(Silsila ya Majibu ya Mwanachuoni Ata bin Khalil Abu Al-Rashtah, Amir wa Hizb ut Tahrir, kwa Maswali ya Wafuasi wa Ukurasa Wake wa Facebook)
Kwa Abdulla Amer
Swali:
Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.
Jana watu walikuwa wakitoka katika swala ya Ijumaa, na mnajua mkusanyiko wa watu mlangoni mwa msikiti, mtu mmoja akasema "Mswalieni Mtume," kisha mtu mwingine akamwambia: "Nyamaza, hiyo ni bid'ah." Swali ni: Je, hiyo ni bid'ah au la? Na Mwenyezi Mungu awalipe heri.
Jibu:
Waalaykum Salaam Warahmatullahi Wabarakatuh,
Kauli ya bwana yule "Mswalieni Mtume" mlangoni mwa msikiti si bid'ah, **na hiyo ni kwa sababu bid'ah ni kukiuka amri ya Mtoaji Sheria (Ash-Shari’) ambayo imekuja na namna maalumu ya utekelezaji (kaifiyah)**. Bid'ah kilugha kama ilivyoelezwa katika Lisan al-Arab: "Mubtadi’ ni yule anayekuja na jambo kwa mfano ambao haukuwepo awali..., na nimeanzisha (abda’tu) kitu: nimevumbua bila kufuata mfano uliotangulia." Na kisheria (istilahan) ni vivyo hivyo, yaani kuwepo kwa "mfano" (utaratibu) uliotekelezwa na Mtume (saw) kisha Mwislamu akaja na kinyume chake. Hii inamaanisha kukiuka namna ya kisheria (kaifiyah shar’iyyah) iliyobainishwa na Shari’ah kwa ajili ya kutekeleza amri ya kisheria, na maana hii ndiyo inayokusudiwa na hadith:
مَنْ عَمِلَ عَمَلًا لَيْسَ عَلَيْهِ أَمْرُنَا فَهُوَ رَدٌّ
"Yeyote atakayefanya amali ambayo haiko katika jambo letu (dini yetu), basi hiyo itakataliwa." (Bukhari na Muslim).
Hivyo basi, yule anayesujudu mara tatu katika swala yake badala ya mbili atakuwa amekuja na bid'ah, kwa sababu amekiuka kitendo cha Mtume (saw). Na yule anayerusha vijiwe vinane badala ya saba katika kurusha vijiwe (jamarat) kule Mina atakuwa amekuja na bid'ah kwa sababu pia amekiuka kitendo cha Mtume (saw). Na yule anayezidisha maneno katika adhana au kupunguza atakuwa amekuja na bid'ah kwa sababu amekiuka adhana aliyoidhinisha Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw)...
Ama kukiuka amri ya Mtoaji Sheria ambayo haikuja na namna maalumu ya utekelezaji (kaifiyah), basi hilo huangukia katika hukumu za kisheria, ambapo husemwa kuwa ni haramu, au makruhu... ikiwa ni khitab taklif (amri ya utekelezaji), au husemwa kuwa ni batili au fasidi... ikiwa ni khitab wad’i (sharti/sababu), na hiyo ni kulingana na kiashiria (qarinah) kinachoambatana na amri hiyo...
Kwa mfano: Muslim amepokea kutoka kwa Aisha (ra) akielezea swala ya Mtume (saw), amesema: Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) alikuwa...
وَكَانَ إِذَا رَفَعَ رَأْسَهُ مِنَ الرُّكُوعِ لَمْ يَسْجُدْ، حَتَّى يَسْتَوِيَ قَائِمًا، وَكَانَ إِذَا رَفَعَ رَأْسَهُ مِنَ السَّجْدَةِ، لَمْ يَسْجُدْ حَتَّى يَسْتَوِيَ جَالِسًا
"...Na alikuwa anapoinua kichwa chake kutoka kwenye rukuu hasujudu mpaka anyooke akiwa amesimama, na alikuwa anapoinua kichwa chake kutoka kwenye sijda hasujudu (sijda ya pili) mpaka akae sawa akiwa ameketi..." (Muslim).
Hapa Mtume (saw) amebainisha kuwa Mwislamu baada ya kuinuka kutoka kwenye rukuu hasujudu mpaka anyooke akiwa amesimama, na anapoinuka kutoka kwenye sijda hasujudu sijda nyingine mpaka akae sawa akiwa ameketi. Hii ni namna ya utekelezaji (kaifiyah) aliyoibainisha Mtume (saw), hivyo yule anayeikiuka atakuwa amekuja na bid'ah. Ikiwa mswali atainuka kutoka kwenye rukuu kisha akasujudu kabla ya kunyooka akiwa amesimama, atakuwa amekuja na bid'ah kwa sababu amekiuka namna ya utekelezaji iliyobainishwa na Mtume (saw), na bid'ah hii ni upotofu na mtendaji wake ana dhambi kubwa.
Lakini kwa mfano, Muslim amepokea kutoka kwa Ubadah bin al-Samit, amesema: Nilimsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw):
يَنْهَى عَنْ بَيْعِ الذَّهَبِ بِالذَّهَبِ، وَالْفِضَّةِ بِالْفِضَّةِ، وَالْبُرِّ بِالْبُرِّ، وَالشَّعِيرِ بِالشَّعِيرِ، وَالتَّمْرِ بِالتَّمْرِ، وَالْمِلْحِ بِالْمِلْحِ، إِلَّا سَوَاءً بِسَوَاءٍ، عَيْنًا بِعَيْنٍ، فَمَنْ زَادَ، أَوِ ازْدَادَ، فَقَدْ أَرْبَى
"(Mtume SAW) Alikataza kuuza dhahabu kwa dhahabu, fedha kwa fedha, ngano kwa ngano, shayiri kwa shayiri, tende kwa tende, na chumvi kwa chumvi, isipokuwa ziwe sawa kwa sawa, mkono kwa mkono, basi yeyote atakayezidisha au kutaka kuzidishiwa, basi amefanya riba." (Muslim).
Ikiwa Mwislamu atakiuka hadith hii na kuuza dhahabu kwa dhahabu kwa ziada, na si uzito kwa uzito, haisemwi kuwa amekuja na bid'ah, bali husemwa kuwa amefanya haramu, yaani riba.
Muhtasari ni kwamba: Kukiuka namna ya utekelezaji (kaifiyah) aliyoibainisha Mtume (saw) ni bid'ah. Ama kukiuka amri ya jumla ya Mtume (saw) bila ya kuwepo kwa ufafanuzi wa namna ya utekelezaji, huingia katika hukumu za kisheria: Haramu, Makruhu... Batili na Fasidi... na hiyo ni kulingana na dalili.
Na katika swali lako, Mtume (saw) hakubainisha namna maalumu ya maneno yanayoambatana na kutoka msikitini baada ya swala ya Ijumaa. Hivyo basi, kauli ya Mwislamu yule wakati akitoka msikitini "Mswalieni Mtume" haiingii katika mlango wa bid'ah, bali inachunguzwa ndani ya hukumu za kisheria, na jambo hilo ni halali na halina neno lolote, bali lina malipo kulingana na nia yake akipenda Mwenyezi Mungu.
Ndugu yenu, Ata bin Khalil Abu Al-Rashtah
Kiungo cha jibu kutoka ukurasa wa Amir wa Facebook: Facebook
Kiungo cha jibu kutoka tovuti ya Amir
Kiungo cha jibu kutoka ukurasa wa Amir wa Google Plus