Silsila ya Majibu ya Mwanachuoni Mtukufu Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah, Amiri wa Hizbut Tahrir, kwa Maswali ya Wageni wa Ukurasa wake wa Facebook "Fiqhi"
Jibu la Swali
Taklifu ya Jumla na Taklifu Maalum
Kwenda kwa Mohammad Abdul Basir
Swali baada ya kutafsiriwa:
Imekuja katika kitabu cha At-Takattul ukurasa wa 50: (e- Na miongoni mwa matatizo yanayokabili da’wah ni ugumu wa kutoa dhabihu katika mambo ya maisha ya dunia kama mali, biashara na mfano wake kwa ajili ya Uislamu na kubeba da’wah yake. Ili kushinda ugumu huu, muumini hukumbushwa kwamba Mwenyezi Mungu ameinunua kwa waumini nafsi zao na mali zao kwa kuwa wao watapata Pepo. Na inatosha kwa ukumbusho huu na anaachiwa hiyari katika kutoa dhabihu katika mambo haya na halazimishwi kwa lolote. Mtume ﷺ aliandika barua kwa Abdullah bin Jahsh alipomtuma kuongoza kikosi kidogo cha kijeshi ili kuivizia Quraish katika eneo la Nakhla kati ya Makka na Taif, na imekuja katika barua hiyo:
وَلَا تُكْرِهَنَّ أَحَداً مِنْ أَصْحَابِكَ عَلَى الْمَسِيرِ مَعَكَ وَامْضِ لِأَمْرِي فِيمَنْ تَبِعَكَ
"Wala usimlazimishe yeyote katika maswahaba zako kwenda nawe, na tekeleza amri yangu kwa yule atakayekufuata.") Mwisho.
Na swali ni: Kwamba kuna hadithi za Mtume ﷺ zinazoashiria kuwa Muislamu lazima amtii anayemuwajibikia (kiongozi wake), na hili ndilo tunaloliona ndani ya Hizb ambalo ni kuwalazimisha Shabab kutekeleza taklifu zinazohitajika hata kama ni nzito kwa kijana bila ya kuachiwa nafasi wala kutolazimishwa kufanya kazi kama ilivyokuja katika hadithi... Sasa tunaanishaje kati ya yaliyokuja katika At-Takattul kipengele "e" kwamba kijana asilazimishwe kufanya jambo, na kati ya hadithi zinazofaidisha kuwa ni wajibu kwa kijana kumtii msimamizi wake? Na naomba radhi kwa kurefusha swali, na Mwenyezi Mungu akujazi kheri.
Jibu:
Walaikum Salaam Warahmatullahi Wabarakatuh,
1- Inaonekana kuna mkanganyiko uliotokea kwako kuhusiana na taklifu (majukumu). Kuna taklifu za jumla ambazo msimamizi (mas’ul) anaziomba kutoka kwa Shabab wote na ni wajibu kwao kuzitekeleza kwa kumtii msimamizi maadamu zimo katika mamlaka yake na zimefungamana na hukmu za Sharia; kama vile kuhudhuria halaqah ya wiki au ya mwezi, kufanya mawasiliano yanayohitajika, na kutangamana na watu katika mipaka ya taklifu zilizoainishwa katika Faili la Kiidara na maelekezo mengine ya kiidara...
Na kuna taklifu maalum, ambapo kijana mmoja au kundi la Shabab hupewa jukumu la kufanya kazi fulani maalum kama vile kufikisha barua kwa rais wa nchi, au kwenda katika ujumbe kwa mtu miongoni mwa watu wenye nguvu (Ahlul Quwwah), au kwenda kuchunguza habari fulani iliyozungukwa na hatari, au kutoa hotuba mbele ya makao makuu ya mmoja wa madhalimu (taghut) au kumkabidhi barua kutoka kwa Hizb... na mfano wa taklifu kama hizo maalum. Kazi kama hizi hapewi taklifu nazo isipokuwa yule anayezikubali. Akikubali, basi anapewa taklifu ya kazi hiyo na anahusabiwa (anawajibishwa) kwa uzembe wake baada ya kukubali kwake. Lakini asipokubali, hana kosa lolote na halazimishwi kwayo, yaani halazimishwi kuitekeleza.
