Mfululizo wa Majibu ya Mwanachuoni Mtukufu Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah, Amir wa Hizb ut-Tahrir, kwa Maswali ya Wageni kwenye Ukurasa Wake wa Facebook "Fiqhi"
Kwa Abdul Jalil Zein
Swali:
Assalamu Alaikum Warahmatullahi Wabarakatuh. Barakallahu fikum, Allah akunusuruni na akujazeni kheri Sheikh wetu mkarimu. Sheikh wetu mkarimu,
Imekuja katika kitabu cha Shakhsia ya Kiislamu (Ash-Shakhsiyyah al-Islamiyyah) Juzuu ya Kwanza kwamba kuna vitendo vinavyopingana na Aqidah ambavyo Waislamu huvifanya lakini haviwaondoi kwenye Aqidah. Ilifafanuliwa kuwa Mwislamu anaweza kusahau akaghafilika kuunganisha dhana zake na Aqidah yake, au akawa hajui mgongano wa dhana hizi na Aqidah, au Shetani anaweza kumshinda akaiacha Aqidah hii katika tendo miongoni mwa vitendo...
Sasa, anakuwaje bado ni Mwislamu anapofanya tendo linalopingana na Aqidah ya Kiislamu? Ikiwa Mwislamu atamkufurisha ndugu yake Mwislamu, si mmoja wao atakuwa amestahiki ukafiri huo, na kutamka kwake hapa ni ukafiri? Na ninajua kuwa vitendo vinajumuisha matamshi au harakati, hivyo ikiwa Mwislamu atasujudia sanamu, anakuwa kafiri kwa tendo hilo. Tafadhali naomba ufafanuzi wa vitendo vinavyopingana na Aqidah lakini Mwislamu anabaki kuwa Mwislamu licha ya kuvifanya? Na je, hukumu hii inajumuisha kuhukumu kwa yale ambayo Allah hakuyateremsha, na usekulari kafiri na mengineyo??
Jazakumullahu khayran.
Jibu:
Wa Alaikum Salaam Warahmatullahi Wabarakatuh.
Kwanza: Swali lako linahusu kile kilichokuja katika mada ya "Mapungufu katika Mwenendo" (Thagharat fi al-Suluk) katika kitabu cha Shakhsia ya Kiislamu Juzuu ya Kwanza. Makusudio ya ibara zilizopo hapo kama vile kauli yake: "Inashuhudiwa kwa Waislamu wengi kudhihirika kwa vitendo vinavyopingana na Aqidah yao ya Kiislamu..." na kauli yake: "... hiyo ni kwa sababu mwanadamu anaweza kusahau akaghafilika kuunganisha dhana zake na Aqidah yake, au akawa hajui mgongano wa dhana hizi na Aqidah yake au na kuwa kwake ni shakhsia ya Kiislamu, au Shetani anaweza kuushinda moyo wake akaiacha Aqidah hii katika tendo miongoni mwa vitendo, akafanya vitendo vinavyopingana na Aqidah hii" na mifano yake ya ibara. Makusudio yake si kile ulichoelewa katika swali lako kuhusu kufanya vitendo vinavyomtoa mtu katika Aqidah ya Kiislamu, bali makusudio ni kufanya vitendo vilivyoharamishwa na maasi yanayopingana na kile kinachowajibishwa na Aqidah ya Kiislamu katika kujisalimisha kwa hukumu za kisheria na kutozihalifu. Ufafanuzi wa hili umekuja katika sehemu zaidi ya moja kwenye mada iliyotajwa, kwa mfano:
"Ukweli ni kwamba kuwepo kwa mapungufu katika mwenendo wa Mwislamu hakumtoi katika kuwa kwake shakhsia ya Kiislamu. Hiyo ni kwa sababu mwanadamu anaweza kusahau akaghafilika kuunganisha dhana zake na Aqidah yake, au akawa hajui mgongano wa dhana hizi na Aqidah yake au na kuwa kwake ni shakhsia ya Kiislamu, au Shetani anaweza kuushinda moyo wake akaiacha Aqidah hii katika tendo miongoni mwa vitendo, akafanya vitendo vinavyopingana na Aqidah hii, au vinavyogongana na sifa za Mwislamu anayeshikamana na dini yake au kinyume na amri za Allah na makatazo Yake. Anafanya hayo yote au baadhi yake wakati ambao bado anaitakidi Aqidah hii na kuifanya kuwa msingi wa fikra zake na mielekeo yake. Kwa sababu hiyo, haisihi kusemwa kwamba katika hali kama hii ameitoka Uislamu au amekuwa shakhsia isiyo ya Kiislamu. Kwa sababu ilimradi Aqidah ya Kiislamu inaitakidiwa na yeye, basi yeye ni Mwislamu, hata kama ameasi katika tendo miongoni mwa vitendo."
