Mfululizo wa majibu ya Mwanachuoni Mheshimiwa Ata bin Khalil Abu al-Rashtah, Amir wa Hizb ut-Tahrir, kwa maswali ya wafuasi wa ukurasa wake wa Facebook "Feqhi"
Kwa: Musa A. Al-Shakur Musa
Swali:
Assalamu Alaikum wa Rahmatullahi wa Barakatuh.
Namuomba Allah barua yangu ikufikie ukiwa katika neema na fadhila za Allah...
Imeelezwa katika Kifungu cha 142: “Ni haramu kurundika mali (kanz) hata kama zaka yake imetolewa.”
Pia imeelezwa katika maelezo ya kifungu hicho kwenye ukurasa wa 77 wa kitabu cha Muqaddimatul Dustur (Utangulizi wa Katiba) Sehemu ya Pili, katika kufafanua hadith ya Abu Umamah isemayo: “Na hii ina maana ya uharamu wa kurundika dhahabu na fedha kwa namna yoyote ile, hata kama ni dinari mbili au dinari moja, mradi tu inachukuliwa kuwa ni kanz.” Nilichoelewa ni kwamba maskini hawezi kuomba kwa watu zaidi ya hitaji lake.
Swali ni: Ni kiwango gani cha juu ambacho maskini anaweza kuomba kwa watu ili asichukuliwe kuwa ni mrundikaji wa mali (kaniz) katika wakati wetu wa sasa? Na nini hitaji lake? Na ni kiasi gani cha pesa anachoweza kuomba kwa watu na kubaki nacho? Na ni lini anapaswa kuacha kuomba?
Jazakumullahu Khayran.
Jibu:
Walaikum Assalam wa Rahmatullahi wa Barakatuh,
Barakallahu fika kwa dua yako kwetu, nasi tunakuombea kheri.
Kwanza: Swali lako kimsingi ni kuhusu mada ya kuombaomba (at-tassawul), ambayo ni mada tofauti na mada ya kanz (kurundika mali)... Kurundika mali hakuna uhusiano na umaskini au utajiri, wala hakuna uhusiano na kuwa na uhitaji au kutokuwa nao. Bali kumejikita katika kukusanya mali, kuirundika, na kuihifadhi bila ya kuwa na hitaji linalokusudiwa kuitumia mali hiyo, bila kujali kama mrundikaji huyo ni tajiri au maskini. Tajiri, ambaye hana uhitaji, anaweza kurundika mali na kuihifadhi kwa ajili ya jambo lisilo la hitaji analolitumia mali hiyo; na maskini vivyo hivyo anaweza kurundika mali na kuihifadhi bila hitaji, ingawa yeye ana uhitaji, lakini hatumii mali aliyonayo kukidhi uhitaji wake bali anairundika na kuihifadhi licha ya kuwepo kwa uhitaji huo. Hivi ndivyo ilivyokuwa kwa baadhi ya Ahl us-Suffah; walikuwa ni watu wenye uhitaji kwa sababu walikuwa wakiishi kwa sadaka za watu, lakini wakati huo huo baadhi yao walikuwa wakirundika dhahabu (dinari moja, dinari mbili) na kuihifadhi bila hitaji la kuitumia...
Mada ya kanz na uharamu wake imefafanuliwa kwa kina katika kitabu cha Nidham al-Iqtisadi (Mfumo wa Kiuchumi), na unaweza kurejea huko kwani kuna maelezo toshelevu, akipenda Allah.
Pili: Tumeshapata kuulizwa huko nyuma kuhusu kurundika mali (kanz) na kuweka akiba (iddikhar), na jibu langu kwa muulizaji mnamo tarehe 13/01/2014 lilikuwa kama ifuatavyo:
(1- Kurundika mali (kanz) ni kuikusanya bila ya kuwa na hitaji. Ikiwa kuna hitaji la kisheria, kama vile unakusanya pesa ili ujenge nyumba, ununue ardhi, ujenge kiwanda, unataka kuoa, au una watoto hivyo unawakusanyia ada zao za shule, au ununue gari, au mfano wa hayo, basi huku ni kukusanya kwa ajili ya hitaji na si kurundika (kanz). Bali, "huo ni uwekaji akiba kwa ajili ya hitaji" (iddikhar li hajah) na ni ukusanyaji halali unaotolewa zaka ikiwa utafikia kiwango (nisab) na kutimiza mwaka...