Imekuja katika Faili la Kiidara chini ya anwani "Waraka wa Jumla/Taklifu Maalum": (Hakika kila anayekubali taklifu maalum anakuwa amelazimika nayo, na haikubaliki kwake kutofanya kile alichokubali kupewa taklifu nacho. Na kutofanya kwake kile alichokubali kukifanya kunachukuliwa kuwa ni nukul (kurudi nyuma/usaliti), na anaadhibiwa kwa hilo).
Kama unavyoona, imetajwa mwanzoni (Hakika kila anayekubali...) yaani asipokubali halazimishwi wala hauchukuliwi hatua.
2- Hii ndiyo mada yenyewe. Na ili picha iwe wazi zaidi, nakunukulia kuhusu kikosi cha Abdullah bin Jahsh ili utambue kuwa haikuwa taklifu ya jumla, yaani kuitisha watu kwa ajili ya vita kama vita vya Tabuk kwa mfano, ambapo Mtume ﷺ aliwaitisha Waislamu kwenda Tabuk kupigana, na ndio maana aliwaadhibu waliobakia nyuma, kwa sababu taklifu hiyo ilikuwa ya jumla, na utiifu kwa msimamizi ni wajibu katika taklifu ya jumla...
Ama kikosi cha Abdullah bin Jahsh, haikuwa wito wa jumla kwa Waislamu katika vita vya jumla, bali ilikuwa ni taklifu maalum kwa idadi ndogo ya watu kwa ajili ya upelelezi wa habari katika mazingira magumu. Ndiyo maana hadithi ya Mtume ﷺ kwa amiri wao Abdullah ilikuwa ni asimlazimishe yeyote:
Imekuja katika Dala’il al-Nubuwwah cha Al-Bayhaqi kutoka kwa Ibn Ishaq, amesema: Alinihadithia Yazid bin Ruman, kutoka kwa Urwah bin Zubair, amesema: Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ alimtuma Abdullah bin Jahsh kwenda Nakhla, akamwambia: "Kuwa hapo mpaka utuletee habari miongoni mwa habari za Quraish" na hakumuamrisha kupigana, na hiyo ilikuwa katika mwezi mtukufu. Na akamuandikia barua kabla ya kumjulisha anakokwenda, akasema: "Toka wewe na maswahaba zako, mpaka utakapopita siku mbili, basi fungua barua yako na utazame yaliyomo, na kile nilichokuamrisha basi kitekeleze, wala usimlazimishe yeyote katika maswahaba zako kwenda nawe." Alipopita siku mbili alifungua barua, akakuta ndani yake: "Kwamba endelea mpaka ushuke Nakhla kati ya Makka na Taif, utuletee habari za Quraish zitakazokufikia kuhusu wao." Akawaambia maswahaba zake alipoisoma barua, akasema: Tumesikia na tumetii. Yeyote kati yenu mwenye shauku ya kufa shahidi basi aende nami, kwani mimi ninatekeleza amri ya Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ, na anayechukia hilo miongoni mwenu basi arudi, kwani Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ amenikataza nisimlazimishe yeyote kati yenu. Basi watu wakaendelea naye...)
