Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

JAWABU LA SWALI: CHANJO DHIDI YA UGONJWA WA KORONA

January 22, 2021
5704

Mfululizo wa Majibu ya Mwanachuoni Mtukufu Ata Bin Khalil Abu al-Rashtah, Amir wa Hizb ut-Tahrir, kwa Maswali ya Wageni wa Ukurasa wake wa Facebook "Fiqhi"

Kwa Um Bilal

Swali:

Assalamu Alaikum Wa Rahmatullahi Wa Barakatuh...

Mwenyezi Mungu akubariki Amir wetu, akunusuru na akusaidie kwa ushindi ulio wazi na Khilafah kwa njia ya Utume itakayoponya vifua vya waumini...

Swali langu ni kuhusu chanjo mpya ambayo mataifa yameanza kuwapa watu dhidi ya ugonjwa wa Korona... Tunaona kuna hofu kubwa miongoni mwa watu kuhusu kuchukua chanjo hii kutokana na kuenea kwa maneno mengi kupitia mitandao ya kijamii kuhusu hatari ya chanjo hii, na kwamba ni njama ya kimataifa ya kibeberu dhidi ya watu... Tunajua kwamba shifa iko mikononi mwa Mwenyezi Mungu pekee, na kwamba kila ajali ina muda wake ulioandikwa. Sisi kama wabebaji da'wah tunauliza kuhusu ukweli wa chanjo hii, na je, ni wajibu kisheria kuichukua huku kukiwa na kuenea kwa janga hili?

Mwenyezi Mungu akubariki.

Jawabu:

Wa Alaikum Salaam Wa Rahmatullahi Wa Barakatuh.

Kama unavyojua, tulishatoa majibu ya maswali huko nyuma kuhusu matibabu, na tukasema ndani yake:

  • Ikiwa dawa ina madhara, basi ni haramu kwa mujibu wa Hadith:

لَا ضَرَرَ وَلَا ضِرَارَ

"Haifai kudhuriana wala kulipiza dhara." (Imepokewa na Ahmad na Ibn Majah)

  • Ama ikiwa dawa haina madhara lakini ina vitu vilivyoharamishwa au najisi, hukumu yake ni makruhu, yaani si haramu; bali inaruhusiwa kuitumia pamoja na kuwa ni makruhu ikiwa mgonjwa hapati dawa ya halali...

  • Ama ikiwa dawa haina madhara na haina vitu vilivyoharamishwa au najisi, basi ni mandub (inapendekezwa)...

Nitakunukulia sehemu muhimu kutoka katika majibu hayo:

[... Kwanza: Jawabu la swali la tarehe 26/01/2011 kuhusu kunufaika na vitu haramu na najisi na kujitibu navyo, ambalo lilisema:

(...3- Matibabu yamevuliwa katika uharamu, hivyo kujitibu kwa kitu haramu au najisi si haramu:

  • Ama kuhusu kujitibu kwa kitu haramu si haramu, ni kwa mujibu wa Hadith ya Muslim kutoka kwa Anas:

رَخَّصَ رَسُولُ اللَّهِ ﷺ أَوْ رُخِّصَ لِلزُّبَيْرِ بْنِ الْعَوَّامِ وَعَبْدِ الرَّحْمَنِ بْنِ عَوْفٍ فِي لُبْسِ الْحَرِيرِ لِحِكَّةٍ كَانَتْ بِهِمَا

"Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) alimpa ruhusa, au ilitolewa ruhusa kwa Zubair bin al-Awwam na Abdurrahman bin Auf kuvaa hariri kutokana na ugonjwa wa mwasho uliokuwa ukiwasumbua." (Imepokewa na Muslim). Na kuvaa hariri kwa wanaume ni haramu, lakini iliruhusiwa kwa ajili ya matibabu...

  • Na ama kuhusu kujitibu kwa najisi si haramu, ni kwa mujibu wa Hadith ya Bukhari kutoka kwa Anas (ra):

أَنَّ نَاساً اجْتَوَوْا فِي الْمَدِينَةِ فَأَمَرَهُمْ النَّبِيُّ ﷺ أَنْ يَلْحَقُوا بِرَاعِيهِ يَعْنِي الْإِبِلَ فَيَشْرَبُوا مِنْ أَلْبَانِهَا وَأَبْوَالِهَا فَلَحِقُوا بِرَاعِيهِ فَشَرِبُوا مِنْ أَلْبَانِهَا وَأَبْوَالِهَا...

