(Silsila ya Majibu ya Mwanachuoni Mtukufu Ata Bin Khalil Abu Al-Rashta, Amir wa Hizb ut-Tahrir, kwa Maswali ya Wafuasi wa Ukurasa Wake wa Facebook "Fiqhi")
Kwa Ahmed bin Hussein
Swali:
Salamu zangu na heshima kwako Sheikh wetu mtukufu. Assalamu Alaikum wa Rahmatullahi wa Barakatuh,
Swali langu: Nilitaka kununua baadhi ya bidhaa kwa awamu (taksiti), lakini nikakumbwa na shaka; nayo ni kwamba katika hali ya kuchelewa kulipa na wanapoingia kwenye akaunti yangu ya posta na kukosa fungu lao la mwezi, wanakata kiasi kidogo cha pesa.
Kwa mfano, ikiwa makubaliano ni kwamba kila mwanzo wa mwezi kakatwe kiasi cha kawaida kilichokubaliwa, lakini kiasi kidogo (dola mbili au tatu) kinakatwa ikiwa wataingia tarehe 2 au 3 na wasikute pesa zao, na jambo hili hufanyika kiotomatiki na linaweza kutokea zaidi ya mara moja kwa siku.
Fahamu kuwa nilipopitia vipengele vya mkataba wa mauzo ya awamu, sharti hili halipo, lakini hufanyika kiotomatiki katika hali ya kuchelewa kulipa. Je, inanijuzia kufunga mkataba huo na kununua mahitaji yangu kukiwa na makato hayo ya kiotomatiki katika hali ya kuchelewa kulipa?
Mwenyezi Mungu akulipe kheri.
Jawabu:
Wa Alaikum Salaam wa Rahmatullahi wa Barakatuh.
Ewe ndugu yangu, swali limenitatiza kidogo. Unasema unataka kununua kwa awamu kisha unaongeza kuwa wanapoingia kwenye akaunti yako ya posta na kukosa fungu lao la mwezi wanakata kiasi cha pesa... Jambo hili haliko wazi. Ninachokijua na ambacho nimeshawahi kuulizwa huko nyuma ni kuwa kuna watu wanaofungua akaunti ya benki, kisha huchukua kadi kutoka benki ambayo huitumia kununua bidhaa kwenye maduka yaliyokubaliwa, na mfanyabiashara huchukua thamani ya bidhaa iliyouzwa kutoka kwenye akaunti ya mteja iliyo benki. Ikiwa akaunti ina pesa, benki humlipa thamani ya manunuzi hayo, na ikiwa kiasi hicho hakipo kwenye akaunti, benki humlipia mfanyabiashara lakini huchukua kiasi fulani cha ziada kutoka kwa mwenye akaunti kama malipo ya huduma hiyo. Ikiwa hiki ndicho unachomaanisha, basi kadi hiyo anayopewa mwenye akaunti inaangukia kwenye mlango wa kadi za mikopo (credit cards)... Na tulishawahi kuulizwa swali kama hili na tukalijibu mnamo tarehe 11/07/2006, na yafuatayo ni matini ya jawabu letu hilo:
(Kadi za mikopo ziko za aina mbalimbali:
- Aina mojawapo ni ile ambayo mbeba kadi anakuwa na akaunti yenye kiasi fulani cha pesa katika benki iliyotoa kadi hiyo, kisha mbeba kadi hufanya manunuzi kwayo kwa kiasi kisichozidi kiasi kilichopo kwenye akaunti yake kutoka kwenye maduka shiriki katika nchi mbalimbali. Mbeba kadi hununua kutoka kwenye maduka haya bila kulipa pesa taslimu, bali huonyesha kadi na kutia saini nyaraka zenye thamani ya manunuzi yake, kisha duka huielekeza benki iliyotoa kadi kuchukua thamani ya manunuzi kutoka kwenye akaunti ya mbeba kadi. Yaani, benki humlipia mfanyabiashara thamani ya bidhaa kutoka kwenye akaunti ya mbeba kadi (mnunuzi).
Aina hii ya kadi inajuzu, na uhalisia wake ni (hawala na wakala). Mnunuzi anamuelekeza muuzaji (hawala) kwa benki iliyotoa kadi, na benki hiyo hufanya kazi kama wakala wa mnunuzi kumlipa muuzaji thamani ya manunuzi kutoka kwenye akaunti ya mnunuzi iliyo benki. Kile ambacho benki hukichukua kutoka kwa mnunuzi (mbeba kadi) badala ya kumlipia muuzaji thamani ya bidhaa huhesabika kuwa ni ujira wa uwakala (ujratul wakala).
