(Mfululizo wa majibu ya mwanachuoni mtukufu Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah, Amir wa Hizb ut-Tahrir, kwa maswali ya wageni wa ukurasa wake wa Facebook "Fiqhi")
Jawabu la Swali
Kwa Khalid Al Yasin
Swali:
Assalamu Alaikum Warahmatullahi Wabarakatuh, Mwenyezi Mungu awahifadhi, nina swali ambalo natumai kupata jibu lake...
Inafahamika kuwa "kodi" ni haramu katika Uislamu, sasa je, Dola ya Kiislamu itawezaje kushughulikia upungufu wa bajeti, hasa ikizingatiwa kuwa leo hii hakuna tena "Tawdhif - Ushuru - Kharaj"?
Jibu:
Wa Alaikum Salaam Warahmatullahi Wabarakatuh,
Inaonekana kuna mkanganyiko fulani katika mada ya swali lako. Unasema: "Kodi ni haramu katika Uislamu", na hili ni sahihi kwa ujumla, lakini lina masharti katika hali maalumu... Kadhalika unasema: "Hakuna leo hii ushuru au kharaj", ukizingatia kuwa ardhi ya Waislamu ni ima ardhi ya ushuru (ushriyya) au ya kharaj (kharajiyya), na zote zipo. Kwa nyongeza, umetaja maneno: "Tawdhif, Ushuru, na Kharaj", neno tawdhif hapa halina nafasi...
Vyovyote iwavyo, nitakufafanulia mada hii ili jibu liwe wazi bila mkanganyiko wala utatanishi, Insha Allah.
1- Sheria imekataza mtawala kutoa kodi kwa Waislamu kwa amri inayotokana na yeye tu kama anavyotaka. Amesema ﷺ:
لا يَدْخُلُ الْجَنَّةَ صَاحِبُ مَكْسٍ
"Hataingia Peponi mtoza maks." (Imepokewa na Ahmad na kusahihishwa na Al-Zayn na Al-Hakim).
Maks ni kodi inayochukuliwa kutoka kwa wafanyabiashara kwenye mipaka ya nchi, lakini katazo hili linajumuisha kila aina ya kodi kwa sababu ya kauli ya Mtume ﷺ katika hadith iliyofanyiwa mwafaka (Muttafaqun Alayhi) kupitia Abu Bakrah:
إِنَّ دِمَاءَكُمْ وَأَمْوَالَكُمْ وَأَعْرَاضَكُمْ عَلَيْكُمْ حَرَامٌ كَحُرْمَةِ يَوْمِكُمْ هَذَا فِي بَلَدِكُمْ هَذَا فِي شَهْرِكُمْ هَذَا...
"Hakika damu zenu, mali zenu na heshima zenu ni haramu kwenu (kudhuriana) kama ilivyo haramu ya siku yenu hii, katika mji wenu huu, katika mwezi wenu huu..."
Hadith hii ni ya jumla, inamjumuisha Khalifa na watu wengine wote... Hivyo basi, haijuzu kwa Khalifa kutoa kodi ili afanye matumizi, bali anapaswa kutumia kutoka Bayt al-Mal.
2- Lakini kuna hali ambazo Sheria imezivua kutoka katika katazo la jumla la utoaji kodi, na hali hizo zimekuja na nusus (maandiko) za kisheria zinazobainisha kuwa matumizi yake ni wajibu kwa Waislamu na si kwa Bayt al-Mal pekee. Hivyo basi, ikiwa kilichopo Bayt al-Mal hakitoshelezi matumizi hayo, jukumu la matumizi huhamia kutoka Bayt al-Mal kwenda kwa Waislamu. Hapo ndipo kodi hutozwa kwa matajiri kwa kiasi cha matumizi ya lazima kwa hali hizo bila ya ziada, na huwekwa katika maeneo yaliyokusudiwa... Kodi katika hali hizo haitotokana na amri ya mtawala kufuata matamanio yake na vile anavyotaka, bali kulingana na amri ya Mwenyezi Mungu, na mtawala anakuwa tu mtekelezaji wa amri aliyoiamrisha Mwenyezi Mungu (swt). Kulingana na hili, kile ambacho Sheria imekifanya kuwa wajibu kwa Bayt al-Mal na kwa Waislamu, hugharamiwa kutoka Bayt al-Mal. Ikiwa hakuna mali katika Bayt al-Mal, au mali imeisha, au kilichopo hakitoshelezi matumizi; basi Khalifa anayo haki ya kutoa kodi kwa matajiri kwa kiasi cha matumizi hayo kulingana na hukumu za kisheria... Na haitakuwa haramu katika hali hii.
3- Kutokana na yaliyotangulia, inabainika kuwa ili ijuzu kutoa kodi kwa ajili ya matumizi ya hali fulani, sharti zifuatazo lazima zitimizwe:
Kusiwe na mali katika Bayt al-Mal inayotoshelezi matumizi ya hali hiyo...
