Mfululizo wa majibu ya mwanachuoni mtukufu Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah, Amir wa Hizb ut-Tahrir
kwa maswali ya wafuasi wa ukurasa wake wa Facebook "Fiqhi"
Jibu la Swali
Bidii Sio Sababu ya Riziki
Kwa Muhammad Al-Khatib
Swali:
Kwa idhini yenu, ningependa kuuliza kuhusu riziki: Je, bidii (kutafuta) huongeza kiwango cha riziki iliyoandikwa? Yaani, mtu aliyeketi nyumbani kwake riziki yake ni ile ile kama angekuwa anafanya kazi, au kwa njia nyingine, je, kutangaza au kukuza biashara huongeza kiwango cha riziki iliyoandikwa? Shukrani. Naomba jibu haraka iwezekanavyo ikiwezekana, na Allah amulinde Sheikh wetu na ampe umri mrefu.
Jibu:
Assalamu Alaikum Warahmatullahi Wabarakatuh,
Inaonekana una utatanishi fulani katika mada ya riziki na bidii... kwa vyovyote vile, jambo hili limefafanuliwa, hasa katika Kijitabu (Al-Kurrasah), na unaweza kukiangalia kwani kimeelezewa huko kikamilifu, lakini nitakufupishia baadhi yake:
[Ama suala la riziki, aya nyingi zenye maana ya mkato (qati’u ad-dalalah) haziachi nafasi kwa anayemwamini Qur'an isipokuwa kuamini kuwa riziki iko mikononi mwa Allah, ampa amtakaye. Na suala la riziki ni tofauti na suala la Qadar, kwani Qadar ni kwamba Allah anajua kuwa jambo fulani litatokea kabla ya kutokea kwake, hivyo likawa limeandikwa na kukadiriwa. Ama riziki, si tu kwamba Allah anajua kuwa fulani ataruzukiwa, hivyo likawa limeandikwa na kukadiriwa, bali pamoja na hayo, yaani pamoja na kuwa amekadiria riziki, Mpaji (ar-Raziq) ni Allah na sio mja. Hivi ndivyo zinavyoashiria aya:
لَا نَسْأَلُكَ رِزْقاً نَّحْنُ نَرْزُقُكَ وَالْعَاقِبَةُ لِلتَّقْوَى
"Hatukuombi riziki, Sisi ndio tunaokuruzuku, na mwisho mwema ni wa uchamungu." (QS Taha [20]: 132)
وَكُلُواْ مِمَّا رَزَقَكُمُ اللهُ حَلاَلاً طَيِّباً وَاتَّقُواْ اللهَ الَّذِيَ أَنتُم بِهِ مُؤْمِنُونَ
"Na kuleni katika vile alivyokuruzukuni Allah vilivyo halali na vizuri, na mcheni Allah ambaye mnamuamini." (QS Al-Ma'idah [5]: 88)...
Aya hizi ni za mkato katika kuonyesha kuwa Allah ndiye Mpaji, na kwamba Yeye humruzuku amtakaye, na kwamba Yeye ndiye anayemkunjulia riziki amtakaye na kumkadiria. Katika aya hizi zote, riziki imeegemezwa kwa Allah, na kwamba hakuna mpaji mwingine asiyekuwa Yeye, jambo ambalo linaonyesha kuwa Yeye ndiye anayeruzuku, na huu ni uegemezo wa kweli (isnad haqiqi)...