Hata hivyo, kile wanachokifanya wabeba kadi hawa cha kununua dhahabu na fedha bila kulipa thamani yake hapo hapo, na kumuelekeza muuzaji kwenye benki ili akapokee malipo, kitendo hiki ni haramu. Hii ni kwa sababu kupeana hapo hapo (taqabudh al-fawri) (mkono kwa mkono) ni sharti katika usahihi wa mauzo ya dhahabu na fedha, vinginevyo itakuwa ni riba.
Haya yote ni ikiwa benki ni taasisi binafsi iliyoanzishwa kwa mkataba sahihi kati ya washirika wake, au inamilikiwa na dola; katika hali hiyo aina hii ya kadi inajuzu.
- Aina ya pili ya kadi hutolewa na benki kwa wateja wake bila wao kuwa na akaunti yenye salio la kutosha kugharamia manunuzi yao. Mbeba kadi hufanya manunuzi kutoka kwenye maduka shiriki na kutia saini nyaraka ambazo duka huchukulia malipo kutoka kwa benki iliyotoa kadi. Kisha benki huandika kiasi hicho kama deni kwa mwenye kadi, ikiongeza na kiasi cha ziada ambacho benki hukitoza kwa mbeba kadi kulingana na mpangilio wa malipo ya awamu fulani.
Uhalisia wa kadi hizi ni kwamba ni dhamana (dhamaan) kutoka kwa benki kwa mnunuzi mbele ya maduka, yaani benki inamdhamini mnunuzi, na maduka yanamuuzia mbeba kadi kwa dhamana ya benki. Hivyo benki iliyotoa kadi ndiyo inayolipa thamani ya manunuzi, yaani kadi ni hati ya dhamana kutoka kwa benki. Katika hili, benki ndiye (mdhamini - dhaamin), mnunuzi mbeba kadi ndiye (mdhaminiwa - madhmun 'anhu), duka la muuzaji ndilo (mwenye kudhaminiwa - madhmun lahu), na thamani ya manunuzi ndiyo (haki ya lazima katika dhima ya mnunuzi).
Hata hivyo, dhamana hii haijatimiza masharti yake ya kisheria (shar'iy). Hii ni kwa sababu dhamana katika Uislamu ni kuunganisha dhima moja na dhima nyingine ili kulipa haki iliyo wajibu juu ya dhima hiyo bila malipo ya ziada (mu'awadha). Mdhamini hulipa haki iliyo wajibu katika dhima ya mdhaminiwa kwenda kwa mwenye kudhaminiwa bila kuchukua malipo ya ziada, lakini benki hulipa thamani ya manunuzi mkabala wa malipo fulani ya ziada. Kwa sababu hiyo, kadi hizi hazijuzu kisheria kwa upande huu, mbali na ukweli kwamba benki huandika thamani ya manunuzi kama deni kwa mnunuzi na kulitoza kwake likiwa na ziada, yaani kwa riba. Hivyo, kadi hizo hazijuzu kisheria pia kwa upande huu.) Mwisho.
Ikiwa hiki ndicho unachomaanisha katika swali lako, basi jawabu hapo juu linatosheleza. Ama ikiwa sivyo unavyomaanisha, basi rudia kuelezea swali lako kwa ufafanuzi wa kutosha ili tuliangalie jawabu lake InshaAllah.
Ndugu yenu, Ata Bin Khalil Abu Al-Rashta
10 Rajab 1439 H Inayosadifiana na 28/03/2018 M
Kiungo cha jawabu kutoka kwenye ukurasa wa Amir (Mwenyezi Mungu amhifadhi) kwenye Facebook
Kiungo cha jawabu kutoka kwenye ukurasa wa Amir (Mwenyezi Mungu amhifadhi) kwenye Google Plus
Kiungo cha jawabu kutoka kwenye ukurasa wa Amir (Mwenyezi Mungu amhifadhi) kwenye Twitter
Kiungo cha jawabu kutoka kwenye ukurasa wa Amir (Mwenyezi Mungu amhifadhi) Wavuti