2- Hakika kukusanya matumizi (nafaqah) kwa ajili yake na wale anaowatunza yanayomtosha kwa mwaka mmoja ni jambo linalojuzu na si kurundika mali, kwa sababu Mtume ﷺ alikuwa akiwapa mama wa waumini (wakeze) nafaqah ya mwaka mmoja. Muslim amepokea kutoka kwa Umar, amesema:
كَانَتْ أَمْوَالُ بَنِي النَّضِيرِ مِمَّا أَفَاءَ اللهُ عَلَى رَسُولِهِ، مِمَّا لَمْ يُوجِفْ عَلَيْهِ الْمُسْلِمُونَ بِخَيْلٍ وَلَا رِكَابٍ، فَكَانَتْ لِلنَّبِيِّ ﷺ خَاصَّةً، فَكَانَ يُنْفِقُ عَلَى أَهْلِهِ نَفَقَةَ سَنَةٍ، وَمَا بَقِيَ يَجْعَلُهُ فِي الْكُرَاعِ وَالسِّلَاحِ، عُدَّةً فِي سَبِيلِ اللهِ
“Mali za Bani Nadheer zilikuwa miongoni mwa ambavyo Allah alimpa Mtume Wake kama faya (mali ya adui aliyoipata bila vita), ambayo Waislamu hawakuiendeshea farasi wala ngamia. Hivyo zilikuwa ni kwa ajili ya Mtume ﷺ pekee. Alikuwa akiwatolea watu wa nyumbani kwake matumizi ya mwaka mmoja, na kilichobaki alikuwa akikifanya kuwa ni kwa ajili ya farasi na silaha, kama maandalizi katika njia ya Allah.”
An-Nawawi anasema katika sharh yake ya Sahih Muslim: (Na kauli yake: "aliwatolea watu wa nyumbani kwake matumizi ya mwaka mmoja" ina maana alikuwa akiwatengea matumizi ya mwaka mmoja, lakini alikuwa akiyatoa kabla ya kuisha kwa mwaka katika nyanja za kheri, hivyo mwaka ulikuwa hauishi huku mali ikiwa imebaki...). Kwa hivyo, kukusanya mali kwa ajili ya matumizi kwa muda wa mwaka mmoja si kurundika (kanz), na hutolewa zaka katika nisab yake ikiwa imetimiza mwaka...) Mwisho wa nukuu kutoka jibu la swali lililopita.
Tatu: Ama kuhusu kuombaomba (at-tassawul), kumekuja dalili za kisheria za kina zinazobainisha hukumu ya kuombaomba na mipaka yake ya kisheria:
1- Sharia imekataza watu kuomba mali za watu wengine bila ya kuwa na hitaji, na imemuamrisha mwenye uwezo kufanya kazi ili kupata mali:
- Allah Subhanahu wa Ta'ala amesema katika kuwasifu mafukara wanaojizuia na kuomba:
لِلْفُقَرَاءِ الَّذِينَ أُحْصِرُوا فِي سَبِيلِ اللَّهِ لَا يَسْتَطِيعُونَ ضَرْباً فِي الْأَرْضِ يَحْسَبُهُمُ الْجَاهِلُ أَغْنِيَاءَ مِنَ التَّعَفُّفِ تَعْرِفُهُمْ بِسِيمَاهُمْ لَا يَسْأَلُونَ النَّاسَ إِلْحَافاً وَمَا تُنْفِقُوا مِنْ خَيْرٍ فَإِنَّ اللَّهَ بِهِ عَلِيمٌ
"Wapewe mafukara ambao wamejitolea katika njia ya Mwenyezi Mungu, wasioweza kusafiri katika ardhi (kwa ajili ya biashara au kazi); asiyewajua hali zao huwadhania kuwa ni matajiri kwa sababu ya kujiheshimu kwao (hawaombi). Utawatambua kwa alama zao; hawaombi watu kwa kuwachosha. Na heri yoyote mnayotoa, basi kwa yakini Mwenyezi Mungu anaijua." (QS. Al-Baqarah [2]: 273) Aya hii inadokeza katazo la kuwaomba watu.
