, kwa sababu yeye ni mjakazi ambaye ameolewa lakini hajaachwa huru.
Kwa hivyo, maana ya wazi (mantuq) ya hadithi inafaa kuwa dalili ya kuthibitisha uharamu wa mwanamume kutazama awra ya mwanamke. Na maana inayofahamika kutokana na nukuu hii (mafhum) ni kwamba inajuzu kwa mwanamume kutazama sehemu isiyo awra ya mwanamke, iwe ni muungwana au mjakazi. Na mwanamume na mwanamke ni sawa katika hili; mwanamume hutazama sehemu isiyo awra ya mwanamke, na mwanamke hutazama sehemu isiyo awra ya mwanamume.
19 Jumada al-Ula 1425 H
06/07/2004 M