Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

JIBU LA SWALI: NGUO ILIYO NA KALONIA NI NAJISI NA SWALA HAISIHI NDANI YAKE

November 05, 2020
5205

Mfululizo wa Majibu ya Mwanachuoni Mtukufu Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah, Ameer wa Hizb ut-Tahrir, kwa Maswali ya Wageni kwenye Ukurasa Wake wa Facebook "Fiqhi"

Jibu la Swali

Kwa Tarek Ifaoui

Swali:

Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Ni nini hukumu ya kuswali na nguo zilizotiwa manukato yenye kileo (alkoholi)? Jazakumullahu Khayran.

Jibu:

Waalaykum Salaam Warahmatullahi Wabarakatuh,

Kwanza: Hakika manukato yaliyochanganywa na alkoholi ya ethili (ethanol) yanachukuliwa kuwa ni khamr (kileo) na yanashughulikiwa kisheria kwa hukumu za khamr, hivyo yanakuwa ni najisi... Na tumeyabainisha hayo yote katika majibu mbalimbali, ikiwemo jibu la swali la tarehe 23 Jumada al-Ula 1435 H sawia na tarehe 24/03/2014 M, ambapo ilielezwa hivi:

(Kama nilivyofahamu kutoka kwa wataalamu wa sayansi ya alkoholi, zipo aina mbili: alkoholi ya ethili (ethanol) na alkoholi ya methili (methanol). Ikiwa jina lililotajwa katika swali "ethanol" ni alkoholi ya ethili, basi jibu ni kama ifuatavyo:

1- Kuna aina ya alkoholi inayoitwa methili (methanol), na nimeambiwa kuwa hiyo hailevishi lakini ni sumu yenye kuua. Spirit ya kuwashia moto ni ya aina ya methili, na hutokana na vumbi la mbao na mengineyo, na kuinywa husababisha upofu na hupelekea kifo ndani ya siku chache. Kwa msingi huo, methili si khamr, na haichukui hukumu ya khamr katika upande wa unajisi na uharamu, isipokuwa tu katika upande wa kuitumia methili kama sumu kwa mujibu wa kanuni ya madhara (dharar). Ibn Majah amepokea kutoka kwa Ubadah bin al-Samit:

لَا ضَرَرَ وَلَا ضِرَارَ

"Hakuna kudhuriana wala kulipizana dhara." (Ibn Majah)

2- Na kuna aina inayoitwa ethili (ethanol), nayo ndiyo inayotumiwa katika vinywaji vyenye kulevya vilivyochachushwa au kuchujwa. Spirit ya kitabibu (surgical spirit) ni ya aina hii, pia alkoholi ya ethili hutumiwa katika viwanda kama kihifadhi cha baadhi ya bidhaa, kama kikaushia unyevu, kama kiyeyushia baadhi ya alikali na mafuta, kama kizuia kuganda kwa barafu (anti-freeze), kama kiyeyushia baadhi ya dawa, na kama kiyeyushia vitu vyenye harufu nzuri kama kalonia (cologne) na manukato, na huingia katika utengenezaji wa baadhi ya vifaa vya useremala. Matumizi haya yamegawanyika sehemu tatu:

a- Sehemu ambayo alkoholi hutumiwa kama kiyeyushia tu, au kama kiongezi kwenye baadhi ya vitu, na matumizi haya hayapotezi asili ya alkoholi wala sifa zake, bali inabaki katika hali yake ya muundo na uwezo wa kulevya. Sehemu hii ni haramu kuitumia kabisa, na mfano wake ni kalonia. Kalonia haijuzu kuitumia na inabaki kuwa najisi kwa sababu unajisi ulichanganyika nayo na alkoholi ilevayo ikabaki katika hali yake. Hivyo, hiyo ni bidhaa iliyochanganywa na khamr, na khamr ni najisi. Dalili ya hayo ni hadith ya Al-Khushani:

Ad-Daraqutni amepokea kutoka kwa Al-Khushani, amesema: Nilisema: Ewe Mtume wa Allah, sisi tunachanganyika na washirikina na hatuna vyungu wala vyombo isipokuwa vyombo vyao. Akasema:

اسْتَغْنُوا عَنْهَا مَا اسْتَطَعْتُمْ فَإِنْ لَمْ تَجِدُوا فَارْحَضُوهَا بِالْمَاءِ فَإِنَّ الْمَاءَ طَهُورُهَا ثُمَّ اطْبُخُوا فِيهَا

