Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

Jibu la Swali: Biashara ya Kielektroniki

December 20, 2024
2129

Mfululizo wa Majibu ya Mwanachuoni Mtukufu Ata bin Khalil Abu al-Rashta, Amir wa Hizb ut Tahrir, kwa Maswali ya Wafuasi wa Ukurasa Wake wa Facebook "Fiqhi"

Jibu la Swali

Biashara ya Kielektroniki

Kwa Humam Ibrahim

Swali:

Assalamu Alaikum Warahmatullahi Wabarakatuh, Allah ayafanye maisha yenu yawe na heri enyi ndugu zangu katika imani,

Nataka kuwauliza swali na naomba jibu la kina,

Swali: Je, inajuzu kufanya biashara ya kielektroniki na kampuni ya Dxn ya Malaysia, ambapo kampuni hii inategemea uuzaji wa virutubisho vya chakula, shampoo, krimu za ngozi... n.k? Kampuni hii unanunua kutoka kwao kwa kiasi fulani cha pesa na wanakupa punguzo la asilimia sita ikiwa pointi zako zitafika pointi 100, na kila pointi zinapoongezeka wanakupa punguzo kubwa zaidi. Pointi hizi hubadilishwa kuwa kiasi cha pesa unachotumiwa ama kwa njia ya bahasha au maandishi yanayokufikia kila mwezi, au hutumwa kwenye akaunti yako ya benki. Na pia unaweza kuingiza wanachama wapya kwenye kampuni hii, na kila mwanachama anayenunua kutoka kwenye kampuni hii anapata pointi, na kwa upande mwingine wewe unapata pointi kwa sababu mwanachama huyu amesajiliwa kupitia wewe. Bila shaka unaweza kusajili idadi ya watu unaotaka, na kila pointi za watu hawa zinapoongezeka, pointi zako huongezeka, na hivyo kiasi cha pesa unachotumiwa huongezeka, na mchakato huu huendelea kukua hadi unaweza kuwa mshirika katika kampuni hii na kupata faida kubwa sana. (Tafadhali someni vizuri kuhusu kampuni hii na mtoe jibu tosha kuhusu hilo) na asante.

Jibu:

Walaikum Assalam Warahmatullahi Wabarakatuh,

Tayari tuliwahi kupokea swali kama hili kutoka kwa mmoja wa akina dada kuhusu kushughulika na kampuni ya Dxn ya Malaysia na tukalijibu mnamo tarehe 07/11/2024 na lilikuwa na maelezo zaidi kuliko swali lako. Nakunukulia swali hilo la awali na jibu letu kwalo, na huenda likatosheleza haja yako InshaAllah:

[Swali: Shekh wetu mtukufu, Assalamu Alaikum Warahmatullahi Wabarakatuh,

Nafanya kazi katika kampuni ya Malaysia inayoitwa Dxn inayojishughulisha na utengenezaji wa bidhaa za afya na bidhaa za utunzaji wa mwili, ambapo nilifahamiana na rafiki kutoka Jordan na akanisajili katika kampuni na kunipa namba ya uanachama. Niliwauliza watu kadhaa kuhusu kazi ya kampuni hiyo ikiwa ni halali au haramu? Walinijibu ni halali. Lakini baada ya kuhudhuria mafunzo na mihadhara kuhusu mpango wa kifedha, nilipata shaka kuhusu utendaji wake na ikiwa kuna haramu ndani yake?

Kazi katika kampuni inategemea njia mbili za uuzaji:

Njia ya kwanza: Njia ya uuzaji wa moja kwa moja (Direct Selling): Ambapo nanunua bidhaa kwa bei ya jumla kwa kutumia namba yangu ya uanachama kutoka kwenye vituo vya uuzaji vya kampuni na kuziuza kwa faida yangu mwenyewe. Kampuni hunipa idadi fulani ya pointi kwa kila bidhaa ninayonunua, na nikikusanya pointi 100 na zaidi kila mwezi, hunipa bonasi ya pesa (cash bonus) ambapo asilimia yangu mwanzoni inakuwa 6%. Lakini nikikusanya pointi chini ya 100, hainipi pesa, lakini pointi hubaki katika akaunti yangu binafsi kwa ajili ya kuzikusanya ili nifikie cheo cha wakala nyota (Star Agent).