Kuwe na nusu (andiko) ya kisheria inayoeleza kuwa matumizi ya hali hiyo ni wajibu kwa Bayt al-Mal na kwa Waislamu...
Kodi inayotozwa isizidi kiasi cha matumizi ya lazima kwa hali hiyo...
Isitozwe isipokuwa kwa matajiri pekee ambao wana ziada ya mahitaji yao ya msingi na ya ziada (kamaliyyat) kwa wema...
4- Hivyo basi, kodi haitolewi katika Uislamu isipokuwa kwa mujibu wa masharti yaliyotajwa hapo juu, yaani Sheria iwe imeelezea kuwa matumizi ya hali fulani si tu jukumu la Bayt al-Mal, bali pia ni jukumu la Waislamu:
- Kwa mfano, matumizi kwa ajili ya mafukara. Ikiwa Bayt al-Mal haitoshelezi kukidhi mahitaji ya mafukara, basi kodi hutozwa kwa kiasi cha hitaji hilo bila ziada, na hutozwa kwa matajiri. Hii ni kwa sababu kuwahudumia mafukara si wajibu kwa Bayt al-Mal pekee, bali pia kwa Waislamu. Al-Hakim amepokea katika Al-Mustadrak kutoka kwa Aisha (ra) kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ amesema:
لَيْسَ بِالْمُؤْمِنِ الَّذِي يَبِيتُ شَبْعَانًا وَجَارُهُ جَائِعٌ إِلَى جَنْبِهِ
"Si muumini yule anayelala akiwa ameshiba na jirani yake ana njaa pembeni yake."
Na katika riwaya ya Al-Tabarani katika Al-Mu’jam Al-Kabir kutoka kwa Anas bin Malik (ra) amesema: Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ amesema:
مَا آمَنَ بِي مَنْ بَاتَ شَبْعَانًا وَجَارُهُ جَائِعٌ إِلَى جَنْبِهِ وَهُوَ يَعْلَمُ بِهِ
"Hakuniamini mimi yule anayelala akiwa ameshiba na jirani yake ana njaa pembeni yake naye analijua hilo."
Na amepokea Al-Hakim katika Al-Mustadrak kutoka kwa Ibn Umar amesema: Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ amesema:
وَأَيُّمَا أَهْلِ عَرْصَةٍ أَصْبَحَ فِيهِمُ امْرُؤٌ جَائِعًا، فَقَدْ بَرِئَتْ مِنْهُمْ ذِمَّةُ اللَّهِ
"Na watu wowote wa mtaa watakaoamka na miongoni mwao muna mtu mwenye njaa, basi dhamana ya Mwenyezi Mungu imejiondoa kwao."
- Na kwa mfano, matumizi kwa ajili ya Jihadi. Ikiwa Bayt al-Mal haitoshelezi kukidhi mahitaji ya Jihadi, kodi hutozwa kwa kiasi cha hitaji hilo bila ziada, na hutozwa kwa matajiri. Hii ni kwa sababu matumizi ya Jihadi si wajibu kwa Bayt al-Mal pekee, bali pia kwa Waislamu. Amesema (swt):
وَجَاهِدُوا بِأَمْوَالِكُمْ وَأَنْفُسِكُمْ فِي سَبِيلِ اللَّهِ ذَلِكُمْ خَيْرٌ لَكُمْ إِنْ كُنْتُمْ تَعْلَمُونَ
"Na piganeni jihadi kwa mali zenu na nafsi zenu katika njia ya Mwenyezi Mungu. Hilo ni bora kwenu ikiwa mnajua." (QS. At-Tawbah [9]: 41)
Na kuna dalili nyinginezo.
- Na kwa mfano, matumizi kwa ajili ya mishahara ya askari. Ikiwa Bayt al-Mal haitoshelezi kukidhi mahitaji ya mishahara ya askari, kodi hutozwa kwa kiasi cha hitaji hilo bila ziada kwa matajiri. Hii ni kwa sababu mishahara ya askari si wajibu kwa Bayt al-Mal pekee, bali pia kwa Waislamu. Ahmad amepokea katika Musnad yake kutoka kwa Abdullah bin Amr amesema: Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ amesema:
لِلْغَازِي أَجْرُهُ، وَلِلْجَاعِلِ أَجْرُهُ وَأَجْرُ الْغَازِي
"Mpiganaji anapata malipo yake, na yule anayemgharamia mpiganaji anapata malipo yake na malipo ya mpiganaji."