"Kwamba baadhi ya watu walipatwa na ugonjwa (ajtawu) mjini Madina, hivyo Mtume (saw) akawaamuru waungane na mchungi wake – yaani wa ngamia – wakanywe maziwa yao na mkojo wao, wakajiunga na mchungi huyo na wakanywa maziwa yao na mkojo wao..." (Imepokewa na Bukhari). Na maana ya ajtawu ni kwamba chakula hakikuwafaa, hivyo wakaugua, na Mtume (saw) akawaruhusu "mkojo" kwa ajili ya matibabu nao ni najisi...] Mwisho.

Pili: Ilikuja katika jawabu la swali la tarehe 19/09/2013:

[... Na jawabu ni kwamba kutumia pombe katika dawa, pamoja na dawa ambayo ndani yake ina kileo... hukumu yake ni kuruhusiwa pamoja na makruhu, na dalili ya hilo ni:

Ibn Majah amepokea kupitia njia ya Tariq bin Suwayd al-Hadrami amesema:

قُلْتُ يَا رَسُولَ اللَّهِ إِنَّ بِأَرْضِنَا أَعْنَاباً نَعْتَصِرُهَا فَنَشْرَبُ مِنْهَا قَالَ لَا فَرَاجَعْتُهُ قُلْتُ إِنَّا نَسْتَشْفِي بِهِ لِلْمَرِيضِ قَالَ إِنَّ ذَلِكَ لَيْسَ بِشِفَاءٍ وَلَكِنَّهُ دَاءٌ

"Nilisema, Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, katika ardhi yetu kuna zabibu tunazozikamua kisha tunazinywa. Akasema: Hapana. Nikamrejea tena nikasema: Hakika tunajishifa kwayo kwa ajili ya mgonjwa. Akasema: Hakika hiyo si shifa, bali ni ugonjwa." (Imepokewa na Ibn Majah). Huku ni kukataza kutumia najisi au haramu "pombe" kama dawa. Lakini Mtume (saw) aliruhusu kujitibu kwa najisi "mkojo wa ngamia". Bukhari ametoa kupitia njia ya Anas (ra):

أَنَّ نَاساً مِنْ عُرَيْنَةَ اجْتَوَوْا الْمَدِينَةَ فَرَخَّصَ لَهُمْ رَسُولُ اللَّهِ ﷺ أَنْ يَأْتُوا إِبِلَ الصَّدَقَةِ فَيَشْرَبُوا مِنْ أَلْبَانِهَا وَأَبْوَالِهَا...

"Kwamba watu kutoka kabila la 'Uraynah walipatwa na ugonjwa Madina, hivyo Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) akawapa ruhusa waende kwa ngamia wa sadaka na wakanywe maziwa yao na mkojo wao..." (Imepokewa na Bukhari). Ajtawu al-Madina: ina maana kwamba hali ya hewa haikuwafaa wakaugua, hivyo Mtume (saw) akawaruhusu wajitibu kwa mkojo wa ngamia nao ni najisi. Vivyo hivyo, Mtume (saw) aliruhusu kujitibu kwa haramu "kuvaa hariri". At-Tirmidhi na Ahmad wametoa, na tamshi ni la At-Tirmidhi kupitia njia ya Anas:

أَنَّ عَبْدَ الرَّحْمَنِ بْنَ عَوْفٍ وَالزُّبَيْرَ بْنَ الْعَوَّامِ شَكَيَا الْقَمْلَ إِلَى النَّبِيُّ ﷺ فِي غَزَاةٍ لَهُمَا، فَرَخَّصَ لَهُمَا فِي قُمُصِ الْحَرِيرِ. قَالَ: وَرَأَيْتُهُ عَلَيْهِمَا

"Kwamba Abdurrahman bin Auf na az-Zubair bin al-Awwam walimlalamikia Mtume (saw) kuhusu chawa katika vita vyao, basi akawaruhusu kuvaa kanzu za hariri. Akasema: Nikaziona zikiwa kwao." (Imepokewa na At-Tirmidhi). Hadith hizi mbili ni kielelezo kwamba makatazo katika Hadith ya Ibn Majah si ya mkazo, yaani kujitibu kwa najisi na haramu ni makruhu.)