"Jiepusheni nazo kadiri muwezavyo, lakini msipopata (nyingine), basi zisafisheni kwa maji, kwani maji ndiyo yenye kuzitwaharisha, kisha pikeni ndani yake." (Ad-Daraqutni)

Mtume ﷺ amesema: "kwani maji ndiyo yenye kuzitwaharisha", yaani vile vyombo vilikuwa najisi kwa kuwekwa khamr ndani yake, na vikawa twahara baada ya kuoshwa. Hii ni dalili kwamba khamr ni najisi. Na swali lilikuwa kuhusu vile vyombo ambavyo ndani yake huwekwa khamr, kama ilivyokuja katika riwaya ya Al-Khushani kwa Abu Dawood kutoka kwa Abu Tha'laba al-Khushani, kwamba alimuuliza Mtume wa Allah ﷺ akisema: Sisi tunaishi jirani na watu wa Kitabu nao hupika nguruwe katika vyungu vyao na kunywa khamr katika vyombo vyao, Mtume wa Allah ﷺ akasema:

إِنْ وَجَدْتُمْ غَيْرَهَا فَكُلُوا فِيهَا وَاشْرَبُوا، وَإِنْ لَمْ تَجِدُوا غَيْرَهَا فَارْحَضُوهَا بِالْمَاءِ وَكُلُوا وَاشْرَبُوا

"Mkipata nyinginezo basi kuleni na kunyweni ndani yake, na msipopata nyingine, basi zisafisheni kwa maji na kuleni na kunyweni." (Abu Dawood)

Hivyo, nguruwe na khamr ni najisi, na hunajisisha chombo kinachowekwa ndani yake, hivyo ni lazima kioshwe ili kukitwaharisha kabla ya kukitumia.

b- Sehemu ambapo alkoholi inabadilika kutoka asili yake, na kupoteza sifa yake ya kulevya, na kutokana nayo na vitu vingine inatokea bidhaa mpya yenye sifa tofauti na sifa za alkoholi, lakini haina sumu. Hii ni bidhaa mpya ambayo haichukui hukumu ya khamr na inakuwa twahara kama bidhaa nyingine yoyote ambayo inafanyiwa kazi kanuni ya "Asili katika vitu ni kuruhusiwa (ubaha) mpaka itapokuja dalili ya kuharamisha".

c- Sehemu ambapo alkoholi inabadilika kutoka asili yake, na kupoteza sifa yake ya kulevya, na kutokana nayo na vitu vingine inatokea bidhaa mpya yenye sifa tofauti na sifa za alkoholi, lakini ina sumu. Hukumu yake ni hukumu ya sumu: ni twahara lakini matumizi yake ni haramu kwa kunywa au kwa kujidhuru mwenyewe au kudhuru wengine.

3- Kwa hiyo, alkoholi ya ethili ikichanganywa na vitu vingine, hukumu yake itategemea kujua ikiwa mchanganyiko huo umepoteza sifa ya kulevya au la, na ikiwa mchanganyiko huo ni sumu au si sumu... Na hili linahitaji uhakiki wa uhalisia (tahqiq al-manat) kulingana na wataalamu. Ikithibitika kisayansi au kivitendo kuwa mchanganyiko huu unalevya, basi unachukua hukumu ya khamr, na hii inaonyesha kuwa ethili katika mchanganyiko huu haijapoteza sifa na asili yake. Ama ikithibitika kisayansi au kivitendo kuwa mchanganyiko huu haulevishi na si sumu, basi hauchukui hukumu ya khamr wala hukumu ya sumu. Na ikithibitika kisayansi au kivitendo kuwa mchanganyiko huu haulevishi lakini ni sumu, basi hauchukui hukumu ya khamr, bali unachukua hukumu ya sumu.

Kwa hiyo, ikiwa mchanganyiko unaozalishwa unalevya kama vile kalonia, basi unachukua hukumu ya khamr, kwa sababu ya kauli ya Mtume ﷺ katika hadith iliyopokelewa na Al-Bukhari na Muslim kutoka kwa Aisha Mama wa waumini (ra), amesema: "Kila kinywaji chenye kulevya ni haramu", na katika hadith iliyopokelewa na Muslim kutoka kwa Ibn Umar, amesema: Mtume wa Allah ﷺ amesema:

كُلُّ مُسْكِرٍ خَمْرٌ، وَكُلُّ مُسْكِرٍ حَرَامٌ

"Kila chenye kulevya ni khamr, na kila chenye kulevya ni haramu..." (Muslim)

Na katika riwaya nyingine ya Ibn Umar: "Kila chenye kulevya ni khamr, na kila khamr ni haramu".

