Mfululizo wa majibu ya mwanachuoni mtukufu Ata bin Khalil Abu al-Rashtah, Amir wa Hizb ut-Tahrir, kwa maswali ya wafuasi wa ukurasa wake wa Facebook "Fiqhi"
Jibu la Swali
Zakat ya Pesa za Karatasi
Kwa Muhammad Yusuf
Swali:
Assalamu Alaikum Warahmatullahi Wabarakatuh,
Kwa kuwa aina sita zilizotajwa katika Riba ni majina yasiyobadilika (asma’ jamidah), na kwa kuwa pesa za karatasi zilichukua hukumu ya dhahabu na fedha zilipokuwa zimefunikwa na dhahabu na fedha, hukumu ilikuwa wazi. Sasa pesa za karatasi hazina hifadhi ya dhahabu wala fedha, je, hukumu inabaki vile vile, na pia katika Zakat ya mali?
Tufahamisheni, Allah awalipe heri na Allah adhibitishe (haki) kupitia mikono yenu.
Jibu:
Wa Alaikum Salaam Warahmatullahi Wabarakatuh.
Tumeeleza jambo hili katika Kitabu cha Al-Amwal – Mlango wa Zakat ya Pesa za Karatasi:
[Pesa za karatasi ni karatasi za kifedha zinazotolewa na dola, na kuzifanya kuwa pesa na sarafu yake, ambazo kwayo thamani ya bidhaa na gharama za huduma hukadiriwa. Pesa hizi za karatasi Zakat yake ni kama Zakat ya dhahabu na fedha, na hukumu za Zakat hutekelezwa kwazo kulingana na uhalisia wake. Uhalisia huu unawakilishwa katika aina tatu:
1- Pesa za karatasi wakili (na’ibah): Hizi ni karatasi za pesa zinazotolewa na dola inayofuata mfumo wa pesa wa metali, zikiwakilisha kiasi maalumu cha dhahabu au fedha, na huwa wakili wake katika mzunguko, na hubadilishwa kwayo pindi zinapohitajiwa. Karatasi hizi wakili huchukuliwa kuwa ni dhahabu au fedha, kwa sababu wakati wowote zinaweza kubadilishwa nazo. Zakat yake ni Zakat ya dhahabu na fedha; ikiwa ni wakili wa dhahabu na kiasi inachowakilisha kikifikia dinari ishirini – yaani gramu 85 – ambayo ndiyo Nisab ya dhahabu, basi Zakat ni lazima pindi mwaka unapopita juu yake (hawl), na kiasi kinachotolewa ni robo ya fungu la kumi (rubu’ul-ushr). Na ikiwa ni wakili wa fedha na kiasi inachowakilisha kikifikia dirham mia mbili – yaani gramu 595 – ambayo ndiyo Nisab ya fedha, basi Zakat ni lazima pindi mwaka unapopita juu yake, na kiasi kinachotolewa ni robo ya fungu la kumi. Dalili ya kuwajibika kwa Zakat ndani yake ni zile zile Hadith zilizotangulia zinazoonyesha kuwajibika kwa Zakat katika dhahabu na fedha; kwa sababu ni wakili na mbadala wa dhahabu na fedha, na wakili huchukua hukumu ya asili.
2- Pesa za karatasi zenye dhamana (wathiqah): Hizi ni karatasi za pesa zinazotolewa na dola, au benki mojawapo inayoaminika ambayo dola imeipa haki ya kutoa pesa, na huwa na hifadhi fulani ya dhahabu au fedha kwa kiwango maalumu, ambacho ni kidogo kuliko thamani ya jina la karatasi hizi, inayohifadhiwa na dola au benki iliyozitoa kama dhamana. Mtoaji huahidi kulipa thamani yake ya dhahabu au fedha iliyowekewa hifadhi kwa mbeba karatasi hiyo pindi anapohitaji. Hifadhi yake haitakuwa kamili, bali ni asilimia fulani ya thamani yake, inaweza kuwa robo tatu, theluthi mbili, nusu, au asilimia nyingine yoyote maalumu.
Karatasi hizi zenye dhamana, kile kiasi kilichohifadhiwa huchukuliwa kama karatasi wakili, dhahabu au fedha, kwa sababu wakati wowote hubadilishwa nazo. Zakat yake ni kama Zakat ya dhahabu na fedha; ikiwa imehifadhiwa kwa dhahabu, na hifadhi yake ni nusu ya thamani yake ya jina kwa mfano, basi Zakat ni lazima ikiwa itafikia dinari arobaini na kupitiwa na mwaka, na Zakat yake itakuwa ni dinari moja ya aina hiyo hiyo. Ikiwa haijafika dinari arobaini, basi hakuna Zakat ndani yake kwa sababu itakuwa chini ya Nisab.
