Mfululizo wa Majibu ya Mwanachuoni Mtukufu Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah, Amir wa Hizb ut-Tahrir, kwa maswali ya wageni wa ukurasa wake wa Facebook "Fiqhi"
Jawabu la Swali
Kwa Muhammad Ishak
Swali:
Assalamu Alaikum Warahmatullahi Wabarakatuh,
Mwenyezi Mungu akubariki na akulinde ewe Sheikh wetu...
Swali: Baadhi ya wanafikra nchini kwetu Indonesia wanakataa kurejea kwenye matumizi ya sarafu za dhahabu na fedha na wanasema kuwa Sharia haiamrishi kutumia sarafu maalum, kwa dalili kwamba Umar bin Al-Khattab alinuia kutengeneza dirham kutokana na ngozi za ngamia. Je, maoni haya ni sahihi? Mwenyezi Mungu akulipe kheri.
Jibu:
Walaikum Assalam Warahmatullahi Wabarakatuh,
1- Tumebainisha dalili za kisheria kuhusu dhahabu na fedha kuwa ndizo sarafu mbili ambazo zinapaswa kutegemewa na dola katika Uislamu. Tumefafanua jambo hili katika kitabu cha An-Nidham al-Iqtisadi (Mfumo wa Kiuchumi) na katika kitabu cha Al-Amwal fi Dawlat al-Khilafah (Mali katika Dola ya Khilafah)... Kadhalika tumelifafanua jambo hili katika kitabu cha Muqaddimat al-Dustur (Utangulizi wa Katiba), Sehemu ya Pili, katika Kifungu cha "167" na ufafanuzi wake... Na nakunukulia yaliyokuja katika Muqaddimat al-Dustur kuhusiana na hili kwa ajili ya uwazi na ulaini wake:
(Kifungu cha 167: Sarafu ya dola ni dhahabu na fedha, iwe ni vipande vilivyogongwa chapa au visivyogongwa chapa, na haijuzu kuwa na sarafu nyingine kando nazo. Inajuzu kwa dola kutoa kitu kingine badala ya dhahabu na fedha kwa sharti kwamba kiwe na kiasi kinacholingana nacho katika hazina ya dola miongoni mwa dhahabu na fedha. Hivyo, inajuzu kwa dola kutoa shaba, shaba nyeusi (bronze), karatasi au kinginecho na kukigonga kwa jina lake kama sarafu yake ikiwa kina thamani inayolingana nacho kikamilifu miongoni mwa dhahabu na fedha.
Uislamu ulipoamua hukumu za biashara na ukodishaji, haukuweka kitu maalum kwa ajili ya kubadilishana bidhaa au kubadilishana juhudi na manufaa ambacho mabadilishano hayo yatafanyika kwa msingi wake kama faradhi. Bali ulimuacha mwanadamu afanye mabadilishano kwa kitu chochote ilimradi kuwe na kuridhiana katika mabadilishano hayo. Inajuzu kwake kumuoa mwanamke kwa kumfundisha ushonaji, na inajuzu kununua gari kwa kufanya kazi kiwandani kwa mwezi mmoja, na inajuzu kufanya kazi kwa mtu kwa kiasi fulani cha sukari, na hivi ndivyo Sharia ilivyoacha wazi mabadilishano kwa wanadamu kwa kile wanachokitaka miongoni mwa vitu. Hii ni kwa dalili ya ujumla ya ushahidi wa biashara na ukodishaji:
وَأَحَلَّ اللَّهُ الْبَيْعَ
"Na Mwenyezi Mungu amehalalisha biashara." (QS. Al-Baqarah [2]: 275)
Kwa kitu chochote kwa kitu chochote, na hadith:
أَعْطُوا الأَجِيرَ أَجْرَهُ قَبْلَ أَنْ يَجِفَّ عَرَقُهُ
"Mpeni mwajiriwa ujira wake kabla ya jasho lake kukauka." (Imepokelewa na Ibn Majah).
