Mfululizo wa majibu ya mwanachuoni mtukufu Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah, Amiri wa Hizb ut-Tahrir, kwa maswali ya wafuasi wa ukurasa wake wa Facebook "Fiqhi"
Jibu la Swali
Kwa Abu Sabih Faisal
Swali:
Assalamu Alaikum Wa Rahmatullahi Wa Barakatuh
Je, ni kweli kwamba Hijra ya Mtume (saw) ilikuwa katika mwezi wa Rabi' al-Awwal? Na ikiwa ni hivyo, mbona Waislamu huadhimisha mwanzo wa mwaka wa Hijria na siku ya Hijra ya Mtume katika mwezi wa Muharram?
Jibu:
Walaikum Assalam Wa Rahmatullahi Wa Barakatuh
Ndiyo, Hijra ilikuwa tarehe kumi na mbili ya Rabi' al-Awwal... Lakini baada ya kupita takriban miaka kumi na saba tangu Hijra ya Mtume ﷺ, katika mwaka wa tatu au wa nne wa utawala wa Umar (ra)... Abu Musa al-Ash'ari, ambaye alikuwa Gavana wa Basra wakati huo, alimtumia barua akimwomba atafute njia mpya ya kupanga kalenda. Hii ilitokea baada ya Abu Musa al-Ash'ari kupokea barua iliyokuwa na tarehe ya mwezi wa "Sha'ban" bila kubainisha mwaka. Hivyo, Al-Ash'ari alimwandikia Khalifah Umar akisema: "Ewe Amir wa Waumini, barua zinatufikia zikiwa na tarehe ya Sha'ban, nasi hatujui ni Sha'ban ipi hii; je, ni ya mwaka uliopita au ya mwaka huu wa sasa?"
Kutokana na hali hiyo, Khalifah Umar aliwakusanya Maswahaba (ra) na wakajadili jambo hili. Maoni yalitofautiana; baadhi yao walipendekeza tarehe ya kuzaliwa kwa Mtume (saw) ichukuliwe kama mwanzo wa kalenda, na mwingine akasema: tuchukue tarehe ya kifo chake. Hata hivyo, maoni yaliyopendwa na wengi yalikuwa ni kuchukua tarehe ya Hijra yake (saw).
Baada ya Khalifah Umar kuwashauri Maswahaba wawili, Uthman bin Affan na Ali bin Abi Talib, kuhusu maoni haya nao wakayaidhinisha, kulifikiwa makubaliano ya kuuchukua mwaka ambao Mtume ﷺ alihama kuwa ndio mwanzo wa kalenda. Tarehe Mosi ya Muharram ilichaguliwa kama mwanzo wa mwaka, na mwezi wa Dhul-Hijjah kama mwisho wake. Kuanzia hapo, mwaka wa Hijria ulianza kuhesabiwa kutokana na Hijra ya Mtume, ambayo iliangukia mwaka 622 Miladi, na kuwa mwaka wa kwanza katika kalenda ya Hijria.
Sisi pia tumeitibari jambo hili kuhusiana na majira ya wakati wa kila siku, tukaufanya kuwa kwa mujibu wa wakati wa Madinah kama ilivyoelezwa katika ufunguzi wa idhaa yetu. Hii ni ili tarehe ya Hijria iliyopitishwa na Maswahaba wakati wa zama za Umar – ambayo ni tarehe ya Hijra kuelekea Madinah – iendeane na wakati tulioupitisha, uwe ni kwa mujibu wa wakati wa Madinah Al-Munawwarah.
Natumai jibu hili liko wazi, na Mwenyezi Mungu ndiye Mjuzi zaidi na Mwenye Hikima zaidi.
Ndugu yenu, Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah
01 Muharram Al-Haram 1444 H Inayolingana na 30/07/2022 M
Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amiri (Mungu amlinde) kwenye Facebook
Kiungo cha jibu kutoka kwenye tovuti ya Amiri (Mungu amlinde) kwenye Web