"... Kwa sababu hiyo, haishangazi kwamba Mwislamu anaweza kuasi akapingana na amri za Allah na makatazo Yake katika tendo miongoni mwa vitendo. Mtu anaweza kuona ukweli unapingana na kuunganisha mwenendo na Aqidah. Anaweza kudhani kuwa maslahi yake yapo katika kile alichokifanya kisha akajuta na kutambua kosa la alichokifanya na kurejea kwa Allah. Hivyo, upingaji huu wa amri za Allah na makatazo Yake hautoi kasoro katika kuwepo kwa Aqidah kwake, bali unatoa kasoro katika kushikamana kwake na Aqidah katika tendo hili pekee. Kwa sababu hiyo, mwasi au fasiqi hachukuliwi kuwa ni murtadi (aliyetoka katika dini), bali anachukuliwa kuwa ni Mwislamu mwasi katika tendo aliloasi kwayo pekee, na huadhibiwa kwa hilo pekee, na anabaki kuwa Mwislamu ilimradi anaitakidi Aqidah ya Uislamu." - Mwisho wa maelezo kutoka katika Shakhsia.
Ni wazi kutokana na maelezo haya kwamba makusudio ni kufanya vitendo vilivyoharamishwa na makosa ya kisheria ambayo hayamtoi Mwislamu katika Aqidah yake ya Kiislamu, kama vile kunywa pombe, kuiba, au kuangalia tupu iliyoharamishwa na mfano wa hayo... hivyo anakuwa kwa maasi hayo ni mwasi fasiqi na hakuwa kafiri ilimradi anaamini Aqidah ya Kiislamu.
Pili: Kuhusu kufanya vitendo kama vile kusujudia masanamu au kutekeleza sala ya Mayahudi au Wakristo, hili si upingaji wa Aqidah na kuiacha tu, bali zaidi ya hapo ni kutoka katika Aqidah ya Kiislamu na katika Uislamu wote... na anayefanya vitendo kama hivi basi anakuwa murtadi kuitoka dini yake. Tumeshafafanua hili huko nyuma katika jibu la swali kwenye Facebook tarehe 30/04/2017 kuhusu kuepuka ukafiri na kufa katika Uislamu.
Tatu: Kuhusu kuhukumu kwa yale ambayo Allah hakuyateremsha, kuna ufafanuzi ambao tumeshauweka wazi katika majibu zaidi ya moja, na muhtasari wake ni kwamba: Kuhukumu kwa hukumu za kikafiri ni tendo miongoni mwa vitendo. Ikiwa tendo hili linaashiria itikadi ya mtendaji, yaani linaonesha kuwa mtendaji haamini Uislamu na anahukumu kwa ukafiri kutokana na kuitakidi kutofaa kwa hukumu za Uislamu, basi anayefanya tendo hili anakuwa kafiri. Ama yule anayehukumu kwa ukafiri lakini anakubali kuwa Uislamu ndio sahihi na ndio unaopaswa kuhukumiwa kwayo, katika hali hii anayefanya tendo hili anakuwa dhalimu na fasiqi na si kafiri... Aya tatu za Surah Al-Ma'idah zimeashiria hilo kuhusu kuhukumu kwa yasiyoteremsha na Allah; moja wapo inamsifu anayehukumu kwa yasiyoteremshwa na Allah kuwa ni kafiri, ya pili inamsifu kuwa ni fasiqi, na ya tatu inamsifu kuwa ni dhalimu... Allah (swt) anasema:
وَمَنْ لَمْ يَحْكُمْ بِمَا أَنْزَلَ اللَّهُ فَأُولَئِكَ هُمُ الْكَافِرُونَ
"Na yeyote asiyehukumu kwa yale aliyoyateremsha Allah, basi hao ndio makafiri." (QS Al-Ma'idah [5]: 44)
وَمَنْ لَمْ يَحْكُمْ بِمَا أَنْزَلَ اللَّهُ فَأُولَئِكَ هُمُ الظَّالِمُونَ
"Na yeyote asiyehukumu kwa yale aliyoyateremsha Allah, basi hao ndio madhalimu." (QS Al-Ma'idah [5]: 45)
وَمَنْ لَمْ يَحْكُمْ بِمَا أَنْزَلَ اللَّهُ فَأُولَئِكَ هُمُ الْفَاسِقُونَ
"Na yeyote asiyehukumu kwa yale aliyoyateremsha Allah, basi hao ndio mafasiqi." (QS Al-Ma'idah [5]: 47)
... Na kujua uhalisia wa mtawala anayehukumu kwa yasiyoteremshwa na Allah ni jambo la lazima kwa ajili ya usahihi wa kutoa hukumu juu yake.
Na miongoni mwa mambo yanayopaswa kuzingatiwa ni kwamba haijuzu kufanya wepesi katika kuwakufurisha watu. Aliyozaliwa na wazazi wawili Waislamu ni Mwislamu, na hadi ahukumiwe ukafiri ni lazima pawepo na ushahidi wa kukata (قطعي) juu ya ukafiri wake. Hivyo, hata kama kungekuwa na 90% ya ushahidi wa ukafiri wake na 10% ya ushahidi wa Uislamu wake, hahukumiwi ukafiri, bali vitendo vyake hufuatiliwa na kuhukumiwa kwa vitendo hivyo vinavyopingana na Sharia kwa kuchukuliwa kuwa ni fasiqi, mwasi, au dhalimu, lakini hahukumiwi ukafiri ilimradi ushahidi wa kukata juu ya ukafiri wake haujapatikana. Suala la takfir linasababisha kupotea kwa roho na kutekelezwa kwa hukumu za ukafi/rida, na linaweza kuleta maafa na jinai ikiwa ukafiri hautathibitishwa kwa kusimamisha hoja ya kukata...