Yaani, mfanyakazi anapaswa kulipwa ujira wake anapomaliza kazi yake, bila kujali aina ya ujira huo. Kadhalika, vitu hivi ambavyo mabadilishano hufanyika kwayo si vitendo (af'al) ili asili yake iwe ni kufungika (kuhitaji dalili), bali ni vitu (ashyaa). Na asili ya vitu ni uhalali (ibahah) ilimradi haijaja dalili ya uharamu, na haijaja dalili inayoharamisha vitu hivi. Kwa hiyo, inajuzu kufanya miamala ya kisheria kwayo kama biashara, ununuzi, zawadi, na mabadilishano... isipokuwa kile kilichokuja na andiko la kuharamisha mabadilishano ndani yake. Kwa msingi huu, mabadilishano ya bidhaa kwa sarafu na sarafu kwa bidhaa kadhalika yanaruhusiwa kwa ujumla, isipokuwa mabadilishano ya sarafu kwa sarafu (kubadilisha fedha), kwani yana hukumu maalum na yamefungwa na hukumu hizo. Vilevile, mabadilishano ya juhudi kwa sarafu na sarafu kwa juhudi yanaruhusiwa kwa ujumla, isipokuwa bidhaa au juhudi ambazo zimekuja na andiko la kuziharamisha. Kwa msingi huu, mabadilishano ya bidhaa kwa kitengo maalum cha sarafu na mabadilishano ya juhudi kwa kitengo maalum cha sarafu yanaruhusiwa pia kwa ujumla, vyovyote kitengo hicho cha sarafu kitakavyokuwa. Iwe kitengo hiki hakina dhamana kabisa kama sarafu za karatasi za lazima (fiat money), au kitengo hiki kina dhamana ya asilimia fulani ya dhahabu kama sarafu za karatasi zenye dhamana (fiduciary money), au kitengo hiki kina dhamana ya dhahabu na fedha inayolingana na thamani yake kikamilifu kama sarafu za karatasi wakili (representative money), zote hizi mabadilishano ndani yake ni sahihi. Kwa sababu hiyo, ni sahihi kubadilisha bidhaa au juhudi kwa kitengo chochote maalum cha sarafu. Hivyo, inasihi kwa Muislamu kuuza kwa sarafu yoyote, kununua kwa sarafu yoyote, kukodisha kwa sarafu yoyote, na kuwa mwajiriwa kwa sarafu yoyote.
Hata hivyo, ikiwa dola inataka kuweka kitengo maalum cha sarafu kwa nchi inayotawala ili kutekeleza hukumu za kisheria zinazohusiana na mali kama mali yenyewe, kama vile Zaka, kubadilisha fedha (sarf), riba na nyinginezo, au hukumu zinazohusiana na mtu anayemiliki mali kama vile faini ya damu (diyah) na kiasi cha wizi na nyinginezo, basi dola haina mkono wa hiari wa kuweka kitengo chochote maalum cha sarafu. Bali inalazimika kuwa na kitengo maalum cha sarafu ambacho haijuzu kwake kuweka kingine kwa namna yoyote ile. Sharia imebainisha kitengo maalum cha sarafu katika jinsi maalum iliyokuja na andiko (nass), nayo ni dhahabu na fedha. Ikiwa dola inataka kutoa sarafu, basi inafungwa na ukweli kwamba sarafu hii lazima iwe ni dhahabu na fedha na si kitu kingine. Sharia haikuiachia dola itoe sarafu inayotaka ya aina yoyote inayopenda, bali imebainisha vitengo vya sarafu ambavyo dola inapaswa kuvifanya kama sarafu yake ikiwa inataka kutoa sarafu kwa vitengo maalum vya sarafu, navyo ni dhahabu na fedha pekee. Dalili ya hili ni kwamba Uislamu umeunganisha dhahabu na fedha na hukumu thabiti zisizobadilika. Wakati ulipofaradhi diyah, uliweka kiasi maalum cha dhahabu, na ulipowajibisha kukatwa mkono kwa mwizi, uliweka kiasi kinachokatwa kwa wizi huo katika dhahabu. Mtume ﷺ alisema katika barua yake aliyowaandikia watu wa Yemen:
وَأَنَّ فِي النَّفْسِ المُؤْمِنَةِ مِاْئَةً مِنَ الإِبِلِ، وَعَلَى أَهْلِ الْوَرِقِ أَلْفُ دِينَارٍ
"Na katika nafsi ya muumini (ikiuawa) kuna ngamia mia moja, na kwa watu wa fedha (warq) ni dinari elfu moja." (Imetajwa na Ibn Qudamah katika Al-Mughni kutokana na yale aliyoyapokea Amr bin Hazm kutoka katika barua ya Mtume ﷺ kwenda kwa watu wa Yemen). Na katika riwaya ya An-Nasa'i kutoka kwenye barua ya Mtume ﷺ kwenda kwa watu wa Yemen (na kwa watu wa dhahabu ni dinari elfu moja) badala ya (watu wa fedha). Na Mtume ﷺ amesema:
لا تُقْطَعُ يَدُ السَّارِقِ إِلاَّ فِي رُبْعِ دِينَارٍ فَصَاعِداً
"Mkono wa mwizi haukatwi isipokuwa katika robo dinari na kuendelea." (Imepokelewa na Muslim kupitia kwa Aisha r.a).