Tatu: Jawabu la swali la tarehe 18/11/2013 kuhusu chanjo na hukumu yake, ambalo lilisema:

[Chanjo ni dawa, na matibabu ni mandub na si faradhi, na dalili ya hilo ni:

1- Bukhari amepokea kupitia njia ya Abu Hurairah amesema: Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema:

مَا أَنْزَلَ اللَّهُ دَاءً إِلَّا أَنْزَلَ لَهُ شِفَاءً

"Mwenyezi Mungu hakuteremsha ugonjwa isipokuwa ameteremsha na shifa yake." (Imepokewa na Al-Bukhari).

Na Muslim amepokea kutoka kwa Jabir bin Abdullah, kutoka kwa Mtume (saw) amesema:

لِكُلِّ دَاءٍ دَوَاءٌ، فَإِذَا أُصِيبَ دَوَاءُ الدَّاءِ بَرَأَ بِإِذْنِ اللهِ عَزَّ وَجَلَّ

"Kila ugonjwa una dawa, na dawa ya ugonjwa ikipatikana, basi mtu hupona kwa idhini ya Mwenyezi Mungu (Az'za wa Jalla)." (Imepokewa na Muslim). Na Ahmad amepokea katika Musnad yake kutoka kwa Abdullah bin Mas'ud:

مَا أَنْزَلَ اللَّهُ دَاءً، إِلَّا قَدْ أَنْزَلَ لَهُ شِفَاءً، عَلِمَهُ مَنْ عَلِمَهُ، وَجَهِلَهُ مَنْ جَهِلَهُ

"Mwenyezi Mungu hakuteremsha ugonjwa isipokuwa ameteremsha na shifa yake, anayeijua anaijua na asiyeijua haijui." (Imepokewa na Ahmad).

Na Hadith hizi zina mwongozo kwamba kila ugonjwa una dawa inayouponya, ili iwe ni kichocheo cha kutafuta matibabu yanayopelekea kupona ugonjwa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu (swt), na huu ni mwongozo na si uwajibu.

2- Ahmad amepokea kutoka kwa Anas amesema: Hakika Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema:

إِنَّ اللَّهَ حَيْثُ خَلَقَ الدَّاءَ، خَلَقَ الدَّوَاءَ، فَتَدَاوَوْا

"Hakika Mwenyezi Mungu alipoumba ugonjwa, aliumba na dawa, basi jitibuni." (Imepokewa na Ahmad). Na Abu Dawood amepokea kutoka kwa Usamah bin Sharik amesema: Nilimjia Mtume (saw) na maswahaba zake kama kwamba kuna ndege vichwani mwao, nikasalamia kisha nikakaa, wakaja mabedui kutoka huku na huku wakasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, je tujiuguze (tujitibu)? Akasema:

تَدَاوَوْا فَإِنَّ اللَّهَ عَزَّ وَجَلَّ لمْ يَضَعْ دَاءً إِلَّا وَضَعَ لَهُ دَوَاءً، غَيْرَ دَاءٍ وَاحِدٍ الْهَرَمُ

"Jitibuni, kwani Mwenyezi Mungu (Az'za wa Jalla) hakuweka ugonjwa isipokuwa ameuwekea dawa, isipokuwa ugonjwa mmoja: uzee." Yaani "isipokuwa kifo". (Imepokewa na Abu Dawood).

Katika Hadith ya kwanza kuna amri ya kujitibu, na katika Hadith hii kuna jawabu kwa mabedui kuhusu kujitibu, na kusemeshwa kwa waja ili wajitibu, kwani Mwenyezi Mungu hakuweka ugonjwa isipokuwa ameweka shifa yake. Na kusemeshwa huko katika Hadith zote mbili kumekuja kwa muundo wa amri, na amri hutoa maana ya ombi la jumla, na haitoi maana ya uwajibu isipokuwa ikiwa ni amri ya mkazo, na mkazo unahitaji kielelezo kinachofahamisha hilo, na hakuna katika Hadith hizi mbili kielelezo choote kinachofahamisha uwajibu. Isitoshe, zimekuja Hadith zinazofahamisha kuruhusiwa kuacha matibabu, jambo ambalo linaondoa maana ya uwajibu katika Hadith hizi mbili. Muslim amepokea kutoka kwa Imran bin Husain kwamba Mtume (saw) amesema:

