Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

Jibu la Swali: Je, Riba Haitokei Isipokuwa Katika Aina Sita Tu?

November 27, 2018
1733

(Mfululizo wa majibu ya mwanachuoni mtukufu Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah, Amir wa Hizb ut-Tahrir, kwa maswali ya wageni kwenye ukurasa wake wa Facebook "Fikhi")

Jibu la Swali

Kwenda kwa: Alaa al-Maqtari

Swali:

Assalamu Alaikum,

Swali kutoka kwa mmoja wa ndugu anaitwa Muhsin al-Jadabi - Sana'a.

Amesema ﷺ: "Mkopo wowote unaovuta manufaa basi huo ni riba". Hadithi zimebainisha kuwa riba iko katika dhahabu, fedha, na baadhi ya aina (tende, zabibu, ngano, na shayiri). Je, sarafu za karatasi za lazima (al-awraq al-ilzamiyyah) hazina riba kwa sababu hazijafungamanishwa na dhahabu wala fedha? Na je, inajuzu kwa mtu kumkopesha mtu mwingine tani moja ya chuma na akasharti amrudishie chuma lakini zaidi ya tani moja, kwa mfano tani moja na nusu?

Jazakumullah Khairan.

Jibu:

Wa Alaikum Salaam Wa Rahmatullahi Wa Barakatuh,

Ndiyo, riba (katika biashara) haitokei isipokuwa katika aina sita: Tende, ngano, shayiri, chumvi, dhahabu, na fedha... Lakini hii ni katika biashara (al-bay’) na biashara ya malipo ya awali (as-salam)... Ama kuhusu mkopo (al-qard), riba hutokea katika kila kitu; hivyo si halali kukopesha kitu ili kirudishwe kikiwa pungufu au zaidi, wala kikiwa cha aina nyingine asili yake. Lakini kirudishwe mfano wa kile ulichokopesha katika aina yake na kiasi chake.

Ama kuhusu kuwa riba iko katika aina hizi sita pekee, ni kwa sababu Ijmai ya Maswahaba ilifungamana nazo, na kwa sababu Rasulullah ﷺ anasema:

الذهب بالذهب والفضة بالفضة والبر بالبر والشعير بالشعير، والتمر بالتمر والملح بالملح، مثلاً بمثل، سواء بسواء، يداً بيد، فإذا اختلفت هذه الأصناف فبيعوا كيف شئتم إذا كان يداً بيد

"Dhahabu kwa dhahabu, fedha kwa fedha, ngano kwa ngano, shayiri kwa shayiri, tende kwa tende, na chumvi kwa chumvi; kiasi sawa kwa kiasi sawa, sawia kwa sawia, mkono kwa mkono. Na zikitofautiana aina hizi, basi uzianu upendavyo ikiwa ni mkono kwa mkono." (HR. Muslim kutoka kwa Ubada bin al-Samit).

Hivyo, Ijmai na Hadithi zimeweka nukuu (nass) juu ya vitu maalumu ambavyo ndani yake mna riba, kwa hiyo haithibiti isipokuwa ndani yake tu. Na haikuja dalili ya uharamu katika aina nyingine nje ya hizi sita, hivyo riba haitakuwa katika vitu vingine, lakini inaingia ndani yake kila kilicho katika jinsi yake (aina yake) na kile kinachoafikiwa na sifa yake. Ama visivyokuwa hivyo havimo. Na hivi ndivyo ilivyo, riba haitokei katika biashara na salamu isipokuwa katika vitu sita pekee: tende, ngano, shayiri, chumvi, dhahabu na fedha; kwani hayo ni majina ya jinsi (asma' jins) ambayo hayafanyiwi qiyasi.

Hata hivyo, zimekuja nukuu wakati wa kuzungumzia Zaka zinazotaja dhahabu na fedha kama pesa (naqd) na si kama jina la jinsi pekee, bali kama pesa ambayo watu wanaitumia kama thamani na ujira. Kutokana na dalili hizi, inatolewa sababu ('illah), nayo ni naqdiyyah (sifa ya kuwa pesa), hivyo sarafu za karatasi za lazima zinafanyiwa qiyasi kwazo kwa sababu sifa hii imepatikana ndani yake. Hivyo, hukumu za zaka ya pesa zinatekelezwa kwazo, kwa kuhesabu thamani yake sokoni katika dhahabu au fedha. Kutoka kwa Ali bin Abi Talib, kutoka kwa Mtume ﷺ amesema:

إذا كانت لك مئتا درهم، وحال عليها الحول، ففيها خمسة دراهم، وليس عليك شيء - يعني في الذهب - حتى يكون ذلك عشرون ديناراً، فإذا كانت لك عشرون ديناراً، وحال عليها الحول، ففيها نصف دينار

"Ikiwa una dirham mia mbili, na mwaka ukapita juu yake, basi ndani yake kuna dirham tano. Na huna wajibu wa kutoa chochote - yaani katika dhahabu - mpaka ifikie dinari ishirini. Ikiwa una dinari ishirini na mwaka ukapita juu yake, basi ndani yake kuna nusu dinari." (HR. Abu Daud).

Pia imepokelewa kutoka kwa Ali akisema: "Katika kila dinari ishirini kuna nusu dinari, na katika kila dinari arobaini kuna dinari moja." Na kutoka kwa Ali (ra) amesema: Rasulullah ﷺ amesema:

فهاتوا صدقة الرقّة، في كل أربعين درهماً، درهماً وليس في تسعين ومائة شيء، فإذا بلغت مائتين ففيها خمسة دراهم

"...Basi toeni sadaka ya al-riqqah (fedha iliyopigwa chapa), katika kila dirham arobaini (toeni) dirham moja, na hakuna chochote katika dirham mia moja na tisini, na ikifikia mia mbili basi ndani yake kuna dirham tano." (HR. Bukhari na Ahmad).