Njia ya pili ya uuzaji (lakini sijafikia huko), nayo ni: Njia ya masoko ya mtandao ya ngazi nyingi (Multi-Level Marketing): Ambapo timu hutengenezwa na udalali huhesabiwa, kwa mfano, kiongozi A anakusanya timu inayoundwa na B, C, na D. Kila mmoja katika timu ya kiongozi A akikusanya pointi 100, kiongozi A hapati faida yake isipokuwa ikiwa yeye mwenyewe amefikisha pointi 100, na kwa upande mwingine, hakuna yeyote katika timu anayepoteza haki yake.

Udalali kwa timu unakuwa kama ifuatavyo: Tofauti kati ya asilimia ya kiongozi na asilimia ya mwanachama wa timu inazidishwa kwa 35% kisha inazidishwa kwa idadi ya pointi alizokusanya mwanachama. Pointi zinazokusanywa na mwanachama na timu hubaki katika akaunti ya mwanachama ya limbikizo hadi anapopata cheo cha wakala nyota.

Naomba radhi kwa kurefusha swali na maelezo.

Mwenyezi Mungu awalinde kwa ajili ya kusimamisha Khilafah ya Rashidah.

Natumai nimefafanua swali vizuri.

Barakallahu fikum na Mwenyezi Mungu atunufaishe sote kwa yale anayoyapenda na kuyaridhia.] Mwisho.

Jibu: [Walaikum Assalam Warahmatullahi Wabarakatuh,

Mwanzoni, Mwenyezi Mungu akubariki kwa dua yako njema kwetu, na sisi tunakuombea kheri.

1- Kuhusu njia ya kwanza ya kushughulika na kampuni, unasema katika swali kuwa unanunua bidhaa kwa bei ya jumla na kuziuza kisha unapata faida, na zaidi ya hapo, ukifanikiwa kuuza kiasi fulani cha bidhaa kulingana na masharti yaliyowekwa na kampuni, unapata faida nyingine kutoka kwa kampuni (bonasi ya pesa)... yaani kampuni inajiwajibisha kukupa (bonasi ya pesa) ikiwa utauza kiwango kinachohitajika cha bidhaa kila mwezi, na uwezekano mkubwa ni kwa ajili ya kuwahamasisha wateja kuongeza mauzo yao.

Ikiwa jambo liko kama tulivyoeleza hapo juu, basi njia hii ya kushughulika inajuzu kisheria kwa sababu kununua bidhaa kwa bei ya jumla na kuziuza kwa kupata faida ni jambo linalojuzu, na ni miongoni mwa biashara zinazojulikana zinazoingia chini ya kauli ya Allah Mtukufu:

وَأَحَلَّ اللَّهُ الْبَيْعَ وَحَرَّمَ الرِّبَا

"Na Allah ameruhusu biashara na akaharamisha riba." (QS. Al-Baqarah [2]: 275)

Kadhalika, kampuni ina haki ya kukuahidi kiasi cha pesa ikiwa utauza kiwango fulani cha bidhaa, na hii inakuwa katika mlango wa hiba (zawadi). Tumetaja katika jibu la swali la tarehe 14/05/2007 kuhusu jambo linalofanana na hili yafuatayo:

[Kumpa yule anayenunua kiasi fulani cha bidhaa nyongeza, zawadi au mfano wake, basi hili linajuzu. Hivyo, uuzaji ni sahihi, na nyongeza hiyo inaingia chini ya hiba na ni sahihi.]

Lakini kujuzu kwa muamala huu na kampuni ni sahihi kwa masharti mawili:

Kwanza: Kununua kwako kwa bei ya jumla kuwe kama bei ya jumla ilivyo sokoni, yaani katika mipaka ya bei ya jumla ya soko na isizidi kiasi ambacho kitasababisha ghabini ya wazi (ghubn fahish) kwa njia ya kumfanyia mnunuzi hadaa kuwa atapata bonasi ya pesa... n.k. Ghabini ya wazi ni haramu, kwani Al-Bukhari amepokea kutoka kwa Abdullah bin Umar (ra) kwamba mtu mmoja alimtajia Mtume ﷺ kuwa anahadaiwa katika biashara, akasema:

إِذَا بَايَعْتَ فَقُلْ لَا خِلَابَةَ

"Unapofanya biashara, sema: Hapana hadaa (khid'ah)."