Na ikiwa imehifadhiwa kwa fedha, na hifadhi yake ni nusu ya thamani yake ya jina kwa mfano, basi Zakat ni lazima ikiwa itafikia dirham mia nne na kupitiwa na mwaka, na Zakat yake itakuwa dirham kumi za aina hiyo hiyo. Ikiwa itapungua chini ya dirham mia nne, basi hakuna Zakat ndani yake kwa sababu itakuwa chini ya Nisab ya fedha.
Dalili ya kuwajibika kwa Zakat ndani yake ni zile zile Hadith zinazoonyesha kuwajibika kwa Zakat katika dhahabu na fedha; kwa sababu ni wakili na mbadala wa dhahabu na fedha katika kiasi kilichohifadhiwa cha thamani yake ya jina ambacho Zakat imewajibika ndani yake, na wakili huchukua hukumu ya asili.
3- Pesa za karatasi za lazima (ilzamiyyah): Hizi ni karatasi za pesa zinazotolewa na dola kwa sheria, na kuziingiza katika mzunguko, na kuzifanya kuwa pesa halali kwa kuwa thamani ya vitu na ujira wa huduma na manufaa, lakini hazibadilishwi kwa dhahabu wala fedha, na hazina hifadhi ya dhahabu wala fedha, na hazidhaminiwi na akiba ya dhahabu au fedha au karatasi za sarafu zenye hifadhi. Karatasi hizi za pesa hazina chochote isipokuwa thamani ya kisheria.
Lakini kwa kuwa karatasi hizi za lazima zimekubaliwa kuwa pesa na thamani ya vitu, na ujira wa manufaa na huduma, na kwayo dhahabu na fedha hununuliwa, kama zinavyonunuliwa bidhaa na vitu vingine vyote, basi sifa ya kuwa pesa (an-naqdiyah) na kuwa thamani (ath-thamaniyah) imepatikana ndani yake, sifa ambazo zinapatikana katika dhahabu na fedha zilizopigwa kuwa dinari na dirham.
Hii ni kwa sababu maandiko (nusus) yaliyokuja kuhusu Zakat ya dhahabu na fedha yamegawanyika sehemu mbili: Kwanza, dalili zinazotaja Zakat ya dhahabu na fedha kama majina ya jinsi, yaani katika dhati ya dhahabu na fedha, na haya ni majina yasiyobadilika (jamidah) ambayo hayafai kwa ajili ya utafiti wa sababu ya hukumu (ta'lil), hivyo haifanyiwi kulinganisha (qiyas). Kwa sababu hiyo, hakuna Zakat katika madini mengine kama chuma, shaba n.k. Abu Hurairah amepokea kuwa Mtume ﷺ amesema:
مَا مِنْ صَاحِبِ ذَهَب وَلَا فِضَّةٍ، لَا يُؤَدِّي مِنْهَا حَقَّهَا، إِلَّا إِذَا كَانَ يَوْمُ الْقِيَامَةِ، صُفِّحَتْ لَهُ صَفَائِحُ مِنْ نَارٍ
"Hakuna mmiliki wa dhahabu wala fedha ambaye hatekelezi haki yake (Zakat), isipokuwa Siku ya Kiyama atatengenezewa mabamba ya moto..." (Imepokewa na watano isipokuwa At-Tirmidhi). Katika Hadith hii, limekuja neno (dhahabu na fedha) na haya ni majina yasiyobadilika ambayo hayatafutiwi sababu ya hukumu.
Pili: Dalili zinazotaja Zakat ya dhahabu na fedha kama pesa ambazo watu huzitumia kama thamani na ujira. Dalili hizi hutolewa sababu (illah) kutoka kwazo, nayo ni u-pesa (an-naqdiyah), hivyo karatasi za pesa za lazima hulinganishwa nazo kwa sababu ya kupatikana kwa sababu hiyo ndani yake. Hivyo hukumu za Zakat ya pesa hutekelezwa kwazo kulingana na thamani yake sokoni katika dhahabu au fedha. Kutoka kwa Ali bin Abi Talib, kutoka kwa Mtume ﷺ amesema:
إذَا كَانَتْ لَك مِائَتَا دِرْهَمٍ، وَحَالَ عَلَيْهَا الْحَوْلُ، فَفِيهَا خَمْسَةُ دَرَاهِمَ، وَلَيْسَ عَلَيْك شَيْءٌ - يَعْنِي فِي الذَّهَبِ - حَتَّى يَكُونَ لَك عِشْرُونَ دِينَاراً، فَإِذَا كَانَتْ لَك عِشْرُونَ دِينَاراً، وَحَالَ عَلَيْهَا الْحَوْلُ، فَفِيهَا نِصْفُ دِينَارٍ
"Ikiwa una dirham mia mbili na mwaka ukapita juu yake, basi ndani yake mna dirham tano, na huna wajibu wa chochote – yaani katika dhahabu – mpaka uwe na dinari ishirini. Ikiwa una dinari ishirini na mwaka ukapita juu yake, basi ndani yake mna nusu dinari." (Imepokewa na Abu Dawood). Pia imepokewa kutoka kwa Ali akisema: "Katika kila dinari ishirini kuna nusu dinari, na katika kila dinari arobaini kuna dinari moja." Na kutoka kwa Ali (ra) amesema: Mtume wa Allah ﷺ amesema:
فَهَاتُوا صَدَقَةَ الرِّقَةِ مِنْ كُلِّ أَرْبَعِينَ دِرْهَماً دِرْهَماً، وَلَيْسَ فِي تِسْعِينَ وَمِائَةٍ شَيْءٌ، فَإِذَا بَلَغَتْ مِائَتَيْنِ فَفِيهَا خَمْسَةُ دَرَاهِمَ
"...Basi toeni sadaka ya riqah (fedha iliyopigwa kuwa sarafu), katika kila dirham arobaini ni dirham moja, na katika dirham mia moja na tisini hakuna kitu, na inapofika mia mbili basi ndani yake mna dirham tano." (Imepokewa na Al-Bukhari na Ahmad). Pia Abdul Rahman al-Ansari amepokea katika barua ya Mtume ﷺ na barua ya Umar kuhusu sadaka:
والورِق لا يؤخذ منه شيء حتى يبلغ مئتي درهم
"...Na wariq (fedha) haichukuliwi kitu mpaka ifikie dirham mia mbili." (Imepokewa na Abu Ubaid).
