Mfululizo wa majibu ya mwanachuoni mtukufu Ata bin Khalil Abu al-Rashtah, Amir wa Hizb ut-Tahrir
kwa maswali ya wafuasi wa ukurasa wake wa Facebook "Fiqhi"
Jibu la Swali
Kwa Al-Rayahi Abu Fatima
Swali:
Ndugu yangu katika Imani, Amir wa Hizb ut-Tahrir, Assalamu Alaikum Warahmatullahi Wabarakatuh.
Je, ni upi usahihi wa Hadithi hii, na ikiwa ni sahihi tunaomba utoe ufafanuzi, na Mwenyezi Mungu akujazi kila la kheri.
Hadithi ya Al-Zubayr bin Adi (r.h) amesema: "Tulimwendea Anas bin Malik (r.a) tukamlalamikia yale tuliyokuwa tukiyapata kutoka kwa Al-Hajjaj, akasema: 'Subirini, kwani hakika hakitakuja kwenu zama yoyote isipokuwa ile itakayofuata baada yake ni mbaya zaidi kuliko hiyo, mpaka mtakapokutana na Mola wenu. Niliisikia (Hadithi hii) kutoka kwa Mtume wenu ﷺ'." Imepokewa na Al-Bukhari.
Jibu:
Mwanzoni, nakumbusha mambo mawili katika misingi (Usul) ili kufafanua jibu:
1- Ikiwa katika dalili kuna utata wa kugongana, basi hufanywa juhudi za kuoanisha kati ya dalili hizo (al-jam'u), kwa sababu kuzitumia dalili zote mbili ni bora kuliko kuipuuza mojawapo.
2- Ikiwa kuoanisha kumeshindikana, basi hufanywa juhudi za kupima uzito (al-tarjih) kati ya dalili hizo kulingana na kanuni za kupima uzito.
Sasa tunajibu swali:
Al-Bukhari ametoa kutoka kwa Al-Zubayr bin Adi, amesema: Tulimwendea Anas bin Malik, tukamlalamikia yale tuliyokuwa tukiyapata kutoka kwa Al-Hajjaj, akasema:
اصْبِرُوا، فَإِنَّهُ لاَ يَأْتِي عَلَيْكُمْ زَمَانٌ إِلَّا الَّذِي بَعْدَهُ شَرٌّ مِنْهُ، حَتَّى تَلْقَوْا رَبَّكُمْ
"Subirini, kwani hakika hakitakuja kwenu zama yoyote isipokuwa ile itakayofuata baada yake ni mbaya zaidi kuliko hiyo, mpaka mtakapokutana na Mola wenu." Niliisikia kutoka kwa Mtume wenu ﷺ.
Hadithi hii inafahamisha kuwa kila zama ni mbaya zaidi kuliko ile iliyotangulia.
Hadithi hii ina utata wa kugongana na Hadithi nyinginezo:
a- Ina utata wa kugongana na Hadithi ya kurejea kwa Khilafah, ambayo ni kheri kuliko utawala wa kidikteta (Mulk Jabri) uliotangulia kabla yake:
Ahmad ametoa katika Musnad yake kutoka kwa Hudhayfah bin al-Yaman amesema: Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ amesema:
ثُمَّ تَكُونُ مُلْكاً جَبْرِيَّةً فَتَكُونُ مَا شَاءَ اللَّهُ أَنْ تَكُونَ ثُمَّ يَرْفَعُهَا إِذَا شَاءَ أَنْ يَرْفَعَهَا ثُمَّ تَكُونُ خِلَافَةً عَلَى مِنْهَاجِ النُّبُوَّةِ
"...kisha utakuwepo utawala wa kidikteta (Mulk Jabri) na utakuwepo kwa muda anaoutaka Mwenyezi Mungu, kisha Atauondoa Atakapotaka Kuuondoa, kisha itakuwepo Khilafah kwa njia ya Utume." Kisha akanyamaza. (HR Ahmad)
b- Na pia Hadithi ya kudhihiri kwa Al-Mahdi (kutoka katika nyumba ya Mtume ﷺ) ambaye ataijaza ardhi uadilifu baada ya dhulma iliyotangulia:
Al-Tabarani ametoa katika al-Mu'jam al-Kabir kutoka kwa Abdullah bin Mas'ud (r.a) amesema: Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ amesema:
لا تَقُومُ السَّاعَةُ حَتَّى يَمْلِكَ رَجُلٌ مِنْ أَهْلِ بَيْتِي، يُوَاطِئُ اسْمُهُ اسْمِي، يَمْلأُ الأَرْضَ عَدْلاً وَقِسْطاً كَمَا مُلِئَتْ ظُلْماً وَجَوْراً
"Kiyama hakitasimama mpaka atawale mtu kutoka katika watu wa nyumba yangu, jina lake linaoana na jina langu, ataijaza ardhi uadilifu na usawa kama ilivyojazwa dhulma na uonevu." (HR Tabarani)
c- Na kadhalika utata wa kugongana na Hadithi ya kushuka kwa Issa (a.s) baada ya kuwepo kwa shari ya Dajjal iliyotangulia kabla yake:
Al-Tabarani ametoa katika al-Kabir kutoka kwa Samurah bin Jundub (r.a) amesema: Nabii ﷺ amesema:
إِنَّ الْمَسِيحَ الدَّجَّالَ يَلْبَثُ فِي الأَرْضِ مَا شَاءَ اللَّهُ، ثُمَّ يَجِيءُ عِيسَى ابْنُ مَرْيَمَ صَلَّى اللُّه عَلَيْهِ مِنَ الْمَشْرِقِ، مُصَدِّقاً بِمُحَمَّدٍ ﷺ وَعَلَى مِلَّتِهِ، ثُمَّ يَقْتُلُ الْمَسِيحَ الدَّجَّالَ
"Hakika Masihi Dajjal atakaa ardhini kwa muda anaoutaka Mwenyezi Mungu, kisha atakuja Issa bin Maryam ﷺ kutokea upande wa mashariki, akiwa mwenye kumsadikisha Muhammad ﷺ na akiwa juu ya dini yake, kisha atamuua Masihi Dajjal." (HR Tabarani)
Hivyo basi, Hadithi isemayo "kila zama ni mbaya zaidi kuliko iliyotangulia" ina utata wa kugongana na Hadithi hizi ambazo zinafahamisha kuwa zama zake ni kheri kuliko zile zilizotangulia na si mbaya zaidi... Na kama nilivyotaja hapo awali, ikiwa inawezekana kuoanisha basi ndiyo bora zaidi, vinginevyo hufanywa juhudi za kupima uzito (tarjih).