Hivyo, uegemezo wa riziki kwa Allah ni uegemezo wa kweli, na zaidi ya hayo, haikuja sehemu yoyote riziki ikiegemezwa kwa mwanadamu kuwa yeye ndiye anayejiruzuku mwenyewe, si katika aya wala hadithi. Bali uegemezo wa riziki katika maandishi yote umekuja kwa Allah Ta'ala. Ama yale yaliyokuja yakiegemeza riziki kwa mwanadamu anayempa mwingine, basi makusudio yake ni "wapeni mali" na wala si kitendo cha kuruzuku. Kwa mfano, Allah Ta'ala amesema:
وَلاَ تُؤْتُواْ السُّفَهَاء أَمْوَالَكُمُ الَّتِي جَعَلَ اللهُ لَكُمْ قِيَاماً وَارْزُقُوهُمْ فِيهَا وَاكْسُوهُمْ
"Wala msiwape wapumbavu mali yenu ambayo Allah ameifanya iwe ni kiamu (msingi wa maisha) yenu, na waruzukuni katika mali hiyo na wavalisheni." (QS An-Nisa [4]: 5)
Na Allah Ta'ala akasema:
وَإِذَا حَضَرَ الْقِسْمَةَ أُوْلُواْ الْقُرْبَى وَالْيَتَامَى وَالْمَسَاكِينُ فَارْزُقُوهُم مِّنْهُ
"Na wakati wa kugawa (urithi) wakihudhuria jamaa na mayatima na masikini, basi waruzukuni katika huo." (QS An-Nisa [4]: 8)
Makusudio katika aya ya kwanza ni "wapeni chakula", na katika aya ya pili ni "wapeni katika riziki hii iliyowafikia". Hivyo ni amri ya kuwapa sehemu ya riziki, na si kuitegemeza riziki kwao (kama wao ndio watoaji wa asili). Riziki haikuwahi kuegemezwa kwa maana ya mtendaji (fa’il) wa riziki isipokuwa kwa Allah pekee. Utakuta katika aya zinasema:
نَّحْنُ نَرْزُقُكُمْ
"Sisi tunakuruzukuni." (QS Al-An'am [6]: 151)
Na katika aya nyingine zinasema:
وَرِزْقُ رَبِّكَ
"Na riziki ya Mola wako." (QS Taha [20]: 131)
Na katika aya nyingine zinasema:
كُلُواْ وَاشْرَبُواْ مِن رِّزْقِ اللهِ
"Kuleni na kunyweni katika riziki ya Allah." (QS Al-Baqarah [2]: 60)
Katika aya hizi zote, Allah anafanya uegemezo wa kitendo cha kuruzuku kuwa ni Wake, na hili linatoa maana isiyokubali tafsiri nyingine (ta’wil), nayo ni kwamba Allah pekee ndiye Mpaji (ar-Razzaq), na kwamba riziki iko mikononi mwa Allah.
Kulingana na hili, ni wajibu kuamini kuwa Allah ndiye anayeviruzuku viumbe, kwa sababu dalili yake ni ya mkato katika ushahidi na mkato katika maana. Hivyo kuiamini ni faradhi na kuikataa ni ukafiri. Mtu asiyeamini kuwa Allah ndiye Mpaji amekufuru, na tunajilinda kwa Allah kutokana na hilo.
Hili ndilo suala la riziki kwa upande wa imani na kwa upande wa dalili. Hata hivyo, Allah Ta'ala pamoja na kuamrisha kuamini kuwa Yeye ndiye Mpaji, amemwamrisha mwanadamu kufanya bidii (sa'y) ili kupata riziki hiyo. Allah Ta'ala amesema:
هُوَ الَّذِي جَعَلَ لَكُمُ الْأَرْضَ ذَلُولاً فَامْشُوا فِي مَنَاكِبِهَا وَكُلُوا مِن رِّزْقِهِ
"Yeye ndiye aliyeifanya ardhi kuwa dhalili (rahisi) kwenu, basi tembeeni katika pande zake na kuleni katika riziki Yake." (QS Al-Mulk [67]: 15)
Na Allah Ta'ala amesema:
فَإِذَا قُضِيَتِ الصَّلَاةُ فَانتَشِرُوا فِي الْأَرْضِ وَابْتَغُوا مِن فَضْلِ اللهِ
"Na itakapokwisha swala, basi tawanyikeni katika ardhi na mtafute fadhila za Allah." (QS Al-Jumu'ah [62]: 10)
Hivyo, Ameamrisha katika aya hizi mbili kufanya bidii kutafuta riziki. Amri hii ya kufanya bidii kutafuta riziki inapounganishwa na aya zinazoeleza wazi kuwa Allah ndiye Mpaji, maana ya kuwa "Allah ndiye Mpaji" inakuwa wazi. Aya za kwanza zinakata shauri kuwa Allah ndiye Mpaji, yaani Yeye ndiye anayetoa riziki na sio mwanadamu, na aya hizi mbili zinaamrisha kufanya kazi ili kupata riziki ya Allah...
