Mfululizo wa Majibu ya Mwanachuoni Mtukufu Ata Bin Khalil Abu Al-Rashta, Amir wa Hizb ut Tahrir
kwa Maswali ya Wageni wa Ukurasa Wake wa Facebook "Fiqhi"
Kwa Salah Fawzi
Swali:
Assalamu Alaikum wa Rahmatullahi wa Barakatuh
Ndugu yangu mpendwa, salamu za heri baada ya hayo,
Imeelezwa katika kitabu cha Mukaddimat ud-Dustur Jz 1 / Ibara ya 95 yafuatayo:
"Ama kuhusu kufungua mashitaka dhidi ya wale walioudhi Uislamu na Waislamu, ni kwa sababu Mtume ﷺ alipofungua Makka, alihalalisha damu ya kundi la watu waliokuwa wakiudhi Uislamu na Waislamu wakati wa Jahiliyyah; alihalalisha damu yao hata kama wangejishikiza kwenye mapazia ya Al-Kaaba, ikijulikana kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu alisema: 'Hakika Uislamu unafuta yaliyotangulia kabla yake' (Imepokelewa na Ahmad na At-Tabarani kutoka kwa Amr bin Al-Aas), yaani, yule aliyeudhi Uislamu na Waislamu anavuliwa (hapotei hukumu yake) katika hadithi hii."
Nimefanya utafiti kuhusu hali ya watu hao na nimegundua kuwa baadhi yao walikuwa Waislamu kisha wakaritadi, na wengine hawakusilimu na wakauawa. Kwa yule aliyekuwa Muislamu na akartadi, msingi ni kuwa aadhibiwe kwa kuritadi kwake, na aliyebaki kwenye ushirikina wake na akawa miongoni mwa walioudhi Uislamu na Waislamu, aliadhibiwa kwa kuuawa au kusamehewa kulingana na uamuzi wa Imam wa Waislamu kama ilivyoelezwa katika ibara hiyo. Lakini katika hali zote mbili, hadithi ya "Uislamu unafuta yaliyotangulia" haitumiki kwao, kwa sababu tunavyojua ni kwamba "Uislamu unafuta yaliyotangulia" inatumika kwa yule aliyesilimu hivi karibuni. Hivyo, kwa nini hadithi hii imetumiwa kama ushahidi katika ibara hii, ikijulikana kuwa baadhi ya Maswahaba walitumia upanga na kuua Waislamu (kabla ya kusilimu kwao) kama Khalid bin Walid na Wahshi bin Harb (ra) na Mtume ﷺ hakuwafanya lolote baada ya kusilimu kwao?
Mwenyezi Mungu awabarikie, aongoze hatua zenu, na ajaalie ushindi upatikane kupitia mikono yenu.
Salah Fawzi - Al-Quds Al-Sharif
Jibu:
Wa Alaikum Salaam wa Rahmatullahi wa Barakatuh,
Inaonekana kuna mkanganyiko katika kuelewa suala hili. Hadithi ya Mtume ﷺ aliyoipokea Ahmad na At-Tabarani kutoka kwa Amr bin Al-Aas:
إِنَّ الإِسْلامَ يَجُبُّ مَا كَانَ قَـبْلَهُ
"Hakika Uislamu unafuta yaliyotangulia kabla yake."
Inaonesha kuwa yule anayesilimu miongoni mwa makafiri, basi yale aliyoyafanya kabla ya Uislamu yanachukuliwa kana kwamba hayakuwepo, yaani hahesabiwi kwa yale aliyoyafanya kabla ya Uislamu. Kuingia kwake katika Uislamu kunafuta dhambi alizofanya kabla ya Uislamu kwa sababu Uislamu unabomoa yaliyotangulia... Lakini kitendo cha Mtume ﷺ wakati wa ufunguzi wa Makka (kuhalalisha damu ya kundi la watu waliokuwa wakiudhi Uislamu na Waislamu wakati wa Jahiliyyah, na kuhalalisha damu yao hata kama wangejishikiza kwenye mapazia ya Al-Kaaba), inaeleweka kutokana na hili kuwa wanabaki kuwajibika kwa yale waliyowaudhi kwayo Waislamu, hata kama wangesilimu. Hii ni kwa sababu kauli ya Mtume ﷺ: (hata kama wangejishikiza kwenye mapazia ya Al-Kaaba) inaonesha kuwa Mtume ﷺ hakuvua hali ya wao kuingia katika Uislamu, bali aliamrisha kuuawa kwao katika kila hali. Tulielewa kutokana na hilo kuwa wale wanaoudhi Uislamu na Waislamu wanaadhibiwa kwa yale wanayoyafanya hata kama wataingia katika Uislamu. Hivyo basi, hadithi ya Mtume ﷺ: "Hakika Uislamu unafuta yaliyotangulia" haiwahusu wao; wao wamevuliwa (hawamo) katika hadithi hii. Maana yake ni kwamba uadui wao kwa Uislamu na Waislamu haufutwi na Uislamu, bali wanawajibika kwayo, na jambo lao baada ya hapo linarudi kwa Imam; akitaka anawasamehe na akitaka anawaadhibu.
