** (Silsila ya majibu ya mwanachuoni mtukufu Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah, Amir wa Hizb ut Tahrir, kwa maswali ya wafuasi wake kwenye ukurasa wake wa Facebook "Fiqhi") **
Jawabu la Swali
Mali ya Riba Baada ya Kusimama kwa Khilafah
Kwa: Safir al-Khilafah
Swali:
Assalam Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh,
Swali kutoka katika kitabu Ajhizat al-Hukm wal-Idarah (Vyombo vya Utawala na Uongozi) kuhusiana na mali ya riba baada ya kusimama kwa Dola ya Khilafah kwa kuwapa wenyewe rasilimali zao... Swali: Tutafanya nini na mali ya riba? Je, inaruhusiwa kwa dola kuizuia na kuiwekeza? Na je, pesa taslimu iliyotokana na riba ya mali kama noti ni haramu yenyewe (kwa dhati yake) au uharamu unarejea kwenye kitendo?
Jibu:
Wa Alaykum Assalam Warahmatullahi Wabarakatuh,
1- Jawabu la swali lako "Tutafanya nini na mali ya riba...", jawabu hili lipo katika kitabu Al-Amwal fi Dawlat al-Khilafah (Mali katika Dola ya Khilafah), kwani kimefafanua jinsi dola inavyoshughulikia mali iliyopatikana kwa njia isiyo ya kisheria kama vile mali ya ghulul (ufisadi/uibaji wa mali ya umma) kutoka kwa watawala na watumishi, riba, kamari... n.k. Imekuja katika mlango wa: "Mali ya Ghulul kutoka kwa Watawala, na Watumishi wa Dola, na Mali ya Mapato Yasiyo ya Kisheria, na Mali ya Faini" ukurasa wa 111-112 yafuatayo:
(Kila kilichotajwa ambacho huchumwa na magavana, wafanyakazi, na watumishi wa dola kwa njia isiyo ya kisheria kinakuwa miongoni mwa mapato ya Bayt al-Mal. Na linaunganishwa na hilo katika mapato ya Bayt al-Mal pia, kila mali inayochumwa na watu binafsi kwa njia miongoni mwa njia zilizokatazwa kisheria kumiliki au kukuza mali kwayo; kwa sababu inakuwa ni chumo la haramu, na haimilikiwi.
Yule anayechuma kitu kupitia njia ya riba kinakuwa ni haramu, na hakitamilikiwa, kwa sababu Mwenyezi Mungu ameharamisha riba, na ameharamisha kukuza mali kupitia kwayo. Amesema Mwenyezi Mungu (swt):
الَّذِينَ يَأْكُلُونَ الرِّبَا لَا يَقُومُونَ إِلَّا كَمَا يَقُومُ الَّذِي يَتَخَبَّطُهُ الشَّيْطَانُ مِنَ الْمَسِّ ذَلِكَ بِأَنَّهُمْ قَالُوا إِنَّمَا الْبَيْعُ مِثْلُ الرِّبَا وَأَحَلَّ اللَّهُ الْبَيْعَ وَحَرَّمَ الرِّبَا فَمَنْ جَاءَهُ مَوْعِظَةٌ مِنْ رَبِّهِ فَانْتَهَى فَلَهُ مَا سَلَفَ وَأَمْرُهُ إِلَى اللَّهِ وَمَنْ عَادَ فَأُولَئِكَ أَصْحَابُ النَّارِ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ
"Wale wanaokula riba hawasimami ila kama anavyosimama yule ambaye Shetani amemgubika kwa kichaa. Hayo ni kwa sababu wamesema: Biashara ni kama riba; hali Mwenyezi Mungu amehalalisha biashara na ameharamisha riba. Basi aliyefikiwa na mawaidha kutoka kwa Mola wake, akajizuia, basi ni vyake vilivyopita, na mambo yake yako kwa Mwenyezi Mungu. Na watakaorejea, basi hao ndio watu wa Motoni, humo watakaa milele." (QS. Al-Baqarah [2]: 275)
Na akasema Mwenyezi Mungu (swt):
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّهَ وَذَرُوا مَا بَقِيَ مِنَ الرِّبَا إِنْ كُنْتُمْ مُؤْمِنِينَ * فَإِنْ لَمْ تَفْعَلُوا فَأْذَنُوا بِحَرْبٍ مِنَ اللَّهِ وَرَسُولِهِ وَإِنْ تُبْتُمْ فَلَكُمْ رُءُوسُ أَمْوَالِكُمْ لَا تَظْلِمُونَ وَلَا تُظْلَمُونَ