Huu ukomo wa hukumu maalum kwa dinari, dirham, na mithqal unafanya dinari kwa uzito wake wa dhahabu na dirham kwa uzito wake wa fedha kuwa kitengo cha sarafu ambacho thamani za vitu na juhudi hupimwa kwacho. Hivyo kitengo hiki cha sarafu ndicho sarafu yenyewe, na ndicho msingi wa sarafu. Kuwa Sharia imeunganisha hukumu za kisheria na dhahabu na fedha kwa nass (andiko) wakati hukumu hizi zinapohusiana na sarafu, ni dalili kwamba sarafu si kitu kingine isipokuwa dhahabu na fedha pekee. Aidha, Mwenyezi Mungu Subhaanahu wa Ta'ala alipowajibisha Zaka ya sarafu, aliwajibisha katika dhahabu na fedha pekee, na akaiwekea nisabu ya dhahabu na fedha. Kuzingatia Zaka ya sarafu kwa dhahabu na fedha kunabainisha kuwa sarafu ni dhahabu na fedha. Vilevile, hukumu za kubadilisha fedha (as-sarf) zilizokuja katika miamala ya sarafu pekee, zilikuja kwa dhahabu na fedha pekee, na miamala yote ya kifedha iliyokuja katika Uislamu ilikuja kwa dhahabu na fedha. Sarf ni kuuza sarafu kwa sarafu, iwe ni kuuza sarafu kwa sarafu hiyohiyo, au kuuza sarafu kwa sarafu nyingine. Kwa maneno mengine, sarf ni kuuza pesa kwa pesa. Kubainisha kwa Sharia miamala ya sarf – ambayo ni muamala wa kisarafu tupu – kwa dhahabu na fedha pekee bila kinginecho, ni dalili ya wazi kwamba sarafu lazima iwe dhahabu na fedha pekee. Mtume ﷺ amesema:
وَبِيعُوا الذَّهَبَ بِالْفِضَّةِ وَالْفِضَّةَ بِالذَّهَبِ كَيْفَ شِئْتُمْ
"Na uzeni dhahabu kwa fedha na fedha kwa dhahabu upendavyo." (Imepokelewa na Al-Bukhari kupitia kwa Abu Bakrah; na Muslim amepokea mfano wake kupitia kwa Ubadah bin Al-Samit). Na Mtume ﷺ amesema:
الذَّهَبُ بِالْوَرِقِ رِباً إِلاَّ هَاءَ وَهَاءَ
"Dhahabu kwa fedha ni riba isipokuwa kwa mkono kwa mkono (papo kwa hapo)." (Muttafaq Alayh kupitia kwa Umar).
Zaidi ya hayo, Mtume ﷺ ameweka dhahabu na fedha kuwa sarafu na akazifanya hizo pekee kuwa kipimo cha kisarafu ambacho hurejewa kama kipimo cha bidhaa na juhudi. Na kwa msingi wa hizo mbili, miamala ilikuwa ikifanyika. Akajalia kipimo cha sarafu hii kuwa ni Awqiyyah, Dirham, Daniq, Qirat, Mithqal, na Dinar. Hivi vyote vilikuwa vikijulikana na kuwa mashuhuri katika zama za Mtume ﷺ watu wakitumia miamala kwayo. Na jambo lililothibiti ni kwamba yeye ﷺ aliviidhinisha. Na vilikuwa vikitumika katika dhahabu na fedha biashara zote na ndoa kama ilivyothibiti katika hadith sahihi. Hivyo, kitendo cha Mtume kuifanya sarafu kuwa ni dhahabu na fedha, na kitendo cha Sharia kuunganisha baadhi ya hukumu za kisheria nazo pekee na kuifanya Zaka ya sarafu kuwa ndani ya hizo pekee, na kufanya sarf na miamala ya kifedha kwayo; yote hayo ni dalili ya wazi kwamba sarafu ya Uislamu ni dhahabu na fedha pekee.) Mwisho wa nukuu kutoka katika kitabu cha Muqaddimat al-Dustur.
