Mfululizo wa Majibu ya Mwanachuoni Mwenye Kuheshimika Ata Bin Khalil Abu al-Rashtah, Amir wa Hizb ut-Tahrir, kwa Maswali ya Wageni kwenye Ukurasa wake wa Facebook "Fikhi"
Jibu la Swali
Hukumu ya Matibabu
Kwa Abu Hanifa Fawalha
Swali:
Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh,
Amir mwenye kuheshimika, naomba radhi ikiwa swali hili litakuwa ni mzigo kwako; kutokana na juhudi zako kubwa unazotumia kutafuta heri kwa ajili ya umma huu uliopatwa na majanga... lakini kuna jambo ambalo sijaliweza kulielewa vyema pande zake, nalo ni: je, matibabu ni wajibu au ni mandub (yaliyopendekezwa), au ni kitu kingine?... Naomba faida, na Mwenyezi Mungu akubarikie, na afungue kila heri kupitia mikono yako.
Jibu:
Waalaykum Salaam Warahmatullahi Wabarakatuh,
Hakika jibu la swali lako lipo katika kijitabu cha Al-Istinsakh (Cloning), na nitakunakilia yaliyomo kuhusu hukumu ya matibabu ukurasa wa 30-32 katika faili la Word:
[... Ili tuchukue hukumu kwa uwazi, ni lazima kupitia dalili zilizopatikana kuhusu matibabu. Al-Bukhari amepokea kutoka kwa Abu Hurairah amesema: Mtume wa Allah ﷺ amesema:
مَا أَنْزَلَ اللَّهُ دَاءً إِلَّا أَنْزَلَ لَهُ شِفَاءً
"Mwenyezi Mungu hakuteremsha ugonjwa isipokuwa ameteremsha na ponyo lake."
Na Muslim amepokea kutoka kwa Jabir bin Abdullah, kutoka kwa Mtume ﷺ amesema:
لِكُلِّ دَاءٍ دَواءٌ، فَإِذَا أُصِيبَ دَواءُ الدَّاءِ بَرَأَ بِإِذْنِ اللَّهِ عَزَّ وَجَلَّ
"Kila ugonjwa una dawa, na dawa ya ugonjwa ikisibu, basi hupona kwa idhini ya Mwenyezi Mungu Aliyeshinda na Aliyetukuka."
Na katika Musnad ya Ahmad kutoka katika Hadithi ya Ibn Mas’ud akiinukuu kwa Mtume:
إِنَّ اللَّهَ عَزَّ وَجَلَّ لَمْ يُنْزِلْ دَاءً إِلَّا أَنْزَلَ لَهُ شِفَاءً، عَلِمَهُ مَنْ عَلِمَهُ وَجَهِلَهُ مَنْ جَهِلَهُ
"Hakika Mwenyezi Mungu Aliyeshinda na Aliyetukuka hakuteremsha ugonjwa isipokuwa ameteremsha na ponyo lake; alijue anayelijua na asilijue asiyelijua."
Hadithi hizi tatu, zina habari kwamba Mwenyezi Mungu Subhaanahu ameteremsha ugonjwa na akateremsha dawa, na kwamba kila ugonjwa una dawa, na kwamba dawa ikipatikana ugonjwa hupona kwa idhini ya Mwenyezi Mungu Ta’ala, alijue hilo alijualo na asilijue asilolijua. Hadithi hizi zina mwongozo (irshad) kwamba kila ugonjwa una dawa ya kuuponya, ili iwe ni kichocheo cha kufanya juhudi ya kupata matibabu yanayopelekea kupona ugonjwa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu Subhaanahu. Kwani ugonjwa unatoka Kwake, na dawa inatoka Kwake, na kupona ni kwa idhini Yake na si kutokana na dawa yenyewe, isipokuwa ameweka katika dawa sifa ya kuponya inapogusa ugonjwa. Na huu ni mwongozo (irshad) na si uamrisho wa lazima (iyjab).
Ahmad amepokea kutoka kwa Anas amesema: Mtume wa Allah ﷺ amesema:
إِنَّ اللَّهَ عَزَّ وَجَلَّ حَيْثُ خَلَقَ الدَّاءَ خَلَقَ الدَّوَاءَ فَتَدَاوَوْا
"Hakika Mwenyezi Mungu Aliyeshinda na Aliyetukuka alipoumba ugonjwa, aliumba na dawa, basi jitibuni."
Na Abu Dawood na Ibn Majah wamepokea kutoka kwa Usamah bin Sharik amesema: Nilikuwa kwa Mtume ﷺ na wakaja Mabedui, wakasema: Ewe Mtume wa Allah, hivi tujitibu? Akasema:
نَعَمْ، يَا عِبَادَ اللَّهِ تَدَاوَوْا، فَإِنَّ اللَّهَ عَزَّ وَجَلَّ لَمْ يَضَعْ دَاءً إِلَّا وَضَعَ لَهُ شِفَاءً...
"Ndiyo, enyi waja wa Allah jitibuni, kwani hakika Mwenyezi Mungu Aliyeshinda na Aliyetukuka hakuweka ugonjwa isipokuwa ameuwekea ponyo..."