"Enyi mlioamini! Mcheni Mwenyezi Mungu, na acheni yaliyobakia katika riba, ikiwa nyinyi ni Waumini. Na ikiwa hamtafanya hivyo, basi fahamuni mtatangaziwa vita na Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na mkitubu, basi rasilimali zenu ni zenu; msidhulumu wala msidhulumiwe." (QS. Al-Baqarah [2]: 278-279)
Ni lazima mali ya riba irejeshwe kwa wenyewe ambao walinyang'anywa (walioliwa) ikiwa wanajulikana, na ikiwa hawajulikani basi hutaifishwa na kuwekwa katika Bayt al-Mal. Hii ni pamoja na adhabu ya kisheria inayowahusu wanaofanya miamala ya riba "mla riba, mlishaji wake, mwandishi wake na mashahidi wake wawili", kama ilivyokuja katika Hadith tukufu:
لَعَنَ رَسُولُ اللهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ آكِلَ الرِّبَا، وَمؤْكِلَهُ، وَكَاتِبَهُ، وَشَاهِدَيْهِ
"Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amemlaani mla riba, mlishaji wake, mwandishi wake, na mashahidi wake wawili," na akasema:
هُمْ سَوَاءٌ
"Wote wako sawa." (Imepokelewa na Muslim kutoka kwa Jabir).
Na yule aliyepata mali kwa njia ya kamari chumo lake ni haramu, na halimilikiwi, na hurejeshwa kwa mwenyewe. Ikiwa mwenyewe hajulikani basi hutaifishwa na kuwekwa katika Bayt al-Mal; hii ni pamoja na adhabu ya kisheria kwa yule anayefanya kamari awe amepoteza au ameshinda. Kwa sababu kukuza umiliki kupitia njia ya kamari haijuzu kisheria, kwani kamari ni haramu. Amesema Mwenyezi Mungu (swt):
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِنَّمَا الْخَمْرُ وَالْمَيْسِرُ وَالْأَنْصَابُ وَالْأَزْلَامُ رِجْسٌ مِنْ عَمَلِ الشَّيْطَانِ فَاجْتَنِبُوهُ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ * إِنَّمَا يُرِيدُ الشَّيْطَانُ أَنْ يُوقِعَ بَيْنَكُمُ الْعَدَاوَةَ وَالْبَغْضَاءَ فِي الْخَمْرِ وَالْمَيْسِرِ وَيَصُدَّكُمْ عَنْ ذِكْرِ اللَّهِ وَعَنِ الصَّلَاةِ فَهَلْ أَنْتُمْ مُنْتَهُونَ
"Enyi mlioamini! Bila shaka ulevi, na kamari, na masanamu, na kutazamia kwa mishale, ni uchafu katika kazi ya Shetani. Basi jiepusheni navyo ili mpate kufanikiwa. Hakika Shetani anataka kuweka kati yenu uadui na chuki kwa ulevi na kamari, na akuzuieni kumkumbuka Mwenyezi Mungu na kusali. Basi je, nyinyi mtaacha?" (QS. Al-Ma'idah [5]: 90-91).
2- Ama sehemu ya pili ya swali kuhusu uharamu wa mali ya riba ikiwa ni kwa dhati yake au kwa kitendo... Jibu ni kwamba mali iliyochumwa kwa kitendo kisicho cha kisheria si haramu kwa dhati yake, bali uharamu ni wa namna ya kuichuma au kuikuza. Ama dhati ya mali si haramu. Hivyo, anayechuma dinari kwa kuuza pombe au kwa riba kwa mfano, dinari hizo hazijawa haramu kwa dhati yake, bali uharamu uko katika namna ya kuzichuma au kuzikuza. Na kwa ajili hiyo, hazimilikiwi na yule aliyezichuma kwa haramu. Ama dhati yake si haramu na ndiyo maana huwekwa katika Bayt al-Mal ya Waislamu, na hutumika katika mambo yao. Na haivuliwi katika hilo isipokuwa mali ambayo dhati yake ni haramu kama vile nguruwe na pombe, kwani hizo ni mali haramu kwa dhati yake.
Ndugu yenu, Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah
Kiungo cha jibu kutoka kwa ukurasa wa Amir kwenye Facebook
Kiungo cha jibu kutoka katika tovuti ya Amir
Kiungo cha jibu kutoka kwa ukurasa wa Amir kwenye Google Plus