Jibu la Swali
Je, inajuzu kupokea zawadi kutoka kwa mtu aliyepata mali kwa njia ya haramu?
Swali:
Je, inajuzu kupokea zawadi kutoka kwa mtu aliyepata mali kwa njia ya haramu (kwa mfano kupitia kamari, riba, mikataba ya bima, au kuuza pombe)? Na je, inajuzu kwa familia yake kupokea matumizi (nafaqah) yake kutoka kwa mali hii aliyoipata kwa njia ya haramu?
Asanteni sana.
Jibu:
Haramu iko ya aina mbalimbali:
- Haramu kutokana na dhati yake (asili yake) kama vile pombe... Na hii haijuzu kutoa zawadi kwayo, kwani ni haramu kwa mwenye pombe na kwa yule aliyepewa zawadi hiyo. Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema:
حُرِّمَتِ الْخَمْرُ بِعَيْنِهَا
"Pombe imeharamishwa kwa dhati yake." (Imepokelewa na An-Nasa'i).
- Haramu kwa sababu ya haki ya mwanadamu kama vile kitu cha kuibwa au kilichochukuliwa kwa nguvu (maghsub)... Hii ni haramu kwa mwizi na mnyang'anyi, na haijuzu kuitumia kama zawadi. Ni haramu kwa aliyeipata na kwa aliyepewa zawadi hiyo, kwa sababu mali hii ni haki ya mwenyewe, na popote inapopatikana ni lazima irudishwe kwa mwenyewe. Na miongoni mwa dalili za hayo ni:
Ahmad amepokea kutoka kwa Samurah, amesema: Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema:
إِذَا سُرِقَ مِنَ الرَّجُلِ مَتَاعٌ، أَوْ ضَاعَ لَهُ مَتَاعٌ، فَوَجَدَهُ بِيَدِ رَجُلٍ بِعَيْنِهِ، فَهُوَ أَحَقُّ بِهِ، وَيَرْجِعُ الْمُشْتَرِي عَلَى الْبَائِعِ بِالثَّمَنِ
"Mtu akibiwa bidhaa, au akipoteza bidhaa yake, kisha akaikuta mikononi mwa mtu fulani hususan, basi yeye ana haki zaidi nayo, na mnunuzi anamrudishia muuzaji ili apewe thamani yake (pesa zake)."
Hii ni nukuu ya wazi kwamba mali ya kuibwa inatakiwa kurudishwa kwa mwenyewe.
Vilevile, mali iliyochukuliwa kwa nguvu (ghasb) inapaswa kudhaminiwa kwa yule aliyenyang’anywa, hivyo ni lazima kwa mnyang’anyi kurudisha kitu hicho kwa mwenyewe, kulingana na yale yaliyopokelewa kutoka kwa Samurah, kutoka kwa Mtume (saw) amesema:
عَلَى اليَدِ مَا أَخَذَتْ حَتَّى تُؤَدِّيَ
"Mkono unawajibika kwa ulichokichukua mpaka ukirudishe." (Imepokelewa na At-Tirmidhi na akasema: Hadithi hii ni Hasan).
- Haramu kutokana na miamala batili kama vile mali ya riba na mali ya kamari... Hii ni haramu kwa yule aliyeichuma pekee, na haramu hiyo haimfikii yule aliyeipata kupitia njia ya kisheria kutoka kwa mla riba au mchezaji kamari. Kwa mfano, kumuuzia mla riba bidhaa na kuchukua thamani yake kutoka kwake, au mwanamke kupata matumizi yake kutoka kwa mla riba, au mla riba kumpa zawadi mmoja wa jamaa zake, au miamala mingine kama hiyo ya kisheria. Hakika dhambi ya mali hii inamwangukia mla riba na si kwa yule anayechukua thamani, matumizi, au zawadi. Hiyo ni kwa sababu haramu haifungamani na dhamana mbili katika hali hii. Na miongoni mwa dalili za hayo ni:
1- Mwenyezi Mungu amesema:
وَلَا تَكْسِبُ كُلُّ نَفْسٍ إِلَّا عَلَيْهَا وَلَا تَزِرُ وَازِرَةٌ وِزْرَ أُخْرَى
"Na kila nafsi haichumi (dhambi) ila ni juu yake mwenyewe; na mbebaji habebi mzigo wa mwingine." (Al-An’am [6]: 164)
2- Kwamba Mtume (saw) alikuwa akifanya miamala na Mayahudi wa Madina, huku akijua kuwa mali zao nyingi zilitokana na riba. Mwenyezi Mungu (swt) amesema:
فَبِظُلْمٍ مِنَ الَّذِينَ هَادُوا حَرَّمْنَا عَلَيْهِمْ طَيِّبَاتٍ أُحِلَّتْ لَهُمْ وَبِصَدِّهِمْ عَنْ سَبِيلِ اللَّهِ كَثِيرًا * وَأَخْذِهِمُ الرِّبَا وَقَدْ نُهُوا عَنْهُ وَأَكْلِهِمْ أَمْوَالَ النَّاسِ بِالْبَاطِلِ
"Kwa sababu ya dhuluma ya wale waliohuwa Mayahudi, tuliwaharamishia vitu vizuri walivyohalalishiwa (mwanzo), na kwa sababu ya kuwazuilia kwao watu wengi na njia ya Mwenyezi Mungu. Na kwa ajili ya kuchukua kwao riba, na hali wamekatazwa; na kula kwao mali za watu kwa dhuluma." (An-Nisa [4]: 160-161).