Katika Hadithi ya kwanza kuna amri ya kutibu, na katika Hadithi hii kuna jibu kwa Mabedui kuhusu kutibu, na kuhutubia waja kuwa wajitibu, kwani Allah hakuweka ugonjwa isipokuwa ameweka ponyo lake. Kuhutubia huku katika Hadithi hizi mbili kumekuja kwa muundo wa amri, na amri hufidisha takwa la kawaida (mutlaq al-talab), na haufidishi wajibu isipokuwa ikiwa ni amri ya mkazo (jazim), na mkazo unahitaji kiashiria (qarina) kinachofahamisha hilo, na hakuna katika Hadithi hizi mbili kiashiria chochote kinachofahamisha wajibu. Na Hadithi tatu zilizotangulia, si chochote isipokuwa ni habari na mwongozo (irshad), jambo linalofanya takwa la matibabu katika Hadithi hizi mbili lisiwe la wajibu. Aidha, zimekuja Hadithi zinazofahamisha kuruhusiwa kwa kuacha matibabu, jambo linalokanusha Hadithi hizi mbili kufidisha wajibu. Hakika Muslim amepokea kutoka kwa Imran bin Husain kwamba Mtume ﷺ amesema:
يَدْخُلُ الْجَنَّةَ مِنْ أُمَّتِي سَبْعُونَ أَلْفًا بِغَيْرِ حِسَابٍ، قَالُوا: مَنْ هُمْ يَا رَسُولَ اللَّهِ؟ قَالَ: هُمْ الَّذِينَ لَا يَسْتَرْقُونَ، وَلَا يَتَطَيَّرُونَ، وَلَا يَكْتَوُونَ، وَعَلَى رَبِّهِمْ يَتَوَكَّلُونَ
"Wataingia Peponi katika umma wangu watu elfu sabini bila hesabu. Wakasema: Ni nani hao, ee Mtume wa Allah? Akasema: Ni wale ambao hawaombi kufanyiwa ruqya, hawapigi ramli, hawajitibi kwa kuchoma na moto (kayy), na wanamtegemea Mola wao."
Na Al-Bukhari amepokea kutoka kwa Ibn Abbas amesema: "Mwanamke huyu mweusi alikuja kwa Mtume ﷺ akasema: Mimi nina kifafa (ninapatwa na degedege), na mimi ninafunuka (nguo zangu), basi niombee kwa Mwenyezi Mungu. Akasema:
إِنْ شِئْتِ صَبَرْتِ وَلَكِ الْجَنَّةُ، وَإِنْ شِئْتِ دَعَوْتُ اللَّهَ أَنْ يُعَافِيَكِ
'Ukipenda subiri na utapata Pepo, na ukipenda nitamuomba Mwenyezi Mungu akupe afueni.'
Akasema: Nitavumilia, kisha akasema: Mimi ninafunuka, basi niombee kwa Allah nisinonekana utupu wangu (nisifunuke), basi akamuombea."
Hadithi hizi mbili zinaonyesha kuruhusiwa kwa kuacha matibabu. Katika Hadithi ya kwanza, sifa za wale watakaoingia Peponi bila hesabu ni kwamba hawaombi kufanyiwa ruqya wala hawajitibi kwa moto, yaani hawatafuti matibabu, bali huacha jambo hilo kwa Mola wao, na kumtegemea Yeye katika mambo yao yote. Na ruqya pamoja na kuchoma kwa moto ni miongoni mwa matibabu. Mtume ﷺ amehimiza matibabu kwa ruqya, na Jibril alimfanyia ruqya, kama ambavyo pia amesema:
الشِّفَاءُ فِي ثَلَاثَةٍ: فِي شَرْطَةِ مِحْجَمٍ، أَوْ شَرْبَةِ عَسَلٍ، أَوْ كَيَّةٍ بِنَارٍ، وَأَنْهَى أُمَّتِي عن الكَيِّ
"Ponyo lipo katika vitu vitatu: chale ya hijamah, au kunywa asali, au kuchoma kwa moto, nami nawakataza umma wangu kutokana na kuchoma kwa moto."
(Imepokewa na Al-Bukhari kupitia kwa Ibn Abbas). Katika Hadithi ya pili, Mtume ﷺ alimpa hiari mwanamke mweusi kati ya kuvumilia kifafa alichonacho na kupata Pepo, au kumuombea Mungu amponye kifafa chake, jambo linaloonyesha kuruhusiwa kuacha matibabu. Kwa hiyo, Hadithi hizi mbili zinabadilisha amri ya matibabu iliyokuja katika Hadithi ya jibu kwa Mabedui, na katika Hadithi iliyo kabla yake, kutoka kwenye wajibu, na kwa sababu ya himizo kubwa la Mtume ﷺ la kutaka matibabu, basi amri ya matibabu iliyokuja katika Hadithi inakuwa ni kwa ajili ya mandub (iliyopendekezwa)] Mwisho.
Ndugu yenu Ata Bin Khalil Abu al-Rashtah
23 Shawwal 1442 H Sawa na 04/06/2021 M
Link ya jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir (Mwenyezi Mungu amuhifadhi) kwenye Facebook
Link ya jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir (Mwenyezi Mungu amuhifadhi) kwenye Web