Mfululizo wa Majibu ya Mwanachuoni Mtukufu Ata bin Khalil Abu Al-Rashtah, Amir wa Hizb ut-Tahrir, kwa Maswali ya Wageni kwenye Ukurasa wake wa Facebook "Fiqhi"
Jibu la Swali
Adhabu ya Mzinifu Muhsan Katika Uislamu Kwa Muhammad Amin
Swali:
Assalamualaikum War. Wab. yes Sheikh wa Amiruna. I would like to ask a question, hopefully you will answer it.
Regarding the death penalty for Muhson, is Qothie categorized in Fiqh Islam? There are some scholars such as Sheikh Abu Zahrah who do not categorize it as Hudud punishment. It is even supported by Sheikh Mustafa Zarqa who states that it is categorized in the sentence of Takzir. How do you think about this issue?
Jazaakumullah khoiron for your convenience answer my question.
Jibu:
Wa Alaikum Salaam Wa Rahmatullahi Wa Barakatuh,
Unauliza kuhusu adhabu ya mzinifu muhsan (aliyewahi kuoa/kuolewa), je ni ya yakini (qat’i) katika Fiqhi ya Kiislamu? Na je, ni miongoni mwa Hudud au si katika Hudud bali ni katika Ta’zir kama wanavyosema baadhi ya wanachuoni katika zama hizi?
Jibu la swali lako ni kama ifuatavyo:
1- Adhabu ya mzinifu muhsan kwa kupigwa mawe hadi kufa (rajm) imo ndani ya mlango wa hukumu za kisheria na si katika mlango wa itikadi (Aqaid). Hivyo basi, kama zilivyo hukumu nyingine zote za kisheria, haishartiwi kuwa dalili yake iwe ya yakini (qat’i) ili ifanyiwe kazi, bali inatosha kwa dhana yenye nguvu (ghalabat ad-dhann) kama inavyofahamika katika Usul al-Fiqh... Kwa hiyo, haina athari ikiwa dalili ya adhabu hii ni ya yakini au si ya yakini katika kuichukua na kuifanyia kazi; jambo muhimu ni kwamba ithibiti katika Sharia dalili juu yake. Na zimepokewa dalili nyingi sahihi katika Sharia zinazobainisha bila kuacha chembe ya shaka kwamba adhabu ya mzinifu muhsan ni kupigwa mawe hadi kufa kama ilivyotajwa hapa chini.
2- Inazingatiwa kwa baadhi ya wanachuoni katika zama hizi kwamba hawafuati mkondo sahihi katika kuchukua hukumu za kisheria kutoka katika dalili zake. Hii ni kwa sababu wanajitahidi, wakati wa kutafuta hukumu ya kisheria, kuendana na zama na kufikia maoni yanayoafikiana na yale yaliyotawala ulimwenguni miongoni mwa hukumu na maoni yaliyowekwa na ustaarabu wa Magharibi kwa watu kwa jina la sheria za kimataifa, mikataba ya haki za binadamu, na mengineyo... Jambo hili si sahihi, kwa sababu kinachotakiwa ni hukumu ya Mwenyezi Mungu na si hukumu yoyote ile, wala hukumu inayokubaliana na kile kinachotawala ulimwenguni miongoni mwa hukumu, sheria, mikataba, na maoni... Wajibu ni kuichukua hukumu ya kisheria kama ilivyo kutoka kwenye dalili zake na kuifanya kuwa ndiyo inayotekelezwa na kutumika, na kufanya ulinganizi na kuitangaza ulimwenguni kote; kwani ndiyo hukumu yenye maslahi kwa wanadamu wote kwa sababu inatoka kwa Muumba wa wanadamu Anayejua hali zao, Subhanahu:
أَلَا يَعْلَمُ مَنْ خَلَقَ وَهُوَ اللَّطِيفُ الْخَبِيرُ
“Je! asijue aliye umba, naye ndiye Mjuzi wa yaliyofichika, Mwenye habari?” (QS. Al-Mulk [67]: 14)
أَلَا لَهُ الْخَلْقُ وَالْأَمْرُ تَبَارَكَ اللَّهُ رَبُّ الْعَالَمِينَ
“Fahamuni! Kuumba na amri ni Vyake. Ametukuka Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa walimwengu wote.” (QS. Al-A'raf [7]: 54)
Kwa hivyo, haipasi kusikiliza kauli za wale wanaopapia katika kutoa kwao hukumu (istinbat) kuendana na zama na kuafikiana na ustaarabu wa Magharibi, iwe wanafanya hivyo chini ya shinikizo la uhalisia au kwa kuwaridhisha makafiri wa Magharibi...