Na al-khilabah (kwa kasra ya herufi Kha) ni hadaa (udanganyifu). Na hadaa ni haramu.

Pili: Njia hii ya kushughulika iwe huru na njia ya pili iliyotajwa katika swali. Yaani ikiwa utekelezaji wa njia hii ya kwanza umetengana na utekelezaji wa njia ya pili. Lakini ikiwa imefungamanishwa nayo na ni sharti kwa ajili ya njia ya pili, basi hilo litahukumiwa kwa yale tutakayoyataja kuhusu njia ya pili.

2- Kuhusu njia ya pili ya kushughulika na kampuni, yale yaliyokuja katika swali hayako wazi sana, lakini inaonekana hayana tofauti kubwa na masoko ya mtandao (Network Marketing) yanayojulikana, na tumeshalijibu suala la masoko ya mtandao katika majibu mengi yaliyopita, na tukabainisha kutojuzu kwake kisheria.

Miongoni mwa majibu hayo, nakutajia majibu mawili kwa maswali yenye mfanano na swali lako:

• Jibu la swali la tarehe 19/08/2015 kuhusu kampuni ya QuestNet, ambayo ni aina ya masoko ya mtandao, na hivi ndivyo ilivyo:

[Baada ya kuangalia uhalisia wa kampuni ya "QuestNet", na tofauti za mbinu zake za kushughulika, ingawa fikra ni moja, nayo ni kwamba kampuni inashughulika na wauzaji (masoko) wanaowaletea wanunuzi (wateja), na inawapa kamisheni kulingana na masharti fulani, yaani wao ni madalali wa kampuni, wanaleta wanunuzi na kuchukua kamisheni kwa ajili yao... Na yeyote anayezingatia uhalisia wa muamala huu itambainikia yafuatayo:

Kwanza: Aina hii ya makampuni inashughulika na mtandao huu wa masoko katika bidhaa nyingi, na makampuni haya yanashurutisha kwa yule anayefanya masoko ya bidhaa zake kununua kitu katika bidhaa hizo, na baada ya hapo inampa haki ya kuleta wateja kwake, na kumpa kamisheni kwa ajili yao "yaani anakuwa dalali wa kampuni anayeiletea wanunuzi na kuchukua kamisheni kwa ajili yao", na hampei kamisheni hadi alete wanunuzi sita kulingana na swali la Asia ya Kati, na hadi alete wanunuzi wawili kulingana na swali la eneo lingine... yaani kulingana na mpango wa kampuni uliotayarishwa kwa lengo hilo.

Kwa maneno mengine, mnunuzi wa kwanza anachukua kamisheni kwa ajili ya wale wawili (au sita) aliowaleta yeye mwenyewe, akiongezewa kamisheni nyingine kwa ajili ya wale wanne walioletwa na wale wawili wa kwanza, au kwa ajili ya sita walioletwa na wale wawili wa kwanza...

Na kazi za masoko (udalali) huendelea kwa mtindo huu, yaani kwa njia ya mnyororo wa udalali au mtandao wa masoko.

Pili: Aina hii ya kazi za kibiashara inapingana na Sheria (Shara), na ufafanuzi wa hilo ni:

1- Kampuni inashurutisha lazima "muuzaji" anunue bidhaa zake ili awe na haki ya kufanya kazi kwake kama dalali kwa kamisheni, yaani aletee wateja na achukue kamisheni kwa ajili yao, iwe ni kamisheni baada ya kuleta wanunuzi sita au baada ya kuleta wanunuzi wawili.

Hii ina maana kwamba mkataba wa ununuzi na mkataba wa udalali ni mikataba miwili katika mkataba mmoja, au mikubaliano miwili katika makubaliano mamoja, kwa sababu yameshurutishwa pamoja. Na hili ni haramu, kwani:

نَهَى رَسُولُ اللهِ ﷺ عَنْ صَفْقَتَيْنِ فِي صَفْقَةٍ وَاحِدَةٍ

"Mtume wa Allah (saw) amekataza mikataba (mikubaliano) miwili katika mkataba mmoja." (Imepokewa na Ahmad kutoka kwa Abdurrahman bin Abdullah bin Mas'ud kutoka kwa baba yake).