- Na kwa mfano, matumizi kwa ajili ya ujenzi wa hospitali katika mji ambao hauna hospitali nyingine na watu watapata madhara isipopatikana hospitali hiyo. Ikiwa Bayt al-Mal haitoshelezi ujenzi wa hospitali hiyo, kodi hutozwa kwa kiasi cha hitaji hilo bila ziada kwa matajiri. Hii ni kwa sababu ujenzi wa hospitali ya lazima ambayo kukosekana kwake kunaleta madhara, ujenzi huo si wajibu kwa Bayt al-Mal pekee bali pia kwa Waislamu kwa sababu katazo la dhara ni la jumla: Al-Hakim amepokea katika Al-Mustadrak (na akasema "Hii hadith ina sanadi sahihi"), kutoka kwa Abu Said Al-Khudri (ra) kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ amesema:
لَا ضَرَرَ وَلَا ضِرَارَ، مَنْ ضَارَّ ضَارَّهُ اللَّهُ، وَمَنْ شَاقَّ شَاقَّ اللَّهُ عَلَيْهِ
"Hakuna kudhuriana wala kulipizana dhara; yeyote anayemdhuru mwenzake na Mwenyezi Mungu atamdhuru, na yeyote anayemtia mwenzake katika uzito na Mwenyezi Mungu atamtia katika uzito."
- Na kwa mfano, matumizi kwa ajili ya majanga yanayowafika raia kama vile njaa, mafuriko, au tetemeko la ardhi... Ikiwa Bayt al-Mal haitoshelezi kukidhi matumizi haya ya dharura, basi kodi hutozwa kwa kiasi cha matumizi hayo bila ziada kwa matajiri. Hii ni kwa sababu kusaidia katika majanga ya dharura si wajibu kwa Bayt al-Mal pekee bali pia kwa Waislamu. Abu Dawood amepokea katika Sunan yake kutoka kwa Ibn Hujayr Al-Adawi amesema: Nilimsikia Umar bin Al-Khattab akipokea kutoka kwa Mtume ﷺ katika kisa hiki akisema:
وَتُغِيثُوا الْمَلْهُوفَ وَتَهْدُوا الضَّالَّ
"Na msaidieni mwenye shida na mmwongoze aliyepotea."
Pia, dalili za njaa tulizozitaja hapo awali zinatumika hapa.
5- Ama matumizi ambayo ni wajibu kwa Bayt al-Mal pekee, na si kwa Waislamu, haya hayagharamiwi isipokuwa tu iwapo kuna mali ya kutosha katika Bayt al-Mal. Ikiwa hakuna mali, basi kodi hazitozwi kwa ajili hiyo, bali husubiriwa mpaka mali itakapopatikana katika Bayt al-Mal. Hii ni kama vile matumizi ya maslahi fulani ya Waislamu ambayo kutokuwepo kwake hakuleti madhara kwao, kama vile kufungua barabara ya pili wakati kuna nyingine, au kufungua hospitali ya pili wakati kuna nyingine inayoweza kutosheleza. Kadhalika miradi ya uzalishaji ambayo kutokuanzishwa kwake hakuletei Umma madhara yoyote, kama vile kuanzisha kiwanda cha madini ya nikel, kohl, au ujenzi wa eneo la kuundia meli za kibiashara, na mfano wa hayo... Mambo haya na mfano wake hayagharamiwi kutoka Bayt al-Mal isipokuwa tu ikiwa kuna mali inayotosheleza kwa ajili hiyo...
6- Ama kuhusu kodi kutotozwa isipokuwa kwa matajiri pekee, ni kwa sababu kodi haichukuliwi kwa mtu isipokuwa kutoka kwenye kile kilichozidi kukidhi mahitaji yake ya msingi na ya ziada kwa wema. Hivyo, Muislamu yeyote mwenye ziada baada ya kukidhi mahitaji yake ya msingi na ya ziada, huchukuliwa kodi, na yule ambaye hana ziada baada ya kukidhi mahitaji hayo hachukuliwi kitu. Hii ni kutokana na kauli ya Mtume ﷺ:
خيرُ الصدقة ما كان عن ظهر غنى
"Sadaka bora ni ile inayotolewa kutokana na utajiri (ziada)." (Imepokewa na Bukhari kupitia Abu Hurairah).
Na utajiri (ghina) ni kile anachoweza mtu kukitosheleza bila kukihitaji kwa ajili ya mahitaji yake. Na Muslim amepokea kutoka kwa Jabir kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ amesema:
ابدأ بنفسك فتصدّق عليها، فإن فَضَلَ شيءٌ فلأهلك، فإن فَضَلَ عن أهلك شيءٌ فَلِذي قرابتك، فإن فَضَلَ عن ذي قرابتك شيءٌ فهكذا وهكذا
"Anza na nafsi yako uitolee sadaka, kikizidi kitu basi kwa familia yako, kikizidi kitu kwa familia yako basi kwa jamaa zako, kikizidi kitu kwa jamaa zako basi hivi na hivi – akisema: mbele yako, kulia kwako na kushoto kwako."