Inathibitisha usahihi wa uelewa huu yale aliyoyapokea An-Nasai katika Sunan yake kutoka kwa Mus'ab bin Sa'd, kutoka kwa baba yake, amesema:
لَمَّا كَانَ يَوْمُ فَتْحِ مَكَّةَ أَمَّنَ رَسُولُ اللَّهِ ﷺ النَّاسَ إِلَّا أَرْبَعَةَ نَفَرٍ وَامْرَأَتَيْنِ وَقَالَ اقْتُلُوهُمْ وَإِنْ وَجَدْتُمُوهُمْ مُتَعَلِّقِينَ بِأَسْتَارِ الْكَعْبَةِ عِكْرِمَةُ بْنُ أَبِي جَهْلٍ وَعَبْدُ اللَّهِ بْنُ خَطَلٍ وَمَقِيسُ بْنُ صُبَابَةَ وَعَبْدُ اللَّهِ بْنُ سَعْدِ بْنِ أَبِي السَّرْحِ فَأَمَّا عَبْدُ اللَّهِ بْنُ خَطَلٍ فَأُدْرِكَ وَهُوَ مُتَعَلِّقٌ بِأَسْتَارِ الْكَعْبَةِ فَاسْتَبَقَ إِلَيْهِ سَعِيدُ بْنُ حُرَيْثٍ وَعَمَّارُ بْنُ يَاسِرٍ فَسَبَقَ سَعِيدٌ عَمَّاراً وَكَانَ أَشَبَّ الرَّجُلَيْنِ فَقَتَلَهُ وَأَمَّا مَقِيسُ بْنُ صُبَابَةَ فَأَدْرَكَهُ النَّاسُ فِي السُّوقِ فَقَتَلُوهُ وَأَمَّا عِكْرِمَةُ فَرَكِبَ الْبَحْرَ فَأَصَابَتْهُمْ عَاصِفٌ فَقَالَ أَصْحَابُ السَّفِينَةِ أَخْلِصُوا فَإِنَّ آلِهَتَكُمْ لَا تُغْنِي عَنْكُمْ شَيْئاً هَاهُنَا فَقَالَ عِكْرِمَةُ وَاللَّهِ لَئِنْ لَمْ يُنَجِّنِي مِنْ الْبَحْرِ إِلَّا الْإِخْلَاصُ لَا يُنَجِّينِي فِي الْبَرِّ غَيْرُهُ اللَّهُمَّ إِنَّ لَكَ عَلَيَّ عَهْداً إِنْ أَنْتَ عَافَيْتَنِي مِمَّا أَنَا فِيهِ أَنْ آتِيَ مُحَمَّداً ﷺ حَتَّى أَضَعَ يَدِي فِي يَدِهِ فَلَأَجِدَنَّهُ عَفُوّاً كَرِيماً فَجَاءَ فَأَسْلَمَ وَأَمَّا عَبْدُ اللَّهِ بْنُ سَعْدِ بْنِ أَبِي السَّرْحِ فَإِنَّهُ اخْتَبَأَ عِنْدَ عُثْمَانَ بْنِ عَفَّانَ فَلَمَّا دَعَا رَسُولُ اللَّهِ ﷺ النَّاسَ إِلَى الْبَيْعَةِ جَاءَ بِهِ حَتَّى أَوْقَفَهُ عَلَى النَّبِيِّ ﷺ قَالَ يَا رَسُولَ اللَّهِ بَايِعْ عَبْدَ اللَّهِ قَالَ فَرَفَعَ رَأْسَهُ فَنَظَرَ إِلَيْهِ ثَلَاثاً كُلَّ ذَلِكَ يَأْبَى فَبَايَعَهُ بَعْدَ ثَلَاثٍ ثُمَّ أَقْبَلَ عَلَى أَصْحَابِهِ فَقَالَ أَمَا كَانَ فِيكُمْ رَجُلٌ رَشِيدٌ يَقُومُ إِلَى هَذَا حَيْثُ رَآنِي كَفَفْتُ يَدِي عَنْ بَيْعَتِهِ فَيَقْتُلُهُ فَقَالُوا وَمَا يُدْرِينَا يَا رَسُولَ اللَّهِ مَا فِي نَفْسِكَ هَلَّا أَوْمَأْتَ إِلَيْنَا بِعَيْنِكَ قَالَ إِنَّهُ لَا يَنْبَغِي لِنَبِيٍّ أَنْ يَكُونَ لَهُ خَائِنَةُ أَعْيُنٍ
"Ilipofika siku ya ufunguzi wa Makka, Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ aliwapa watu amani isipokuwa watu wanne na wanawake wawili, akasema: 'Waueni hata mkiwakuta wamejishikiza katika mapazia ya Al-Kaaba: Ikrimah bin Abi Jahl, Abdullah bin Khatal, Maqis bin Subabah, na Abdullah bin Sa'd bin Abi Al-Sarh.' Ama Abdullah bin Khatal, alikamatwa akiwa amejishikiza kwenye mapazia ya Al-Kaaba, Said bin Huraith na Ammar bin Yasir wakakimbilia