- Na Muslim amepokea katika Sahih yake katika mlango huo huo kutoka kwa Abu Hurairah amesema: Mtume wa Allah ﷺ amesema:
مَنْ سَأَلَ النَّاسَ أَمْوَالَهُمْ تَكَثُّراً فَإِنَّمَا يَسْأَلُ جَمْراً فَلْيَسْتَقِلَّ أوْ لِيَسْتَكْثِرْ
“Mwenye kuwaomba watu mali zao kwa ajili ya kutaka kujitajirisha, basi hakika anaomba kaa la moto; basi apunguze au akithirishe.” Imeelezwa katika Sharh ya An-Nawawi kwa Muslim yafuatayo: [Kauli yake ﷺ "Mwenye kuwaomba watu mali zao kwa ajili ya kutaka kujitajirisha, basi hakika anaomba kaa la moto; basi apunguze au akithirishe", Al-Qadhi amesema maana yake ni kwamba ataadhibiwa kwa Moto, na inawezekana ikawa katika maana yake ya dhahiri, kwamba kile anachokichukua kitakuwa ni kaa la moto atakaloingizwa nalo kama ilivyothibiti kwa mnyimaji wa zaka].
- Pia imekuja katika Sahih Muslim katika mlango huo huo kutoka kwa Abu Hurairah amesema: Nilimsikia Mtume wa Allah ﷺ akisema:
لَأَنْ يَغْدُوَ أَحَدُكُمْ فَيَحْطِبَ عَلَى ظَهْرِهِ فَيَتَصَدَّقَ بِهِ وَيَسْتَغْنِيَ بِهِ مِنَ النَّاسِ خَيْرٌ لَهُ مِنْ أَنْ يَسْأَلَ رَجُلاً أَعْطَاهُ أَوْ مَنَعَهُ ذَلِكَ فَإِنَّ الْيَدَ الْعُلْيَا أَفْضَلُ مِنَ الْيَدِ السُّفْلَى وَابْدَأْ بِمَنْ تَعُولُ
“Ni bora mmoja wenu aende asubuhi na akusanye kuni mgongoni mwake na kisha akazitoa sadaka na akajitosheleza nazo kutokana na watu, kuliko kumuomba mtu ampe au amnyime. Hakika mkono wa juu ni bora kuliko mkono wa chini, na anza na wale unaowatunza.”
2- Sharia imeruhusu kuwaomba watu mali zao katika hali maalum zilizobainishwa na Mtume ﷺ. Katika hadith aliyoipokea Muslim katika Sahih yake kutoka kwa Qabisah bin Mukhariq al-Hilali amesema: Nilibeba dhamana ya deni la kusuluhisha watu (hamalah), kisha nikamwendea Mtume wa Allah ﷺ kumuomba msaada katika hilo, akasema: "Subiri mpaka itujie sadaka, tutakuamrisha upewe." Anasema: Kisha akasema:
يَا قَبِيصَةُ إِنَّ الْمَسْأَلَةَ لَا تَحِلُّ إِلَّا لِأَحَدِ ثَلَاثَةٍ؛ رَجُلٍ تَحَمَّلَ حَمَالَةً فَحَلَّتْ لَهُ الْمَسْأَلَةُ حَتَّى يُصِيبَهَا ثُمَّ يُمْسِكُ، وَرَجُلٌ أَصَابَتْهُ جَائِحَةٌ اجْتَاحَتْ مَالَهُ فَحَلَّتْ لَهُ الْمَسْأَلَةُ حَتَّى يُصِيبَ قِوَاماً مِنْ عَيْشٍ أَوْ قَالَ سِدَاداً مِنْ عَيْشٍ، وَرَجُلٌ أَصَابَتْهُ فَاقَةٌ حَتَّى يَقُومَ ثَلَاثَةٌ مِنْ ذَوِي الْحِجَا مِنْ قَوْمِهِ لَقَدْ أَصَابَتْ فُلَاناً فَاقَةٌ فَحَلَّتْ لَهُ الْمَسْأَلَةُ حَتَّى يُصِيبَ قِوَاماً مِنْ عَيْشٍ أَوْ قَالَ سِدَاداً مِنْ عَيْشٍ، فَمَا سِوَاهُنَّ مِنَ الْمَسْأَلَةِ يَا قَبِيصَةُ سُحْتاً يَأْكُلُهَا صَاحِبُهَا سُحْتاً
“Ewe Qabisah, hakika kuombaomba hakuruhusiwi isipokuwa kwa mmoja kati ya watatu: mtu aliyebeba dhamana ya deni (hamalah), basi inaruhusiwa kwake kuomba mpaka alipate (deni hilo) kisha anaacha. Na mtu aliyekumbwa na janga (jaihah) lililomaliza mali yake, basi inaruhusiwa kwake kuomba mpaka apate mahitaji ya kimsingi ya maisha. Na mtu aliyekumbwa na umaskini uliokithiri (faqa) mpaka wasimame watu watatu wenye akili katika watu wake na kusema 'hakika fulani amekumbwa na umaskini', basi inaruhusiwa kwake kuomba mpaka apate mahitaji ya kimsingi ya maisha. Basi kuomba kwingine kando na hawa, ewe Qabisah, ni haramu (suht) na mwenye kuila anaishi kwa haramu.” Ni wazi kutokana na hadith hii kwamba makundi yanayoruhusiwa kuomba ni: Mtu aliyebeba deni katika kusuluhisha baina ya watu, mtu aliyekumbwa na janga, na fukara mwenye umaskini uliokithiri...