Hivyo, alichelewesha yule ambaye matumizi yake ni lazima kwake baada ya nafsi yake. Na kodi ni mfano wa hili; kwa sababu ni kama matumizi na ni kama sadaka. Na Mwenyezi Mungu (swt) anasema:
وَيَسْأَلُونَكَ مَاذَا يُنفِقُونَ قُلِ الْعَفْو
"Na wanakuuliza watoe nini? Sema: Kilichozidi (mahitaji)." (QS. Al-Baqarah [2]: 219)
Yaani kile ambacho katika kukitoa hakuna ugumu, nacho ni kile kilichozidi mahitaji. Hivyo, kodi huchukuliwa kutoka kwenye mali iliyozidi hitaji, yaani kutoka kwa matajiri pekee. Hivyo basi, kodi haichukuliwi kwa mafukara, na matajiri wanafahamika katika idara ya Zaka.
7- Ama kuhusu kodi kutotozwa isipokuwa kwa kiasi cha hitaji na utoshelevu, ni kwa sababu maandiko ya kisheria yameruhusu kuchukua kodi ili kukidhi mahitaji ya makundi fulani maalumu. Hili ndilo lililovuliwa katika katazo la kuchukua mali ya mtu bila ridhaa yake. Kwa hiyo, ni lazima iishie katika kiwango kilichotajwa katika maandiko, vinginevyo itakuwa ni dhulma. Haijuzu kuchukua mali ya mtu isipokuwa kwa ridhaa yake, na kuna hali maalumu ambazo maandiko yameruhusu kutoza kodi kwa ajili yake kwa kiasi cha hitaji na utoshelevu pekee.
8- Kutokana na yaliyotangulia, inabainika kuwa dhana ya kuwepo kwa upungufu wa "kudumu au karibu wa kudumu" katika "bajeti" ndani ya Dola ya Khilafah ni dhana isiyo na mashiko. Upungufu, yaani mapato kutotosheleza matumizi, ni jambo kinyume na asili ikiwa Uislamu utatekelezwa vyema... Hii ni kwa sababu ya mambo mawili muhimu:
a- Hukumu za kisheria zimebainisha kwa kina jinsi ya kukusanya mali na serikali na jinsi ya kuzitumia, na hazikuacha jambo hilo kwa ijtihadi ya watu na makadirio yao... Na imefanya matumizi ya baadhi ya mambo kutofungamana na kuwepo au kutokuwepo kwa mali katika Bayt al-Mal kwa sababu kuyagharamia ni wajibu kwa Bayt al-Mal na kwa Waislamu... Na tumebainisha hapo juu mambo ambayo ni lazima yagharamiwe iwe mali ipo Bayt al-Mal au haipo... Na haya ndiyo yanatolewa kodi ikiwa mali haipo Bayt al-Mal.
Ama matumizi yaliyo wajibu kwa Bayt al-Mal pekee na si kwa Waislamu, hayafanyiki isipokuwa tu ikiwa kuna mali ya kutosha katika Bayt al-Mal ya Waislamu na hayatolewi kodi kama tulivyobainisha hapo awali...
b- Mapato ya kudumu ya Bayt al-Mal ni: Fay-i, ghanima, anfal, kharaj, jizya... vilevile mapato ya umiliki wa umma wa aina zote, mapato ya milki za dola, ushuru, khums ya rikazi, madini, na mali za Zaka... Asili ni kwamba mali za mapato ya kudumu ya Bayt al-Mal zinapaswa kutosheleza matumizi yaliyo wajibu kwa Bayt al-Mal, iwe katika hali ya kuwepo mali au kutokuwepo mali... Kwa hivyo, kutokea kwa upungufu wa kifedha wa kugharamia matumizi haya ni jambo ambalo ni vigumu kutokea.
Na kuna maelezo zaidi tuliyoyabainisha katika vitabu vyetu; Mfumo wa Kiuchumi (An-Nidham al-Iqtisadi), Mali katika Dola ya Khilafah (Al-Amwal fi Dawlat al-Khilafah), na Utangulizi wa Katiba (Muqaddimat ad-Dustur)...
Natumai jibu hili linatosheleza kwa idhini ya Mwenyezi Mungu.
Ndugu yenu, Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah
12 Shaban 1437 H 19/05/2016 M
Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Facebook wa Amir: https://www.facebook.com/AmeerhtAtabinKhalil/photos/a.122855544578192.1073741828.122848424578904/477762799087463/?type=3&theater
Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Google Plus wa Amir: https://plus.google.com/100431756357007517653/posts/9STRE6zJ8Bg
Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Twitter wa Amir: https://twitter.com/ataabualrashtah/status/733256120828067840?lang=ar
Kiungo cha jibu kutoka kwenye tovuti ya Amir