** (Mfululizo wa majibu ya mwanachuoni Ata bin Khalil Abu Al-Rashtah, Amiri wa Hizb ut-Tahrir, kwa maswali ya wafuasi wake kwenye ukurasa wake wa Facebook)**
Kwa Sawt Altahrir
Swali:
Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.
Ni ipi hukumu ya mfanyakazi wa taasisi isiyo ya serikali kujiunga na bima ya taasisi hiyo ambayo imeingia mkataba na kampuni ya bima ya afya?
Na ni ipi hukumu kwa mfanyakazi anayeiwakilisha taasisi katika mkataba na majadiliano na kampuni ya binafsi ya bima ya afya?
Jibu:
Wa Alaykum Assalam Warahmatullahi Wabarakatuh.
Huenda ndugu yangu ukalifafanua swali hili zaidi...
Vyovyote iwavyo, ikiwa maana ya swali inakusudia hukumu ya bima ya afya kwa wafanyakazi kutoka kwa taasisi zao wanazofanyia kazi, yaani taasisi inakata sehemu ya mshahara wa mfanyakazi mkabala wa kugharamia matibabu yake na familia yake... basi hili ndilo jibu lake:
Kuhusu bima ya afya:
Ikiwa imeunganishwa na mkataba wa kazi, yaani kama sharti miongoni mwa masharti yake na wala si mkataba unaojitegemea, basi inajuzu. Lakini ikiwa ni mkataba unaojitegemea, basi haijuzu.
Ufafanuzi wa jambo hilo ni kwamba, ikiwa mwajiri atakubaliana na mfanyakazi kuwa mwajiri atawajibika na matibabu ya mfanyakazi pekee au pamoja na wanafamilia wake mkabala wa kukata sehemu ya mshahara wa mfanyakazi, basi hili linajuzu. Hii ni kwa sababu mkataba wa msingi ni mkataba wa ajira (ijarah) na hili linafahamika, na kuwajibika kwa mwajiri na matibabu ya mfanyakazi au wanafamilia wake ni sharti lililoambatana na mkataba wa kazi. Masharti katika mikataba hayakatazwi isipokuwa kama kuna andiko linaloyakataza, kama vile kuhalalisha haramu au kuharamisha halali. Masharti hayahitaji andiko la kuyaruhusu ili yajuzu, bali yanahitaji kutokuwepo kwa andiko linaloyakataza. Yaani masharti si kama vitendo (af'al) ambavyo asili yake ni kufungamana na sheria hivyo kuhitaji andiko la kuruhusu kufanywa kwake, bali masharti ya mikataba yanajuzu isipokuwa kama pamekuja andiko la kuyakataza. Imepokelewa kutoka kwa Kathir bin Abdullah bin Amr bin Awf al-Muzani, kutoka kwa baba yake, kutoka kwa babu yake, kwamba Mtume wa Allah (saw) amesema:
وَالْمُسْلِمُونَ عَلَى شُرُوطِهِمْ إِلَّا شَرْطًا حَرَّمَ حَلَالًا أَوْ أَحَلَّ حَرَامًا
"Na Waislamu watawajibika na masharti yao, isipokuwa sharti linaloharamisha halali au kuhalalisha haramu." (Imepokelewa na At-Tirmidhi).
Hii ni upande mmoja, na upande mwingine ni kwamba sehemu hiyo inayokatwa ni sehemu ya ujira wa mfanyakazi. Kwa hiyo, bima ya afya kutoka kwa mwajiri kwenda kwa mfanyakazi na wanafamilia wake mkabala wa kukata sehemu ya mshahara inajuzu, iwe ni kwa ajili ya mfanyakazi na familia yake tangu mwanzo, au iwe ni kwa mfanyakazi pekee kisha familia yake ikaunganishwa baadaye kwa makubaliano kati ya mfanyakazi na mwajiri na ikawa sehemu ya mkataba; yote hayo yanajuzu.
Ama ikiwa mkataba wa bima ya afya ni mkataba unaojitegemea, yaani kama vile kuanzishwa kwa taasisi na kutangaza kwa umma kuwa yeyote anayetaka imtibie akiumwa basi alipe kiasi fulani kila mwezi mkabala wa kutibiwa pindi anapougua, basi hili haijuzu. Hii ni kwa sababu ni mkataba juu ya kitu kisichojulikana (majhul), kwani hajui ni lini ataugua, na je, ugonjwa wake utakuwa mkubwa au mdogo...
Ndugu yenu, Ata bin Khalil Abu Al-Rashtah
Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Facebook wa Amiri: Facebook
Kiungo cha jibu kutoka kwenye tovuti ya Amiri: Tovuti ya Amiri
Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Google Plus wa Amiri: Google Plus