Kwa kuzizingatia Hadithi hizi, inabainika kuwa inawezekana kuoanisha kwa kufahamu Hadithi ya Al-Bukhari (kila zama ni mbaya zaidi kuliko iliyotangulia) si kwa ujumla wake bali ni mahususi kwa hali zisizokuwa zile zilizotajwa hapo juu, yaani kabla ya kurejea kwa Khilafah Rashidah ya pili kwa njia ya Utume... Na kana kwamba hili linaafikiana na Hadithi ya Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ aliyoitoa Al-Bukhari:
عَنْ النَّبِيِّ ﷺ قَالَ: خَيْرُ النَّاسِ قَرْنِي ثُمَّ الَّذِينَ يَلُونَهُمْ ثُمَّ الَّذِينَ يَلُونَهُمْ ثُمَّ يَجِيءُ مِنْ بَعْدِهِمْ قَوْمٌ تَسْبِقُ شَهَادَتُهُمْ أَيْمَانَهُمْ وَأَيْمَانُهُمْ شَهَادَتَهُمْ
Kutoka kwa Nabii ﷺ amesema: "Bora ya watu ni karne yangu, kisha wale wanaowafuata, kisha wale wanaowafuata, kisha watakuja baada yao watu ambao ushahidi wao unatangulia viapo vyao na viapo vyao vinatangulia ushahidi wao." (HR Bukhari)
Pia Muslim ameitoa kwa tamshi: "Bora ya watu ni karne yangu kisha wale wanaowafuata kisha wale wanaowafuata – sijui katika ya tatu au ya nne amesema – kisha watakuja baada yao watu ambao ushahidi wa mmoja wao unatangulia kiapo chake na kiapo chake kinatangulia ushahidi wake." Na Ibn Abi Shaybah ametoa katika Musannaf yake kutoka kwa Abi Burdah kutoka kwa baba yake amesema: Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ amesema:
وَأَصْحَابِي أَمَنَةٌ لِأُمَّتِي فَإِذَا ذَهَبَ أَصْحَابِي أَتَى أُمَّتِي مَا يُوعَدُونَ
"Na maswahaba wangu ni ulinzi kwa Umma wangu, watakapoondoka maswahaba wangu, yataufika Umma wangu yale waliyoahidiwa."
Na hivyo basi, kila zama inapokuwa karibu zaidi na Mtume wa Mwenyezi Mungu na maswahaba wake, ndivyo kheri inavyokuwa nyingi zaidi na shari inakuwa mbali zaidi, mpaka itakaporejea Khilafah Rashidah upya, basi kheri itarejea ndani yake badala ya shari iliyokuwepo kabla yake katika utawala wa kidikteta.
Na bila shaka, kinachokusudiwa katika kila zama ni kile kinachotawala zaidi (al-ghalib) ndani yake na si kudhihiri kwa watu mmoja mmoja walio tofauti na hali hiyo ya jumla. Kwa mfano, Khalifa Umar bin Abdul Aziz alikuwa katika uadilifu wake tofauti na makhalifa wengine wa Bani Umayya, kisha baadhi ya makhalifa katika zama za Abbasia na Othmania mpaka Khilafah ilipoishia 1342 H - 1924 M, na kufuatiwa na shari kubwa ya utawala wa kidikteta, na baada yake itarejea Khilafah kwa njia ya Utume upya na kheri itang'ara pamoja nayo.
وَيَوْمَئِذٍ يَفْرَحُ الْمُؤْمِنُونَ * بِنَصْرِ اللَّهِ يَنْصُرُ مَنْ يَشَاءُ وَهُوَ الْعَزِيزُ الرَّحِيمُ
"Na siku hiyo waumini watafurahi * Kwa nusura ya Mwenyezi Mungu. Yeye humnusuru amtakaye, Naye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu." (QS Ar-Rum [30]: 4-5)
Hili ndilo ninalolipa uzito katika suala hili, na Mwenyezi Mungu ndiye Mjuzi zaidi na Mwenye Hekima zaidi.
Ndugu yenu Ata bin Khalil Abu al-Rashtah
13 Rabi’ al-Akhir 1443 H Muwafaka 18/11/2021 M
Link ya jibu kutoka ukurasa wa Amir (Mwenyezi Mungu amuhifadhi) kwenye Facebook
Link ya jibu kutoka ukurasa wa Amir (Mwenyezi Mungu amuhifadhi) kwenye Web