Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

JIBU LA SWALI: DHAHABU YA KARA "18" INA THAMANI NA INATOLEWA ZAKA

July 05, 2019
4408

Mfululizo wa majibu ya mwanachuoni mtukufu Ata bin Khalil Abu al-Rashtah, Amiri wa Hizb ut-Tahrir

kwa maswali ya wafuasi wa ukurasa wake wa Facebook "Fiqhi"

Jibu la Swali

Kwa Samir Ibrahim

Swali/Maoni:

(Kuhusu bango nambari 836 "Zingatio katika Zaka ni dhahabu safi").

Sawa, kwani dhahabu ya kara 18 haina thamani ya kimali pia?) Mwisho.

Jibu:

Hakika maoni yako uliyoyataja ni kuhusu bango nambari 836 ambalo ni sehemu ya jibu la swali la tarehe 02 Safar 1437 H / 14/11/2015 M, na haya ndiyo yaliyokuja katika bango lililoashiriwa:

(Hakika hukumu ya Zaka katika dhahabu ni mahususi kwa dhahabu safi "kara 24" na vivyo hivyo hukumu ya Zaka katika fedha ni mahususi kwa fedha safi. Hivyo, ikiwa dhahabu imechanganywa na kitu kingine au fedha imechanganywa na kitu kingine, basi hukatwa kutoka kwenye uzito kiasi kile cha mchanganyiko ili kile kinachobaki baada ya kukata mchanganyiko kifikie nisabu. Ikiwa mtu anamiliki "gramu 85" za dhahabu ya kara "18", basi atakuwa hajamiliki nisabu kwa sababu dhahabu safi iliyomo ni chini ya gramu 85... Hivyo, Zaka ya kipande cha dhahabu ya 24 inatofautiana na Zaka ya kipande chenye uzito ule ule cha dhahabu ya 18. Dhahabu safi hukadiriwa wakati wa kuhesabu nisabu; hivyo nisabu ya dhahabu ya 24 ni gramu 85, lakini nisabu ya dhahabu ya 18 ni zaidi ya hapo kwa sababu imechanganywa na madini yasiyo ya dhahabu kwa kiasi cha robo. Yaani, dhahabu ya kara 18 ina dhahabu safi inayolingana na robo tatu ya dhahabu ya kara 24. Kwa hiyo, nisabu ya dhahabu ya 18 ni mara moja na thuluthi ya nisabu ya dhahabu safi, yaani gramu 113.33. Hivyo basi, yule anayemiliki gramu 85 za dhahabu safi ya 24 atakuwa amemiliki nisabu, na mwaka ukipita juu yake, atatoa Zaka yake 2.5% ya uzito wake. Lakini yule anayemiliki gramu 85 za dhahabu ya 18 hatakuwa amemiliki nisabu mpaka kile anachomiliki kifikie gramu 113.33, na mwaka ukipita juu yake, atatoa Zaka yake 2.5% ya uzito wake. Ni wazi hapa kwamba zingatio katika Zaka ni dhahabu safi.) Mwisho.

Nimeshangazwa na maoni yako kwa sababu inaeleweka kutoka kwayo kuwa sisi katika jibu hilo tumeupuuza thamani ya dhahabu ya kara "18" na tukaifanya haina thamani, pamoja na kwamba ni wazi katika jibu kuwa dhahabu ya kara "18" ina thamani na inatolewa Zaka. Lakini thamani yake ni ndogo kuliko thamani ya dhahabu ya kara "24" ikiwa uzito ni mmoja. Kwa sababu hiyo, tulibainisha katika kuainisha nisabu ya Zaka ya dhahabu ya kara "18" kuwa ni (mara moja na thuluthi ya nisabu ya dhahabu safi, yaani gramu 113.33. Hivyo basi, yule anayemiliki gramu 85 za dhahabu safi ya 24 atakuwa amemiliki nisabu, na mwaka ukipita juu yake, atatoa Zaka yake 2.5% ya uzito wake. Lakini yule anayemiliki gramu 85 za dhahabu ya 18 hatakuwa amemiliki nisabu mpaka kile anachomiliki kifikie gramu 113.33, na mwaka ukipita juu yake, atatoa Zaka yake 2.5% ya uzito wake). Kwa hiyo, thamani ya dhahabu ya kara "18" haijapuuzwa katika jibu, bali thamani yake ni thabiti na inatolewa Zaka ikifikia nisabu sawasawa na inavyotolewa Zaka dhahabu ya kara "24" ikifikia nisabu. Kila kilichopo ni kwamba kiwango cha nisabu cha kila mmoja wao ni tofauti na kiwango cha nisabu cha mwenzake kwa sababu dhahabu ya kara "18" imechanganywa na madini mengine kwa kiasi cha robo.

Sijui sababu ya maoni yako isipokuwa labda uliyasoma kwa haraka! Basi yarudie kuyasoma kwa mazingatio, Mwenyezi Mungu akurehemu... Na namuomba Mwenyezi Mungu awaongoe wote katika jambo lililo sahihi zaidi.

Ndugu yenu, Ata bin Khalil Abu al-Rashtah

01 Dhu al-Qi'dah 1440 H Inayosadifiana na 04/07/2019 M

Link ya jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amiri (Mungu amuhifadhi) kwenye Facebook

Link ya jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amiri (Mungu amuhifadhi) kwenye Tovuti

Share Article

Share this article with your network