Yaani kama kusema kwangu kwako: Ikiwa utaniuzia, nitakodisha kwako au nitakufanyia udalali, au nitanunua kutoka kwako... n.k. Na ni wazi kuwa uhalisia huu ndio uliopo kulingana na swali, hivyo uuzaji na udalali uko katika mkataba mmoja, yaani lazima kununua kutoka kwa kampuni ni sharti la kufanya kazi ya udalali, yaani kwa ajili ya kufanya masoko kwa kamisheni kwa wanunuzi walioletwa kwenye kampuni.

2- Udalali ni mkataba kati ya muuzaji na yule anayemletea wateja, na kamisheni ya udalali katika mkataba huu inawajibika kwa wale ambao mtu amewaleta kwenye kampuni, na si kwa wale walioletwa na mtu mwingine. Na kwa kuwa kamisheni ya udalali katika muamala wa kampuni iliyotajwa inachukuliwa na dalali (muuzaji) kwa wateja aliowaleta yeye mwenyewe ili wanunue kutoka kwa kampuni, na pia kwa wale walioletwa na wengine, basi hili linapingana na mkataba wa udalali.

3- Bei ya ununuzi kutoka kwa kampuni huambatana na ghabini ya wazi (ghubn fahish), na ingawa mnunuzi anakuwa anajua hilo, lakini jambo hilo haliachi kuwa na hadaa kutokana na mbinu "potofu" zinazotumiwa na kampuni katika kukuza kazi zake kiasi kwamba inampelekea mnunuzi kulipa bei kubwa kwa bidhaa ya kampuni ambayo hailingani na sehemu ndogo ya thamani halisi... na yote hayo ni kwa sababu ya yale yanayopigiwa upatu na kampuni kuhusu mustakabali (mng'aro) kwa mnunuzi huyu kwa sababu atapata fursa ya kufanya masoko ya bidhaa ya kampuni kwa kamisheni kwa (wanunuzi) atakaowaleta kwenye kampuni, na pia kwa wanunuzi watakaoletwa na wale aliowaleta yeye kwanza!

Na wakati mnunuzi anaposhindwa kuleta wanunuzi, hasa wale walioko mwishoni mwa mnyororo wa wanunuzi, hadaa inakuwa imemzunguka, na anapoteza bei kubwa aliyoilipa mkabala wa bidhaa isiyofikia hata sehemu ya kumi ya kile alicholipa! Na hadaa katika Uislamu ni haramu. Mtume wa Allah ﷺ amesema:

الخَدِيعَةُ فِي النَّارِ...

"Hadaa (udanganyifu) imo Motoni..." (Imepokewa na Al-Bukhari kutoka kwa Ibn Abi Awfa).

Na Mtume wa Allah ﷺ alimwambia mtu mmoja aliyekuwa akihadaiwa katika biashara:

إِذَا بَايَعْتَ فَقُلْ لاَ خِلاَبَةَ

"Unapofanya biashara, sema: Hapana hadaa (khid'ah)." (Imepokewa na Al-Bukhari kutoka kwa Abdullah bin Umar ra).

Na al-khilabah ni hadaa. Hili ndilo tamko la hadithi, na ufahamu wake unaashiria kuwa hadaa ni haramu. Na hivyo, muamala huu haujuzu kisheria.

Muhtasari ni kwamba muamala wa kampuni ya QuestNet kwa sura iliyobainishwa katika maswali ni muamala unaopingana na Sheria...] Mwisho.

Hili ndilo ninaloliona kuwa na nguvu katika suala hili, na Mwenyezi Mungu ndiye Mjuzi zaidi na Mwenye Hikima zaidi.

Na yote haya yanamaanisha kuwa njia ya pili iliyotajwa hapo juu haiafikiani na Sheria. 07/11/2024]

Na natumai kuwa katika jibu letu la awali lililotajwa hapo juu kuna kitakachotosheleza haja, na Mwenyezi Mungu ndiye wa kuombwa msaada..]] Mwisho

Ndugu yenu Ata bin Khalil Abu al-Rashta

17 Jumada al-Akhirah 1446 H Sawa na 19/12/2024 M

Link ya jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir (Mungu amuhifadhi) kwenye Facebook:

Share Article

Share this article with your network