2- Hivyo tunapata dalili za kisheria zikishirikiana katika kuashiria kuwa sarafu ambayo dola inachukua katika Uislamu ni dhahabu na fedha na kwamba haichukui sarafu nyingine. Pamoja na kwamba kule kuidhinisha kwa Mtume ﷺ sarafu hizi mbili kunatosha peke yake kuthibitisha hukumu ya kisheria katika suala la sarafu katika Uislamu, lakini Sharia haikuishia tu katika kuidhinisha kwa Mtume ﷺ sarafu hizo mbili, bali ilivuka hapo na kuweka dalili katika mlango wa riba, mlango wa zaka, na mlango wa diyat (faini za damu)... n.k., zinazoashiria kuzingatiwa kwa dhahabu na fedha kama sarafu kisheria maadamu hukumu hizi za kisheria zipo, yaani mpaka siku ya Kiyama. Hivyo hakuna njia ya kusema kuwa tuchukue sarafu nyinginezo kisheria...
3- Imepokewa kutoka kwa Umar (r.a) kwamba alinuia (hamma) kuchukua dirham kutokana na ngozi za ngamia, na hilo limekuja kwa mujibu wa tulivyolifuatilia kupitia njia mbili:
Al-Baladhuri amepokea katika kitabu chake Futuh al-Buldan (3/ 578): "Alituhadithia Amr al-Naqid akisema: Alituhadithia Ismail bin Ibrahim akisema: Alituhadithia Yunus bin Ubayd, kutoka kwa Al-Hasan akisema: Watu walikuwa, na hali wao ni watu wa ukafiri, walishatambua nafasi ya dirham hii miongoni mwa watu, hivyo wakaifanya iwe nzuri na safi. Ilipofika kwenu mkaichanganya na uchafu na kuifisidi. Na Umar bin Al-Khattab alisema: Nilinuia nifanye dirham zitokane na ngozi za ngamia. Akaambiwa: Ikiwa ni hivyo, hakutakuwa na ngamia. Basi akaacha."
Abdur-Razzaq Al-San'ani (aliyefariki 211 H) amepokea katika kitabu chake Tafsir Abdur-Razzaq kutoka kwa Ma'mar na Yahya, kutoka kwa Ayyub, kutoka kwa Ibn Sirin kwamba Umar bin Al-Khattab alitaka kupiga dirham kutokana na ngozi za ngamia, wakasema: "Basi ngamia wataisha", hivyo akaziacha.
Baadhi ya watu wamejaribu kutumia hili kama dalili kwamba inajuzu kwa dola katika Uislamu isifanye sarafu yake kuwa dhahabu na fedha na ichukue sarafu kutokana na mali yoyote inayokubaliwa kama vile ngozi na mfano wake... Na kama ulivyotaja katika swali lako, baadhi ya watu wa zama hizi wanakataa kurejea kwenye msingi wa dhahabu na fedha na wanakubali sarafu za karatasi za lazima (fiat money) wakitegemea kwa madai yao kauli hii iliyopokewa kutoka kwa Umar (r.a)... Na jibu la jambo hili ni kupitia nyanja kadhaa:
a- Kama tulivyotaja na kubainisha hapo awali, dalili za kisheria zinashirikiana katika kuashiria kuwa sarafu katika Uislamu ni dhahabu na fedha, na hiyo inatokana na kuidhinisha kwa Mtume ﷺ na kutokana na kuunganisha kwa Sharia hukumu nyingi na dhahabu na fedha kwa kuzingatia kuwa ni sarafu... Sasa itakuwaje dalili hizi zote ziachwe na kuwekwa kando, kisha itumiwe riwaya kutoka kwa Umar (r.a) ili kuthibitisha kauli kinyume na dalili hizo thabiti na zilizo wazi? Je, hili si jambo la ajabu na lililo mbali na utoaji dalili sahihi kwa kutumia dalili za kisheria?!
b- Kwa upande wa sanad (mfululizo wa wapokezi), kuna tatizo katika riwaya hii kupitia njia zote mbili ilizopokewa. Katika sanad mbili za riwaya hii kuna mkatiko (inqita'), kwa sababu mpokezi wa kwanza kutoka kwa Umar bin Al-Khattab ni Al-Hasan al-Basri na yeye hakumdiriki Umar (r.a) wala hakuchukua kutoka kwake, kwani alizaliwa mwishoni mwa ukhalifa wa Umar muda mfupi kabla ya kifo chake. Na mpokezi katika riwaya ya pili ni Ibn Sirin, na yeye kadhalika hakumdiriki Umar bin Al-Khattab wala hakupokea kutoka kwake; inasemekana alizaliwa mwishoni mwa ukhalifa wa Umar na inasemekana katika ukhalifa wa Uthman... Sasa inasihi vipi kuchukua riwaya hizi ambazo zina mkatiko katika sanad mkabala na hadith za Mtume zilizo thabiti na sahihi?!