Ukweli ni kwamba bidii (sa'y) sio sababu (sabab) ya riziki. Hii ni kwa sababu sababu huzalisha kinachosababishwa (musabbab) bila shaka, na kinachosababishwa hakitokei isipokuwa kupitia sababu yake. Kisu ni sababu ya kukata, hivyo ndicho kinachokata. Moto ni sababu ya kuungua, hivyo ndio unaounguza. Hakuna kukatika kunakotokea bila kisu (au kifaa chenye makali), na hakuna kuungua kunakotokea bila moto (au kitu kinachounguza). Hii ndiyo sababu (sabab). Ikiwa bidii ya kutafuta riziki ingekuwa hivyo, basi ingekuwa sababu ya riziki, na hali halisi ingekuwa kwamba bidii ndiyo inayoleta riziki, kama vile kisu kinavyokata na moto unavyounguza. Lakini bidii ya kutafuta riziki haiko hivyo; yaani, si kama kisu katika kukata wala si kama moto katika kuunguza. Kwani inaweza kutokea bidii ya kutafuta riziki ikafanyika lakini riziki isipatikane, na inaweza kutokea riziki ikapatikana bila kufanyika bidii ya kuitafuta. Yaani sababu inaweza kuwepo lakini kinachosababishwa kisitokee, na kinachosababishwa kinaweza kutokea bila sababu yake, bali pengine bila sababu yoyote miongoni mwa sababu. Hili linaonyesha kwa dalili ya mkato kuwa bidii sio sababu ya riziki.
Mifano ya hilo katika uhalisia wa maisha ni mingi sana. Mfanyabiashara anayefanya bidii ili kupata faida, lakini matokeo ya biashara yake yakawa hasara au kutopata faida; hapa bidii imefanyika lakini riziki haikupatikana. Yaani sababu imekuwepo lakini haikuleta kinachosababishwa. Na kwa kuwa haikuleta matokeo, basi hiyo sio sababu, kwani sababu lazima ilete kinachosababishwa...
Pia, mrithi wa mali hupata riziki bila kufanya bidii kuitafuta. Kama bidii ingekuwa ndiyo sababu ya riziki, basi mali isingepatikana bila bidii, kwa sababu kinachosababishwa hakitokei isipokuwa kupitia sababu inayokisababisha. Hivyo kupatikana kwa mali kupitia urithi bila bidii ni dalili kwamba bidii sio sababu ya riziki, kwani riziki imepatikana bila kuwepo kwa bidii...
Haya yote yanathibitisha kwa njia ya mkato kuwa bidii ya kutafuta riziki sio sababu ya riziki. Yaani, siyo inayokuja na riziki. Hivyo si kama kisu ambacho ndicho kimefanya kitendo cha kukata, wala si kama moto ambao ndio umefanya kitendo cha kuunguza. Kwa hivyo, bidii siyo inayoleta riziki kwa sababu si sababu yake...]
Hivyo basi, Mpaji ni Allah (swt) na hili ni miongoni mwa itikadi (aqida), lakini kufanya bidii ni hukumu ya kisheria (hukm shar’i). Ukifanya bidii, utapata riziki yako aliyokukadiria Allah na utapata thawabu za kufanya bidii ya kutafuta riziki. Na usipofanya bidii, utapata riziki aliyokukadiria Allah lakini utakuwa umehalifu hukumu ya kisheria kwa sababu hukufanya bidii kama Allah alivyokuamrisha.
Na katika hayo kuna kutosheleza InshaAllah... na kama nilivyokutajia awali, mada hii imetajwa kwa ukamilifu katika Kijitabu (Al-Kurrasah). Ikiwa jambo lolote litakutatiza, unaweza kurejea kwenye kijitabu hicho kwani ndani yake mna kutosheleza, na Allah yu pamoja nawe.
Ndugu yenu, Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah
27 Safar Al-Khair 1445 H Sawa na 12/09/2023 M
Link ya jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir (Allah amuhifadhi) kwenye: Facebook