** (Mfululizo wa majibu ya mwanachuoni Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah, Amir wa Hizb ut-Tahrir, kwa maswali ya wageni kwenye ukurasa wake wa Facebook) **
** Kwa: Yusuf Yusuf **
Swali:
Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh
Mwanachuoni mtukufu, ndugu Ata Bin Khalil, baada ya salamu:
Sisi sote tunajua kuwa Umma leo uko karibu zaidi kuliko wakati wowote uliopita kutangaza Dola ya Khilafah, ambayo labda itafunikwa na habari za dharura tunazoweza kuzisikia wakati wowote kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Lakini swali langu, kutokana na nafasi yako na ufahamu wako wa mwenendo wa matukio, je, Umma wa Kiislamu uko tayari sasa kwa jambo hili kubwa? Hasa tukizingatia kuwa majukumu yanayofuata kusimamishwa kwa dola labda ni magumu zaidi kuliko kazi ya kuisimamisha yenyewe. Je, Umma uko tayari kubeba majukumu kama haya?
Jibu:
Wa Alaykum Salam Warahmatullahi Wabarakatuh
Hakika suala lenyewe, ewe ndugu yangu, ni kuwa Mwenyezi Mungu (swt) atunusuru kisha tusimamishe Dola ya Khilafah. Ama kuhusu ikiwa Umma uko tayari kubeba majukumu haya? Jibu ni ndiyo, na kile kinachoupungua ni uongozi mchamungu na safi utakaouongoza kuelekea kwenye kheri chini ya kivuli cha Khilafah ya Rashidah. Hakika Mwenyezi Mungu (swt) anaufafanua Umma huu:
كُنْتُمْ خَيْرَ أُمَّةٍ أُخْرِجَتْ لِلنَّاسِ تَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَتَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنْكَرِ وَتُؤْمِنُونَ بِاللَّهِ
"Ninyi mmekuwa bora ya Umma walio tolewa watu, kwa kuwa mnaamrisha mema na mnakataza maovu, na mnamuamini Mwenyezi Mungu." (QS. Ali 'Imran [3]: 110)
Ni kweli kwamba tamaduni haribifu, fikra batili, na dhana hatari zimeingia ndani ya Umma, na mafungamano ya Kiislamu yamedhoofika na badala yake kumeenea mafungamano ya utaifa na kizalendo... Lakini haya yote hayako ndani ya vilindi vya sehemu kubwa ya Umma, bali yanaelea juu tu kutokana na ushawishi wa watawala madhalimu na vyombo vya habari vinavyofuata mkondo wao. Pamoja na hayo, kheri ipo, na labda unafuatilia shughuli za Hizb na unaona kuwa Khilafah sasa imekuwa na maoni ya umma (ra'y 'amm) baada ya kuwa haipo, na imekuwa hitaji la jumla linalovutia umakini baada ya kuwa kuitolea wito kulionekana kama ni aibu!
Ewe ndugu yangu, mataifa yaliyo hai hata yakikumbwa na sababu za udhaifu na mfarakano... ni lazima yanyanyuke. Majeshi ya msalaba yalikaa katika nchi zetu kwa takriban miaka mia mbili, na huko Jerusalem pekee kwa takriban miaka 90, kisha kukatokea vita vya Hittin mnamo Rabi' al-Akhir mwaka 583 AH, na kukombolewa kwa Jerusalem mnamo Rajab 583 AH. Baadaye waliwafukuza wanajeshi hao kwa fedheha kubwa baada ya Salahuddin kuwaangamiza Mafatimi nchini Misri na kurejesha umoja kwenye Khilafah ya Abbasid... Vilevile, Watartari waliiharibu Baghdad na kumuua Khalifah mnamo 656 AH, kisha Khilafah ikahamia Misri na haikupita miaka miwili hadi ikatokea vita vya Ain Jalut mnamo 658 AH, na kuangamizwa kwa Watartari...
Hivyo basi, ewe ndugu mpendwa, kurejeshwa kwa Khilafah chini ya uongozi wake mchamungu na safi kutaurudisha Umma, kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, kwenye utukufu na ushindi wake. Na jambo hilo si gumu kwa Mwenyezi Mungu.
Mwenyezi Mungu akubarikie kwa hima na juhudi zako.
Ndugu yenu, Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah
Link ya jibu kwenye ukurasa wa Amir wa Facebook