3- Adhabu ya uzinifu kwa muhsan ambayo ni kupigwa mawe hadi kufa (rajm) na kwa asiyekuwa muhsan ambayo ni kupigwa mijeledi mia moja, ni adhabu iliyoingia katika Uislamu katika mlango wa Hudud. Tumebainisha hukumu za hadd ya uzinifu katika kitabu cha Nidham al-Uqubat (Mfumo wa Adhabu) kwa ufafanuzi wa kina na wa kutosha, na ninakunukulia kutoka katika kitabu cha Nidham al-Uqubat baadhi ya yaliyokuja katika mlango wa “Hadd ya Uzinifu”:
[Wanasema baadhi kuwa hadd ya mzinifu mwanamke na mwanamume ni mijeledi mia moja kwa muhsan na asiyekuwa muhsan sawa, na hakuna tofauti kati yao, kwa sababu ya kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:
الزَّانِيَةُ وَالزَّانِي فَاجْلِدُوا كُلَّ وَاحِدٍ مِّنْهُمَا مِائَةَ جَلْدَةٍ ۖ وَلَا تَأْخُذْكُم بِهِمَا رَأْفَةٌ فِي دِينِ اللَّهِ
“Mzinifu mwanamke na mzinifu mwanamume, mpigeni kila mmoja wao mijeledi mia moja. Wala isiwanyakue kwa ajili yao huruma katika dini ya Mwenyezi Mungu.” (QS. An-Nur [24]: 2).
Na walisema haijuzu kuacha Kitabu cha Mwenyezi Mungu kwa njia ya yakini na hakika kwa ajili ya habari za mmoja mmoja (akhbar al-ahad) ambazo zinawezekana kuwa na uongo, na kwa sababu hii inapelekea kufuta (naskh) Kitabu kwa Sunnah na jambo hilo haijuzu. Lakini wanasema wanachuoni wote miongoni mwa Maswahaba na Tabi’ina, na wale waliokuja baada yao miongoni mwa wanachuoni wa miji katika karne zote kwamba asiyekuwa muhsan anapigwa mijeledi mia moja, na muhsan anapigwa mawe hadi kufa kwa sababu Mtume (saw): “alimpiga mawe Ma’iz” na kwa yale yaliyopokewa kutoka kwa Jabir bin Abdullah “kwamba mwanamume alizini na mwanamke, Mtume (saw) akaamuru apigwe mijeledi, kisha akajulishwa kuwa ni muhsan, akaamuru apigwe mawe”.
Mwenye kuangalia dalili anaona kuwa kauli yake Mtukufu: (Mzinifu mwanamke na mzinifu mwanamume, mpigeni kila mmoja wao mijeledi mia moja) ni ya jumla (aam), kwani neno "mzinifu mwanamke" na neno "mzinifu mwanamume" ni miongoni mwa maneno ya ujumla, hivyo yanajumuisha muhsan na asiyekuwa muhsan. Na ilipokuja Hadith ambayo ni kauli yake (saw): “Nenda ewe Unais kwa mke wa huyu, akiri basi mpige mawe”, na imethibiti kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) alimpiga mawe Ma’iz baada ya kuuliza kuhusu u-muhsan wake, na alimpiga mawe mwanamke wa Al-Ghamidiyyah na mengineyo miongoni mwa Hadith sahihi, basi Hadith inakuwa ni yenye kuhusisha (mukhasis) aya hiyo. Hivyo basi, Hadith hizi zimehusisha huu ujumla ulioko katika aya kwa asiyekuwa muhsan, na zikamtoa humo muhsan. Kwa hiyo Hadith zimehusisha ujumla huu na hazikufuta Quran, na kuhusisha Quran kwa Sunnah (takhsis al-Quran bi al-sunnah) kunajuzu, na kumetokea katika aya nyingi ambazo zilikuja kwa ujumla kisha ikaja Hadith na kuzihusisha.
