(Silsila ya majibu ya mwanachuoni Ata bin Khalil Abu al-Rashta, Amir wa Hizbut Tahrir kwa maswali ya wafuasi wa ukurasa wake wa Facebook)
Kwa Firas Khbou
Swali:
Assalamu Alaykum
Nilitaka kuuliza kuhusu hukumu ya kutumia pafyumu zinazokuwa na aina fulani za alkoholi? Mwenyezi Mungu akubarikini.
Jibu:
Wa Alaykum Salam wa Rahmatullahi wa Barakatuh,
Kuhusu pafyumu/manukato yaliyo na alkoholi, hukumu za khamr hutumika kwake. Hii ni kwa sababu Mtume (saw) anasema katika hadith iliyopokelewa na Muslim kutoka kwa Ibn Umar, amesema: Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema:
كُلُّ مُسْكِرٍ خَمْرٌ، وَكُلُّ مُسْكِرٍ حَرَامٌ
"Kila chenye kulevya ni khamr, na kila chenye kulevya ni haramu." (HR. Muslim)
Na anasema (saw) katika hadith iliyopokelewa na Abu Dawud kutoka kwa Jabir bin Abdullah:
مَا أَسْكَرَ كَثِيرُهُ، فَقَلِيلُهُ حَرَامٌ
"Kile ambacho wingi wake unalevya, basi uchache wake ni haramu." (HR. Abu Dawud)
Hivyo, Mtume (saw) amebainisha ni kioevu gani kinachoitwa khamr; nacho ni kila chenye kulevya, kiwe kidogo au kingi, hicho ni khamr. Hapa ndipo inakuja nafasi ya uhakiki wa kiuhalisia (tahqiq al-manat) ili kujua je, pafyumu hii au kolonia na mfano wake hulevya iwapo itanywewa, iwe kidogo au nyingi? Ikiwa inalevya, basi hiyo ni khamr na hukumu za khamr hutekelezwa kwake kwa kuharamishwa katika aina kumi kulingana na hadith iliyopokelewa na Al-Hakim katika Mustadrak yake kutoka kwa Abdullah bin Abdullah bin Umar, kutoka kwa baba yake, kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema:
لَعَنَ اللَّهُ الْخَمْرَ، وَلَعَنَ سَاقِيهَا، وَشَارِبَهَا، وَعَاصِرَهَا، وَمُعْتَصِرَهَا، وَحَامِلَهَا، وَالْمَحْمُولَةَ إِلَيْهِ، وَبَايِعِهَا وَمُبْتَاعَهَا، وَآكِلَ ثَمَنِهَا
"Mwenyezi Mungu ameilaani khamr, na amemlaani mnyweshaji wake, mnywaji wake, mkamuaji wake (mzalishaji), mkamuliwa wake (mwenye kuagiza itengenezwe), mbebaji wake, mbebwa kuelekea kwake, muuzaji wake, mnunuzi wake, na mlaji wa thamani yake (pesa itokanayo nayo)." (HR. Al-Hakim)
Kulingana na kauli za wataalamu kuhusu athari za dutu ya alkoholi iliyochanganywa katika vioevu, kioevu hiki huwa ni chenye kulevya kikinywewa. Na kwa kuwa Mtume (saw) anasema: "Kila chenye kulevya ni khamr na kila khamr ni haramu" iliyopokelewa na Muslim, kwa sababu hiyo, hukumu za khamr zinatumika kwa pafyumu zilizochanganywa na alkoholi.
Ndugu yenu, Ata bin Khalil Abu al-Rashta
Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir wa Facebook
Kiungo cha jibu kutoka kwenye tovuti ya Amir
Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir wa Google Plus