Hili ni jambo muhimu, na ushahidi wa kisheria unaonesha hilo, ikiwemo:
1- يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا ضَرَبْتُمْ فِي سَبِيلِ اللَّهِ فَتَبَيَّنُوا وَلَا تَقُولُوا لِمَنْ أَلْقَى إِلَيْكُمُ السَّلَامَ لَسْتَ مُؤْمِنًا تَبْتَغُونَ عَرَضَ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا فَعِنْدَ اللَّهِ مَغَانِمُ كَثِيرَةٌ كَذَلِكَ كُنْتُمْ مِنْ قَبْلُ فَمَنَّ اللَّهُ عَلَيْكُمْ فَتَبَيَّنُوا إِنَّ اللَّهَ كَانَ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرًا
"Enyi mlioamini! Mnaposafiri katika njia ya Allah, basi fanyeni uchunguzi, wala msimwambie aliyekutoleeni salamu: 'Wewe si Muumini', kwa kutafuta manufaa ya maisha ya dunia. Kwani kwa Allah kuna ghanima nyingi. Hivyo ndivyo mlivyokuwa nanyi hapo kabla, kisha Allah akawafanyia hisani. Basi fanyeni uchunguzi. Hakika Allah ana khabari za mnayoyatenda." (QS An-Nisa [4]: 94)
Na katika sababu za kushuka kwa aya hii yamepokelewa hadithi, miongoni mwake: Ahmad amepokea katika Musnad yake kutoka kwa Abi Dhibyan, amesema: Nilimsikia Usama bin Zaid akihadithia akisema: "Rasulullah (saw) alitutuma kwenda Al-Huraqah kutoka kabila la Juhaynah. Akasema: Tukawashambulia asubuhi na tukapigana nao. Akawa miongoni mwao mtu ambaye walipokuja watu alikuwa mkali sana dhidi yetu, na walipokimbia alikuwa mlinzi wao. Akasema: Nikamvamia mimi na mtu mmoja katika Maansari. Akasema: Tulipomvamia, akasema: La ilaha illa Allah. Yule Ansari akajizuia naye, lakini mimi nikamuua. Habari hizo zikamfikia Mtume (saw) akasema: 'Ewe Usama, umemuua baada ya kusema: La ilaha illa Allah?' Akasema: Nikasema: Ewe Rasulullah, hakika alikuwa akijikinga tu na kifo. Akarudia hilo kwangu mpaka nikatamani lau nisingekuwa nimesilimu ila siku ile."
2- Rasulullah (saw) amesema: لَا أَزَالُ أُقَاتِلُ النَّاسَ حَتَّى يَقُولُوا: لَا إِلَهَ إِلَّا اللَّهُ، فَإِذَا قَالُوا: لَا إِلَهَ إِلَّا اللَّهُ، فَقَدْ عَصَمُوا مِنِّي أَمْوَالَهُمْ وَأَنْفُسَهُمْ إِلَّا بِحَقِّهَا، وَحِسَابُهُمْ عَلَى اللَّهِ عَزَّ وَجَلَّ "Sitaacha kuwapiga vita watu mpaka waseme: La ilaha illa Allah. Pindi watakaposema: La ilaha illa Allah, watakuwa wameilinda damu yao na mali zao kutokana nami isipokuwa kwa haki yake, na hesabu yao ipo kwa Allah (Azaza wa Jalla)." (Imepokelewa na Ahmad katika Musnad yake)
3- Imekuja katika Sahih Al-Bukhari kutoka kwa Abdullah bin Umar (ra): Kwamba Rasulullah (saw) amesema: أَيُّمَا رَجُلٍ قَالَ لِأَخِيهِ يَا كَافِرُ، فَقَدْ بَاءَ بِهَا أَحَدُهُمَا "Mtu yeyote atakayemwambia ndugu yake: 'Ewe kafiri', basi mmoja wao ameshastahiki neno hilo." Na Muslim amepokea katika Sahih yake kutoka kwa Nafi', kutoka kwa Ibn Umar, kwamba Mtume (saw) amesema: إِذَا كَفَّرَ الرَّجُلُ أَخَاهُ فَقَدْ بَاءَ بِهَا أَحَدُهُمَا "Mtu atakapomkufurisha ndugu yake, basi mmoja wao ameshastahiki neno hilo."
Kwa hivyo, haisihi kufanya haraka na wepesi katika kumhukumu Mwislamu ukafiri, bali ni lazima kuhakiki na kufanya uchunguzi wa kina...
Ndugu yenu Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah
10 Sha'ban 1438 H Sawiya na 07/05/2017 M
Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir kwenye Facebook: Facebook
Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir kwenye Google Plus: Google Plus
Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir kwenye Twitter: Twitter
Kiungo cha jibu kutoka kwenye tovuti ya Amir (Amir Web): Amir Web