Hukumu ya kisheria ambayo dalili za kisheria zinaonyesha, yaani Kitabu na Sunnah, ni kwamba adhabu ya uzinifu ni kumpiga mijeledi mia moja asiyekuwa muhsan kwa kuifanyia kazi Kitabu cha Mwenyezi Mungu, na kumfukuza nchi kwa mwaka mmoja kwa kuifanyia kazi Sunnah ya Mtume wa Mwenyezi Mungu. Isipokuwa kwamba kumfukuza nchi (taghrib) kunajuzu na si wajibu, na jambo hilo limeachiwa Imam (Khalifa), akitaka atampiga mijeledi na kumfukuza nchi mwaka mmoja, na akitaka atampiga mijeledi na hatomfukuza. Lakini haijuzu kumfukuza na kutompiga mijeledi, kwa sababu adhabu yake ni mijeledi. Ama adhabu ya muhsan ni kumpiga mawe hadi kufa, kwa kuifanyia kazi Sunnah ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) ambayo imekuja kuhusisha Kitabu cha Mwenyezi Mungu. Na inajuzu kwa muhsan kukusanyishiwa mijeledi na kupigwa mawe; akapigwa mijeledi kwanza kisha akapigwa mawe. Na inajuzu kufanya adhabu ya kupigwa mawe pekee asipigwe mijeledi, lakini haijuzu kufanya adhabu ya mijeledi pekee kwa sababu adhabu yake ya wajibu ni kupigwa mawe.
..........
Ama dalili ya adhabu ya muhsan ni Hadith nyingi. Kutoka kwa Abu Hurairah na Zaid bin Khalid kwamba walisema: Mwanamume mmoja katika mabedui alimjia Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) akasema: "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, nakuomba kwa jina la Mwenyezi Mungu unihukumu kwa Kitabu cha Mwenyezi Mungu." Na mwenzake ambaye alikuwa mwelewa zaidi akasema: "Ndiyo, tuhukumu kwa Kitabu cha Mwenyezi Mungu na niruhusu niseme." Mtume (saw) akasema: "Sema." Akasema: "Hakika mwanangu alikuwa kibarua kwa huyu, akazini na mke wake, nami nikaambiwa kuwa mwanangu anapaswa kupigwa mawe, nikalipa fidia ya kondoo mia moja na mtumishi mwanamke mmoja. Kisha nikawauliza watu wa elimu wakaniambia kuwa mwanangu anapaswa kupigwa mijeledi mia moja na kufukuzwa nchi mwaka mmoja, na kwamba mke wa huyu anapaswa kupigwa mawe." Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) akasema: “Naapa kwa Yule ambaye nafsi yangu imo mkononi Mwake, nitahukumu baina yenu kwa Kitabu cha Mwenyezi Mungu; yule mtumishi mwanamke na kondoo warudishwe kwako, na mwanao apigwe mijeledi mia moja na kufukuzwa nchi mwaka mmoja. Na nenda ewe Unais – kwa mwanamume kutoka kabila la Aslam – kwa mke wa huyu, akiri basi mpige mawe.” Akasema: Akamwendea naye akakiri, Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) akaamuru apigwe mawe, akapigwa mawe. Na al-asif ni kibarua. Hapa Mtume aliamuru kupigwa mawe kwa muhsan na hakumpiga mijeledi. Na kutoka kwa Al-Sha’bi “kwamba Ali (ra) alipompiga mawe mwanamke alimpiga mijeledi siku ya Alhamisi, na akampiga mawe siku ya Ijumaa, akasema: Nime mpiga mijeledi kwa Kitabu cha Mwenyezi Mungu na nime mpiga mawe kwa Sunnah ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw)”. Na kutoka kwa Ubada bin al-Samit amesema: Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema: “Chukueni kutoka kwangu, chukueni kutoka kwangu, hakika Mwenyezi Mungu ameshawafanyia njia; bikira kwa bikira (ambao hawajawahi kuoa/kuolewa) ni mijeledi mia moja na kufukuzwa nchi mwaka mmoja, na aliyewahi kuoa/kuolewa kwa aliyewahi kuoa/kuolewa ni mijeledi mia moja na kupigwa mawe.” Hapa Mtume anasema kuwa adhabu ya muhsan ni mijeledi na kupigwa mawe, na Ali anampiga mijeledi muhsan na kumpiga mawe. Na kutoka kwa Jabir bin Samurah kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) alimpiga mawe Ma’iz bin Malik na hakutaja mijeledi. Na katika Bukhari kutoka kwa Sulayman bin Buraidah kwamba Mtume (saw) alimpiga mawe mwanamke wa Al-Ghamidiyyah na hakutaja mijeledi. Na katika Muslim kwamba Mtume (saw) aliamuru kuhusu mwanamke wa Juhayna, yakafungwa nguo zake vizuri kisha akaamuru apigwe mawe, na hakutaja mijeledi. Hiyo inaonyesha kuwa Mtume alimpiga mawe muhsan na hakumpiga mijeledi, na kwamba alisema: “Aliyewahi kuoa/kuolewa kwa aliyewahi kuoa/kuolewa ni mijeledi mia moja na kupigwa mawe.” Hiyo inaonyesha kuwa kupigwa mawe ni wajibu, ama mijeledi ni jambo linalojuzu, na linaachiwa maoni ya Khalifa. Na hakika imefanywa mijeledi kuwa miongoni mwa hadd ya muhsan pamoja na kupigwa mawe ili kukusanya baina ya Hadith hizi. Wala haisemwi kuwa Hadith ya Samurah ya kwamba (saw) hakumpiga mijeledi Ma’iz, bali aliishia kumpiga mawe tu, ni yenye kufuta (nasikh) Hadith ya Ubada bin al-Samit inayosema: “Aliyewahi kuoa/kuolewa kwa aliyewahi kuoa/kuolewa ni mijeledi mia moja na kupigwa mawe”. Haisemwi hivyo kwa sababu haijathibiti chenye kuonyesha kuchelewa kwa Hadith ya Ma’iz kuliko Hadith ya Ubada, na bila ya kuthibiti kuchelewa kwake, basi kutoitaja mijeledi hakupelekei kuibatilisha, na kufuta hukumu yake. Hivyo, kutokuthibiti cha kwanza na cha pili miongoni mwa Hadith hizo mbili kunakanusha kufutwa kwa hukumu (naskh), na hakuna chenye kutoa upendeleo kwa moja juu ya nyingine. Na yale yaliyokuja katika Hadith miongoni mwa ziada juu ya kupigwa mawe yanachukuliwa kuwa ni jambo linalojuzu na si wajibu, kwani wajibu ni kupigwa mawe, na yale yaliyozidi juu ya hapo basi Imam ana hiyari nayo ili kukusanya baina ya Hadith...] Mwisho wa nukuu kutoka kitabu cha Nidham al-Uqubat.
Muhtasari: Adhabu ya mzinifu muhsan ni kupigwa mawe hadi kufa (rajm), na dalili sahihi na thabiti kutoka katika Sunnah ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) katika Sahih mbili (Bukhari na Muslim) na katika vitabu vingine vya Hadith zimeonyesha hivyo, na ni adhabu iliyoingia katika Hudud na si katika mlango wa Ta’zir.
Mwenyezi Mungu Mtukufu ndiye Mjuzi zaidi na Mwenye Hekima zaidi.
Ndugu yenu Ata bin Khalil Abu Al-Rashtah
12 Muharram 1441 H Sawia na 11/09/2019 M
Link ya jibu kutoka ukurasa wa Amir (Mungu amuhifadhi) kwenye Facebook Link ya jibu kutoka ukurasa wa Amir (Mungu amuhifadhi) kwenye Tovuti