3- Wanaunganishwa na makundi haya watatu walio katika hukumu yao, kama vile mwenye deni binafsi ambaye hana mali ya kulipa deni lake kwa sababu anaingia chini ya neno "wenye madeni" (gharimin) katika kauli ya Allah:
إِنَّمَا الصَّدَقَاتُ لِلْفُقَرَاءِ وَالْمَسَاكِينِ وَالْعَامِلِينَ عَلَيْهَا وَالْمُؤَلَّفَةِ قُلُوبُهُمْ وَفِي الرِّقَابِ وَالْغَارِمِينَ وَفِي سَبِيلِ اللَّهِ وَابْنِ السَّبِيلِ فَرِيضَةً مِنَ اللَّهِ وَاللَّهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ
"Hakika sadaka (zaka) hupewa mafukara, na maskini, na wanaozitumikia, na waunganishwa nyoyo zao, na katika kukomboa watumwa, na wenye madeni, na katika njia ya Mwenyezi Mungu, na wasafiri; ni faradhi itokayo kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi, Mwenye hikima." (QS. At-Tawbah [9]: 60)
Vilevile mtu mwenye nguvu lakini asiyepata kipato, yaani asiyepata kazi ya kufanya ili kupata riziki yake na hana mali wala jamaa wa kumlisha, kwa kauli yake ﷺ katika hadith aliyoipokea An-Nasa'i na wengineo kutoka kwa Hisham bin Urwah, amesema: Aliniambia baba yangu, amesema: Aliniambia Ubaidullah bin Adiy bin al-Khiyar kwamba watu wawili walimwambia kuwa walimwendea Mtume wa Allah ﷺ wakimuomba sadaka, akawaangalia kwa makini na kuwaona ni wenye nguvu, kisha Mtume wa Allah ﷺ akasema:
إِنْ شِئْتُمَا وَلَا حَظَّ فِيهَا لِغَنِيٍّ وَلَا لِقَوِيٍّ مُكْتَسِبٍ
“Mkitaka (nitawapa), lakini hakuna fungu katika hii (sadaka) kwa tajiri wala kwa mwenye nguvu anayeweza kupata kipato.” (Al-Albani amesema: Ni sahihi).
Pia yule anayebeba jukumu la kulipa fidia ya damu (diyah) kwa niaba ya jamaa yake au rafiki yake mwuaji ili ailie kwa walii wa aliyeuawa, na ikiwa hatoilipa jamaa yake huyo atauawa, kutokana na hadith aliyoipokea Ahmad katika Musnad yake kutoka kwa Anas bin Malik, kutoka kwa Mtume ﷺ amesema:
إِنَّ الْمَسْأَلَةَ لَا تَحِلُّ إِلَّا لِأَحَدِ ثَلَاثٍ ذِي دَمٍ مُوجِعٍ أَوْ غُرْمٍ مُفْظِعٍ أَوْ فَقْرٍ مُدْقِعٍ
“Hakika kuombaomba hakuruhusiwi isipokuwa kwa mmoja wa watatu: mwenye damu inayoumiza (fidia ya damu), au deni linaloangamiza, au umaskini uliokithiri.”
Makundi haya yanaruhusiwa kuomba mpaka yakidhi hitaji waliloombea, na hairuhusiwi kwa makundi haya kuomba baada ya hapo kulingana na maelezo yaliyotajwa hapo juu... Na haijuzu kwa wengineo kando na makundi haya yaliyotajwa katika hadith ya Qabisah na walio katika hukumu yao, haijuzu kwao kuwaomba watu mali zao...
