Mfululizo wa Majibu ya Mwanachuoni Mkubwa Ata bin Khalil Abu Al-Rashtah, Amir wa Hizb ut Tahrir
kwa Maswali ya Wageni kwenye Ukurasa wake wa Facebook "Fikihi"
Jibu la Swali
Je, Qur’an ni kiumbe au si kiumbe?
Kwa Inayat Ur Rahman Noori
Swali:
Assalamualaikum!
Nataka kukuuliza, je, Qur’an ni miongoni mwa viumbe (makhluk) vya Allah, na kwa nini?
Kwa sababu Imamu Abu Hanifa alisema: kila kitu ni kiumbe isipokuwa Qur’an kwa sababu ni maneno ya Allah.
Sasa, unaweza kunifafanulia jambo hilo. Wassalam!
السلام عليكم،
Nataka kuuliza je, Qur’an ni miongoni mwa viumbe vya Allah, na kwa nini?
Kwa sababu Imamu Abu Hanifa anasema: Kila kitu ni kiumbe isipokuwa Qur’an, kwani hiyo ni maneno ya Allah.
Sasa, je, unaweza kufafanua hilo?
Wassalam!
Jibu:
Walaikum Salaam Warahmatullahi Wabarakatuh,
Kuhusu suala la kama Qur’an ni kiumbe au si kiumbe, hakika Qur’an ni maneno ya Allah, na namna (kaifiyyah) ya maneno kutoka kwa Allah Subhanahu haidirikiwi namna ilivyo... Kwa sababu hiyo, akili ya mwanadamu haiwezi kufanya utafiti katika namna ya maneno ya Allah, kama ni kiumbe au si kiumbe. Badala yake, inapaswa kuaminiwa kama ilivyokuja katika nukuu (nass), hivyo tunaamini kuwa Qur’an ni maneno ya Allah na hiyo inatosha.
Kwa ajili ya ufahamu, tafiti za makundi ya Kiislamu yaliyopita kama Mu'tazila na wengineo katika mada hii, ambazo ziliegemea kwenye mantiki katika mambo yasiyohisika (ghayr al-mahsusat), tafiti hizo si sahihi. Zinapelekea kwenye matokeo yanayogongana kwa sababu hazikujengwa juu ya utafiti wa vitu vinavyohisika (al-mahsusat)... Tumebainisha hayo katika vitabu vyetu:
1- Ash-Shakhsiyyah al-Islamiyyah Juzuu ya Kwanza - ukurasa wa 58-61 faili la Word: Mlango wa "Makosa ya Mbinu ya Mutakallimin":
[..."Kwa mfano, inasemwa kimantiki kuwa Qur’an ni maneno ya Allah nayo yameundwa na herufi zilizopangika zinazofuatana katika kuwepo kwake, na kila maneno yaliyoundwa na herufi zilizopangika zinazofuatana katika kuwepo kwake ni tukio jipya (hadith), basi natija yake ni kuwa Qur’an ni tukio jipya na ni kiumbe... Mpangilio huu wa hoja (qadaya) umepelekea kwenye natija ambayo haipo chini ya hisia, hivyo hakuna njia kwa akili kuifanyia utafiti au kuitolea hukumu. Kwa sababu hiyo, hiyo ni hukumu ya kidhanifu isiyo ya kiuhalisia, mbali na kuwa ni miongoni mwa mambo ambayo akili imezuiwa kuyafanyia utafiti, kwani kufanya utafiti katika sifa za Allah ni kufanya utafiti katika dhati Yake, na haijuzu kufanya utafiti katika dhati ya Allah kwa namna yoyote ile."
Pia, inawezekana kupitia mantiki hiyo hiyo kufikia natija inayopingana na natija hii "kwa kusema Qur’an ni maneno ya Allah nayo ni sifa Yake, na kila sifa ya Allah ni ya tangu na tangu (qadim), basi natija ni kuwa Qur’an ni ya tangu na tangu na si kiumbe"... Kwa hiyo, mgongano wa kimantiki unajitokeza katika suala lile lile moja. Na hivi ndivyo ilivyo katika masuala mengi yanayotokana na kupanga mambo ya kimantiki juu ya mambo mengine ya kimantiki; mfuata mantiki hufikia natija zenye migongano mikubwa na za ajabu sana. Ama kupanga mambo yanayohisika juu ya mambo yanayohisika, ikiwa mwanzo wake ni wa kihisia katika hoja na mwisho wake ni wa kihisia katika natija, basi natija hiyo inakuwa sahihi... nk.] Mwisho.
2- Katika kitabu hicho hicho - ukurasa wa 126 faili la Word, mlango wa "Sifa za Allah":
(Na kwa sababu hii, utafiti wa Mutakallimin wote katika sifa za Allah hauko mahali pake na ni kosa tupu. Sifa za Allah ni tawqifiyyah (zinategemea maandiko pekee); zile zilizoingia katika maandiko thabiti (nass qat'i) tumezitaja kwa kiasi kilichokuja katika maandiko hayo na si zaidi. Haijuzu kwetu kuongeza sifa ambayo haikuja, wala kufafanua sifa kwa kile kisichokuja kuihusu katika maandiko thabiti).