Hadith hizi zote zimeashiria sifa ya kuwa pesa na thamani; kwani maneno kama riqah pamoja na kiashiria cha "katika kila dirham arobaini", wariq, dinari, na dirham ni maneno yanayotumika kwa dhahabu na fedha zilizopigwa na kutengenezwa sarafu, yaani ambazo ni pesa na thamani. Kutumia maneno haya kunaonyesha kuwa u-pesa na u-thamani ndio uliokusudiwa katika Hadith hizi, na kwayo hukumu nyingi za kisheria zimefungamanishwa kama Zakat, fidia ya damu (diyat), kafara, kukatwa mkono kwa wizi, na hukumu nyinginezo.
Na kwa kuwa karatasi za lazima sifa hii ya u-pesa na u-thamani imepatikana ndani yake, basi zinaingia katika Hadith za kuwajibika kwa Zakat katika sarafu mbili (dhahabu na fedha). Hivyo, Zakat ni lazima ndani yake kama inavyowajibika katika dhahabu na fedha, na hukadiriwa kwa dhahabu na fedha. Yule aliye na kiasi cha karatasi hizi za lazima kinacholingana na thamani ya dinari ishirini za dhahabu – yaani gramu 85 za dhahabu – ambayo ndiyo Nisab ya dhahabu, au ana kiasi kinacholingana na thamani ya dirham 200 za fedha – yaani gramu 595 za fedha – na kupitiwa na mwaka, basi Zakat ni lazima kwake, na ni lazima kutoa robo ya fungu la kumi.
Dhahabu hutolewa Zakat kwa dhahabu, au kwa karatasi wakili, au karatasi zenye dhamana. Na fedha hutolewa Zakat kwa fedha, au kwa karatasi wakili na zenye dhamana. Vilevile inajuzu kutoa Zakat ya dhahabu kwa fedha na karatasi za lazima, na Zakat ya fedha kwa dhahabu na karatasi za lazima; kwa sababu zote ni pesa na thamani, hivyo moja hutosheleza badala ya nyingine, na inajuzu kutoa moja badala ya nyingine kwa sababu lengo la jambo hilo limefikiwa. Na yameshapita katika mlango wa Zakat ya mazao na matunda dalili za kuchukua thamani badala ya dhati ya mali ambayo Zakat imewajibika ndani yake.]
Kama unavyoona, karatasi za lazima zinatimiza sababu (illah) (u-pesa na u-thamani), na kwa sababu hiyo Zakat ni lazima ndani yake ikiwa thamani yake itafikia Nisab na kupitiwa na mwaka. Hii ina maana kwamba Muislamu anayeishi katika dola isiyotumia dhahabu na fedha kama pesa yake kama inavyowajibisha Sharia, bali inatumia pesa za karatasi za lazima, Muislamu huyu anapaswa kutoa Zakat ya mali yake ya pesa za karatasi ikiwa thamani yake itafikia Nisab na kupitiwa na mwaka, kwa kiwango kile kile ambacho dhahabu na fedha hutolewa Zakat kama pesa.
Natumai jibu hili linatosheleza, na Allah ni Mjuzi zaidi na Mwenye hekima zaidi.
Ndugu yenu, Ata bin Khalil Abu al-Rashtah
27 Ramadhan 1443 H Mtawalia 28/04/2022 M
Kiungo cha jibu kutoka ukurasa wa Amir (Allah amhifadhi) kwenye Facebook: https://www.facebook.com/HT.AtaabuAlrashtah/posts/538970827790291
Kiungo cha jibu kutoka tovuti ya Amir (Allah amhifadhi): http://archive.hizb-ut-tahrir.info/arabic/index.php/HTAmeer/QAsingle/4240