Na katika Sirah ya Ibn Hisham: (Abdullah bin Jahsh aliposafiri kwa muda wa siku mbili, alifungua barua na kuitazama, akakuta ndani yake: "Utakapotazama barua yangu hii, basi endelea mpaka ushuke Nakhla, kati ya Makka na Taif, wavizie hapo Quraish na utujulishe habari zao." Abdullah bin Jahsh alipotazama katika barua hiyo alisema: Tumesikia na tumetii. Kisha akawaambia maswahaba zake: Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ ameniumrisha niende Nakhla, niwavizie hapo Quraish mpaka nimletee habari zao, na amenikataza nisimlazimishe yeyote kati yenu. Basi yeyote kati yenu anayetaka kufa shahidi na ana shauku nayo basi na aende, na anayechukia hilo basi arudi. Ama mimi, ninatekeleza amri ya Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ. Basi akaendelea na wakaendelea naye maswahaba zake, hakuachwa nyuma hata mmoja kati yao).
Kama unavyoona, taklifu hiyo ilikuwa ni taklifu maalum, na ndiyo maana hakumlazimisha yeyote katika taklifu hii, ambayo ni taklifu ya kufia dini (shahada). Katika maandishi hayo, kiongozi wao Abdullah aliwaambia (Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ ameniumrisha niende Nakhla, niwavizie hapo Quraish mpaka nimletee habari zao, na amenikataza nisimlazimishe yeyote kati yenu. Basi yeyote kati yenu anayetaka shahada na ana shauku nayo basi na aende, na anayechukia hilo basi arudi. Ama mimi, ninatekeleza amri ya Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ. Basi akaendelea na wakaendelea naye maswahaba zake, hakuachwa nyuma hata mmoja kati yao). Pamoja na hayo, kama unavyoona, hakuachwa nyuma hata mmoja kati yao; yaani ingawa hawakulazimishwa kwa taklifu hii maalum, lakini hakuna aliyebaki nyuma, Mwenyezi Mungu awabarikie.
3- Na sasa turejee katika kipengele "e" kilichotajwa hapo juu katika At-Takattul. Kimekuja katika mlango wa Tafa’ul (kutangamana na umma), na matatizo yanayokabili mwingiliano huu wakati wa Shabab kufanya kazi hii. Kipengele hiki kinahusiana na kutoa dhabihu katika mambo ya maisha ya dunia wakati wa kufanya kazi za mwingiliano (tafa’ul). Na kazi za mwingiliano zinahitaji kufanya kazi maalum zilizozungukwa na hatari ambazo kuzifanya kunakinzana na mambo ya maisha ya dunia kama mali na biashara... nk. Hivyo, yule ambaye hakubali kufanya taklifu maalum zinazohitajika katika hatua ya mwingiliano (Tafa’ul), basi halazimishwi nazo, bali inatosha kwake kufanya kazi za jumla huku akiendelea kukumbushwa kwa msukumo wa uchamungu (taqwa) na kwamba Mwenyezi Mungu ameinunua kwa waumini nafsi zao na mali zao kwa kuwa wao watapata Pepo... na inatosha kwa ukumbusho huu na anaachiwa hiyari katika kutoa dhabihu...
Kama unavyoona, maandishi hayo hapo juu yamejikita katika kutoa dhabihu kutokana na ugumu wa taklifu maalum...
4- Muhtasari ni kwamba kile ambacho kijana halazimishwi nacho ni taklifu maalum, na kile anacholazimika nacho ni taklifu ya jumla na kumtii msimamizi katika hilo maadamu limo katika mamlaka yake na kulingana na hukmu za Sharia.
Natumai picha imekuwa wazi, na Mwenyezi Mungu ndiye Mpaji wa taufiki.
Ndugu yenu, Ata bin Khalil Abu Al-Rashtah
20 Safar al-Khair 1440 H Inayoafikiana na 29/10/2018 M
Kiungo cha jibu kutoka kwa ukurasa wa Amiri (Mwenyezi Mungu amuhifadhi) kwenye: Facebook
Kiungo cha jibu kutoka kwa ukurasa wa Amiri (Mwenyezi Mungu amuhifadhi) kwenye: Google Plus
Kiungo cha jibu kutoka kwa ukurasa wa Amiri (Mwenyezi Mungu amuhifadhi): Web