Hivyo, alikuwa akipokea zawadi kutoka kwao kama ilivyopokelewa kutoka kwa Ibn Abbas: Kwamba mwanamke mmoja katika Mayahudi alimpa zawadi Mtume (saw) mbuzi aliyetia sumu, akatuma ujumbe kwake na kusema: "Ni nini kilichokupelekea kufanya ulichofanya?" Akasema: "Nilipenda - au nilitaka - ikiwa wewe ni Mtume, basi Mwenyezi Mungu atakujulisha, na ikiwa wewe si Mtume, basi niwapumzishe watu kutokana na wewe."
3- Imesihi kutoka kwa baadhi ya Maswahaba na Matabi'ina kuruhusu kwao zawadi kutoka kwa mla riba:
a- Mtu mmoja alikuja kwa Ibn Mas'ud akasema: "Nina jirani mla riba, na mara kwa mara anatualika." Akasema: "Kwako ni faida (mahna’uh) na kwake ni dhambi." (Imepokelewa na Abdur-Razzaq as-San’ani katika Musannaf yake).
b- Al-Hasan aliulizwa ikiwa inafaa kula chakula cha wabadilishaji fedha (wanaojishughulisha na riba)? Akasema: "Mwenyezi Mungu amekwisha waambia kuhusu Mayahudi na Manasara, kwamba wanakula riba, na amewahalalishia nyinyi chakula chao." (Imepokelewa na Abdur-Razzaq as-San’ani katika Musannaf yake kutoka kwa Ma’mar).
c- Kutoka kwa Mansur amesema: Nilimwambia Ibrahim: "Nimefikia kwa kiongozi mmoja wa serikali (‘amil), akanikaribisha na kunizawadia." Akasema: "Kubali." Nikasema: "Hata akiwa ni mla riba?" Akasema: "Kubali mradi hukumwamrisha wala kumsaidia (katika riba hiyo)." (Imepokelewa na Abdur-Razzaq as-San’ani katika Musannaf yake kutoka kwa Ma’mar).
4- Pamoja na hayo, ni bora kutofanya miamala na wamiliki wa mali haramu inayotokana na riba. Hivyo wasiuziwe bidhaa wala isipokewe zawadi kutoka kwao kama sehemu ya ucha-Mungu (wara’i), ili muuzaji asichukue thamani iliyochafuliwa na riba kwa bidhaa yake, na asipokee zawadi yao ili isiwe miongoni mwa mali ya riba. Hivyo Muislamu ajiepushe mbali na kila kitu kisicho safi. Maswahaba wa Mtume (saw) walikuwa wakijiepusha na milango mingi ya halali kwa kuhofia kukaribia haramu. Imesihi kutoka kwa Mtume (saw) kwamba amesema:
لَا يَبْلُغُ العَبْدُ أَنْ يَكُونَ مِنَ المُتَّقِينَ حَتَّى يَدَعَ مَا لَا بَأْسَ بِهِ حَذَرًا لِمَا بِهِ البَأْسُ
"Mja hafikii kuwa miongoni mwa wachamungu mpaka aache yale yasiyo na neno (halali) kwa kuhofia kuangukia katika yale yenye neno (haramu)." (Imepokelewa na At-Tirmidhi na akasema hadithi hii ni Hasan).
Kwa muhtasari: Inajuzu kumuuzia bidhaa yule anayefanya miamala ya riba na benki au nyinginezo, na inajuzu kupokea zawadi yake, lakini ni bora zaidi kutomuuzia wala kutopokea zawadi yake.