3- Muhtasari ni kwamba Qur’an ni maneno ya Allah Subhanahu na haitafitiwi ikiwa ni kiumbe au si kiumbe, kwa sababu kufanya utafiti katika sifa ni kufanya utafiti katika dhati. Jambo hili akili haiwezi kulifanyia utafiti kwa sababu dhati ya Allah Subhanahu haipo chini ya hisia zetu ili akili iweze kuifanyia utafiti. Hivyo, tunaamini sifa za Allah kama zilivyokuja katika maandiko thabiti bila kuongeza wala kupunguza, bali kama zilivyokuja katika maandiko thabiti ikiwemo:
هُوَ اللَّهُ الَّذِي لَا إِلَهَ إِلَّا هُوَ عَالِمُ الْغَيْبِ وَالشَّهَادَةِ هُوَ الرَّحْمَنُ الرَّحِيمُ * هُوَ اللَّهُ الَّذِي لَا إِلَهَ إِلَّا هُوَ الْمَلِكُ الْقُدُّوسُ السَّلَامُ الْمُؤْمِنُ الْمُهَيْمِنُ الْعَزِيزُ الْجَبَّارُ الْمُتَكَبِّرُ سُبْحَانَ اللَّهِ عَمَّا يُشْرِكُونَ* هُوَ اللَّهُ الْخَالِقُ الْبَارِئُ الْمُصَوِّرُ لَهُ الْأَسْمَاءُ الْحُسْنَى يُسَبِّحُ لَهُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَهُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ
"Yeye ndiye Allah, ambaye hakuna mungu ila Yeye, Mjuzi wa yaliyofichikana na yanayoonekana. Yeye ndiye Mwingi wa Rehema, Mwenye kurehemu. Yeye ndiye Allah, ambaye hakuna mungu ila Yeye, Mfalme, Mtakatifu, Mwenye amani, Mtoaji wa amani, Mlinzi, Mwenye nguvu, Anayelazimisha, Mkubwa. Ametakasika Allah na yale wanayomshirikisha nayo. Yeye ndiye Allah, Muumbaji, Mwanzishi, Mtengenezaji. Yeye ana majina mazuri kabisa. Vinamtukuza Yeye vilivyomo mbinguni na ardhini, naye ni Mwenye nguvu, Mwenye hekima." (Surat Al-Hashr 59: 22-24)
na maandiko mengine thabiti.
Pia tunaamini kuwa Qur’an ni maneno ya Allah kama ilivyo katika maandiko thabiti:
وَإِنْ أَحَدٌ مِنَ الْمُشْرِكِينَ اسْتَجَارَكَ فَأَجِرْهُ حَتَّى يَسْمَعَ كَلَامَ اللَّهِ ثُمَّ أَبْلِغْهُ مَأْمَنَهُ ذَلِكَ بِأَنَّهُمْ قَوْمٌ لَا يَعْلَمُونَ
"Na ikiwa mmoja wa washirikina akikuomba ulinzi, basi mpe ulinzi mpaka asikie maneno ya Allah, kisha mfikishe mahali pake pa amani. Hilo ni kwa sababu wao ni watu wasiojua." (Surat At-Tawbah 9: 6)
أَمْ يَقُولُونَ افْتَرَى عَلَى اللَّهِ كَذِباً فَإِنْ يَشَأِ اللَّهُ يَخْتِمْ عَلَى قَلْبِكَ وَيَمْحُ اللَّهُ الْبَاطِلَ وَيُحِقُّ الْحَقَّ بِكَلِمَاتِهِ إِنَّهُ عَلِيمٌ بِذَاتِ الصُّدُورِ
"Au wanasema: Amemzulia Allah uongo? Lakini Allah akitaka Anaweza kuupiga muhuri moyo wako. Na Allah anafuta batili na anathibitisha haki kwa maneno Yake. Hakika Yeye ni Mjuzi wa yaliyomo vifuani." (Surat Ash-Shura 42: 24)
لَا تُحَرِّكْ بِهِ لِسَانَكَ لِتَعْجَلَ بِهِ * إِنَّ عَلَيْنَا جَمْعَهُ وَقُرْآنَهُ * فَإِذَا قَرَأْنَاهُ فَاتَّبِعْ قُرْآنَهُ * ثُمَّ إِنَّ عَلَيْنَا بَيَانَهُ
"Usiitikise ulimi wako kwa ajili hiyo (Qur’an) ili kuifanyia haraka. Hakika ni juu yetu kuikusanya na kuisoma. Basi tutakapoisoma, ifuate usomaji wake. Kisha ni juu yetu kuibainisha." (Surat Al-Qiyamah 75: 16-19)
وَاتْلُ مَا أُوحِيَ إِلَيْكَ مِنْ كِتَابِ رَبِّكَ لَا مُبَدِّلَ لِكَلِمَاتِهِ وَلَنْ تَجِدَ مِنْ دُونِهِ مُلْتَحَداً
"Na some yale uliyofunuliwa (kwa wahyi) katika Kitabu cha Mola wako. Hakuna wa kubadilisha maneno Yake, wala hutapata kimbilio kinyume naye." (Surat Al-Kahf 18: 27)
Nikitarajia kuwa katika haya kuna utoshelevu, na Allah ni Mjuzi zaidi na Mwenye hekima zaidi.
Ndugu yenu, Ata bin Khalil Abu Al-Rashtah
15 Jumada al-Akhira 1444 H Inayoafikiana na 08/01/2023 M
Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir (Mwenyezi Mungu amuhifadhi) kwenye Facebook