يَدْخُلُ الْجَنَّةَ مِنْ أُمَّتِي سَبْعُونَ أَلْفاً بِغَيْرِ حِسَابٍ

"Wataingia Peponi miongoni mwa umma wangu watu elfu sabini bila hesabu." Wakasema: Ni nani hao ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu? Akasema:

هُمُ الَّذِينَ لَا يَكْتَوُونَ وَلَا يَسْتَرْقُونَ، وَعَلَى رَبِّهِمْ يَتَوَكَّلُونَ

"Ni wale ambao hawajitibi kwa kuchomwa na moto wala hawaombi kuchanjwa chale za kishari, na wanamtegemea Mola wao." (Imepokewa na Muslim). Na chale na kuchomwa moto ni miongoni mwa matibabu. Na Bukhari amepokea kutoka kwa Ibn Abbas amesema: ...Huyu mwanamke mweusi alimjia Mtume (saw) akasema: Mimi nina kifafa na mimi hufunuka, basi niombee kwa Mwenyezi Mungu. Akasema:

إِنْ شِئْتِ صَبَرْتِ وَلَكِ الجَنَّةُ، وَإِنْ شِئْتِ دَعَوْتُ اللَّهَ أَنْ يُعَافِيَكِ

"Ukitaka subiri na utapata Pepo, na ukitaka nitakuombea kwa Mwenyezi Mungu akupe afya." Akasema: Nitavumilia, akasema: Hakika mimi hufunuka, basi niombee kwa Mwenyezi Mungu nisifunuke.

فَدَعَا لَهَا...

"Basi akamuombea..." (Imepokewa na Al-Bukhari). Hadith hizi mbili zinaonyesha kuruhusiwa kuacha kujitibu.

Yote haya yanaonyesha kwamba amri iliyokuja "basi jitibuni", "jitibuni" si ya uwajibu, na kwa hivyo amri hapa ni ima kwa ajili ya uhalali au kupendekezwa, na kutokana na ukali wa kuhimiza kwa Mtume (saw) juu ya matibabu, basi amri ya kujitibu iliyokuja katika Hadith ni ya kupendekezwa (mandub).

Kwa hivyo, chanjo hukumu yake ni mandub, kwa sababu chanjo ni dawa, na matibabu ni mandub. Isipokuwa ikithibiti kwamba aina fulani ya chanjo ina madhara kama vile vifaa vyake kuwa vimeharibika au vina madhara kwa sababu fulani... basi kuchanja katika hali hii kwa kutumia vitu hivi inakuwa ni haramu kwa mujibu wa kanuni ya madhara kutokana na Hadith ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) ambayo Ahmad ametoa katika Musnad yake kutoka kwa Ibn Abbas, amesema: Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema:

لَا ضَرَرَ وَلَا ضِرَارَ

"Haifai kudhuriana wala kulipiza dhara." (Imepokewa na Ahmad). Isipokuwa hizi ni hali chache...

Ama katika dola ya Khilafah, kutakuwa na chanjo dhidi ya magonjwa yanayohitaji hilo kama vile magonjwa ya kuambukiza na mengineyo, na dawa itakuwa safi kutokana na kila aina ya kasoro, na Mwenyezi Mungu (swt) ndiye mponyaji:

وَإِذَا مَرِضْتُ فَهُوَ يَشْفِينِ

"Na nitakapougua, basi Yeye ndiye anayenishifa." (Ash-Shu'ara [26]: 80). Inajulikana kisheria kwamba huduma za afya ni miongoni mwa majukumu ya Khalifah kutokana na mlango wa kusimamia mambo ya raia akifanyia kazi kauli ya Mtume (saw):

الإِمَامُ رَاعٍ وَهُوَ وَمَسْؤُولٌ عَنْ رَعِيَّتِهِ

"Imamu ni mchungaji na anawajibika kwa raia wake." (Imepokewa na Al-Bukhari kutoka kwa Abdullah bin Umar). Na hili ni andiko la jumla juu ya jukumu la dola kuhusu afya na matibabu kwa sababu vinaingia katika usimamizi (ri'ayah) wa lazima kwa dola.