Khamr ni haramu katika mambo kumi na siyo tu inaponywewa, kwani At-Tirmidhi amepokea kutoka kwa Anas bin Malik, amesema:

لَعَنَ رَسُولُ اللَّهِ ﷺ فِي الخَمْرِ عَشَرَةً: عَاصِرَهَا، وَمُعْتَصِرَهَا، وَشَارِبَهَا، وَحَامِلَهَا، وَالمَحْمُولَةُ إِلَيْهِ، وَسَاقِيَهَا، وَبَائِعَهَا، وَآكِلَ ثَمَنِهَا، وَالمُشْتَرِي لَهَا، وَالمُشْتَرَاةُ لَهُ

"Mtume wa Allah ﷺ amewalaani kumi kuhusiana na khamr: mkamuaji wake, anayekamuliwa (kwa ajili yake), mnywaji wake, mbebaji wake, anayebebewa, mnyweshaji wake, muuzaji wake, mlaji wa thamani yake, mnunuzi wake, na anayenunuliwa." (At-Tirmidhi)

Basi yeyote kati ya hawa kumi ni haramu.) Mwisho wa nukuu.

Pili: Manukato yaliyo na alkoholi kama kalonia kwa mfano ni najisi. Na miongoni mwa masharti ya usahihi wa swala ni usafi (twahara) wa nguo na mwili kama inavyoonekana katika dalili zifuatazo:

1- Kuhusu sharti la twahara ya mwili kwa ajili ya swala: Hadith iliyopokelewa na Ibn Abbas kutoka kwa Mtume ﷺ amesema:

تَنَزَّهُوا مِنَ الْبَوْلِ فَإِنَّ عَامَّةَ عَذَابِ الْقَبْرِ مِنْهُ

"Jitakaseni kutokana na mkojo, kwani hakika adhabu nyingi za kaburi zinatokana nao." (Ibn Hamid)

Na hadith iliyopokelewa na Ad-Daraqutni kutoka kwa Abu Hurairah amesema: Mtume wa Allah ﷺ amesema:

أَكْثَرُ عَذَابِ الْقَبْرِ في الْبَوْلِ

"Adhabu nyingi za kaburi zinatokana na mkojo." (Ad-Daraqutni)

2- Kuhusu sharti la twahara ya nguo kwa ajili ya swala: Kauli yake Allah Ta'ala:

وَثِيَابَكَ فَطَهِّرْ

"Na nguo zako uzitwaharishe." (QS. Al-Muddaththir [74]: 4)

Na hadith aliyoipokea Al-Bukhari katika Sahih yake kutoka kwa Asma bint Abi Bakr as-Siddiq kwamba alisema: Mwanamke mmoja alimuuliza Mtume wa Allah ﷺ akasema: Ewe Mtume wa Allah, unaonaje mmoja wetu ikisibu nguo yake damu ya hedhi, afanye nini? Mtume wa Allah ﷺ akasema:

إِذَا أَصَابَ ثَوْبَ إِحْدَاكُنَّ الدَّمُ مِنْ الْحَيْضَةِ فَلْتَقْرُصْهُ ثُمَّ لِتَنْضَحْهُ بِمَاءٍ ثُمَّ لِتَصَلِّي فِيهِ

"Ikiwa damu ya hedhi itasibu nguo ya mmoja wenu, basi aisugue, kisha ainyeshee maji (aioshe), kisha aswali ndani yake." (Bukhari)

3- Kwa hiyo, kuswali kukiwa na manukato yenye alkoholi kwenye nguo au mwili ni swala isiyo sahihi.

Hivi ndivyo ninavyoona katika suala hili na Allah ni Mjuzi zaidi na Mwenye Hekima zaidi.

Ndugu yenu, Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah

19 Rabi’ al-Awwal 1442 H Sawia na 05/11/2020 M

Kiungo cha jibu kutoka ukurasa wa Ameer (Allah amuhifadhi) kwenye Facebook Kiungo cha jibu kutoka ukurasa wa Ameer (Allah amuhifadhi) kwenye Tovuti

Share Article

Share this article with your network