4- Tumetaja kiwango cha utajiri ambacho kuomba hakuruhusiwi nacho, na hicho kimo katika kitabu cha Al-Amwal fi Dawlat al-Khilafah (Mali katika Dola ya Khilafah), mlango wa "Matumizi ya Zaka" kama ifuatavyo:
[...Na Allah ameharamisha kwa matajiri kuchukua sadaka. Ahmad na wamiliki wa Sunan wamepokea kutoka kwa Abdullah bin Amr, amesema: Mtume wa Allah ﷺ amesema:
لَا تَحِلُّ الصَّدَقَةُ لِغَنِيٍّ، وَلَا لِذِي مِرَّةٍ سَوِيٍّ
“Sadaka hairuhusiwi kwa tajiri, wala kwa mwenye nguvu timamu.”
Na dhu mirrah ni mwenye nguvu, na uwezo, anayeweza kupata kipato; ikiwa hatopata cha kupata kipato chake huchukuliwa kuwa ni fukara. Na tajiri ni yule anayejitosheleza bila ya wengine, na akawa na ziada ya kile kinachotosheleza mahitaji yake. Zimekuja hadith zilizobainisha tajiri ni nani. Kutoka kwa Abdullah bin Mas'ud amesema: Mtume wa Allah ﷺ amesema:
مَا مِنْ أَحَدٍ يَسْأَلُ مَسْأَلَةً، وَهُوَ عَنْهَا غَنِيٌّ، إِلاَّ جَاءَتْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ كُدُوحاً، أَوْ خُدُوشاً، أَوْ خُمُوشاً فِي وَجْهِهِ. قِيلَ: يَا رَسُولَ اللهِ، وَمَا غِنَاهُ، أَوْ مَا يُغْنِيهِ؟ قَالَ: خَمْسُونَ دِرْهَماً، أَوْ حِسَابُهَا مِنَ الذَّهَبِ
“Hakuna yeyote anayeomba ombi (la mali) hali ya kuwa anajitosheleza (tajiri), isipokuwa litakuja Siku ya Kiyama likiwa ni kovu, au mchubuko, au mkwaruzo katika uso wake. Ikasemwa: Ewe Mtume wa Allah, ni upi utajiri wake (unaomfanya asiruhusiwe kuomba)? Akasema: Dirham hamsini, au thamani yake ya dhahabu.” (Imepokewa na watano).
Hivyo yule anayemiliki dirham hamsini za fedha, yaani gramu 148.75 za fedha, au thamani yake ya dhahabu, ikiwa ni ziada ya chakula chake, mavazi yake, makazi yake, na matumizi ya familia yake, mtoto wake, na mtumishi wake, anachukuliwa kuwa tajiri, na hairuhusiwi kwake kuchukua sadaka.] Mwisho wa nukuu. Na kwa mujibu wa hayo, haijuzu kwa tajiri kama huyo kuwaomba watu.
Nne: Tatizo la kuombaomba na utatuzi wake:
Kinachostahili kuzingatiwa ni kwamba kuenea kwa jambo la kuombaomba katika nchi za Kiislamu kunatokana na kuondolewa kwa Sharia ya Kiislamu katika utabikishaji na uzembe mkubwa unaofanywa na watawala katika kusimamia mambo ya watu... Ni jambo la kusikitisha na kuliza kuona makundi ya waombaji katika nchi za Waislamu mbele ya misikiti, barabarani na katika njia panda... wakati nchi za Waislamu ndizo ghala la mali na utajiri... Lawama haziwaangukii waombaji kwanza, bali zinawaangukia watawala wasiotabikisha Sharia, na zaidi ya hapo hawasimamii mambo ya watu wala hawakidhi mahitaji yao wala hawawapi kima cha maisha... Hakika dola ya Khilafah Rashidah inayokuja hivi karibuni kwa idhini ya Allah, itakuwa miongoni mwa vipaumbele vyake kutibu jambo la umaskini katika nchi za Kiislamu na mambo mabaya yanayotokana nao kama vile kuombaomba... Na tumebainisha katika vitabu vyetu jinsi Uislamu ulivyotibu tatizo la umaskini, hususan yale yaliyokuja katika kitabu cha Nidham al-Iqtisadi kwani yamefafanuliwa humo na inawezekana kurejelewa...).
Ndugu yenu Ata bin Khalil Abu al-Rashtah
19 Jumada al-Akhirah 1443 H Muwafaka 22/01/2022 M
Link ya jibu kutoka kwa ukurasa wa Amir (Allah amhifadhi) kwenye Facebook