Pia Abdurrahman al-Ansari amepokea katika barua ya Rasulullah ﷺ na barua ya Umar kuhusu sadaka:

والورِق لا يؤخذ منه شيء حتى يبلغ مئتي درهم

"...Na al-wariq (fedha iliyopigwa chapa) haichukuliwi kitu mpaka ifikie dirham mia mbili." (HR. Abu Ubaid).

Hadithi hizi zote zimeashiria juu ya sifa ya kuwa pesa (naqdiyyah) na uthamani (thamaniyyah); kwa sababu maneno al-riqqah pamoja na kiashiria cha "katika kila dirham arobaini", na al-wariq, dinari, na dirham, ni maneno yanayotumika kwa dhahabu na fedha zilizopigwa chapa, yaani ambazo ni pesa na thamani. Kutumika kwa maneno haya kunaonyesha kuwa naqdiyyah na thamaniyyah ndizo zinazokusudiwa katika hadithi hizi, na kwayo yamefungamanishwa hukumu nyingi za kisharia kama vile Zaka, fidia ya damu (diyat), kafara (kaffarat), kukata mkono kwa mwizi, na hukumu nyinginezo.

Na kwa kuwa sarafu za karatasi za lazima zimetimiza sifa hizi za naqdiyyah na thamaniyyah, yaani kuwa thamani ya vitu na ujira wa manufaa na huduma, na kwazo dhahabu na fedha hununuliwa, kama ambavyo bidhaa nyingine na vitu hununuliwa, basi itakuwa imetimiza sifa ya naqdiyyah na thamaniyyah zilizomo katika dhahabu na fedha zilizopigwa chapa kama dinari na dirham. Hivyo, zinajumuishwa katika hadithi za uwajibifu wa zaka katika pesa mbili (dhahabu na fedha), kwa hiyo zaka ni wajibu ndani yake kama ilivyo wajibu katika dhahabu na fedha, na hukadiriliwa kwa dhahabu na fedha. Mtu yeyote aliye na kiasi cha sarafu hizi za karatasi kinacholingana na thamani ya dinari ishirini za dhahabu - yaani gramu 85 za dhahabu - ambayo ni nisabu ya dhahabu, au kiasi kinacholingana na dirham 200 za fedha - yaani gramu 595 za fedha - na mwaka ukapita juu yake, basi zaka ni wajibu kwake, na ni wajibu kutoa robo ya fungu la kumi (2.5%).

Na zaka ya dhahabu hutolewa kwa dhahabu, au kwa karatasi mbadala (al-awraq al-na'ibah) na karatasi zenye dhamana (al-awraq al-wathiqah). Na zaka ya fedha hutolewa kwa fedha, na kwa karatasi mbadala na zenye dhamana. Vilevile inatosheleza kutoa zaka ya dhahabu kwa fedha au kwa sarafu za karatasi za lazima, na zaka ya fedha kwa dhahabu au kwa sarafu za karatasi za lazima; kwa sababu zote hizo ni pesa na thamani, hivyo moja inatosheleza badala ya nyingine ili kutimiza lengo hilo.

Na maadamu zaka ni wajibu ndani yake, basi vilevile zitatekelezwa kwake hukumu za mali kama vile riba, fidia ya damu (diyat), kafara (kaffarat), kukata mkono kwa mwizi, na hukumu nyinginezo. Hivyo basi, hukumu za riba katika dhahabu na fedha kama pesa (naqd) na si kama jinsi (aina ya madini) zinatumika kwa sarafu za karatasi za lazima kama pesa kwa sababu sababu ('illah) ya naqdiyyah imepatikana ndani yake.

Ama mkopo (al-qard), unajuzu katika aina hizi sita na katika nyinginezo, na katika kila kitu kinachoweza kumilikiwa na kufaa kutolewa katika umiliki. Riba haiingii ndani yake isipokuwa ikiwa mkopo huo umevuta manufaa, kama alivyopokea al-Harith bin Abi Usamah kutoka kwa hadithi ya Ali (ra) kwa tamko: "Kuwa Mtume ﷺ alikataza mkopo unaovuta manufaa" na katika riwaya nyingine: "Kila mkopo unaovuta manufaa basi huo ni riba". Na kinavuliwa katika hayo kile ambacho ni katika mlango wa uzuri wa kulipa bila ya nyongeza (iliyoshartiwa), kama alivyopokea Abu Daud kutoka kwa Abu Rafi' amesema: "Rasulullah ﷺ alikopa mwana-ngamia, kisha ngamia wa sadaka wakamjia, akaniamuru nimlipe yule bwana mwana-ngamia wake. Nikasema: Sijapata katika ngamia isipokuwa dume aliyekomaa (ruba'iyan). Akasema: Mpe huyo, kwani hakika mbora wa watu ni yule ambaye ni mbora wao katika kulipa".

Kutokana na hayo, mkopo wowote katika aina sita au nyinginezo ni lazima urudishwe kwa mwenyewe bila nyongeza ya "manufaa", vinginevyo utakuwa ni riba. Kwa hiyo, haijuzu kukopa tani moja ya chuma na kuirudisha ikiwa tani moja na nusu, kwani hilo litakuwa ni riba.

Natumai jibu liko wazi In Shaa Allah.

Ndugu yenu, Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah

14 Rabi' al-Akhar 1439 H Inayoafikiana na 01/01/2018 M

Link ya jibu kutoka kwa ukurasa wa Amir (Mwenyezi Mungu amlinde) kwenye Facebook

Share Article

Share this article with your network