kumuua, Said akamtangulia Ammar naye alikuwa kijana zaidi kati yao, akamuua. Ama Maqis bin Subabah, watu walimkuta sokoni wakamuua. Ama Ikrimah, alipanda chombo baharini akakumbwa na dhoruba kali, wenye chombo wakasema: 'Ikhlasini (mwombeni Mungu mmoja) kwani miungu yenu haitawafaa kitu hapa.' Ikrimah akasema: 'Wallahi, ikiwa hakuna kitakachoniokoa baharini isipokuwa Ikhlas, basi hakuna kitakachoniokoa nchi kavu isipokuwa hiyo. Ee Mwenyezi Mungu, naweka ahadi Kwako kwamba ukiniokoa na hali niliyo nayo, nitamwendea Muhammad ﷺ mpaka niweke mkono wangu mkononi mwake, na hakika nitamkuta ni mwenye kusamehe na mkarimu.' Akaja na akasilimu. Ama Abdullah bin Sa'd bin Abi Al-Sarh, alijificha kwa Uthman bin Affan, na Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ alipowaita watu kutoa Bay'ah, Uthman alimleta na kumsimamisha mbele ya Mtume ﷺ akasema: 'Ee Mtume wa Mwenyezi Mungu, mpe Bay'ah Abdullah.' Mtume akainua kichwa chake na kumtazama mara tatu, na kila mara alikuwa akikataa, kisha akampa Bay'ah baada ya mara ya tatu. Kisha akawageukia maswahaba zake akasema: 'Je, hakuwa miongoni mwenu mtu mwenye busara ambaye angemsimamia huyu alipoona nimezuia mkono wangu kumpa Bay'ah na akamuua?' Wakasema: 'Tujuaje ee Mtume wa Mwenyezi Mungu yaliyomo nafsini mwako, kwa nini usituashirie kwa jicho lako?' Akasema: 'Haimpasi Mtume kuwa na ishara ya jicho ya hiana (khainat ul-a'yun).'" (Imepokelewa na An-Nasai)
Hivyo basi, Mtume ﷺ alitaka Waislamu wamuue Abdullah bin Abi Sarh ingawa alikuja kwake akiwa Muislamu akiomba Bay'ah. Hii inaonesha kuwa kuhalalishwa kwa damu ya kundi hili kulikuwa kwa ujumla, na kuingia kwao katika Uislamu hakuwakingi na adhabu hiyo lazima, bali jambo lao linarudi kwa Imam; akitaka anawaadhibu na akitaka anawasamehe... Kwa msingi huu, kutokuadhibiwa kwa baadhi ya wale waliosilimu miongoni mwa makafiri waliokuwa wakiwaudhi Waislamu, kama ilivyotokea kwa Ikrimah bin Abi Jahl kwa mfano, kunaingia chini ya msamaha wa Imam kama ilivyoelezwa katika kitabu cha Al-Ajhiza: "Na kwa kuwa Mtume ﷺ aliwasamehe baadhi yao baadaye kama alivyomsamehe Ikrimah bin Abi Jahl; kwa hiyo inaruhusiwa kwa Khalifah kufungua kesi dhidi ya watu hao au kuwasamehe."
Natumai mkanganyiko katika kuelewa suala hili umeondoka.
Ndugu yenu, Ata Bin Khalil Abu Al-Rashta
17 Rabi'ul Awwal 1445 H Sawa na 02/10/2023 M
Link ya jibu kutoka ukurasa wa Amir (Mwenyezi Mungu amhifadhi) kwenye Facebook: Facebook