c- Riwaya ya Al-Hasan al-Basri inaonyesha kuwa Umar bin Al-Khattab (r.a) alisema: (Nilinuia nifanye dirham zitokane na ngozi za ngamia), yaani jambo hilo halikuvuka kwa Umar zaidi ya kuwa ni "nuia" (hamma) ya kufanya kitendo hicho, na hakukifanya... Sasa tunategemea vipi jambo hilo katika kuhalalisha kuchukua sarafu isiyokuwa dhahabu na fedha? Yaani, tunategemea vipi "nuia" tupu ya Umar ambayo haikutekelezwa mkabala na dalili kutoka katika Qur'an Tukufu na dalili thabiti kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ ambazo ziko wazi katika kubainisha sarafu katika Uislamu?! Je, hili si jambo la ajabu?!
d- Jambo thabiti ni kwamba Makhalifa Waongofu walitumia kama alivyotumia Mtume ﷺ dhahabu na fedha kwa kuzizingatia kuwa ni sarafu. Yaani Umar (r.a), sarafu iliyokuwa ikitumiwa katika zama za ukhalifa wake ilikuwa ni Dinar ya dhahabu na Dirham ya fedha... Sasa tunaachaje jambo hili thabiti na endelevu la zama za Mtume ﷺ na Makhalifa Waongofu akiwemo Umar, kisha tunachukua riwaya inayosema kuwa Umar (r.a) alinuia kuchukua dirham kutokana na ngozi za ngamia?! Yaani, tunachukua vipi riwaya ya "nuia" yake na kuacha yale yaliyothibiti kutokana na kitendo chake cha kutumia dhahabu na fedha kama sarafu katika zama za ukhalifa wake (radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu ya Maswahaba wote)?
Hivyo inabainika kuwa utoaji dalili kupitia kauli iliyopokewa kutoka kwa Umar (r.a) ni utoaji dalili usio na nafasi yake, na kwamba hausimami kama dalili ya kauli inayodai kuwa Uislamu haukubainisha sarafu kwa ajili ya dola kuichukua, kadhalika haufai kupingana na dalili zilizo imara zaidi na thabiti zaidi...
4- Pamoja na yaliyotajwa hapo juu, kuacha kufanya kazi kwa msingi wa dhahabu na fedha ulimwenguni na kuchukua karatasi za lazima (fiat money), kumepelekea madhara mengi na makubwa, kama vile kuyumbayumba kwa viwango vya kubadilisha fedha, kudhibitiwa kwa masoko na dola ya Marekani, kuathirika kwa sarafu za nchi dhaifu, na kupungua kwa nguvu yake ya ununuzi kwa asilimia kubwa sana... n.k. miongoni mwa madhara yanayojulikana kwa kila anayefuatilia nyanja za kisarafu, kifedha, na kiuchumi... Na haiwezekani kuondokana na madhara haya na udhibiti wa nchi kubwa za kirasimali na hususan Marekani, isipokuwa kwa kurejea kwenye msingi wa dhahabu na fedha na kuzifanya kuwa sarafu, na kuuvuta ulimwengu kuzifanya kuwa sarafu ili kuondoa madhara hayo yanayotokana na utawala wa sarafu ya karatasi ya nchi kafiri mabeberu na udhibiti wa uchumi wa dunia, hususan kutoka kwa Marekani... Na Dola ya Khilafah ndiyo dola yenye sifa za kufanya hivyo kwa idhini ya Mwenyezi Mungu...
Yote yaliyotangulia yanabainisha wazi uwajibu wa kuwa dhahabu na fedha ndizo sarafu ya kisheria ya Dola ya Khilafah na si kitu kingine... Na Mwenyezi Mungu ndiye Mjuzi zaidi na mwenye Hekima zaidi.
Ndugu yenu Ataa bin Khalil Abu al-Rashtah
24 Muharram al-Haram 1442 H Inalingana na 12/09/2020 M
Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir (Mwenyezi Mungu amhifadhi) kwenye Facebook
Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir (Mwenyezi Mungu amhifadhi) Web