Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

Jibu la Swali: Kuhusu Hukumu ya Mkataba wa Murabahah

May 30, 2013
4841

(Mfululizo wa majibu ya mwanachuoni Ata bin Khalil Abu al-Rashtah, Ameer wa Hizb ut-Tahrir, kwa maswali ya wafuasi wa ukurasa wake wa Facebook)

Imeelekezwa kwa: Muhamad Abdallah

Swali:

Assalamu Alaikum Warahmatullahi Wabarakatuh,

Sheikh wetu na Ameer wetu Ata bin Khalil Abu al-Rashtah, nina swali linalosema: Ni ipi hukumu ya mkataba wa Murabahah; je, ni halali, ni fasidi (wenye kasoro), au ni batili? Imetokea kwamba ndugu zetu walikubaliana mkataba wa Murabahah, na baada ya muda wakajua kuwa hausihi (si sahihi). Upande wa kwanza uliotoa mtaji ulichukua kiasi sawa na mtaji wake na nusu zaidi, na sasa anadai baki ya faida baada ya kujua kuwa mkataba huo haujuzu.

Swali ni: Ni ipi asili ya mkataba huu kwa upande wa uhalali na uharamu? Je, mali aliyochukua ni halali au haramu? Na je, ana haki ya kudai baki ya faida baada ya kuchukua mtaji wake na ziada, pamoja na kwamba ndugu wanajua kuwa asili ya vitendo ni kufungamana na hukumu ya kisheria?

Tufahamishe, na Allah akujaze heri. Abu Suhayl – Berlin.

Jibu:

Wa Alaikum Salaam Warahmatullahi Wabarakatuh,

Kile ulichokiita mkataba wa Murabahah kulingana na yale yaliyokuja katika swali lako—kwamba mwenye mali huitoa kwa upande mwingine ili aifanyie biashara au aitumie... na anampa faida ya uhakika—basi jambo hili halijuzu katika Uislamu. Kinachojuzu ni mwenye mali kumpa mwingine mali yake ili aifanyie biashara na wakubaliane kiwango cha asilimia ya faida watakayopata pande zote mbili ikiwa kutakuwa na faida. Na ikiwa hakuna faida, basi hakuna chochote kwa yeyote kati yao. Na ikiwa kuna hasara, basi mwenye mali ndiye anayebeba hasara hiyo kwa sababu upande mwingine uliotoa juhudi na kufanya biashara utakuwa umepoteza juhudi zake. Yaani, haipandikizwi faida ya uhakika kwa mwenye mali, bali ni kama tulivyosema hapo awali.

Na huu ndio unaoitwa katika Uislamu mkataba wa Mudharabah.

Na Mudharabah ni aina miongoni mwa aina za shirka (ushirika) kwa sababu ni ushirika wa mwili (kazi) na mali. Ushirika ni miongoni mwa miamala ambayo Sharia imeeleza kujuzu kwake. Kutoka kwa Abu Hurairah amesema: Amesema Mtume (saw):

إِنَّ اللَّهَ يَقُولُ: أَنَا ثَالِثُ الشَّرِيكَيْنِ، مَا لَمْ يَخُنْ أَحَدُهُمَا صَاحِبَهُ، فَإِذَا خَانَهُ خَرَجْتُ مِنْ بَيْنِهِمَا

"Hakika Allah anasema: Mimi ni wa tatu wa washirika wawili, maadamu mmoja wao hamfanyii hiana mwenzake; anapomfanyia hiana, mimi hujiondoa miongoni mwao." (Imepokewa na Abu Daud).

Na Maswahaba (ra) waliafikiana (ijma) juu ya kujuzu kwa Mudharabah. Umar (ra) alitoa mali ya yatima kama Mudharabah kama ilivyopokewa katika Musannaf ya Ibn Abi Shaybah. Ama kuhusu faida katika Mudharabah, hiyo ni kulingana na kile walichoshartiiana waliofanya mkataba. Na ama kuhusu hasara, hiyo ni juu ya mali (mtaji). Abd al-Razzaq al-San’ani ametoa katika Musannaf yake kutoka kwa Ali (ra) kuhusu Mudharabah:

الْوَضِيعَةُ عَلَى الْمَالِ، وَالرِّبْحُ عَلَى مَا اصْطَلَحُوا عَلَيْهِ

"Hasara iko juu ya mali, na faida ni kulingana na kile walichokubaliana."

Na neno al-wadhi'ah linamaanisha hasara.

Kwa ufahamu zaidi, istilahi ya Murabahah katika Sharia imekuja katika masuala ya kuuza na kununua, na si katika mikataba ya kazi. Wale wanaotumia neno Murabahah katika mikataba ya kazi kati ya mwenye mali na mfanya kazi (mudharib), wanaitumia pasina mahali pake kisheria. Hii ni kwa sababu Murabahah kilugha inamaanisha kupata faida; husemwa: Nimeuza bidhaa kwa murabahah, au nimeinunua kwa murabahah.

Na katika istilahi: Ni muuzaji kutoa bidhaa yake kwa ajili ya kuuza kwa kiwango cha gharama iliyomgharimu pamoja na faida inayojulikana. Nayo ni miongoni mwa mauzo ya amana (buyu’ al-amanat) kwa sababu inategemea uaminifu wa muuzaji katika kuelezea gharama ya bidhaa kwake.

Nayo inajuzu kisheria kwa sababu ni ununuzi kwa faida juu ya bei ambayo muuzaji aliinunulia. Ikiwa muuzaji atasema: "Ninakuuzia bidhaa hii kwa faida kadhaa juu ya bei niliyoifanyia ununuzi," na mnunuzi akajulishwa bei hiyo na akakubali, basi hii inajuzu kwa sababu ni mauzo yanayojulikana.

Ndugu yenu, Ata bin Khalil Abu al-Rashtah

Link ya jibu kutoka kwa ukurasa wa Ameer kwenye Facebook: https://web.facebook.com/AmeerhtAtabinKhalil/photos/a.122855544578192.1073741828.122848424578904/134432773420469/?type=3&theater

Link ya jibu kutoka kwa tovuti ya Ameer: http://archive.hizb-ut-tahrir.info/arabic/index.php/HTAmeer/QAsingle/3346/

Link ya jibu kutoka kwa ukurasa wa Ameer kwenye Google Plus: https://plus.google.com/u/0/b/100431756357007517653/100431756357007517653/posts/K4qVCe7ubH9?sfc=false

Share Article

Share this article with your network