Kuna dalili maalum juu ya afya na matibabu:

Muslim ametoa kupitia njia ya Jabir amesema:

بَعَثَ رَسُولُ اللَّهِ ﷺ إِلَى أُبَيِّ بْنِ كَعْبٍ طَبِيباً فَقَطَعَ مِنْهُ عِرْقاً ثُمَّ كَواه عَلَيْهِ

"Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) alimtumia Ubayy bin Ka'b daktari, akamkata mshipa kisha akamchoma kwa moto juu yake." (Imepokewa na Muslim). Na Al-Hakim ametoa katika Al-Mustadrak kutoka kwa Zaid bin Aslam kutoka kwa baba yake amesema:

مَرِضْتُ فِي زَمَانِ عُمَرَ بِنَ الْخَطَّابِ مَرَضاً شَدِيداً فَدَعَا لِي عُمَرُ طَبِيباً فَحَمَانِي حَتَّى كُنْتُ أَمُصُّ النَّوَاةَ مِنْ شِدَّةِ الْحِمْيَةِ

"Niliumwa sana wakati wa zama za Umar bin al-Khattab, basi Umar akaniitia daktari naye akanizuia kula baadhi ya vitu mpaka nilikuwa nikifyonza kokwa kutokana na ukali wa kuzuiliwa chakula." (Imepokewa na Al-Hakim).

Mtume (saw) akiwa kama mtawala alimtumia daktari Ubayy, na Umar (ra) Khalifah wa pili Mwongofu alimuita daktari kwa ajili ya Aslam ili amtibu, na hizi ni dalili mbili kwamba afya na matibabu ni miongoni mwa mahitaji ya kimsingi kwa raia ambayo dola lazima iyatoe bure kwa anayeyahitaji miongoni mwa raia.] Mwisho wa nukuu kutoka katika majibu.

Muhtasari:

1- Chanjo hukumu yake ni mandub, yaani inapendekezwa na si faradhi.

2- Ikiwa ndani yake kuna viambata vyenye madhara basi ni haramu.

3- Ikiwa haina madhara lakini inajumuisha vitu najisi au vilivyoharamishwa, basi inaruhusiwa pamoja na kuwa ni makruhu, yaani ni makruhu na si haramu.

4- Kwa hivyo, Mwislamu mgonjwa anapaswa kutafuta kwanza dawa iliyo halali, na asipoipata basi inaruhusiwa kwake kutumia dawa ya makruhu.

5- Hivyo basi, jawabu la swali lako kwa mujibu wa maelezo hapo juu ni kama ifuatavyo:

Hakika kuchanja kwa kutumia chanjo zenye vitu vilivyoharamishwa au najisi inaruhusiwa pamoja na makruhu kwa sababu chanjo inaingia chini ya mlango wa matibabu, na matibabu kwa kutumia vitu haramu na najisi kama ilivyobainishwa hapo juu inaruhusiwa pamoja na makruhu... isipokuwa ikibainika kuwa ina madhara, hapo haitaruhusiwa.

Na hadi sasa, sijafikia uamuzi wa uhakika juu ya madhara na kero ya dawa hii, na kwa hivyo naliacha jambo hili kwa vijana wa kiume na wa kike kufuata kile wanachoridhika na usahihi wake kwa mujibu wa yaliyotajwa hapo juu, na tunamuomba Mwenyezi Mungu (swt) atulinde sisi na Waislamu wote dhidi ya kila ugonjwa, hakika Yeye ni Msikivu na Mwenye kuitikia.

Wassalamu Alaikum Wa Rahmatullahi Wa Barakatuh.

Ndugu yenu, Ata bin Khalil Abu al-Rashtah

09 Jumada al-Akhira 1442 H Sawiya na 22/01/2021 M

Kiunganishi cha jawabu kutoka kwa ukurasa wa Amir (Mwenyezi Mungu amlinde) kwenye Facebook Kiunganishi cha jawabu kutoka kwa ukurasa wa Amir (Mwenyezi Mungu amlinde) tovutini

Share Article

Share this article with your network